Zana wezeshi za Montessori kwa madarasa ya elimu ya awali
- Jacqueline Mwombeki
- Feb 23
- 4 min read
Updated: Apr 17
NGAZI
Na Jacqueline Mwombeki
Ngazi ni zana mojawapo ya Montessori itumikayo kujifunzia na kufundishia katika madarasa ya Awali ili kufikisha elimu ya usahihi wa vipimo kwa mlengwa, kama tulivyosoma kupitia kitendo cha Mnara kuwa zimeandaliwa kisayansi ili kujibu dhana ya utimilifu, usahihi, upelelezi, utaratibu, mahesabu, lugha na utamaduni.
Ngazi ama (The Brown Stair) kwa lugha ya kiingereza
Vifaa vyake
Vipande 10 vya michemstatili rangi ya kahawia
Vyenye urefu sawa wa cm. 20, vinavyo tofautiana katika unene (thickness) kutoka kwenye cm. 10 hadi cm.1 mzunguko wake.
Hapa tunazungumzia michemstatili 10 inayopungua unene wa cm. moja moja kutoka kipande kinene kuelekea chembamba huku urefu wake ukibaki unalingana ambao ni cm. 20, ambamo mtoto kupitia uzoefu alionao wa upelelezi wa mnara, hubaini uwepo wa mahusiano baina ya vipande vya mnara na vipande vya ngazi. Kipekee, katika matumizi yake mtoto hugundua kuwa kipande kidogo cha mwanzo cha ngazi, vimo vipande vidogo 20 vya cm.1 vya kipande cha kwanza cha mnara.
Dhumuni mojawapo
Kwa kutumia mlango wa kuona, mtoto anajenga taswira na dhana ya ngazi kupitia kujenga na kupeleleza mantiki ya mfuatano wa vipimo katika nyuso tatu za mwelekeo kwa kubagua vipimo kwa kufuata mfululizo wake.
Matumizi ya zana NGAZI
Katika mwendelezo wa simulizi ya zana wezeshi makala iliyopita tulizungumzia zana inayoitwa mnara ambapo kupitia picha na maelezo, tumeona kuwa kuzingatiwa kwa vipimo kumesababisha mwonekano linganifu wa vipimo.
Katika makala hii nimewiwa kuwashirikisha wasomaji zana nyingine pendwa ambayo watoto katika darasa la Montessori hawajawahi kuipatia muda wa kupumzika isipokuwa wakati wa likizo au mwisho wa darasa. Ni zana ambayo haijawahi kuhisi upweke watoto wawapo darasani.
Ni kana kwamba ndani yake ina sauti ya mluzi inayowapelekea kushindwa kujizuia kuitazama, kuigusa na kuhakikisha wanaifanyia kazi kweli kweli huku wengine wakihamasika na kuangaliana nani atakuwa mwenye bahati ya mtende kuigusa baada ya huyo.
Sisi walimu tunakiona kinachowavuta na kuifanya zana hiyo iwe pendwa haswa! Kwanza mtoto anauona mnara ndani ya ngazi japo kuwa huo sio mnara na pili anaona ukweli ambao ni dhana ya ngazi inayoonekana kuwa kwenye umbo dogo na hata kama akijaribiwa kukanyaga au kutembea juu yake, zoezi hilo hawezi kufanikiwa kwani tayari mipaka ama nidhamu ya kitendo tayari imewekwa.
Kwa mantiki hiyo basi aidha, atafanya kama anavyoelekezwa na mwalimu au kwa kuongozwa na mwonekano wa zana hiyo yaani umbo na unene wa michemstatiri hiyo. Hapa ndipo vipaji huanza kuonekana kwa kumkuta mtoto anaangaika kujibu maswali lukuki yaliyosababishwa na zana hiyo yaliyomo katika fikra zake yanayotokana na mambo mbalimbali anayoyaona kwenye mazingira yake na kupitia kitendo hiki kimoja hutaka majibu yote yapatikane.
