top of page

TARI kuzalisha mbegu za kukabiliana na udumavu.

Updated: 2 days ago

Na Anord Kailembo

Mkulima anapopanda mbegu huwa na matarajio ya kupata mavuno mazuri yanayokidhi mahitaji yake na ili mavuno hayo yapatikane ni lazima mbegu hiyo ihudumiwe vizuri ili iweze kuchipua na kutoa mazao mazuri.


Mkulima huwa na wajibu wa kuweka ufuatiliaji wa mbegu hiyo tangu inapopandwa lakini pia kuihudumia katika kila hatua ili kuweza kufikia matarajio ya uvunaji.


Vivyo hivyo kwa mama mjamzito mimba inapotungwa wanandoa na familia kwa ujumla hufurahi wakijua wanakwenda kumpata mtoto, mtoto ambaye humuwekea matarajia makubwa ya maisha yake duniani hata kabla ya kumpata.


Na ili kufikia tunda zuri kwa maana kupata mtoto lakini pia kuwa mtoto mwenye kufikia matarajio ya wazazi ni lazima mimba na aliyebeba mimba hiyo wahudumiwe vizuri pengine kwa kuzingatia ushauri wa wataalam.


Hapa nazungumzia suala la lishe kwa mama mjamzito lakini pia mtoto anapozaliwa kuendelea kuhudumiwa vizuri katika nyanja ya lishe ili kumtengenezea uimara katika afya yake kimwili na kiakili.


Wataalam wanatwambia kipindi cha siku 100 tangu kutungwa kwa mimba ni siku muhimu sana za kuimarisha lishe ya mtoto kwani ni kipindi ambacho mtoto huandaliwa kikamilifu kiakili na kimwili ambayo yatakuwa ni matokeo ya fikra na utendaji wake ukubwani.


Wengine uenda mbali zaidi na kusema ulivyo sasa katika nyanja ya kufikiri na kutenda ni matokeo ya huduma ya lishe uliyopatiwa tangu kutungwa kwa mimba yako hadi kufikisha miaka miwili na ndiyo maana ukawepo msisitizo zaidi wa wataalam wa afya katika suala la lishe kwa watoto wa umri huo.


Tunapozungumzia suala la lishe ni pamoja na chakula anachokula mjamzito au mtoto kwa umri huo, kiwe ni chenye kumpatia virutubisho vyote vinavyohitajika ndio maana mama mjamzito anatakiwa kupata lishe ya kutosha kipindi cha mimba na anapojifungua kuhakikisha anamnyonyesha mtoto kwa ufanisi na kwa muda lengwa wa miaka 2 lakini pia mtoto kupatiwa chakula chenye makundi yote kuanzia umri wa miezi 6 kwani itakapofanyika kinyume chake mtoto hupata udumavu.


Udumavu ni moja za changamoto za kiafya ambazo zimekuwa zikiwakabili watoto nchini hasa walio chini ya umri wa miaka 5 sambamba na wajawazito, na hii ni kutokana na tangu mama akiwa mjamzito kukosa matumizi mazuri ya vyakula vya lishe.


Inaelezwa asilimia 30 ya watoto nchini wanautapiamulo, hii ina maana kwamba waliko watoto watatu mmoja ana utapiamulo, jambo hili ni hatari kwa watoto kwani uharibu ndoto zao za kimaisha na afya.


Mkoa wa Kagera ni kati ya mikoa ya Tanzania inayotajwa kuwa na kiwango kikubwa cha udumavu kwa watoto walio chini ya miaka 5 ambapo asilimia 34 ya watoto walio chini ya miaka 5 wana utapiamulo licha ya jitihada mbalimbali za wadau na serikali za kukabiliana na tatizo hilo kuwepo.


Wakati mkoa huo ukitajwa kuwa na udumavu kwa watoto wadogo bado ni mkoa wenye wingi wa vyakula mbalimbali vinavyokamilisha makundi ya chakula bora.


