Kijana ni nguvu kazi ya taifa
- Elisa KAIMUKILWA
- Jun 23
- 4 min read
Updated: Jun 27
Na Elisa Kaimukilwa
Kijana na maandalizi ya maisha yajayo.
Kijana ni mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 35, umri huu ni kipindi ambacho kijana anakuwa na nguvu na utayari wa kufanya mambo makubwa ambayo kwa asilimia kubwa ni ndoto yake au msaada katika maisha yake hapa duniani.
Ndugu msomaji leo hii nataka kuongea na kijana wa kiume, katika matoleo yaliyopita tulimuongelea msichana katika makala iliyosema “msichana tunza usichana wako” juu ya namna ya kujitunza na kuifikia ndoto yake, nikionesha fursa zilizo mbele yake iwapo atakuwa na vipaumbele na kujilinda lakini pia vikwazo iwapo hatashindwa kujilinda kwenye kuzifikia ndoto alizonazo.
Baada ya kuongea na binti nikugeukie wewe kijana wa kiume ambaye mbali na kujitafutia unatambua kuwa wakati ujao utakuwa hautafuti kwa ajili yako pekee yako bali utakuwa ukitafuta kwa ajili ya familia utakayokuwa nayo mbeleni maana tunaambiwa kuwa mwanaume ndiye kichwa cha familia.
Imezoeleka kuwa kijana ni nguvu kazi ya familia pamoja na taifa kwa ujumla, na jamii imekuwa ikiamini kuwa kila familia yenye kijana wa kiume ni familia imara ambayo huwezi kuiingilia utakavyo.
Kijana wa kiume katika familia huandaliwa kwa ajili ya kuitunza familia tangu akiwa kwa wazazi/walezi wake katika mambo mbalimbali mfano kupasua kuni, kuchunga mifugo, utafutaji kama kufanya biashara ndogo ndogo lengo likiwa ni kumuandalia msingi imara wa kujitegemea yeye na familia yake hapo baadaye.
Lengo la kumuandaa kijana wa kiume katika mazingira hayo ni ili akiwa na familia yake aweze kuwa bora katika kutimiza wajibu wake kama baba.
Ili hayo yote yanayofanywa na wazazi au walezi kwa kijana huyo yaweze kutimia, ni lazima kijana mwenyewe ajitambue kwa sababu baada ya maisha yake kwa wazazi, maisha yajayo yanamuhusu yeye mwenyewe.
Yampasa kusimama imara kuhakikisha anajiepusha na mambo yote yanayoweza kumuondoa kwenye msingi wa ndoto zake kwa kujiepusha na tabia na mienendo hasi inayoweza kuharibu dira ya maisha yake ya baadaye mfano kutokujiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya, wizi, ubakaji n.k
Mvulana unatakiwa kuanza kujiadhari na tabia za aina hiyo kabla ya kipindi cha barehe chini ya uangalizi wa wazazi/walezi kwani walio wengi hujikuta katika matendo hayo wakati wa kipindi hicho ambacho huwafanya kujiona wana uwezo wa kufanya na kumudu kila kitu kilicho mbele yao.
Ni kipindi ambacho kijana anakuwa na maswali mengi na majibu ya aina mbalimbali mazuri na mengine ya kukatisha tamaa, na kwa kipindi hicho kijana anaweza kutunga mimba na wakati huo kijana ujiona tayari anaweza kuwa kama baba wa familia.
Kijana jiulize swali kwa nini ukubali kuhusishwa na mambo mabaya kama hayo wakati wewe ndiyo nguvu kazi ya jamii na taifa kwa ujumla?
Wazazi/walezi wametumia nguvu nyingi kukulea, kukutunza, kukuelimisha na kuwekeza gharama kubwa kwako wewe kijana, kiasi cha kuuza vitu ambavyo vingewasadia na kukusaidia hata wewe hapo baadaye.
Na wakati mwingine wanachukua mikopo umiza kwa ajili ya kuboresha maisha na ustawi wako hivyo kabla ya vyote inakupasa uwe na huruma na upendo kwa hao waliokulea maana wamekuwa msaada mkubwa kwako kwa kukulea hadi kukufikisha hapo ulipo.
Na haya ni baadhi ya mambo ambayo unatakiwa kujiepusha nayo ili kujiandalia msingi ulio bora katika kuzifikia ndoto zako kimaisha:
Kujiepusha na makundi hasi: Makundi hasi ni makundi ya watu wenye ushawishi wa kufanya maovu ambayo hatima yake ni mbaya kwako kama kijana.
