top of page

NGUVU YA MSUKUMO WA NDANI

  • 16 hours ago
  • 4 min read

NGUVU YA MSUKUMO WA NDANI KATIKA KUPAMBANIA NDOTO YA MAISHA PASIPO KUKATA TAMAA

Katika maisha ya mwanadamu, kila mmoja huzaliwa akiwa na ndoto, malengo na matarajio anayokusudia kuyafikia, wapo wanaoota kuwa viongozi wakubwa, wafanyabiashara wenye mafanikio, wanamichezo mashuhuri, waandishi, wanataaluma au watu wenye mchango mkubwa katika jamii.


Hata hivyo, safari ya kuelekea kwenye ndoto hizo si rahisi. Mara nyingi hujaa changamoto, vikwazo, maneno ya kukatisha tamaa, kukosa mitaji, kukataliwa na hata kushindwa mara kwa mara, katika mazingira hayo, kitu kikubwa kinachoweza kumfanya mtu aendelee kusimama ni msukumo wa ndani.


Msukumo wa ndani ni ile nguvu inayotoka moyoni mwa mtu inayomfanya aendelee kusonga mbele hata pale mazingira yanapokuwa magumu, ni sauti ya ndani inayomwambia mtu kwamba bado ana uwezo wa kufanikiwa licha ya kushindwa alikokutana nako.


Msukumo huu hauhitaji makofi kutoka kwa watu wala sifa kutoka kwa jamii ili mtu aendelee kujituma, ni nguvu inayomfanya mtu aamke kila siku akiwa na matumaini mapya ya kupambania maisha yake.


Watu wengi wamekuwa wakishindwa kufikia ndoto zao si kwa sababu hawana uwezo, bali kwa sababu wamekosa uvumilivu wa kuendelea kupambana, Dunia ya leo imejaa ushindani mkubwa na changamoto nyingi zinazoweza kumfanya mtu akate tamaa. Wengine huanza biashara lakini zikikumbana na hasara huamua kuachana nazo.


Wapo wanaoanza masomo lakini wakikutana na ugumu wa maisha huona hawawezi kuendelea, wengine hujaribu vipaji vyao lakini wakikosa kuungwa mkono mapema huamini kwamba hawafai, ukweli ni kwamba mafanikio mengi duniani yamejengwa juu ya misingi ya kuvumilia maumivu, kushindwa na changamoto mbalimbali.


Historia inaonesha kuwa watu wengi waliofanikiwa hawakufika kileleni kwa urahisi. Walipitia vipindi vigumu lakini hawakuruhusu changamoto zizime ndoto zao, walikuwa na msukumo wa ndani uliowafanya waamini kwamba ipo siku watafanikiwa.


Hii inatufundisha kwamba mafanikio si safari ya siku moja, bali ni matokeo ya jitihada za muda mrefu zinazoambatana na subira na nidhamu binafsi.


Msukumo wa ndani humfanya mtu kutambua thamani yake hata kama wengine hawaioni. Kuna wakati mtu anaweza kubezwa, kudharauliwa au kuambiwa hawezi kufanikiwa, lakini ndani yake akaendelea kuamini kuwa ana uwezo mkubwa wa kufanya mambo makubwa.


Mara nyingi watu wanaofanikiwa huwa ni wale walioweza kuamini ndoto zao hata pale dunia iliposhindwa kuziamini, hii ndiyo sababu ni muhimu kwa kila mtu kujifunza kusikiliza sauti yake ya ndani badala ya kuendeshwa na maneno ya watu.


Aidha, msukumo wa ndani humsaidia mtu kuwa na uthubutu wa kuanza tena baada ya kushindwa, kushindwa si mwisho wa maisha. Mara nyingi kushindwa ni somo linalomfanya mtu kuwa imara zaidi.


Watu wengi waliokata tamaa walifanya hivyo hatua moja kabla ya mafanikio yao. Kama wangekuwa wavumilivu kidogo, huenda wangeyaona matokeo waliokuwa wakiyatafuta. Ndiyo maana ni muhimu kuelewa kuwa changamoto ni sehemu ya safari ya mafanikio.


Katika maisha, hakuna anayepaswa kukata tamaa kwa sababu ya hali ngumu anayopitia kwa sasa. Hali ya leo siyo mwisho wa maisha ya kesho, mtu anaweza kuwa maskini leo lakini akawa tajiri kesho.


Anaweza kushindwa leo lakini akashinda kesho, anaweza kubezwa leo lakini akaheshimiwa kesho, kitu muhimu ni kuendelea kuwa na imani, juhudi na msukumo wa ndani wa kupambana bila kuacha.


