top of page

Mbegu bora, mazao bora.

Na Anord Kailembo

Tanzania ni moja ya nchi zinazotegemea sana kilimo, sekta hii ni moja ya sekta kubwa na muhimu nchini katika ukuaji wa uchumi, ajira na kupunguza umasikini, ikichangia takriban asilimia 26.5 ya Pato la Taifa na asilimia 30 ya mauzo ya nje.


Kwa mujibu wa utafiti wa kilimo wa mwaka 2022–23 uliofanywa na ofisi ya taifa ya takwimu NBS unaeleza kuwa kaya 8,970,096 zilijishughulisha na kilimo nchini Tanzania, kati ya hizo kaya 8,814,646 zilikuwa Tanzania Bara na kaya 155,450 zilikuwa Zanzibar.


Utafiti huo unaeleza kuwa uzalishaji wa mazao upo kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na ufugaji.


Wakati idadi hiyo ya wakulima ikijishughulisha na kilimo nchini bado sekta hii muhimu inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo wakulima wengi kukosa elimu sashihi ya mbinu bora za kilimo, matumizi ya mbegu zisizo bora, matumizi mabaya ya ardhi na rasilimali za asili, magonjwa na wadudu wa mimea pamoja na  changamoto za kiuchumi na kibiashara.

 

Hii inamaanisha kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuweka kipaumbele katika kuboresha kilimo na kuhakikisha kuwa wakulima wanatumia mbinu bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kufikia malengo ya endelevu ya kilimo na uchumi wa taifa.

 

Kilimo bora huzingatia matumizi sahihi ya rasilimali za kilimo na mbinu bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji na tija, kilimo bora hulenga kuhakikisha wakulima wanatumia mbinu bora za kilimo kulingana na aina ya udongo, hali ya hewa, na mazingira yao ili kupata mazao bora zaidi na kwa wingi.


Misingi hiyo ni pamoja na kuwa na mpango wa ulimaji kabla ya kuanza kwa shughuli yenyewe kwa maana ya uchaguzi sahihi wa zao la kilimo, kulifahamu zao unalotaka kulima, gharama za uendeshaji wa shughuli za kilimo hadi kuvuna sambamba na hatima ya mavuno kwa maana ya masoko au matumizi.


Mbali na mpango ni lazima kujua kuwa katika kilimo bora kuna baadhi ya mambo yanahitajika kufanyika katika umaira na kitaalam zaidi ambayo ni utayarishaji wa shamba, usimamizi na uvunaji.


Lakini ili utayarishaji wa shamba kitaalam uwe na ufanisi ni lazima kinachowekwa shambani kwa maandalizi ya mavuno (mbegu) iwe bora, kwa kuthibitishwa na wataalam wa mazao na mbegu kuwa ina uwezo mzuri wa kuzalisha lakini pia kuendana na mazingira ya shughuli inakofanyika.


Msomaji hii leo nataka tuangazie moja ya eneo muhimu katika kilimo bora ambalo ni matumizi ya mbegu bora katika kufikia malengo yako ya uzalishaji kwenye sekta ya kilimo utaunganishwa na mtaalam wa utafiti kutoka taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania TARI - Maruku.


Makala hii inaandaliwa kufuatia uwepo wa asilimia kubwa ya wakulima kutumia mbegu zisizo na ubora na mwisho wa siku kuvuna chini ya matarajio ukilinganisha na nguvu na gaharama zilizowekezwa kabla.

Dkt. Mpoki Shimwela (pichani) ni mkuu wa TARI - Maruku anasema kilimo bora na mavuno bora hutokana na mbegu bora.


“Katika mapinduzi ya kilimo duniani kitu cha kwanza yaliletwa na mbegu bora, kwa sababu mbegu bora zinakupa uzao mkubwa, hukinzana na magonjwa mengi pamoja na kuhimiri mazingira” anasema


“Kuna mwanasayansi mmoja wa Marekani aliyeitwa Norman Borlaug ambaye alikuwa chanzo kikubwa cha mapinduzi ya kijani, alishiriki kuleta mbegu bora katika mazao kama ngano na Mpunga”


Anasema mbegu bora ni mbegu zilizofanyiwa utafiti na kudhibitishwa na taasisi ya kudhibiti ubora wa mbegu TOSCI na kwamba ndio maana taasisi ya TARI inapotafiti mbegu huzipeleka TOSCI kwa ajili ya udhibitisho na baada ya hapo ndipo hupelekwa kwa wakulima.

 

Dkt. Mpoki anasema kuwa mbegu bora ni ile ambayo huotaji wake ni mzuri kwa maana ya kwamba inakupa matokeo uliyoyatarajia angalau kwa zaidi ya asilimia 90.


Anaongeza kuwa mbegu bora siku zote huwa ni aina moja pale mkulima anapoluwa katika uzalishaji lakini inapotokea mkulima amechanganya mbegu zaidi ya moja kwenye shmaba moja hapo hubora upotea na si jambo zuri kitaalam.


Anasema matumizi ya mbegu bora kwa mkulima yana manufaa makubwa sana, kwanza huumpa nafasi mkulima ya kuchagua aina sahihi ya mbegu inayomfaa kulingana na eneo, nyakati (hali ya hewa) na aina ya udongo.


