top of page

White Mercury (2)

Updated: Apr 17


Na Charles Mwebeya.


ILIPOISHIA

Nilipochungulia dirishani na kuona majengo marefu ya ghorofa  huku baadhi ya abiria wakiwa wamesimama na kuanza kutoa mizigo yao, nikagundua kuwa tulikuwa tumefika Arusha, kuangalia saa yangu nikaona kuwa ni saa 10 alasiri.


,,sasa inaendelea,,,

Ile nashuka tu kutoka kwenye basi, nikapokelewa na jamaa wawili ambao tayari walikuwa wamekuja na taxi, wanasema walipigiwa simu (sio hizi za mkononi) na shayo  kwani kabla ya kuondoka nilimuarifu Shayo rangi ya  mavazi nitakayokuwa  nimevaa na  yeye akawataarifu hao jamaa.


Wakati naingia katika Taxi nikiwa nimelishika kwa umakini begi langu nikamuona mmoja wa wale watu walionipokea akimuaga mwenzake, hivyo tukaondoka tukiwa watatu, mimi, dereva pamoja na yule mwenyeji wangu aliyesalia ambaye alijitambulisha kwa jina moja tu,, Urio.


“Mzigo umekuja nao?” akaniuliza, nikamwambia ninao kisha akauliza tena, “hivi vitu huko kwenu Bukoba vinapatikana sana eeeh?” nikamwambia si sana.


Hoteli ya 77 ya Arusha  ilikuwa ni kati ya hoteli tatu  maarufu miaka hiyo, ukiacha Kilimanjaro iliyokuwepo Dar es Salaam  pamoja na Mwanza hoteli  ya Mwanza  hizi zilikuwa ni hoteli zenye hadhi kubwa ambazo zilikuwa zikitumiwa na viongozi pamoja na watalii tu.


Sasa baada ya kutoka stendi tukaenda hadi katika hoteli  ya 77 ambayo wenyeji wangu walinichagulia lakini yote kwa yote walikuwa wamenilipia kabisa!!


Tukaingia katika ukumbi fulani ambapo Urio  alininunulia chakula aina ya  ndizi mshale  pamoja na mtori moja ya chakula pendwa kwa watu wa Arusha kisha  tukapanda wote ghorofani katika hoteli hiyo ambapo alinionyesha  chumba changu.


“Baadaye tutaonana” akasema Urio huku akinionyesha mlango wa  chumba changu. Kwa kuwa nilikuwa nimeshiba nikaamua kupumzika kidogo nikiwasubiri hao wateja ambao niliahidiwa na Urio kuwa ningekutana nao muda mfupi ujao ili tumalize biashara iliyokuwa imenileta.


Lakini kutokana na uzuri wa chumba na mandhari yake nikaona nioge kwanza, lakini nikashtuka na kujiuliza hivi nawezaje kwenda kuoga  ilhali nimeliacha begi langu lenye mzigo likiwa kitandani? Na mazingira ya pale ni kwamba hakuna funguo, ukisharudisha lock kwa ndani basi mlango ndio umeufunga hivyo!!


Nikachukua begi langu lililokuwa na ule mzigo nikaliweka kwenye karo nikaanza kujimwagia maji na nilipomaliza nikaagalia saa, ilikuwa ni mida ya saa kumi na mbili hivi kasoro kisha nikaangusha gari (nikalala)


“Ngrrrrrrrrrrrr”  kengele ya mle chumbani ikaniamsha usingizini, kuangalia saa ilikuwa majira ya saa kumi na mbili na nusu jioni, nikajivuta hadi mlangoni, bahati nzuri pale mlangoni kulikuwa na lensi ambayo unaweza kuangalia na kuona vizuri mtu anayebisha hodi mlangoni pako kwa nje, ile kuangalia namna hii, nikamuona Urio ambaye kwa wakati huo alikuwa kabadili mavazi yake.