Pia, mazingira ya maisha yasimfanye mtu apoteze matumaini, wapo waliotoka katika mazingira magumu sana lakini leo wamekuwa mfano wa mafanikio duniani, wengine walikosa hata mahitaji muhimu ya msingi lakini hawakukubali mazingira yao yawe mwisho wa ndoto zao.


Walitumia changamoto walizokutana nazo kama sababu ya kuongeza bidii badala ya kukata tamaa, hii inaonesha kwamba mafanikio hayaamuliwi na mazingira pekee, bali huamuliwa zaidi na mtazamo wa mtu na nguvu yake ya ndani.


Msukumo wa ndani pia hujengwa kwa kuwa na malengo yanayoeleweka. Mtu asiyejua anachokitafuta maishani ni rahisi kukata tamaa lakini mwenye ndoto iliyo wazi ndani yake huwa na sababu ya kuendelea kupambana kila siku.


Ndoto humpa mtu mwelekeo wa maisha yake. Humfanya ajue kwanini anapaswa kufanya kazi kwa bidii, kuvumilia na kujituma zaidi, ndiyo maana ni muhimu kila mtu kuwa na maono ya maisha yake badala ya kuishi bila mwelekeo.


Sambamba na hilo, ni muhimu kujifunza kujipa moyo binafsi, kuna nyakati ambapo hakuna mtu atakayekutia moyo zaidi ya wewe mwenyewe, watu wanaweza wasione juhudi zako, wasikuelewe au hata wasikuunge mkono.


Katika hali hiyo, mtu anatakiwa ajifunze kujikumbusha sababu ya kwanini alianza safari yake, kujisemea maneno chanya na kuamini uwezo wako ni sehemu muhimu ya kuendeleza msukumo wa ndani.


Kadhalika, nidhamu ni msingi mkubwa wa mafanikio. Watu wengi wana ndoto kubwa lakini hawana nidhamu ya kuzifanikisha, msukumo wa ndani haupaswi kubaki kwenye mawazo pekee, bali unapaswa kuonekana katika matendo.


Mtu anatakiwa kuwa tayari kufanya kazi kwa bidii, kutumia muda vizuri, kujifunza kila siku na kuwa mvumilivu katika safari yake, hakuna mafanikio ya kweli yanayopatikana bila juhudi.


Ni muhimu pia kuzungukwa na watu wenye mtazamo chanya. Marafiki na mazingira yana mchango mkubwa katika maisha ya mtu, ukiwa karibu na watu wanaokatisha tamaa, wanaopenda kubeza ndoto za wengine au wanaokata tamaa haraka, unaweza kupoteza nguvu ya kuendelea kupambana.


Lakini ukiwa na watu wanaokutia moyo na kukuamini, ni rahisi kuendelea kuwa na matumaini hata katika nyakati ngumu.


Vilevile, mtu anatakiwa kujifunza kushukuru hatua anazopiga hata kama ni ndogo. Mafanikio makubwa huanza na hatua ndogo ndogo, wengine hukata tamaa kwa sababu wanataka kuona matokeo makubwa kwa haraka, ukweli ni kwamba kila safari ya mafanikio huhitaji muda, unapojifunza kuthamini maendeleo yako ya kila siku, unajijengea nguvu ya kuendelea mbele.


Kwa upande mwingine, maombi na kumtegemea Mungu vina nafasi kubwa katika kuimarisha msukumo wa ndani, kuna nyakati ambazo nguvu za kibinadamu pekee hazitoshi.


Kumtegemea Mungu humpa mtu amani, matumaini na nguvu mpya ya kuendelea kupambana hata pale mambo yanapoonekana magumu, imani humfanya mtu aamini kuwa ipo siku hali yake itabadilika.


Kwa ujumla, msukumo wa ndani ni silaha muhimu sana katika safari ya maisha. Bila msukumo wa ndani ni rahisi mtu kukata tamaa na kuacha ndoto zake njiani lakini mwenye nguvu ya ndani huwa tayari kusimama tena kila anapoanguka.


Hata kama dunia itamkataa, ataendelea kuamini kuwa ipo siku atafanikiwa, kila mtu anatakiwa kuilinda ndoto yake, kuipambania kwa moyo wote na kutokubali changamoto zimzuie kufikia malengo yake.


Maisha ni safari yenye milima na mabonde, lakini mwenye msukumo wa ndani huendelea kutembea hadi afike anapokusudia, hivyo basi, usikubali maumivu ya leo yakufanye uache ndoto yako ya kesho.


Endelea kupambana, endelea kuamini na endelea kuwa na matumaini. Inawezekana leo ukaonekana wa kawaida, lakini kesho ukawa mfano wa mafanikio kwa wengi. Siri kubwa ni moja tu usikate tamaa.

 
 
 

Comments


bottom of page