“Kutokana na tabia ya mbegu anayokuwa ameichagua basi humuwezesha mkulimwa kujua ni muda gani atavuna, mahitaji katika makuzi ya mbegu au mazao, muda sahihi wa kukomaa kwa mazao yake tofauti na zinavyokuwa mchanganyiko” Dkt. mpoki


Ameongeza kuwa mbegu zilizofanyiwa utafiti zina tabia ya kutoa mavuno mengi kwa mkulima kwa sababu mbali na ubora katika kuimiri mazingira lakini pia watafiti hulenga kumsaidia mkulima anapokuwa amezalisha aweze kupata mavuno ya kutosha pia apate ziada ya chakula.


“Wapo wanaolima kibiashara hivyo matarajio yao ni wazalishe kwa wingi na hivyo anapotumia mbegu bora na kuzingatia kanuni nyingine bora za kilimo wana uwezo wa kupata zaidi ya kawaida” anasema Dkt. Mpoki.


Dkt. Mpoki anaongeza kuwa mbegu bora zimekuwa na kawaida ya kustahimili mazingira na kukabiliana na magonjwa ya mimea na kwamba lengo la utafiti ni kujibu changamoto zinazolikabili zao husika, hivyo kama wakulima wanalia na magonjwa au kuathiriwa na hali ya hewa wataalam hufanya utafiti na kuja na mbegu zinazotibu tatizo hilo.


“Mkulima anapokuwa akihitaji mbegu za kupanda kabla hajachukua maamuzi ya kununua ni vyema akawashirikisha wataalam wa kilimo na mbegu juu ya aina ya mbegu anayotakiwa kuipanda kulingana na mazingira, hii itamsaidia kwa sababu zipo mbegu nyingi na bora za kilimo ambazo zinastahimili mazingira mengine” anasema Dkt. Mpoki


Anaongeza kuwa tabia ya mbegu bora ni kukua kwa usawa bila kuzidiana kwa maana mbegu hiyo ni moja tofauti na ambavyo mkulima akichanganya mbegu ambapo huzidiana katika makuzi kutokana na kila mbegu kuwa na tabia yake.


Anasema imekuwepo faida kubwa sana kwa wakulima wanaotumia mbegu bora za kilimo kubwa zaidi ikiwa ni kupata mavuno mengi.


“Hapa nchini na dunia kwa ujumla kuna ongezeko la watu ambapo mahitaji ya mazao ya kilimo yamekuwa makubwa hivyo wakulima wanapata fursa ya kuwa na soko kubwa na la uhakika la mazao” anasema Dkt. Mpoki


Anasema zamani mkulima alikuwa akilima kwa ajili ya mahitaji yake binafsi kwa maana ya chakula lakini kutokana na mabadiliko ya mfumo wa maisha  mahitaji ya chakula yamekuwa ni makubwa hivyo mbali na kulima kwa ajili ya matumizi yake pia ziada inayopatikana inauzwa ili kuchangia pato la familia ya mkulima.


“Mwanzoni wakati tukileta mbegu za zao la fhia mkoani Kagera ilikuwa ni changamoto kwa wakulima wakiikataa kwa madai tofauti ikiwemo suala la radha lakini baada ya muda limekuja kuwa moja ya ndizi pendwa yenye soko kubwa nje ya Bukoba” anasema Dkt. Mpoki.


Anasema baadhi ya watu wamekuwa na imani potofu juu ya mbegu zilizofanyiwa utafiti na kuletwa kwao wakiamini mbegu zao za asili ndizo bora na kwamba wengine uenda mbali zaidi na kudai kuwa mbegu mpya zinaletwa kuharibu mbegu zao za asili suala ambalo amesema siyo sahihi.


Anawataka wananchi kutambua kuwa TARI inapoleta mbegu kwa wakulima inakuwa tayari imejua tija yake kwa mkulima na kuwa hakuna mbegu inaweza kuletwa kwa ajili kumuharibu mbegu nyingine.


Anaongeza kuwa utafiti uliofanyika na kuonesha mbegu bora zina faida ni pamoja na mbegu za mahindi ambapo mbegu za asili kwa hekali moja uzaa gunia 5 lakini mbegu iliyoboreshwa ni zaidi ya gunia 25.


Msomaji nchi ya Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 60, watu hawa wote kila iitwapo leo wanakula mlo zaidi ya mmoja na chakula wanachokula ni matokeo ya shughuli ya kilimo inayofanywa na mkulima.


Ni tamaa ya Montessori Tanzania kuona kupitia matumizi ya mbegu bora zinazozalishwa na watafiti, zenye uwezo wa kuzalisha mavuno mengi zinatumiwa na wakulima kujiinua kiuchumi lakini pia kuliwezesha taifa kufikia mafanikio makubwa ya kiuchumi na uzalishaji wa chakula.


Pale wataalam wanapozalisha mbegu na kupitishwa na TOSCI ni matumaini yetu wataalam wa kilimo wakiwemo maafisa ugani kuchukua hatua ya kuwaelimisha wakulima juu ya umuhimu wa matumizi ya mbegu hizo bora.


Taifa lenye mafanikio kwenye kilimo ni taifa tajiri.

Comments


bottom of page