Nikamfungulia mlango akaingia lakini hakukaa, akawa amesimama, akaniambia anawafuata wateja na kwamba wako tayari tumalize biashara leo hii: Akaniaga tena akaondoka nikajua mambo  sasa yanakwenda kama tulivyopanga, nikajitupa tena kitandani.

Baada ya kama ya robo saa kengele ikalia tena, nikaenda kuchungulia na kumuona tena Urio akiwa mlangoni.


“Karibu” nikamwambia huku nikifungua mlango lakini kumbe nyuma yake wakatokea   vijana wengine wawili waliokuwa wamevalia mafulana yaliyokatwa mikono (makawoshi)  na kaptula na mmoja alikuwa amebeba Suitcase ambayo akilini nilijua ndio iliyokuwa imebeba mzigo wa hela.


“Mzigo upo?” Urio akaniuliza

“Upo” nikamwambia  huku baadhi yao wakitaka niutoe.


Basi nikatoa begi langu nililokuwa nimeliweka uvunguni na kutoa baadhi ya nguo zangu kisha nikatoa mfuko ambao nilikuwa nimezungushia kichupa hicho na  kuwaonyesha .

“Ndio huu   hapa” nikasema.


Nilipoutoa wakaanza kukiangalia kile kichupa, mmoja akachukua ile chupa akamwaga kidogo kama matone mawili kwenye kiganja chake cha mkono wa kushoto ili kuhakiki  kisha wakateta kidogo huku wakinong’ona  na kunigeukia.


“Mzigo sisi tumeuona na tumeridhika nao na hela tumekuja nayo wewe unasemaje?” mmoja wao akaniuliza .


“Mimi  nauza milioni tisa tu” nikawaambia.


“Huu mzigo ni mali, hiyo milioni tisa ni hela ndogo kaka, sisi tutakupa 13” akaniambia yule alikuyekuwa ameshika ile suitcase.


Moyoni nikashtuka na kujiuliza, hawa ni wachagga na hela wanaipenda, sasa inakuwaje waniongezee bei wakati wao ndiyo wananunua?!!


Basi tukakubaliana wanipe hiyo milioni 13 tena wanipe hapo hapo.

Ile Suitcase ikafunguliwa, yakaonekana mabulungutu ya hela! zilikuwa ni noti za shilingi mia mia nyekundu (wakati huo noti za shilingi elfu kumi hazikuwepo).


Ikaanza kazi ya kuzihesabu, tukakaa nao pale kitandani kwa ajili ya kuzihesabu, tukahesabu, tukahesabu, tukahesabu weeee.. lakini bado hazikuisha. Wenzangu walikuwa wepesi katika zoezi  hilo kuliko mimi ambaye nilionekana ni kama mgeni katika kuhesabu hela kwani vidole vyangu havikuwa na kasi ya kutosha.


Baada kama ya saa tatu hivi zoezi likakamilika! Nikakusanya fedha zangu na kuzitia kwenye begi kisha nikafunga zipu ya begi! tukaagana  na wale jamaa, nikajisemea  moyoni, sasa nimeukata, nimekuwa tajiri!


Walipoondoka nikafunga mlago na kiwewe cha hela kikaanza kunisumbua, nikawaza sijui nikaoge, sijui  nilale  tena ama niondoke katika hoteli hii nirudi Dar es Salaam, wazo jingine likaja hapana au nilale kesho ndio niondoke?


Wakati nawaza hayo, ghafla kengele ya mlangoni ikaita tena “Ngrrrrrrrrrrrrrrrrrrrrrrrrrrrrrrr”

Kuchungulia kwenye lensi, nikamuona tena Urio, nikajua huenda amefuata bakshishi yake si unajua yeye ndiye aliyenitafutia wateja? Kwanini  nisimpe kitu kidogo?


Nikamfungulia, akaingia ndani kisha akageuka na kufungua tena mlango, wakaingia wale jamaa waliokuwemo mle chumbani muda mfupi uliopita lakini akaongezeka mwingine ambaye nilikuwa sijamuona hapo kabla,,

ITAENDELEA TOLEO LIJALO

Comments


bottom of page