top of page

Yawekee “expiry date” matatizo yako

  • 2 days ago
  • 4 min read

Maisha ya mwanadamu hayajawahi kuwa mstari ulionyooka, kila mmoja wetu, bila kujali hadhi, elimu au kipato, hukutana na changamoto za aina mbalimbali za kifedha, mahusiano, afya, au hata kisaikolojia.


Lakini tofauti kubwa kati ya wanaofanikiwa na wanaobaki nyuma si kukosekana kwa matatizo, bali ni namna wanavyoyashughulikia, ndiyo maana kauli hii, “yawekee expire date matatizo yako,” ina uzito mkubwa sana.


Inatukumbusha kuwa hatupaswi kuruhusu matatizo yaishi milele ndani ya maisha yetu; badala yake, tunapaswa kuyapa muda maalum wa kuyatatua na kusonga mbele.


Kuwekea tatizo “expiry date” ni mtazamo wa kimaamuzi, ni uamuzi wa ndani unaosema: “Ninakubali kuwa nina changamoto, lakini sitaruhusu inifunge milele.” Huu si mtazamo wa kukwepa matatizo, bali ni njia ya kujipa mipaka ya muda na mkakati wa kuyashinda.


Watu wengi hukosea kwa kukubali kuishi na matatizo yao kana kwamba ni sehemu ya kudumu ya maisha yao. Hapo ndipo tatizo linapogeuka kuwa mzigo wa kudumu badala ya changamoto ya muda mfupi.


Fikiria mfano wa kijana anayekosa ajira baada ya kumaliza chuo. Badala ya kuchukua hatua, anakaa nyumbani mwaka hadi mwaka akilalamika kuwa hakuna kazi, hapa, tatizo lake halina “expiry date.” Linaendelea kuishi kwa sababu halijapewa kikomo.


Lakini kijana mwingine katika hali kama hiyo anaweza kuamua: “Ndani ya miezi sita nitakuwa nimepata kazi au nimeanzisha shughuli yangu.” Ndani ya muda huo, anajifunza ujuzi mpya, anajitolea sehemu ili kupata uzoefu, au hata kuanza biashara ndogo. Tofauti yao si bahati ni mtazamo.


Katika maisha halisi, kuweka “expiry date” ya tatizo kunahitaji hatua kadhaa muhimu. Kwanza ni kukubali ukweli, usikimbie tatizo lako, ukwepaji huongeza muda wa tatizo kuishi, kama una deni, ukubali kuwa una deni, kama una changamoto ya mahusiano, tambua kuwa ipo, kukubali si udhaifu, bali ni mwanzo wa suluhisho.


Hatua ya pili ni kupanga muda maalum wa kushughulikia tatizo, huu muda unatakiwa kuwa wa kweli na unaotekelezeka. Kwa mfano, mtu mwenye changamoto ya kifedha anaweza kuamua: “Ndani ya mwaka mmoja, nitakuwa nimepunguza madeni yangu kwa asilimia 70.” Hii inaleta mwelekeo na motisha ya kuchukua hatua kila siku, bila muda maalum, akili ya mwanadamu hupoteza mwelekeo na kuruhusu uvivu.


Hatua ya tatu ni kujifunza kupitia wengine, Dunia imejaa mifano ya watu waliowahi kupitia hali kama yako na wakashinda. Badala ya kukaa peke yako na mateso yako, tafuta simulizi zao, soma vitabu, sikiliza mafunzo, au hata ongea nao moja kwa moja, mfano hai ni mama mmoja aliyeanza biashara ya kuuza mboga sokoni baada ya kufiwa na mumewe.


Hakujua chochote kuhusu biashara, lakini alijifunza kutoka kwa wengine waliokuwa tayari wanafanya kazi hiyo, leo hii ana duka kubwa na anawasaidia wengine, hakuruhusu tatizo la kifedha liishi milele.


Hatua ya nne ni kufikiri njia mbadala. Mara nyingi tunakwama si kwa sababu hakuna suluhisho, bali kwa sababu tunang’ang’ania njia moja, kama njia uliyokuwa unategemea haifanyi kazi, badilisha mkakati.


Mfano, kama umetuma maombi ya kazi mara nyingi bila mafanikio, jaribu kujiajiri au kushirikiana na wengine kuanzisha kitu kidogo, ulimwengu wa leo unatoa fursa nyingi lakini zinahitaji ubunifu na ujasiri.


