KUJITAMBUA
- Anord Jovin
- 16 hours ago
- 3 min read
Kujitambua ni mojawapo ya silaha muhimu zaidi ambazo kijana anaweza kuwa nazo katika safari ya maisha, hata hivyo, ni dhana ambayo mara nyingi hupuuzwa au kutopewa uzito unaostahili.
Vijana wengi wanapoteza miaka yao ya nguvu na ubunifu kwa kuishi bila mwelekeo, bila kufahamu wao ni nani, wanataka nini na wana uwezo gani. Kujitambua siyo kujijua jina au mahali unapotoka pekee, bali ni mchakato wa kina wa kuelewa utu wako, uwezo wako, mipaka yako, ndoto zako, maadili yako na nafasi yako katika jamii.
Kijana aliyejitambua anajua anasimama wapi na anakoelekea. Anajua anachokipenda, anachokiamini na anachokithamini, kujitambua kunamjengea kijana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, kuchagua marafiki wanaomjenga, na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuharibu maisha yake.
Kijana ambaye hajitambui ni rahisi kuyumbishwa na mazingira, kushawishika kirahisi na kuiga maisha ya wengine bila kufikiri hatima yake.
Swali muhimu ni: kijana anawezaje kujitambua? Kwanza, kujitambua kunaanza na kujitathmini binafsi, kijana anapaswa kujiuliza maswali ya msingi kama: Mimi ni nani? Niko bora katika nini? Napenda kufanya nini hata bila kulipwa? Nini kinanifanya nijisikie mwenye thamani? Maswali haya humsaidia kijana kugundua vipaji, ndoto na mwelekeo wa maisha.
Mfano hai ni kijana anayependa kuzungumza na watu, kuongoza au kusaidia wenzake. Huyu anaweza kuwa na kipaji cha uongozi, ualimu au kazi za kijamii, lakini bila kujitambua anaweza kujikuta anasoma au kufanya kazi asiyoipenda, hatimaye kukosa furaha na tija.
Pili, kujitambua kunahitaji kijana kukubali udhaifu wake. Hakuna binadamu mkamilifu. Kujitambua siyo kujiona bora kuliko wengine, bali ni kukubali unachoweza na usichoweza, kijana anayejitambua hatishwi na kushindwa, bali hutumia kushindwa kama somo.
Mfano, kijana aliyeshindwa mtihani au biashara yake ikafeli, badala ya kukata tamaa au kulaumu mazingira, anajitathmini na kujifunza kosa lilipotokea. Huu ni msingi wa ukuaji wa kweli.
Tatu, kujitambua kunajengwa kupitia kusikiliza ushauri na kujifunza kutoka kwa wengine. Wazazi, walimu, viongozi na watu waliopitia maisha wana hazina kubwa ya maarifa.
Kijana anayejitambua hachukui ushauri kama dharau, bali kama mwanga unaomsaidia kuona mbali. Kwa mfano, vijana wengi wanaotumbukia katika matumizi ya dawa za kulevya au uhalifu walipata onyo mapema lakini walilipuuzia kwa sababu hawakujitambua wala kuthamini maisha yao ya baadaye.
Kujitambua kuna tija gani kwa kijana? Kwanza kabisa, kujitambua kunampa kijana mwelekeo wa maisha, kijana anajua kwa nini anaamka asubuhi, anajua anapambana kwa ajili ya nini.
Hili humjengea nidhamu, bidii na uvumilivu. Pili, kujitambua kunamjengea kijana kujiamini, anapojua thamani yake, hawezi kujidharau wala kukubali kudharauliwa, kujiamini humsaidia kijana kusimama imara hata anapokutana na changamoto au kukataliwa.
Faida nyingine kubwa ya kujitambua ni kumsaidia kijana kupanga malengo ya muda mfupi na muda mrefu, kijana aliyejitambua anajua leo anapaswa kufanya nini ili kesho yake iwe bora.
Mfano, kijana anayejitambua kuwa ndoto yake ni kuwa mjasiriamali, ataweka mkazo katika kujifunza ujasiriamali, nidhamu ya fedha na ubunifu badala ya kupoteza muda mwingi katika anasa zisizo na tija.
Kujitambua mapema ukiwa kijana kunasaidia sana kuepuka kupoteza muda. Ujana ni rasilimali adimu; una nguvu, muda na uwezo mkubwa wa kujifunza, kijana anayejitambua mapema hutumia ujana wake kujijenga, siyo kujiharibu.
Mfano hai ni vijana waliotumia ujana wao kujifunza stadi, kusoma, kujitolea au kuanzisha miradi midogo, leo wamekuwa watu wa mfano katika jamii.
Kinyume chake, vijana waliopuuza kujitambua walipoteza muda mwingi katika starehe, makundi mabaya na maamuzi yasiyo na mwelekeo, na baadaye hujikuta wakilaumu serikali, familia au jamii.
Lakini kwa nini baadhi ya vijana wanashindwa kujitambua? Sababu mojawapo ni ukosefu wa malezi na mwongozo sahihi, vijana wengi hukua bila mtu wa kuwaelekeza au kuwasikiliza.
Wengine hukua katika mazingira yenye migogoro, umasikini au msongo wa mawazo, hali inayowafanya washindwe kujiona kwa jicho chanya. Sababu nyingine ni kuiga maisha ya mitandaoni na watu mashuhuri bila kutafakari uhalisia wa maisha yao binafsi, vijana wengi huishi maisha ya “copy and paste”, wakitaka kuwa kama wengine badala ya kugundua wao ni nani.
Pia, hofu ya kushindwa ni kikwazo kikubwa cha kujitambua. Vijana wengi wana ndoto lakini wanaogopa kuanza, wanajilinganisha na wenzao, wanaogopa kuchekwa au kukataliwa, hofu hii huwafanya wakae eneo la faraja bila kukua. Kujitambua kunahitaji ujasiri wa kujaribu, kushindwa na kujaribu tena.
Kwa ujumla, kujitambua ni safari, siyo tukio la siku moja. Ni mchakato unaohitaji muda, uvumilivu na nia ya dhati ya kujiboresha. Kijana anapojitambua, anakuwa suluhisho badala ya tatizo katika jamii.
Anakuwa chanzo cha mabadiliko chanya, siyo mzigo. Ni wajibu wa kila kijana kuamua kuishi maisha yenye maana kwa kuanza na kujitambua.
Ujumbe kwa vijana ni mmoja: usisubiri maisha yakulazimishe ujitambue baada ya maumivu na majuto. Anza sasa, jijue, jikubali, jiamini na jiamue. Maisha yako ya baadaye yanategemea maamuzi unayofanya leo, kujitambua siyo anasa, ni hitaji la msingi kwa kijana anayetamani mafanikio ya kweli.






Comments