top of page

"Safari yangu ughaibuni" kisa cha kweli (1)

Updated: Mar 16


Method Kamuanda Bagoka
Method Kamuanda Bagoka

Na Charles Mwebeya

Naitwa Method Kamuhanda Bagoka, nina umri wa miaka 63. Mzaliwa wa kijiji cha Kanazi wilaya ya Bukoba  ni mtoto wa pili katika familia ya Marehemu Joseph Rwegasha Bagoka.


Nataka nikurudishe katika tukio lililonikuta  miaka zaidi ya arobaini iliyopita nikifanya kazi  katika wizara ya ujenzi kama fundi msaidizi wa magari daraja la pili  jijini Dar es Salaam.


Kelele za magari katikati ya mitaa ya jiji la Dar Es Salama nilikuwa nimekwisha zizoea pamoja na hali ya joto kali tofauti na kule kwetu Kanazi, Bukoba, lakini pia hata mitaa ya jiji hilo nayo haikunipa tabu kwani hata elimu ya kidato cha nne niliipata  katika shule ya sekondari ya Tambaza.


Shule hiyo ilikuwa maarufu hapa nchini na   kwa wakati huo ilijulikana kama shule dume kutokana na utukutu wa  wanafunzi waliosomea hapo ambao wengi wao walikuwa watoto wa matajiri pamoja na viongozi wakubwa na watumishi wa kati serikalini.

Kumbuka wakati huo shule za sekondari za binafsi zilikuwa chache mno na shule pekee zilizokuwa zikiwika ni zile za serikali.


Nilimaliza kidato cha nne mwaka 1984 katika shule  hiyo nami nikijifanya mtoto wa mjini kwani toka najiunga na shule hiyo niliiishi maeneo ya Upanga katika mtaa wa Olimpio ambapo nilikutana na vijana kadha wa kadha, wengi wao wakiwa watoto wa wakubwa na hata wale wa uswahilini.


Nikiwa mitaa ya Upanga nilikuwa nikiishi na mtoto wa shangazi yangu aliyejulikana kama mama Alice aliyekuwa akifanya kazi katika benki ya NBC  ambaye kwa sasa ni marehemu, aliishi na mumewe  aliyekuwa akifanya kazi katika Tume iliyoundwa na Rais kwa ajili ya kurekebisha mashirika ya umma.


Hawa walikuwa ni watu wenye uwezo na waliweza kufahamiana na watu wengi serikalini ndio maana haikuwa vigumu kwangu kupata ajira katika wizara ya ujenzi na wakati huo huo nikiendelea na masomo ya ufundi wa magari katika chuo cha ufundi Chang’ombe.


Kadiri nilivyokuwa nikipiga hatua moja hadi nyingine ya kupata kazi na kuendelea na masomo ya chuo ndivyo ambavyo nilikuwa nikijipatia marafiki wengi kazini, chuoni na mitaani.


Katika mtaa wa Olimpio wengi walinifahamu kutokana na ucheshi niliokuwa nao pamoja na umahiri wangu katika kucheza drafti katika kijiwe chetu mtaani ambapo nyakati za jioni watu wengi wa rika na rangi tofauti walikuwa wakikusanyika na kupiga soga.


Ukitaka kusikia mambo ya siasa unayapata hapo! Mpira hapo! Na hata stori nyingine za watu pia zilipatikana kijiweni hapo. Wengi walikuwa wakija lakini mmoja wa watu waliokuwa wakifika hapo alikuwa kijana mmoja wa mjini aliyeitwa Magai.


Magai ni kijana aliyekuwa akifahamiana na watu wengi wa mjini hasa mabaharia na kijiwe chake kikubwa kilikuwa eneo la Mt Depot karibu na bohari kuu ya serikali maeneo ya Keko.


Kijiwe hicho kilikuwa na shughuli nyingi ikiwemo kubadilisha fedha kwa dola kwa njia zisizo halali lakini pia ni eneo ambalo lilikuwa na baa kadhaa ambazo zilikutanisha  mabaharia wengi waliokuwa wakienda ulaya na meli.


