top of page

Zana wezeshi zatajwa kurahisisha mawasiliano

Updated: Apr 17


Baadhi ya wanafunzi wakitengeneza zana
Baadhi ya wanafunzi wakitengeneza zana

"Tunajifunza kupitia makosa"


Na Alodia Babara


Zana wezeshi ni vifaa au vitendo vinavyotumika katika ujifunzaji na ufundishaji ili kujenga dhana ya umahiri uliokusudiwa. Zana hizo hutumiwa na mwalimu katika ufundishaji ili kuinua kiwango cha uelewa kwa wanafunzi.


Ujifunzaji wa kutumia zana wezeshi umetajwa kuwa njia ambayo inamrahisishia mwalimu kufundisha, kutatua changamoto za watoto na kufahamu wapi pakuwasaidia watoto hao.


Hata hivyo, ujifunzaji usiotumia zana unaonekana kumfanya mtoto kushindwa kuelewa haraka na kuhitaji mwalimu arudie mara kwa mara.


Maandalizi duni ya mwalimu kabla ya kufundisha na kutotumia zana mbalimbali za kujifunzia na kufundishia, inaweza ikawa sababu mojawapo ya baadhi ya wanafunzi kushindwa kuelewa somo, hivyo kusababisha washindwe kufaulu majaribio na mitihani.


Walimu katika chuo cha Ualimu cha Partage Montessori, kwa nyakati tofauti wakizungumza na Montessori Tanzania wameeleza umuhimu wa kutumia zana wezeshi katika ufundishaji.


Mwalimu Theodozia Domisian anasema kuwa, walimu hutumia zana hizo kuwafikishia elimu watoto, hasa wenye umri wa kuanzia miaka mitatu hadi sita kutokana na watoto wa umri huo kuelewa zaidi wanapofundishwa kwa kutumia vitendo.

 

Amesema anajuta kwa jinsi alivyojifunza pasipo kutumia vitendo wakati akiwa mtoto, na kwamba hata kama alipata uelewa lakini sio kama ambavyo angejifunza kwa vitendo.

 

“Najutia njia aliyotumia mwalimu wangu kunifundisha, ilikuwa si kwa vitendo, natamani wanafunzi sasa katika shule zote wajifunze kwa vitendo, kwani watapata uelewa mzuri zaidi’ anasema.


Anasema kutokutumia zana wezeshi katika ujifunzaji na ufundishaji ni kutokutenda haki kwa watoto, maana elimu inabaki kwenye maswali na watoto hawaelimishwi kwa kina.


“Jamii unakuta inamhukumu mtoto kuwa hana akili kumbe ni mfumo anaotumia kujifunza haumwezeshi kupata uelewa kwa kina, mzazi/mlezi hajui nini atafanya kwa mtoto wake, hili nalo ni tatizo” anasema Domisian.


Mwalimu Justa Macholi naye anaunga mkono maelezo ya mwalimu mwenzake, kuwa ujifunzaji na ufundishaji wa kutumia zana ni tofauti na wa kawaida, maana wa kawaida ni kuona na kusikia.


Anasema mwalimu anapomfundisha mtoto kwa kutumia zana wezeshi, anakuwa kama anamletea ulimwengu karibu, ili aweze kupeleleza na kudadisi kwa lengo la kupata taarifa.


Naye mwalimu Eradius Theonest anasema mwalimu anapotumia zana wezeshi, mwanafunzi hupata faida kwa kujifunza zaidi kwa kugusa, kuonja, kunusa na kusikia, hivyo kurahisisha uwasilishaji maana uasili wa binadamu lazima aguse, aone na apeleleze.


“Humsaidia kubadilisha mazingira ya kupatia maarifa na ujuzi, kumfanya afurahie somo na kulipenda. Pia, humfanya mtoto kuona ukweli, kupenda shule na ni vigumu kusahau alichofundishwa” anasema.

 

Aidha anataja athari za mwalimu kutotumia zanawezeshi kuwa huhitaji kuongea zaidi, ili aweze kueleweka kwa anaowafundisha, maana wanafunzi wanategemea kupata maarifa kutoka kwake.

 

Kwa mujibu wa mtandao wa elimu ya awali Tanzania, zana za ufundishaji zina umuhimu mkubwa katika kujifunza kwa watoto, ambapo wanawashauri walimu wote tarajali na waliokazini, kuwa tayari kuzingatia angalau matumizi ya zana ili kusaidia kueleweka kwa haraka darasani.


Mtandao huo unaeleza kuwa, zana yaweza kuwa ya kutengeneza, kununua, kuazima, kuchora, kuokota lakini vilevile ikashauriwa mwalimu asirudie sana utumiaji wa zana ya aina moja.


Kwa mantiki hiyo, walimu katika shule zote zikiwamo binafsi na za serikali, wanapaswa kutilia maanani umuhimu wa kutumia zana wezeshi katika ufundishaji, ili kuhakikisha watoto wanaowafundisha wanaelewa haraka

コメント


bottom of page