top of page

Zana wezeshi za Montessori kwa madarasa ya elimu ya awali

Updated: Apr 17

MNARA


Na Jacqueline Mwombeki


Kupitia makala zetu za zana wezeshi msomaji atapata kufahamu zana mbalimbali za Montessori zitumikazo kujifunzia na kufundishia katika madarasa ya Awali ili kufikisha ujumbe kamili wa kielimu kwa mtoto.


Nipende kukukaribisha msomaji kuanza kufuatilia makala za zana wezeshi katika tovuti hii (website) ili upate kufahama mengi zaidi juu ya mfumo wa Dkt Maria Montessori na matumizi yake.


Makala za zana wezeshi za Montessori zitazungumziwa katika njia ya simulizi badala ya somo. Lengo ni kumgusa kila msomaji wetu lakini pia ni faida kubwa kwa wale walio wapenzi wa Montessori na wale wanaofundisha kwa kutumia mfumo huo madarasani.










Zana za Montessori katika karakana ya Chuo cha Ualimu Partage

Montessori zikiwa zimeandaliwa tayari kwa matumizi.


Ni yangu nia na matarajio kwamba msomaji wetu atapata kujua zana moja baada ya nyingine hivyo kuweza kuzipambanua na zana nyinginezo duniani, lakini pia atapata kusikia dhumuni moja tu la jumla la zana itakayokuwa inazungumziwa. Ukitia nia, mengine utayakuta darasani.


Zana za kimontessori zipo kwa ajili ya kusisimua hisia ya ujifunzaji, udadisi na upelelezi kwa mtoto na wakati huo huo zikilenga kujibu hitaji alilonalo mtoto la kiu ya usahihi wa

taarifa. Hivyo basi, zimeandaliwa kisayansi ili kujibu dhana ya utimilifu, usahihi, upelelezi, utaratibu, mahesabu, lugha na utamaduni. Elimu ya mtoto iko kwenye ncha zake za vidole kwani anatarajia kujifunza kupitia kugusa, na milango ya fahamu. Lakini ili hayo yote yajengeke, ni lazima mtoto aoneshwe matumizi sahihi, kuongozwa na kupewa muda wa kupeleleza.


ZANA YA MNARA (kwa maandalizi ya mhandisi wa kesho)

Ifuatayo ni zana ya Mnara ijulikanayo kwa kimombo kama (The Pink Tower)

Vifaa vyake

Miche-mraba 10 yenye rangi moja na ukubwa tofauti Mche-mraba wa kwanza una cm.1 na mche-mraba wa mwisho una cm. 10.


Dhumuni mojawapo

Kwa kutumia mlango wa kuona, mtoto aweze kujenga mnara kwa kubagua vipimo kufuatana na mfululizo wake.

Utangulizi

Je, umewahi kukutana na zana hii nje ama ndani ya darasa la Montessori au pengine kuona kitu kinachoelekea kufanana na hicho? Na je, mwonekano wake unakwambia nini?


Ni maswali ambayo si mtu mzima pekee anayeweza kujiuliza, bali pia na mtoto anaweza kujiuliza swali lile lile anapokutana na mazingira kama hayo. Hivyo tunaamini chochote kinachibua maswali ni elimu. Yamkini mwonekano wa zana hii unashabiiana na vitu vingi kwenye mazingira yetu ambavyo pia vimebeba jina sawa na hilo; minara ya mawasiliano kwa mfano. Minara yote hujengwa kwa kutumia kanuni moja ya hesabu, kwa kuanza na kilicho kizito kuelekea chepesi au kikubwa kuelekea kidogo, au kinene kuelekea chembamba ili kimoja kiweze kubeba uzito wa vingine vinavyofuata.