Wakati wanaharakati na wadau mbalimbali wakikabiliana na udumavu, taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania TARI kituo cha Maruku mkoani Kagera imeguswa na changamoto hiyo na kuamua kuzalisha mbegu za kisasa zinazolenga kuwasaidia walaji kukabiliana na tatizo hili.

Emmanueli Masamaki pichani ni mtafiti wa zao la migomba Tanzania katika kituo cha utafiti Maruku. Akizungumza katika mahojiano maalum na Montessori Tanzania amesema TARI imeamua kuzalisha mbegu ya mgomba zinayotoa ndizi yenye Vitamini A kwa ajili ya kukabiliana na udumavu.


Amesema kuwa utafiti juu ya mbegu hiyo ya mgomba umekamilika na tayari imewasilishwa kwenye mamlaka inayohusika na ukaguzi wa mbegu TOSCI na baada ya kurasimishwa itapelekwa kwa wakulima wa migomba kwa ajili ya uzalishaji wa chakula hicho.


Anasema kuwa mbegu hiyo imeandaliwa kulingana na mazingira ya eneo la uzalishaji kwa maana ni yenye kuvumilia ukame, kustahimili magonjwa na inao uwezo wa kuzalisha ndizi kubwa na  yenye radha nzuri kwa walaji.


Ameongeza kuwa endapo TOSCI itakaporuhusu mbegu hiyo kwenda kwa wakulima mashamba yapo tayari kuzalisha kwa wingi na kuzipeleka kwa wakulima.


Amesema kuwa ndizi zitakapoanza kuzalishwa zinaweza kuandaliwa kwa namna tofauti ya mapishi ikiwemo kupikwa kama chakula cha kawaida, kukaangwa, kuchomwa na kutengeza unga lishe.


“Wakulima na wananchi kwa ujumla wanatakiwa kuwa tayari kushirikiana na TARI katika kuhakikisha matokeo yaliyokusudiwa kwa ndizi hizo ya kukabiliana na utapiamulo basi inafanikiwa kwa kulima na kuzitumia kama chakula” anasema Dkt. Masamaki.


Mbali na ndizi pia taasisi ya TARI inazo mbegu za zao la maharage ambazo ni maalum kwa ajili ya lishe vilevile. Tayari aina nne zimethibitishwa na TOSCI kuwa na ubora na tija kwa jamii ya watumiaji wa chakula hicho ambazo kitafiti wamezipa majina yafuatayo TARIBEAN 4, TARIBEAN 5 na TARIBEAN 6.

Scholastica Masanja Elias pichani ni mtafiti wa zao la maharage katika kituo cha TARI Maruku anasema aina hizi za maharage pamoja na kumsaidia mkulima kulima na kuzalisha kwa ajili ya biashara lakini lengo kuu ni kumuwezesha mtumiaji kuimarisha afya yake.


Amesema kuwa maharage hayo yana kiini cha lishe Vitami A, madini ya  chuma na Zinc lakini pamoja na kwamba zimetengenezwa kwa ajili ya kuimarisha usalama wa chakula lakini lengo kuu ni kukabilina na udumavu unaoukumba mkoa wa Kagera na mikoa mingine.


Schorastica amezitaja sifa za maharage hayo kuwa iwapo mkulima akizingatia kanuni bora za kilimo katika ulimaji wake zitatoa mazao ya kutosha (kuzaa kwa wingi) lakini pia yanaweza kupikwa kwenye chakula, kuandaliwa kama mboga, unga kwa ajili ya uji pamoja na kukaangwa.


“Katika utafiti wa maharage hayo tumezingatia matakwa ya wakulima na watumiaji kwa maana ya uzuri wa maharage, kiwango kikubwa cha uzalishaji, radha nzuri kwa mlaji na kadhalika ili kufikia lengo la kuondoa udumavu kwa watoto” na kuongeza kuwa,


“Tunaiomba jamii yatakapoanza kuzalishwa maharage haya basi iwe tayari kuyatumia lakini pia kuwapatia watoto wao ili kukabiliana na suala la utapiamulo.”


