top of page

"White mercury" 1 kisa cha kweli

Updated: Apr 17


Na Charles Mwebeya

Mimi Method Kamuhanda Bagoka, baada ya jaribio la kutaka kwenda ng’ambo kutofanikiwa niliendelea na maisha yangu kama kawaida ingawa dhamira ya kupata mali iliendelea kukolea ndani ya kichwa changu na hali hii ilijengwa na matamanio ya kutaka kuishi vizuri kama familia nyingine nilizokuwa naziona hapo Upanga nilipokuwa nikiishi kwa mama Alice.


Akili yangu ilikuwa ni kutafuta pesa licha ya kwamba nilikuwa na uhakika wa kupata mshahara wa kila mwezi serikalini nilipokuwa nafanya kazi katika idara ya ujenzi. Mshahara wa shilingi 810 ni kweli ulinisaidia katika kukidhi mahitaji muhimu ya maisha yangu lakini nilitaka zaidi ya pesa hizo!


Nikafikiria maisha waliyonayo baadhi ya marafiki zangu akina Magai na wengine wengi ambao walikuwa wakifanya kazi zisizo rasmi lakini walikuwa na uwezo mkubwa wa kifedha  lakini pia baadhi ya watu waliofanikiwa kuzamia meli ambao walikuwa wakija hapa Dar es Salaam na vitu vingi vya thamani.


Nitafanya nini ili nipate mali? Ili nami nitembee kwa mikogo kama wenzangu? Mimi Method Bagoka nitapiga hatua za maisha kweli? Nikaona nisije tena kupata mawazo ya kwenda ng’ambo, ngoja nitulie na kazi yangu.


Siku moja wakati natoka kazini nikakuta kuna mgeni nyumbani. Huyu alikuwa Mwalimu mstaafu Mzee John Kamwangili. Alikuwa akifundisha shule kadhaa huko Bukoba lakini pia alikuwa rafiki mkubwa wa marehemu baba yangu.


Nikakumbuka jinsi alivyokuwa akija nyumbani kwetu  wakati huo nikiwa kijana mdogo, alikuwa ni mtu anayejiheshimu nasi alitupenda sana na wakati mwingine tulikuwa tukienda nyumbani kwake kumsalimia.


“Sasa mwanangu nimekuja kushughulikia masuala yangu ya kiinua mgongo, lakini pamoja na hilo kuna jambo nataka nikueleze” alizungumza taratibu akiwa ananong’ona tukiwa katika chumba cha wageni hapo kwa mama Alice.


Ghafla nikaona akiingiza mkono katika begi lake halafu akatoa kichupa kidogo kilichokuwa kimefungwa kwenye karatasi.


”Unakiona  hiki kichupa ?” akaniuliza na kunitazama kwa makini.

“Ndiyo nakiona baba” Nikamjibu.


Kilikuwa kichupa chenye kitu kama kimiminika hivi ndani yake, wakati nikiendelea kukitafakari kichupa hicho akaniambia “mimi amenipa mdogo wangu ambaye anafanya kazi  huko Ngara,ameniambia nimtafutie wateja nasikia hii kemikali inatumika sana kusafishia madini".


Niliposikia hivyo nikanyanyuka kukishika na kuongeza umakini katika mazungumzo hayo ,akili yangu yote ikaruka!! “kweli baba?” nikamuuliza.


“Ndio tena kitakuwa na thamani kubwa” akasema. Nikakiangalia vizuri kile kichupa na kusoma karatasi iliyokuwa imebandikwa kwa mzunguko, kilikuwa kimeandikwa White Mercury!


“Sasa kwa kuwa wewe umeshakuwa mzoefu hapa Dar es Salaam na unajuana na watu wengi basi nitafutie wateja, kiasi kitakachopatikana tutaona namna gani tunaweza kugawana" akasema mzee Kamwangili huku akinikabidhi kichupa hicho.


