Usilete mzaha katika unyonyeshaji
- 3 days ago
- 5 min read
Unyonyeshaji wa mtoto ni zawadi ya asili ambayo mama hupewa kwa lengo la kuhakikisha mtoto anaanza maisha kwa msingi imara wa afya, ukuaji na maendeleo ya kiakili.
Kwa muda mrefu, wataalamu wa afya wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa maziwa ya mama kama chakula kamili kwa mtoto mchanga, lakini bado kuna baadhi ya wazazi wanaochagua kutowanyonyesha watoto wao kwa sababu za maslahi binafsi, mitazamo potofu, au hofu zisizo na msingi wa kisayansi.
Ni muhimu kwa wazazi kuelewa kwamba unyonyeshaji si suala la hiari linalopaswa kuamuliwa kwa kuangalia urahisi wa mzazi pekee, bali ni msingi wa ustawi wa mtoto kimwili, kiakili na kihisia.
Mtoto anaponyimwa maziwa ya mama bila sababu za kitabibu, ananyimwa pia fursa muhimu ya kuimarisha ubongo wake, kinga yake na uwezo wake wa baadaye wa kufanya vizuri shuleni na katika maisha kwa ujumla.
Maziwa ya mama ni chakula kamili chenye virutubisho vyote muhimu vinavyohitajika katika miezi ya mwanzo ya maisha ya motto, yaana uwiano sahihi wa protini, mafuta, wanga, vitamini na madini yanayoweza kumeng’enywa kwa urahisi na mwili wa mtoto.
Tofauti na maziwa ya kopo au vyakula mbadala, maziwa ya mama hubadilika kulingana na umri na mahitaji ya motto, katika siku za kwanza baada ya kujifungua, mama hutoa maziwa ya awali yanayojulikana kama colostrum ambayo yana kiwango kikubwa cha kingamwili.
Haya humlinda mtoto dhidi ya maambukizi mbalimbali kama homa ya mapafu, kuhara na magonjwa mengine yanayoweza kuhatarisha maisha, mtoto anayeanza maisha kwa kinga imara huwa na nafasi kubwa ya kukua bila maradhi ya mara kwa mara, hali ambayo pia huathiri moja kwa moja maendeleo yake ya ubongo, ubongo wa mtoto hukua kwa kasi kubwa katika miaka ya mwanzo ya maisha.
Kipindi hiki ni nyeti sana kwa sababu seli za ubongo huunganishwa kwa kasi, na miunganisho hiyo huathiri uwezo wa mtoto kufikiri, kukumbuka, kuelewa na kujifunza, maziwa ya mama yana mafuta maalum yanayosaidia katika ukuaji wa ubongo, yakiwemo asidi ya mafuta ya DHA na ARA ambazo ni muhimu kwa maendeleo ya seli za neva.
Tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa watoto waliopata maziwa ya mama kwa muda unaopendekezwa huwa na alama za juu zaidi katika vipimo vya utambuzi na uwezo wa kufikiri kuliko wale ambao hawakunyonyeshwa au walinyonyeshwa kwa muda mfupi sana.
Hii ina maana kuwa maamuzi ya wazazi kuhusu unyonyeshaji yanaweza kuwa na athari za muda mrefu katika mafanikio ya kitaaluma ya mtoto.
Ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wazazi wakichagua kutowanyonyesha watoto wao kwa sababu ya kuhofia mabadiliko ya mwili, kupoteza muda wa kazi, au kutaka kurejea haraka katika ratiba zao za kawaida bila kuzingatia mahitaji ya mtoto.
Ingawa ni kweli kwamba maisha ya sasa yana changamoto nyingi, ni muhimu kutambua kwamba miezi ya mwanzo ya mtoto haiwezi kurudiwa, kipindi hiki ni cha kipekee na kina mchango mkubwa katika kumjengea mtoto msingi wa maisha yake yote.
Kuweka mbele mwonekano wa mwili au ratiba binafsi kuliko afya na maendeleo ya mtoto ni uamuzi unaopaswa kutafakariwa kwa kina, watoto hawana sauti ya kuchagua kile kilicho bora kwao; jukumu hilo liko mikononi mwa wazazi.
Zaidi ya lishe, unyonyeshaji huimarisha uhusiano wa karibu kati ya mama na mtoto.
Wakati wa kunyonyesha, mtoto huhisi joto la mwili wa mama, husikia mapigo ya moyo wake na hupata faraja ya kihisia, ukaribu huu huchochea utolewaji wa homoni zinazosaidia mtoto kujisikia salama na kupendwa.
Hisia za usalama katika utoto wa mapema zina mchango mkubwa katika kuunda utu wa mtoto, uwezo wake wa kujiamini na hata namna anavyohusiana na wengine anapokua.