Sambamba na kuzalisha maharage na migomba TARI Maruku pia imezalisha mbegu ya Viazi lishe ambapo Mwichande Ahmedi Mwichande ni mtafiti wa zao hilo.


Mwichande nasema viazi ni kati ya mazao ambayo yamekuwa yakilimwa mkoani Kagera kwa kipindi kirefu lakini vimekuwa vikilimwa viazi vya asili.


kutokana na kuchoka kwa udongo, magonjwa na mabadiliko ya hali ya hewa uwezo wake wa kukabiliana na changamoto hizo unashuka na hivyo mazao hupungua kwa kuliona hilo TARI Maruku kwa kushirikiana na vituo vingine vya utafiti wa zao hilo kimeleta mbegu ambazo zitasaidia kuvumilia changamoto tajwa lakini pia zenye virutubisho vingi.



Ameongeza kuwa katika mpango wa TARI wa kuja na mbegu za mazao zenye kutoa mchango katika kukabiliana na udumavu wataalam walikaa na kuzalisha mbegu mpya ya kiazi yenye uwezo mkubwa wa kutoa Vitamini A kwa wingi kwa mlaji ukilinganisha na viazi vya asilia.


Miongoni mwa mbegu za viazi lishe zilizozalishwa ni pamoja na KABODE na TARI SP4 mbegu hizi zinakuwa na kiazi chenye rangi ya chungwa au karoti ambazo zina kiasi kikubwa cha virutubisho vya vitamini A lakini virutubisho vyake vinazidiana kutokana na rangi ya sehemu ya kula (fresh part) viazi vyenye rangi ya machungwaau karoti iliyokolea zaidi ndio huwa na virutubusho vingi vya Vitamini A


Amesema kuwa mbegu hizi tayari zimepitishwa na TOSCI kwa ajili ya matumizi na zipo kituoni lakini pia ziko kwa wazalishaji mbegu ambao wameandaliwa na kupatiwa mafunzo ya namna ya kuandaa mbegu kwa ubora na kuwauzia wakulima.


Kadhalika ameongeza  kuwa tayari mkoa wa Kagera unao wazalishaji wa mbegu hizo 23 kwa maana ya Misenyi 8, Kyerwa 4, Bukoba dc 6 na Karagwe 5 na kwamba mapokeo ya mbegu hizi kwa wakulima ni mazuri kwani yalifanyika majaribio ya wakulima kushiriki moja kwa moja na kutoa mrejesho.


Amesema kuwa sio tu suala la lishe pia mbegu hizi zinamuwezesha mkulima kupata mavuno mengi.


Mfuatiliaji wa makala hii hakika kinachofanywa na taasisi hii ya utafiti ya TARI Maruku ndio uzalendo halisi unaolenga si tu kuimarisha ustawi wa chakula lakini pia kulinda  afya za watanzania.


Hapa TARI inamsaidia mkulima na mtumiaji wa chakula kutokunyemelewa na magonjwa mbalimbali kwani mbali na mazao hayo kudhibiti udumavu lakini pia mchango wa mazao hayo ya chakula ni kuimarisha kinga ya mtumiaji suala linalomuondolea changamoto za afya zinazosababishwa na ulaji duni.


Sanjari na elimu, ni tunatambua kuwa ni kupitia chakula bora ambapo mtu hujenga afya ya mwili na akili vinavyopelekea fikra tunduizi na ufanisi katika kazi.


Ni wajibu wetu wakulima na watumiaji wa vyakula kuhakikisha tafiti hizi zilizobeba maono chanya zinaleta tija kwa jamii kwa maana ya kufikia lengo kusudiwa na taasisi ya TARI Maruku na serikali kwa ujumla.


Yatupasa kutambua kuwa tafiti hizi hutumia muda na gharama kubwa hadi kukamilika na ili kuonesha thamani ya muda na gharama vilivyotumika haikuwa kazi bure ni lazima tafiti hizo ziwe kwenye matumizi.


Kagera na Tanzania bila udumavu inawezekana ni wakati sahihi wa kupambana na hali hiyo.

 
 
 

Comentários


bottom of page