Mfano ukijiunga na kundi la wezi utambue kuwa unaweza kufanya hivo na ikawa chanzo cha kuvurugika kwa ndoto zako, hivi ukienda kuiba ukadhurika kwa kukatwa mguu au kukamatwa na ukafungwa jera miaka kadhaa au kupoteza maisha utakuwa umetimiza lililojema kwako.
Kwa athari hizo na nyingine nyingi unatakiwa kutambua kuwa wizi tu, unaweza kufanya ndoto yako kukwama na hivyo unatakiwa kutafakari juu ya njia mbadala ya kufanya badala ya kuiba na hii iende sambamba na kutodharau kazi iliyo ya halali na inayokubalika katika jamii.
Unaweza kufanya kazi ya kawaida na ikakusaidia kutimiza matakwa yako pasipo kuiba kwa mfano kujihusisha na kilimo ambacho kinaendana na maeneo yako maana wengi wameinuka na kuwa mabilionea kupitia kilimo japo imekuwepo mitazamo hasi juu ya dhana ya kilimo kwa baadhi ya watu.
Sio kilimo tu zipo shughuli nyingi unazoweza kijana na zisikuhitaji gharama kubwa isipokuwa nguvu na utayari wako kuzifanikisha.
Pia kijana ujiadhari na makundi ya matumizi ya dawa za kulevya, hizi ni dawa zozote zisizo rasmi ambazo kitaalam zimekuwa zikisababisha madhara kiakili kwa mfano matumizi ya bangi, mirungi na kuvuta unga n.k.
Kundi hili ni hatari kwani tumeshuhudia vijana wengi waliokuwa na msingi mzuri wa kimaisha na kuaminiwa na jamii lakini baada ya kujiingiza kwenye kundi hili wamejikuta wakikwamia hapo katika maisha yao yote, kijana anayejitambua anatakiwa kutokudhubutu kujaribu kujiunga na kundi hili.
Ubaya wa kundi hili ni kwamba unapovuta bangi inadhoofisha akili na nguvu ya mwili na hivyo kuwafanya wanaokutegemea likiwemo taifa kushindwa kujivunia uwepo wako, hivi hali hii binafsi unaipenda?
Tambua kuwa ukishakuwa zezeta, ukakosa nguvu, na muda mwingine kuwa kichaa unarudisha utegemezi kwa jamii, taifa na familia yako ambayo ilitumia gharama kubwa kukulea tangu ukiwa mimba mpaka unakuwa mtu mzima na malipo unayowaachia ni maumivu nap engine kukulilia kama mtu aliyekufa angali uko hai, kiukweli inauma sana.
Pia kijana jiepushe na mahusiano ya kimapenzi kabla ya wakati sahihi, tunao vijana wengi ambao kwa sasa wanajilaum na mwelekeo wa maisha yao umevurugika na kupotea kabisa kutokana na kujiingiza mwenye mahusiano ya kimapenzi mapema na kujikuta wakipata matokeo hasi badala ya kile walichokitarajia.
Wapo wanaotumikia vifungo gerezani baada ya kuwapa mimba wanafunzi na kuhukumiwa miaka 30 jera, wapo waliopata magonjwa sugu na hatari yasiyo na tiba ikiwemo UKIMWI, wapo wanaoishi maisha ya kukosa uhuru wakikimbia matokeo yaliyotokea baada ya kuingia kwenye mahusiano na kuamua kukimbia kwa ajili ya kujificha n.k.
Kwa nini, jambo kama hilo la kujidhibiti ukubali likusababishie matatizo makubwa kama hayo? Kuna haja gani ya kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi kama hujawa tayari au hujafikia umri wa kuwa na mwenza wa kuishi naye? Haya ni maswali ya msingi ya kujiuliza.
Lakini pia mbali na kuharibu ndoto zako pia kama ni binti (mwanafunzi) umempatia mimba na kufukuzwa shule ujue umeharibu ndoto yake ya kimaisha na uenda hatopata kabisa fursa ya kuendelea kutetea ndoto uliyoiharibu wewe.
Na hata ungetaka muishi wote na kumlea mtoto wenu sheria na taratibu haziruhusu ni lazime wewe uende jera na jera na kumuacha akiangaika na mimba.
Yawezekana haya nilioandika ni machache kati ya mengi unayotakiwa kuyafahamu kuhusu maisha yako kama kijana ili kujikwamua kimaisha lakini itoshe kukwambia kuwa maisha yako ni zaidi ya chochote, yape kipaumbele maisha yako ili utimize takwa la kimungu la kukuleta duniani.
Comments