Namba za msasa
- Jacqueline Mwombeki
- 2 days ago
- 4 min read
Na Jacqueline Mwombeki
Vifaa
Vipande kumi vinavyolingana vya mbao vyenye namba za msasa kuanzia 0 hadi 9.
Dhumini mojawapo
Kumtambulisha mtoto alama za majina ya namba za msingi kwa njia ya kuzipapasa, kuzisoma, kuzihusisha na kuziandika kwa lengo la kujenga dhana kamili ya namba na majina yake.
Utangulizi
Mpendwa msomaji wetu, tunakusihi uendelee kufuatilia makala zetu za elimu ya vitendo vya Montessori na hapa tutazungumzia kitendo kinachoitwa Namba za Msasa kinachopatikana katika madarasa ya kimontessori kinachotambulisha alama za namba za msigi.
Alama hizi huwakilisha kiasi alichokipeleleza hapo awali kupitia fito za hesabu hivyo kwa kupitia zana hii mtoto anapewa lugha rasmi ambazo ni matamshi sahihi ya majina ya alama za namba.
Kwa kuwa kila namba ina kiasi chake, hivyo basi namba za msingi hutambulishwa kupitia hatua kuu 2 kwa nyakati tofauti ya kwanza ni dhana ya kiasi na ya pili ni dhana ya alama.
Lengo la kutenga taarifa katika ufundishaji ni kumrahisishia mtoto mchakato uliopo wa kusajiri taarifa hizo ubongoni mwake, matumizi ya taarifa hizo, kanuni na taratibu zake.
Kimontessori zaidi, mtoto anayetambulishwa namba za msasa ni yule ambaye tayari ametambulishwa kiasi cha namba za msingi kupitia vizima vya fito 10 za hesabu yaani (Number rods)
Vile vile huyu ni mtoto ambaye tayari jina ‘2’ ina thamani ya vitu 2, jina ‘3’ ina thamani ya vitu 3 nk, kwa kusikia, kuona na kugusa ama kuhesabu kiasi hicho kupitia fito.
Alama hizi ambazo ni kitu dhahania, hufuata kama hatua ya pili kwa mtoto baada ya kujenga dhana ya kiasi ambapo alama huletwa kwa mtoto kama ushahidi wa kitu kilichokuwepo kwa mantiki hiyo ni fito; hivyo basi mtoto hupata nafasi ya kuhukumu mahusiano yaani kwa mfano ‘jina tano limezaa vitu 5 na vitu 5 kumbe vyaweza wakilishwa na alama tu, yaani 5!’
Dunia ya leo sote sasa twajua kuwa mtoto anatengenezwa na mazingira aliyomo na mtoto anapokuwa kwenye umri wa miaka 0-6, huchukua taarifa sawa na mtu mwenye njaa asivyoweza kubagua wala kuchagua yeye huona kila kitu chamfaa na hiyo ndio huitwa akili ya kufyoza ama akili sharabifu. Hivyo basi, kutambua na kuchukua hatua kunapelekea maandalizi mema yatakayowezesha mtoto kupata taarifa chanya na sahihi.
Zana hii ni kati ya zana zinazomtengea mtoto taarifa za sayansi ya namba ambazo pengine akili yake imekwishachukua na kama bado basi aweze kuzipata kwa usahihi toka mwanzoni.
Hivyo basi, namba ziko huwa kwenye mwonekano wa mkwaruzo ili wakati wa kupapasa, kuwepo na mwamsho wa hisia katika mlango wa kuhisi wa mtoto hali mchakato wa kutunza taarifa hizo ubongoni mwake ukiwa unaendelea kupitia ncha zake za vidole.
Kumbuka hapo awali alisisimua musuli na kuujengea uzoefu na kumbukumbu ya uzito mbalimbali kupitia vizima vya fito zilizo na urefu tofauti kwa kunyanyua, kuhesabu na kupanga hivyo kuwa rahisi kubeba dhahania ya jina na kiasi ambacho sasa anakiona kidhahania zaidi kupitia alama au picha ya namba.
Kwa yeyote anayejua elimu ya Montessori kwa dhati, anajua fika ambavyo ujifunzaji wa mtoto ulivyorahisishwa. Tunajua mtoto ndogo ndo umri sahihi wa kuakikisha kila kilichochema kinawezeshwa kwa muda huo, maana ni rahisi kujifunza na kukichukua kikawa sehemu ya maisha yake hivyo hata katika hesabu, hatuna budi kumwezesha mtoto kupata misingi hiyo mapema.