Kutokana na urafiki wetu na Magai nami nikajikuta nikiingia katika biashara ya kubadilisha fedha bandarini, kwa nini nisiifanye wakati wenzangu akina Magai walikuwa wakinufaika? Walikuwa wakipata fedha nyingi kirahisi  wakati wengine tulikuwa tukipata mshahara kiduchu kwa kutoa  jasho na damu nyingi kazini?


Kama mtaji nilikuwa nao hivyo nikalazimika kutoa kiasi Fulani cha fedha  na kuanza kuifanya kazi hiyo nyakati za jioni mara baada ya saa za kazi na wakati mwingine niliwapa mtaji kina Magai wanifanyie biashara hiyo haramu.


Nilifanya yote hayo kwa kuwa mwenyeji wangu mama Alice alikuwa akinipa uhuru wa kutosha, wakati mwingine nilikuwa nikirudi usiku mnene na wakati mwingine nilirudi asubuhi bila ya kuulizwa. Kama kijana nilifurahia sana  hali hiyo!!


Uhuru huo ambao haukuwa na mipaka uliniingiza katika tabia za ulevi, kwani wakati huo nilikuwa nimeongeza marafiki wa karibu, mbali na Magai nilikuwa na rafiki mwingine aliyeitwa Francis ambaye tulimuita Fambo na maeneo yetu ya kujidai yalikuwa kwa Mbowe (Club Billicanas), Holiday Hotel pamoja na Sea View.


Tulikunywa, tulicheza muziki pamoja na marafiki wengine kwa kweli mambo yalikuwa mazuri mno na wakati mwingine tulipitiliza hadi asubuhi tukila raha!


Starehe na mambo mengine yaliyofungamana na urafiki wetu hayakubadilisha uaminifu wangu kazini, nilikwenda kwa wakati na kutekeleza majukumu yangu kikamilifu.


Nikiwa kazini siku moja nilipewa barua iliyonitaka kwenda Lindi kikazi, kubwa ilikuwa ni kwenda kusimamia na kuyafanyia matengenezo magari yaliyokuwa yakisaidia ujenzi wa barabara ya Nangurukuru Kibiti mpaka Lindi .


Katika muda wote wa ujenzi wa barabara hiyo, nilikuwa nikienda Lindi na kukaa katika kipindi kama cha miezi miwili hivi, kisha kurudi tena jijini Dar es Salaam .


Ratiba hii ya ujenzi wa barabara hiyo ilinitenga kwa kiasi Fulani na marafiki zangu akina Magai na John pamoja na watu wengine niliyowazoea katika maeneo ya starehe na hata ile kazi ya kubadilisha fedha nikamuachia Magai na Fransis.


Baada ya zamu yangu ya kwenda Nangurukuru kumalizika nikajiunga tena na wenzangu katika kijiwe chetu cha kubadilisha fedha. Siku moja tukiwa pale Mission to Seamen maeneo ya Kurasini tukakutana na kijana mmoja aliyejulikana kama Chudos.


Huyu nilifahamu sifa zake toka nilipokuwa Bukoba, alikuwa akiishi maeneo ya Kibeta na alikuwa ni  kati ya vijana wa mwanzo kutoka kwetu  kwenda ulaya akiwa kama baharia wa meli. Huyu Chudos alikuwa na marafiki wengi nje ya nchi na alikuwa akitupa stori nyingi kuhusu maisha ya ulaya huku akitutajia marafiki kadhaa aliokuwa nao hivyo kutusisimua sana .


Stori zake za ulaya  zikaamsha ari  kubwa moyoni mwangu  kutaka  kwenda ulaya, kwani alituhadithia mambo mengi mazuri yaliyopo huko, Magai naye akawa akinitaka kuangalia maisha mengine kwani kazi ya kuajiriwa ni kama vile walikuwa wakiibeza .


Kebehi hizo zikahanikizwa na rafiki mwingine wa Magai aliyeitwa Shomari ambaye alikuwa akiishi maeneo ya Ilala Bungoni. Huyu Shomari naye alikuwa baharia na kila siku kauli zao kwangu zikawa Muhaya ,,, zamia ,,usilemae, hapa bongo hapafai.