Mtoto anayekua katika mazingira ya upendo na ukaribu huwa na utulivu wa kihisia unaomwezesha kuzingatia masomo darasani badala ya kubeba mizigo ya hofu au kukosa usalama.
Katika mazingira ya shule, watoto waliopata lishe bora katika miaka yao ya awali huonyesha uwezo mzuri wa kuzingatia masomo, kukumbuka wanachofundishwa na kushiriki kikamilifu katika shughuli za darasani.
Ubongo uliopata virutubisho vya kutosha tangu mwanzo huwa na msingi mzuri wa kupokea na kuchakata taarifa mpya, watoto hawa huwa na uwezekano mdogo wa kupata matatizo ya ukuaji wa akili au ucheleweshaji wa maendeleo, hivyo basi, unyonyeshaji si suala linaloishia nyumbani au katika miezi ya kwanza tu, bali lina athari zinazoonekana hata miaka kadhaa baadaye mtoto anapoanza safari yake ya elimu.
Wazazi wanapaswa pia kuelewa kuwa maziwa ya mama ni salama, safi na yanapatikana kwa wakati wote bila gharama za ziada, katika hali ambapo familia zinatumia gharama kubwa kununua maziwa ya kopo, kuna wakati mtoto hukosa kiasi kinachotosha kutokana na uwezo mdogo wa kifedha.
Hali hii inaweza kusababisha utapiamlo au kupunguza kiwango cha lishe kinachohitajika kwa ukuaji wa ubongo, kwa kuchagua kunyonyesha, mama anampa mtoto wake chanzo cha uhakika cha lishe bila kutegemea mambo ya nje yanayoweza kubadilika.
Hii haimaanishi kwamba hakuna changamoto katika unyonyeshaji. Baadhi ya akina mama hukumbana na maumivu, uchovu au changamoto za kiafya hata hivyo, changamoto hizi mara nyingi zinaweza kutatuliwa kwa kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya au vikundi vya msaada kwa akina mama wanaonyonyesha.
Badala ya kukata tamaa mapema, ni vyema kutafuta msaada na kupewa mwongozo sahihi, jamii pia ina wajibu wa kuwaunga mkono akina mama kwa kuunda mazingira rafiki ya unyonyeshaji, kazini na nyumbani, ili kuhakikisha mtoto anapata haki yake ya msingi ya lishe bora.
Ni muhimu kubadili mtazamo unaoona unyonyeshaji kama kikwazo cha maendeleo ya mama, kinyume chake, unyonyeshaji ni uwekezaji katika maendeleo ya kizazi kijacho, mtoto anayekua akiwa na afya bora, akili iliyokua vizuri na uwezo mzuri wa kujifunza atakuwa mtu mzima mwenye mchango chanya katika familia na taifa kwa ujumla.
Wazazi wanapochagua kunyonyesha, wanachangia moja kwa moja katika kujenga jamii yenye watu wenye uwezo wa kufikiri kwa kina, kufanya maamuzi sahihi na kushindana katika dunia yenye ushindani mkubwa.
Kwa wazazi wanaofikiria kuachana na unyonyeshaji kwa sababu ya mitazamo ya kijamii au shinikizo kutoka kwa marafiki, ni wakati wa kutafakari upya, maamuzi yanayohusu afya na maisha ya mtoto hayapaswi kuamuliwa kwa kufuata mitindo au maoni yasiyo na msingi wa kitaalamu.
Kila mzazi anatamani kuona mtoto wake akifaulu darasani, awe na afya njema na awe na maisha yenye mafanikio, njia mojawapo ya kuhakikisha hilo inaanza tangu siku za mwanzo kabisa kwa kumpa mtoto maziwa ya mama.
Kwa kumalizia, unyonyeshaji ni nguzo muhimu katika makuzi ya mtoto kimwili, kiakili na kihisia, ni msingi wa ukuaji wa ubongo unaomwezesha mtoto kufikiri, kuelewa na kufanya vizuri darasani.
Ni kinga dhidi ya magonjwa na ni daraja la kujenga uhusiano wa karibu kati ya mama na motto, wazazi wanapaswa kuweka maslahi ya mtoto mbele na kutambua kwamba miezi ya mwanzo ya maisha yake ni ya thamani isiyopimika.
Kuachana na tabia ya kutowanyonyesha watoto kwa sababu za binafsi ni hatua muhimu katika kuhakikisha watoto wetu wanapata mwanzo bora wa maisha. Kila tone la maziwa ya mama ni mchango katika mustakabali wa mtoto, na kila uamuzi wa kunyonyesha ni uwekezaji katika akili, afya na mafanikio ya kizazi kijacho.



Comments