Mtoto wa umri huu ni mtendaji kuliko msikilizaji hivyo kama elimu zake zinaenda kiutendaji zaidi mtoto hujifunza mambo mengi kwa muda mfupi sana kwani kujifunza kwake ni kupitia michezo; hapa hatuna maana ya michezo ya kurukaruka tu, kukimbizana tu, tuna maana ya shughuli ambazo yeye akizifanya bado anahisi ni michezo. Tunaishi kwenye ulimwengu wa utandawazi, hebu walau jielimishe kupitia video fupi za wachina.
Jinsi ya kutambulisha namba za msasa
· Wakati wa kutambulisha mtoto anatakiwa kushirikishwa kila hatua. Kabla ya kutambulisha zana hii unahitaji kuhakikisha ncha za vidole vya mtoto vinalo nyuzi joto 37° kwa kufanya mambo 2 yafuatayo: kumsaidia kusugua taratibu vidole vyake kwenye kitambaa kilichotiwa na uvuguvugu au kwa kufikicha dole gumba kwenye nyuso za ncha za vidole kwa sekunde kadhaa.
· Wakati wa kuchagua namba, muhusishe mtoto na fito na jaribu kujua kama zipo namba ambazo tayari anazitambua kwa picha na jina husika kisha mpe jina la kitendo ‘namba za msasa’ kama anavyoziona.
· Chagua namba 3 zenye sura tofauti na matamshi yasiyoelekeana; mfano (1, 8 na 2) kwa lugha ya kiswahili na hapa hutegemeana mtu lugha anayoitumia.
· Zipeleke aidha mezani au kwenye mkeka na kuzifunika kulia kwako. Kwa uchache wa maneno, hatimaye mkumbushe mtoto fito na jinsi alivyokuwa akizitumia. Rudia kumtamkia tena jina la kitendo ambacho ni namba za msasa.
· Waweza kuanza kwa kumkumbushia wimbo wowote wa namba anao ufahamu na baada ya kusikika akiitaja namba fulani, sita kidogo na kwa mshangao mkubwa wa furaha mwulize kama angependa kuona picha ya namba hiyo. Itafute kati ya zile tatu zilizofunikwa na kuiweka katikati mbele yenu. Jifanye unahakiki kama bado vidole vina joto kwa kugusa shavu lako ikiwa ni baridi, basi vifikiche tena kabla ya kuipapasa namba hiyo.
· Wakati wa kupapasa, ni vyema kutumia vidole 2 vinavyofuata baada ya dole gumba yaani vile vinavyo saidiana na gumba kushika kifaa cha kuandikia.
· Sema, ‘Hii ni picha ya namba mf. moja, acha mtoto arudie kusema picha ya namba moja. Ipapase na sema tena neno moja baada ya kuipapasa. Acha mtoto arudie matendo yaliyofanywa na mwalimu. Hakikisha unaipapasa namba hiyo kwa usahihi huku mtoto akiona hatua zote kuanzia mwanzo wa kupapasa.
· Baada ya kuitamka na kuipapasa namba hiyo, iondoe mbele na kuirudisha kulia kwako aidha juu au chini ya zile mbili ambazo hazijatambulishwa kwa kuifunika.
· Kupitia wimbo mtambulishe alama nyingine kwa kufuata utaratibu namba 1, baadaye 8.
· Rudia tena kuleta namba 2 na kuipapasa wewe na mtoto na kutaja jina lake mara ya pili na kufanya hivyo kwa namba zilizosalia mara hii pasipo kumkumbushia kwa wimbo. Rudia hatua hii ya pili kwa utaratibu uleule lakini mara hii ukiiacha kila namba wazi mbele ya mtoto.
· Tambulisha hatua ya pili ya somo na ya tatu kama unazijua.
· Baada ya mtoto kutambulishwa, hupewa fursa ya kuandika namba hizo kwenye mchanga, kibao kisichokuwa na miraba, kibao chenye miraba na baadaye kwenye karatasi zisizo na miraba na hatimaye zenye miraba.
· Kama amejua namba zote tatu vizuri na kuonyesha shauku ya kutaka kujua nyingine, mwalimu anaweza kufanya hivyo ingawa sio lazima kwa kukadilia uwezo wa upokeaji wa mtoto na kumwongezea namba nyingine 3 mpya au mbili mpya na moja kati ya zile alizotambulishwa awali ambayo inaonekana kumpa changamoto.
Hatua zilizoelezwa ni za utambulisho wa mtoto mmoja mmoja na endapo unalenga kuwatambulisha watoto zaidi ya mmoja, hebu basi buni utaratibu maalum utakaofaa kushirikisha watoto wote.
Comments