Pia ni muhimu kuelewa kuwa matatizo mengine yanahitaji msaada wa nje, kuna watu wanaokaa na msongo wa mawazo au huzuni kwa muda mrefu wakiamini wataweza kujisaidia wenyewe, lakini hali inazidi kuwa mbaya.


Katika hali kama hizi, kuzungumza na mshauri nasaha, rafiki au mtu unayemwamini ni hatua muhimu sana, kuweka “expiry date” ya tatizo haimaanishi kupambana peke yako bila msaada.


Mfano mwingine wa maisha halisi ni mwanafunzi aliyefeli mtihani muhimu, wapo wanaokata tamaa kabisa na kuamini kuwa maisha yao yameharibiwa lakini wapo wengine wanaotumia kushindwa kama darasa, wanarudia kusoma, wanatafuta walimu wa ziada, na hatimaye kufaulu. Tofauti yao ni kwamba mmoja aliruhusu tatizo liishi, mwingine aliliwekea mwisho.


Ni muhimu pia kuwa na nidhamu binafsi, kuweka muda wa kumaliza tatizo hakutoshi kama huna juhudi za kulitekeleza, nidhamu ni kufanya kile kinachopaswa kufanywa hata kama huna hamasa, ni kuamka mapema, kufanya kazi kwa bidii, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, au hata kuacha tabia zinazokurudisha nyuma. Bila nidhamu, “expiry date” inabaki kuwa maneno tu.


Wakati huo huo, kuwa na imani na mtazamo chanya ni silaha muhimu, watu wengi hushindwa si kwa sababu ya ukubwa wa tatizo, bali kwa sababu ya mtazamo wao, ukiamini kuwa huwezi, mara nyingi utashindwa hata kabla ya kuanza lakini ukiamini kuwa unaweza, utaanza kuona fursa hata katikati ya changamoto, imani hii haipaswi kuwa ya maneno tu, bali iambatane na vitendo.


Hata hivyo, ni muhimu kuwa mkweli si matatizo yote yanatatuliwa haraka, baadhi yanahitaji muda mrefu, uvumilivu na juhudi kubwa lakini hata katika hali hizo, bado unaweza kuweka hatua ndogo ndogo za kufikia suluhisho.


“Expiry date” si lazima iwe siku moja ya mwisho, bali inaweza kuwa mchakato wenye hatua zinazoonekana kila hatua unayopiga ni ushindi dhidi ya tatizo.


Katika jamii zetu, kuna tabia ya kuruhusu matatizo yaendelee kwa muda mrefu kwa sababu ya hofu ya kuanza, watu wanaogopa kushindwa, kuonekana vibaya, au hata kubadili mwelekeo wa maisha lakini ukweli ni kwamba, kubaki palepale kwa muda mrefu ni hatari zaidi kuliko kujaribu na kushindwa, kushindwa kunaweza kukufundisha, lakini kusimama bila kufanya chochote hakujengi chochote.


Maisha ni yako, hakuna mtu mwingine atakayekuja kuweka mwisho wa matatizo yako isipokuwa wewe mwenyewe, unaweza kuamua leo kuwa changamoto unayokabiliana nayo haitakuwa sehemu ya maisha yako milele, unaweza kuanza kwa hatua ndogo kuandika mpango, kuzungumza na mtu, au kuchukua hatua moja tu kuelekea suluhisho.


Kumbuka, matatizo ni sehemu ya maisha, lakini hayapaswi kuwa makazi ya kudumu. Yawekee mipaka, yapangie muda, na pambana kuyamaliza, jifunze kupitia wengine, tafuta njia mbadala, na kuwa na nidhamu ya kuchukua hatua, usikubali tatizo liwe utambulisho wako. Wewe ni mkubwa kuliko changamoto zako.


Ujumbe wa mwisho ni huu: 

Usiruhusu matatizo yako yaamue hatima ya maisha yako, yatazame kama changamoto za muda mfupi zenye mwisho unaoonekana, yawekee “expiry date,” fanya kazi kwa bidii kuyashinda, na songa mbele ukiwa na uzoefu na nguvu mpya, maisha yanaendelea na wewe unastahili kuyaishi kwa uhuru, si kwa kifungo cha matatizo yasiyo na mwisho.

 
 
 

Comments


bottom of page