top of page

Wizi: Dhambi inayochafua nafsi, inayodhalilisha hadhi na kudhihirisha uvivu wa kimaadili

Wizi ni tendo ambalo kwa macho ya wengi huonekana kama njia rahisi ya kupata kile ambacho mtu hana, lakini kwa hakika ni mojawapo ya maamuzi mabaya zaidi ambayo mwanadamu anaweza kuyafanya dhidi ya nafsi yake, jamii yake na Muumba wake.


Tangu enzi za kale, wizi umetambuliwa kama dhambi kubwa katika vitabu vyote vitakatifu, lakini zaidi ya hukumu ya kidini, wizi ni ishara ya kuporomoka kwa maadili, kupotea kwa utu na kushindwa kwa dhamira ya kibinadamu, kitendo kinachomnyima mtu heshima yake, kinachovunja imani, na kinachodhihirisha wazi hali ya uvivu wa fikra na moyo.


Vitabu vitakatifu vimeweka msimamo usio na utata kuhusu wizi. Biblia inakataza waziwazi: “Usiibe,” ikiwa ni amri isiyo na masharti, isiyo na visingizio na Qurani Tukufu nayo inaonya vikali dhidi ya wizi, ikionyesha uzito wa kosa hili mbele ya Mwenyezi Mungu.


Mafundisho haya hayakuwekwa kwa bahati mbaya, bali ni kwa sababu wizi ni chanzo cha maovu mengine mengi: chuki, vurugu, kukosa amani na kuvunjika kwa mahusiano ya kijamii.


Anayeiba si tu kwamba anamkosea mwenzake, bali anamkosea Mungu, dhamiri yake na mustakabali wake mwenyewe.


Zaidi ya kuwa dhambi, wizi ni alama ya kudhalilika kwa hadhi ya mwanadamu, mtu aliyeumbwa kwa heshima, akili na uwezo wa kufanya kazi halali, anapochagua kuiba, anajishusha hadhi yake mwenyewe hadi kiwango cha kudharaulika.


Wizi humvua mtu utu wake, humfanya aonekane mdogo hata machoni pake mwenyewe, haijalishi anaiba kiasi gani au kwa siri kiasi gani, ndani ya moyo wake anajua kuwa amejidhalilisha. Hakuna fahari ya kweli katika mali iliyoibiwa, kwani kila kitu kilichopatikana kwa dhuluma hubeba laana ya aibu na hofu.


Wizi pia ni ushahidi wa uvivu wa kimaadili na kiakili mwizi hachagui wizi kwa sababu hana uwezo wa kufanya kazi, bali kwa sababu hataki kutumia jasho, subira na juhudi, ni rahisi kuchukua kilicho cha mwingine kuliko kujituma kujijengea halali.


Lakini urahisi huo wa muda mfupi huzaa mateso ya muda mrefu. Mwizi huishi kwa woga, akitazama nyuma kila wakati, akihofia kufichuliwa, kukamatwa au kulaaniwa, uvivu huu wa kutokubali kujituma huzaa maisha ya wasiwasi na kukosa amani ya ndani.


Jamii yoyote inayovumilia au kupuuza wizi hujijengea msingi dhaifu wa maadili, wizi unapokubalika, hata kwa kiwango kidogo, huanza kuvunja misingi ya uaminifu, majirani hawaaminiani, wafanyakazi hawaaminiki, viongozi wanashukiwa, na hatimaye jamii nzima huishi katika hofu na tahadhari.


Hakuna maendeleo ya kweli yanayoweza kupatikana katika mazingira ambayo mali haithaminiwi na haki haizingatiwi. Wizi ni sumu inayopenya polepole katika mishipa ya jamii, na madhara yake huonekana baada ya muda kwa machungu makubwa.


Kwa mtu anayefikiria kuchukua cha mwenzake bila ridhaa, ni muhimu atafakari kwa kina kabla ya kufanya uamuzi huo. Jiulize: Je, mali hii itakupa amani ya moyo? Je, itakupa heshima mbele ya watu na mbele ya Mungu? Je, itakujengea mustakabali bora au itakuwekea mtego wa aibu na majuto? Ukweli ni kwamba, hakuna wizi unaomalizika bila gharama.


Gharama hiyo inaweza isiwe ya haraka, lakini huja kwa namna moja au nyingine: kupoteza heshima, kuvunjika kwa mahusiano, adhabu ya kisheria, au mateso ya dhamiri yasiyo na mwisho.


Ni lazima pia tukumbuke kuwa kila mali ina jasho la mwenyewe. Unapoiba, unaiba muda, nguvu, ndoto na matumaini ya mtu mwingine, unamnyima haki yake ya kufurahia matunda ya juhudi zake, hili si jambo dogo.


Ni ukatili wa kimya kimya unaovaa sura ya ujanja. Lakini haki ina tabia ya kujirudia, na dhuluma haidumu milele, kile unachokichukua leo kwa dhuluma kinaweza kuwa chanzo cha anguko lako kesho.


Makala hii inakusudia kumfanya kila msomaji ajitazame upya, kama umewahi kuiba, iwe ni mali, pesa, muda au hata wazo la mtu mwingine, bado una nafasi ya kubadilika, toba ya kweli huanza kwa kuchukia kabisa wizi na kuamua kwa dhati kutorudia tena.


Hakuna aibu kubwa kuliko kuendelea na kosa huku ukijua ni kosa, lakini pia hakuna ushindi mkubwa kuliko kuacha uovu na kuchagua njia ya haki, kubadilika si udhaifu, bali ni ushahidi wa nguvu ya ndani.


Kwa wale ambao hawajawahi kuiba, makala hii iwe ukumbusho wa kusimama imara katika maadili. Dunia ya leo imejaa vishawishi, visingizio na sababu za kuhalalisha wizi kwa majina mengine: ujanja, dili, njia ya mkato.


Lakini ukweli unabaki pale pale: kuchukua kisicho chako bila ridhaa ni wizi, na wizi unabaki kuwa wizi bila kujali jina unaloupa, simama upande wa haki, hata kama inaonekana ni ngumu au inachelewesha mafanikio.


Kwa kumalizia, wizi si tu kuvunja sheria za dini au za nchi, bali ni kuvunja misingi ya utu wa mwanadamu, ni tendo linalomfanya mtu ajichukie, jamii imdharau na Muumba wake aghadhibike.


Ni ishara ya uvivu wa kutotaka kujituma na kushindwa kuamini kuwa halali ina baraka kuliko haramu, kila anayesoma makala hii na akawa na wazo la kuiba, basi wazo hilo likome hapa.


Chukia wizi, epuka wizi, kataa wizi kwa moyo wako wote, chagua heshima badala ya aibu, amani badala ya hofu, na haki badala ya dhuluma, hapo ndipo utu wa kweli wa mwanadamu unapopatikana, na hapo ndipo jamii yenye maadili hujengwa.

 
 
 

Comments


bottom of page