Kwa mtoto, majibu ya maswali yake mara nyingi hupatikana kwa kugusa kulingana na umri. Hivyo basi kitendo cha mnara ni miongoni mwa zana za Montessori zinazopatikana kwenye darasa la Awali kwa lengo la kumletea ulimwengu wa vipimo kwa ukaribu na kupata uhalisia wake kwa njia ya upelelezi wa kugusa ili kuondoa kiu na mashaka aliyonayo mtoto ya kuhusiana na dhana ya vipimo.


Matumizi ya zana ya MNARA

Hii ni zana iitwayo mnara, lakini haitoshi kusema mnara, bali ni mnara wenye rangi ya pinki/waridi. Na hivyo ndivyo zana hii inavyojulikana duniani kote. “The pink tower” asili yake ni Montessori, na ina maana kwamba ukikutana na zana kama hii imepakwa rangi ya kijani ama tofauti na pinki, basi utakuwa umeiondoa zana hii katika uasili na uhalisia wake ambavyo mtu anaweza kuanzia hapo kuhoji; kwani duniani kote zana ama vitendo vya Montessori rangi ya zana fulani ni ile ile na sababu ni kulinda na kuhifadhi urithi wake.



Mnara ukiwa katika matumizi tunduizi ya mtoto


Kwa nini ni pinki; labda mwenye wazo la jina hilo kama angelikuwa hai, angetwambia, ila tunaamini jina linasababisha kuipambanua zana hii na zana nyingine, lakini sababu nyingine yaweza pia kuwa rangi ya pinki ni tulivu.


Kitendo hiki kinapatikana katika darasa linalotumia programu za Montessori lakini pia mzazi mmoja mmoja anaweza kuwanayo nyumbani kwake. Basi ni vyema kufahamu matumizi yake ili wakati mwingine kitumike kwenye njia iliyo sahihi na

salama kwa mtoto.


Kwa nini zana hii inaongelewa?

Mbali na kitendo hiki kushawishi, kwa kutazama na macho yako tayari unaona kuwa umbo ni moja, japo linaonekana kuwa kwenye ukubwa tofauti na bila shaka swali lako la msingi ni kwa nini kipimo kimetofautiana?


Licha ya hiyo, unabaini kuwa, kipimo kinachopungua ama kuongezeka ni kile kile jambo ambalo ni kweli, na mwonekano huo ndio unaomshawishi mtoto kuiendea zana hii na kuitumia pasipo kikomo kwani tayari kuwepo kwake, utimilifu, na mwonekano wake, huibua mashaka na maswali ya vipimo, ukamilifu, udadisi, upelelezi, utimilifu, mahesabu, marudio na makadilio.


Zana hii imetengenezwa kujibu hayo yote hali kadhalika na mengine ambayo hayakutajwa kama utaratibu na mfululizo, nk.


Lakini majibu ya mashaka na maswali hayo hayapatikani kwa kuitazama zana, bali kwa kuitenda mara kadhaa na dhana ya uhandisi na nyinginezo hujengeka kupitia hayo, na hili wala halihitaji utafiti ndio mtu aone ukweli huu.


Pamoja na kwamba hii ni zana iliyotengenezwa kwa ajili ya watoto wadogo, ajabu yake ni kwamba hata kwa mtu mzima nidhamu ni ile ile kwani hata wewe utahitaji kutumia ukazo wa fikra yakinifu kuupanga mnara huo kwenda juu katika usahihi wake wa vipimo na uwiano kwa umakini wa hali ya juu kabisa.


Lugha zote zilizomo na mahesabu huonekana wazi wazi kwa mtumiaji pasipo kujali umri. Kwa hiyo zana hii kuwa na rangi moja ni kuleta mahusiano ya vipimo na vipande

vyake ili akili ijikite zaidi katika kutafuta ukweli wa mazingira ya kitu kinachoitwa mnara.


Kwa hiyo utamkuta mtumiaji anahangaika kuleta ukamilifu wake binafsi, na hii ni mojawapo ya zana ya Montessori iliyowekwa darasani kwa jaribio lakini ikaonekana kupendwa sana na watoto wote duniani.


Comments


bottom of page