Baada ya  wahaka wa kutaka kusafiri kwenda  ulaya kunizidi ,nikamueleza rafiki yangu mwingine ambaye tulikuwa tukifanya naye  kazi katika wizara ya ujenzi, juu ya mpango wangu huo.


“Mbilo nataka kuzamia meli niende ng’ambo" nikamueleza nikiwa nimemuinamia katika meza yake.


“Bagoka uko siriasi kweli?” akaniuliza, ikabidi nimueleze jinsi vijana wengine wanavyopata fedha baada ya kuajiriwa kwenye meli mbalimbali zinazoleta mizigo bandarini na nyakati hizo za mwaka 1986 vuguvugu la vijana kuzamia meli lilikuwa kubwa mno kiasi kwamba hata bendi ya vijana Jazz ilitunga wimbo wa Ngapulila uliowahusia vijana kuacha kuzamia meli.


Mbilo akanielewa na  kuvutiwa na mpango wangu huo na kutaka naye ajiunge nami katika mipango ya safari ya kuzamia Meli kwenda ulaya, Magai sasa ndio akawa anaratibu safari yetu hiyo akiitunganisha na watu mbalimbali wanaofanya kazi katika meli kadhaa.


Wakati huo hatukuwa na nyaraka yoyote ya safari, lakini Magai akatutia moyo akatukabidhi kwa mfanyakazi mmoja wa meli anayeitwa Chande ambaye alituhakikishia kufika kule tunakotaka kwenda.


Kituo cha kwanza katika mawazo yetu  kilikuwa Cape town au  Durban nchini Afrika ya Kusini, ambapo kwa maelekezo ya Chande tukifika hapo basi tungepanga kutafuta vibarua  katika meli nyingine na hatimaye kusonga mbele hadi ulaya.


Waswahili wanasema usiku wa deni haukawii, ndipo siku ya siku ilipofika nikiwa bado naishi kwa mama Alice, nikakusanya baadhi ya nguo zangu na vitu muhimu nikaondoka bila ya kumuaga hadi kanisa la St Joseph ambalo linaangaliana na lango kuu  la Bandari ambapo nilimkuta rafiki yangu Mbilo akiwa ameshafika.


Nilikuwa na  wasiwasi sana pamoja na  mawazo mengi kichwani, nikitafakari mustakabali wa safari iliyo mbele yetu kwani hata kazini sikuaga, nilijisemea moyoni endapo safari hiyo itaingia dosari na tukarudishwa nchini, je kazini itakuwaje?


Nikamwambia Chande tusogee langoni mwa bandari ambapo tuliwakuta watu wengi wakiwemo madereva wa taxi ambao tulifahamiana nao.


“Vipi Muhaya, mbona leo una begi unasafiri?” aliniuliza dereva mmoja wa taxi kwa utani, mimi nilibaki nikicheka tu.


Tukamuulizia Chande ambaye alikuwa ndani ya Meli, baada ya kumtuma mmoja wa  mfanyakazi wa meli bandarini hapo, Chande akaja baada ya kama dakika 20 hivi “Mizigo iko wapi?” akauliza akiwa kama mtu aliyekuwa katika shughuli kubwa huko ndani.


Akachukua mizigo yetu na kuingia nayo ndani  ya geti kisha akatuambia tumsubiri kwanza. Baada ya muda akarudi na kisha akatuchukua hadi kwenye Meli.


Akatupeleka  chini ya meli kwenye Dock room ambapo ni sehemu  ya ghala la kuhifadhia mizigo katika meli, hapo  tulikuta mizigo mingi ikiwa tayari kusafirishwa.


Tulikuta kazi ya kushusha mizigo ikiendelea na ilikuwa ni kazi ya kuteremsha ma-rollers makubwa ya karatasi kwa kutumia Crane (mashine za kushusha na kupakia mizigo bandarini).


Kwa kuwa safari yenyewe haikuwa na uhalali wowote ilibidi tujifiche kwenye Crane wakati wa shughuli yote hiyo. Ilitubidi tuchuchumae kwenye Crane ili tusionekane. Bahati nzuri mtu aliyekuwa akiendesha Crane alikuwa akijua mpango wote huo hivyo akatutunzia siri.


Itaendelea..................

Comments


bottom of page