Kwa kuwa kila zana ina mipaka yake, mtoto hushindwa kuyapata majibu kwa wakati mmoja na hapo akili za mtoto huenda mbali zaidi na kujiongeza kwa kuendea zana nyingine zinazoelekeana na ngazi na kuzitumia kwa wakati mmoja ili kupanua na kuendeleza utafiti wake yaani fikra tunduizi.
Usayansi ndani ya zana ya ngazi
Kwa tafsiri ya haraka, sayansi ni kuzingatia kanuni, vipimo, na maumbo ambavyo hupelekea majibu ya jambo hilo kudhihirika.
Kutokana na zana ya mnara iliyoelezwa katika makala iliyopita, inatupa ujasiri wa kusema kuwa zana za kujifunzia na kufundishia za Montessori zina usayansi ndani yake.
Zana hii ya ngazi ambayo haitofautiani sana na mnara kimtazamo, lakini kielimu ipo sababu ya kwa nini ule ni mnara na hii ni ngazi; mionekano yake, ujenzi na matumizi ndicho chanzo cha kuongelea tofauti zake kwani vipimo hupelekea kuwa na upelelezi tofauti.
Kwa mwonekano wake tu tayari inatoa viashiria vya umakinifu katika matumizi kupitia usahihi wa vipimo na utimilifu wa kiasi, na kwamba mtumiaji kupitia nidhamu iliyomo majibu yoyote atakayoyapata baada ya kutenda, yatamwonyesha dhahiri ukamilifu na dhumuni lililokusudiwa ndani ya zana husika, wakati huo huo kitendo kuwa na rangi moja humsaidia mtumiaji aweze kuzama ndani akiwa anatafuta majibu na usahihi uliokusudiwa.
Katika kutafuta ukweli wa mahusiano ya vipimo, mtoto badala ya kufuata mfululizo, huanza kufaragua kwa vyovyote awezavyo na kupitia hii, tunaona kwamba akili ama elekeo la ubunifu liko kazini.
Dunia tunamoishi, tunaona kwamba kitu fulani chaweza kudhihirishwa kwa namna nyingi mfano nyumba; ambavyo sayansi na teknolojia kutwa kucha vinatutaka tuboreshe maisha yetu kwa kutumia urithi tulionao. Majengo na miundombinu tunavyoviona kila kuchwao ni dhahiri kwamba binadamu hana kikomo cha upelelezi na ubunifu na kila mara tunatafuta kitu tusichokijua, kwanza tunakifikia kwa kuwaza na tunapokileta kwenye ukweli tunakuta mambo kadhaa yanahitajiana ili kujikamilisha.
Hii ndiyo maana tunaona uhandisi unazidi kushika kasi kwa sababu tu watu wanavumbua teknolojia zinazowezesha hiyo nguvu kuvutana na kitu kikajengwa na kubaki imara kama tunavyoona kwenye majengo kadhaa yaliyojengwa tofauti na hivyo tukaviita ni vivutio vya utalii.
Haya hayaji kwenye ndoto bali kwa mtoto kupewa muda wa kufanya na kuridhisha kiu hiyo. Muda mtoto anaopewa kucheza na zana hizi zenye mahesabu ndani yake, humwezesha mtoto kutengeneza ubunifu wake mwenyewe na kumfanya mtoto atekwe na kitendo hicho.
Mtoto huyu katika masomo yake ya baadaye, huonekana mwenye furaha, mwelewa, mdadisi na mwepesi katika kujifunza na elimu nyingine za ngazi zinazofuata hujegwa juu yake pasipo ugumu wowote na ni zana za jinsi hii zinazopalilia ubunifu ambazo hukosekana kwa watoto walio wengi hivyo baadaye kupelekea vijana ambao ni nguvu kazi kukosa ubunifu na fikra tunduizi katika kazi zao kwani uwezo wa kufikiri unakuwa ni mdogo.
Nataka niamshe hisia kwa viongozi, nataka niamshe hisia kwa watumiaji, nataka niamshe hisia kwa wale ambao hawajawahi kuvitumia lakini kuanzia hapa waone umuhimu sasa wa kuwapeleka watoto kwenye shule za Montessori, na kama siyo kuanzisha, basi waweze kufikiria na kuwezesha kitu cha namna hiyo katika jamii zetu.
Comentários