top of page

Yafanyie tathimini malengo yako

  • Jan 3
  • 2 min read

 Kujifanyia tathimini ya malengo uliyoweka ni hatua muhimu katika safari ya maendeleo binafsi, kwani humsaidia mtu kuelewa alipo, alikotoka na anakokwenda.


Tathimini siyo kujilaumu au kujisifu, bali ni mchakato wa kujitathmini kwa uhalisia ili kubaini kama juhudi unazofanya zinaendana na malengo uliyokusudia kuyafikia, ili tathimini iwe sahihi, inahitaji uaminifu kwa nafsi, utulivu wa mawazo na utayari wa kukubali ukweli hata pale ambapo matokeo hayaridhishi.


Hatua ya kwanza ya tathimini ni kukumbuka kwa uwazi malengo uliyoyaweka mwanzoni, jiulize malengo hayo yalikuwa nini, kwa nini uliyaweka na ulikuwa unatarajia kuyafikia kwa muda gani.


Malengo yaliyoandikwa huwa rahisi kuyatathmini kuliko yale yaliyobaki akilini, hivyo kama uliyaandika, yarudie tena, kama hukufanya hivyo, jitahidi kuyabainisha upya kwa maneno sahihi ili uweze kuyapima kwa uhalisia kulingana na hali ya sasa.


Baada ya kubaini malengo, hatua inayofuata ni kujitathmini kwenye utekelezaji, hapa ni muhimu kujiuliza kama uliweka juhudi za kutosha, muda wa kutosha na mbinu sahihi.


Angalia kama ulifuata mpango uliouweka au kama ulipoteza mwelekeo njiani, tathmini hii inahitaji mtu kuangalia mwenendo wa kila siku, maamuzi aliyokuwa akifanya na nidhamu yake katika kusimamia muda na vipaumbele vyake.


Sehemu muhimu nyingine ni tathimini ya rasilimali ulizokuwa nazo, jiulize kama ulikuwa na maarifa, ujuzi, fedha, muda au msaada wa watu wengine wa kutosha kufanikisha malengo yako.


Kama haukufanikiwa, inaweza isiwe kwa sababu ya uzembe bali kutokana na upungufu wa rasilimali Fulani, kutambua hili hukusaidia kuepuka kujilaumu kupita kiasi na badala yake kupanga namna ya kujiongezea uwezo kabla ya kuendelea.


Tathimini sahihi pia inahusisha kuangalia changamoto na vikwazo vilivyojitokeza. Hakuna safari ya mafanikio isiyo na vizingiti, hivyo ni muhimu kubaini ni changamoto zipi zilikuwa nje ya uwezo wako na zipi zilitokana na maamuzi yako binafsi, hii hukusaidia kujifunza kutokana na makosa, kuboresha mbinu na kuwa na maandalizi bora zaidi siku zijazo.


Aidha, ni vyema kutathmini matokeo halisi uliyoyapata ukilinganisha na matarajio ya awali, jiulize ni kwa kiwango gani umefanikiwa, hata kama hukufikia lengo kikamilifu.

Wakati mwingine maendeleo madogo huonekana kama kushindwa, ilhali ni hatua muhimu kuelekea mafanikio makubwa, kutambua mafanikio madogo hukupa motisha na kujiamini ili kuendelea mbele.


Katika mchakato wa tathimini, ni muhimu pia kuangalia hali yako ya kisaikolojia na kimwili, jiulize kama ulikuwa na afya njema, motisha, kujiamini na msukumo wa ndani wa kutosha.


Malengo mengi hushindikana si kwa sababu ya ukosefu wa uwezo, bali kutokana na uchovu wa akili, hofu, au kukata tamaa, kujitambua kihisia hukusaidia kupanga mbinu za kujijenga upya.


Hatimaye, tathimini bora haikamiliki bila kuchukua hatua, baada ya kubaini kilichofanyika vizuri na kilichokwenda tofauti, chukua maamuzi ya kuboresha. Unaweza kurekebisha malengo, kubadilisha mbinu, kuongeza muda au kutafuta msaada.


Tathimini ya kweli inalenga kukuandaa kwa hatua inayofuata, si kukufunga katika majuto ya yaliyopita. Kwa kufanya tathimini mara kwa mara, mtu hujijengea nidhamu ya kujifunza, kubadilika na kukua kuelekea mafanikio endelevu.

 
 
 

Comments


bottom of page