top of page

Waambie kabla hawajaaribikiwa

Updated: May 25

Mtoto wa leo ni mzazi wa kesho ambaye atakuwa na familia itakayomuandaa mzazi wa kesho kutwa. Mtoto huyu anahitaji kupata misingi yote ya kimalezi ili afikiapo ukubwa wa kumiliki familia basi akatimize wajibu wake katika kuendeleza mnyororo wa malezi kwa vizazi vijavyo.


Mtoto katika hatua za makuzi anazo haki zake za msingi ikiwemo za kulindwa, kulindwa kwa mtoto ni kuhakikishiwa usalama, kuhakikisha hapatwi na lolote baya linaloweza kuathiri uhai na makuzi yake.


Yapo mambo mengi ambayo mtoto asipo simamiwa na kuwekewa ulinzi anaweza kupoteza mwelekeo wa kimaisha kwa kukatisha ndoto zake, kuwa katili, kupoteza maisha na mambo mengine mengi.


Ulinzi kwa mtoto sio kumuwekea askari wala mgambo, hapana, ulinzi unaanzia katika malezi namna unavyomfunza kubaini na kunusa hatari zote kwa maana ya namna ya kumjengea uwezo wa kujitetea, kutoa taarifa lakini pia kupambana mwenyewe kiakili pale anaponusa hatari.


Msomaji makala hii inabebwa na kichwa “Waambie kabla hawajaaribikiwa” ikilenga kukumbusha wajibu wako wa kuongea na mtoto juu ya mambo ambayo yatamuepusha na hatari ya kuharibikiwa mapema kabla ya kuifikia hatari hiyo.


Kwa siku za hivi karibuni yamekuwa yakishuhudiwa matukio ya ukatili kwa watoto ambayo yamewaachia makovu ya kudumu katika maisha yao kiroho, kimwili na hata kimaisha.


Kinachosikitisha zaidi matukio haya ya ukatili yamekuwa yakitendwa na watu wazima kwa maslahi yao binafsi yenye nia ovu kwa mtoto bila kujali hatima ya mtoto huyo.


Moja ya ukatili wanaofanyiwa watoto ni ubakaji, na kwa mujibu wa jeshi la polisi mkoani Kagera wingi wa matukio ya ukatili yanayopokelewa na jeshi hilo ni ubakaji huku waanga zaidi wakiwa watoto wenye umria wa kuwa shule.


Moja ya madhara ya ukatili huu ni kukatisha masomo kwa mabinti baada ya kupatiwa mimba na hivyo kuaharibu kabisa ndoto zao za kimaisha zilizobebwa na elimu.


Kinachosikitisha zaidi baadhi ya wanaofanya ukatili huo kwa watoto ni watu wa karibu wa mtoto huyo ambao pengine jamii ilitarajia wawe walinzi namba moja wa mtoto huyo, imefikia hatua hata ndugu na wazazi wamehusika katika kuwafanyia ukatili watoto.


Wazazi hawawaamini tena ndugu zao katika suala la kuwaachia watoto, hii ni ishara tosha kuwa jamii imechafuka na watoto wako hatarini zaidi hivyo mbali na sisi kuwalinda wanatakiwa kujua namna bora ya wao kujilinda pale wanapokuwa mbali na wazazi au walezi.


Anasimulia mmoja wa wakazi wa manispaa ya Bukoba ambaye jina lake linahifadhiwa ambaye mwanae alibakwa na mtu wa karibu na familia.


Anasema kuwa kwa kipindi kirefu wamekuwa na mtu huyo katika familia yao kama mfanya usafi na mbeba taka, mbali na kwamba wamekuwa hawaishi naye lakini ni mtu ambaye wamekuwa wakishinda naye wakila na kunywa pamoja.


Anasema kuwa wakati mwingine wamekuwa wakimuachia watoto pale inapotokea yeye na mume wake wametoka wakijua ni mtu salama kwa watoto wao na familia yao.


Anadai kuwa siku moja majira ya asubuhi akiwa ameenda kuhemea mjini alimuachia mtoto wa kike miaka 3, wakati huo mume wake akiwa kazini, lakini cha kushangaza aliporejea hakumkuta mtu nyumbani akaanza kuwatafuta akijua watakuwa kwa majirani zake.


“Baada ya kuuliza kwa majirani bila mafanikio nikaingiwa wasiwasi, nikashikwa na tumbo la uzazi nikaungana na majirani tukimtafuta pamoja mmoja wetu akawa ameenda kwenye moja ya nyumba ambayo haijakamilika (ghofu) na kukuta mtoto amelala akiwa tayari amebakwa”


Anasema aliishiwa na nguvu na ndipo wakamkimbiza hospitali kwa ajili ya huduma ya matibabu na cha kushangaza mtu huyo hakuwahi kuonekana tena baada ya tukio hilo.

 

Msomaji huo ni mfano mmoja wa mzazi ambaye alimuamini mtu wa karibu wa familia yake lakini akamjeruhi kwa kumfanyia ukatili mwanae lakini yapo matukio mengi ya kikatili wanayofanyiwa watoto.


Mifano hii iliyowatokea wenzetu ni lazima ituachie funzo na kuitumia kutafuta suluhu  ya tatizo, hivi unatambua kuwa mtoto mdogo akifundishwa jambo analishika na kulitekeleza kama mtu mzima? Hivi unajua kuwa mtoto huyu anaweza kuziona dalili za kutaka kufanyiwa jambo baya akachukua hatua.


Maana yangu hapa ni kwamba kuna kila sababu ya wazazi kuongea na watoto wetu, tuwaeleze ukweli wa machafuko ya dunia ya sasa kwao, tuwajengee hali ya kutushirikisha jambo lolote wakati wowote na tuwaweke karibu yetu zaidi ili wawe tayari kutushirikisha.


Mbali na hilo pia tuwaeleze madhara ya wao kufanyiwa ukatili huo, tuwape motisha na mwongozo wa namna ya kufikia ndoto zao tukishirikiana na wadau wengine kama walimu kwa kuwaonesha namna ukatili unavyoweza kukwaza ndoto hizo.


Lakini kwako wewe ambaye unamtendea unyama huu mtoto ebu jiulize angekuwa mtoto wako ndiye anayetendewa unyama huu ungejisikiaje, inabidi kubadilika na kujua kuwa hatima ya kesho ya mtoto huyu inakuhitaji hata wewe.


Yawezekana umeshatenda tukio hilo huko nyuma ni vyema ukakaa chini na kutafakari madhara makubwa ya kitendo ulichokifanya kwa mtoto lakini pia muombe mwenyezi Mungu akusamehe na kukufanya mwema na kuwa balozi wa kupinga ukatili huo.


Katika kukabiliana na vitendo hivyo vya ukatili jeshi la polisi mkoani Kagera tayari limeanza kutembelea shule za msingi na sekondari kupitia kampeini yao ya waambie kabla hawajaaribikiwa lakini pia kufanya mikutano kwa jamii kuwahimiza wazazi na walezi kuzungumza na watoto wao juu ya mwenendo wa kimaisha kabla hawajaharibikiwa ili kujilinda.


Kampeini hiyo inaamini iwapo wadau wote wa malezi na makuzi ya mtoto wakisimama kidete na kutimiza wajibu wao katika kumuongoza mtoto na kumwambia ukweli kuhusu hatima yao ya baadae na vikwazo vilivyo mbele yao basi itawasaidia.

Comments


bottom of page