Moja kwa moja nikakiweka kwenye sanduku langu na hapo akili yangu ikawa inazunguka nikitafakari ni nani atakayeweza kufanya kazi ya kunitafutia wateja.


Sasa hata akili ya kufanya kazi ikawa kushoto, mawazo yangu yote yakawa katika kile kichupa. Siku moja baada ya kumaliza kunywa chai katika mgahawa mmoja hapo karibu na ofisini, nikakutana na kijana mmoja, mwembama mweupe sana aliyekuwa akifanya kazi katika gereji moja maeneo ya Temeke Stereo. Huyu anaitwa Shayo ni mwenyeji sana wa Arusha ingawa yeye ni mchaga.


Nikamueleza Shayo juu ya kichupa nilichokuwa nacho nikamwambia kinahitaji wateja ili tukiuze. “Kinataka Shi’ngapi  aisee?” Shayo akaniuliza katika lafudhi ya kichagga. Nikamwambia kama shilingi milioni 9 hivi.


“Yaani hicho hata 10 utauza, hiyo White Mercury Arusha inatafutwa sana kusafishia Tanzanite” akasema Shayo huku akichezesha chezesha spana zake.


“Sasa bro we nenda keshokutwa uje, mi ntakuunganisha na jamaa zangu wa Arusha wanaofanya biashara zao kule Mererani" tukaagana kila mmoja akashika njia yake.


Baada ya siku mbili nikafunga tena safari kwenda kumuona Shayo pale Temeke stereo kwenye  gereji yake, wakati nikiwa nasalimiana na watu wengine, mara ghafla Shayo akatokea uvunguni mwa gari akafuata uelekeo wangu  tukasalimiana.


Akaniambia kama niko tayari niupeleke ule mzigo Arusha kwani kuna watu amekwishaongea nao huko na nikiwa tayari nimjulishe ili waweze kunipokea stendi.


Basi baada ya wiki moja nikawa tayari kwa safari ya kwenda Arusha, kama kawaida yangu sikuaga nyumbani wala Kazini. Niliona nikimuaga Mama Alice ataweza kuleta nongwa na safari inaweza hata kuvunjika lakini pia sikutaka ajue nakwenda kufanya kitu gani.


Alfajiri siku iliyofuata nikajiandaa kwenda Arusha  na muda si mrefu nikajikuta tayari nimefika kwani kutoka Upanga hadi ilipokuwa stendi ya mabasi ya Kisutu si mbali hivyo nilitembea kwa muda mfupi kwa miguu na kujikuta tayari nimekwishafika stendi.


Nikakaa kwenye kiti cha pembeni (dirishani)huku nimekumbatia begi langu la safari ambalo nilikuwa nimeweka nguo zagu huku katikati ya begi nikiweka kile kichupa ambacho ndio kilikuwa chanzo cha safari hiyo.


Wakati basi linaondoka hapo stendi ya Kisutu nilikuwa nawaza vitu vingi kichwani. Kikubwa nilichokuwa nakiwaza ni harufu ya utajiri kwani nilihisi tayari nimeshakuwa na mali nyingi kutokana na biashara nitakayokwenda kuifanya huko Arusha.


Nikaliwaza gari moja aina ya Peugeot 504 lililokuwa linauzwa na mmoja wa majirani zetu  katika flat tuliyokuwa tunaishi, nilitamani sana kuwa na gari hilo, nikajisemea kimoyomoyo kuwa limeshakuwa langu!!


Mawazo, ndoto na usingizi mtamu usio na mawaa ukatawala hisia zangu, nikagutuka kutoka usingizini baada ya kusikia kelele za wachuuzi walioingia kwenye basi wakiuza bazoka(jojo) pamoja na sigara.


Nilipochungulia dirishani na kuona majengo marefu ya ghorofa  huku baadhi ya abiria wakiwa wamesimama na kuanza kutoa mizigo yao, nikagundua kuwa tulikuwa tumefika Arusha, kuangalia saa yangu nikaona kuwa ni saa 10 alasiri.

ITAENDELEA…

Comments


bottom of page