top of page

Uwe mcha Mungu na mwenye upendo

Updated: Apr 17

wanandoa

Na Charles Mwebeya

Maneno hayo kuntu ya kichwa cha makala hii utayasikia kwa watafuta ndoa wengi, utasikia kauli hiyo ikitamkwa na mtafuta mchumba kuwa “Mwenza ninayemtaka lazima awe na sifa zifuatazo, awe na kazi halali inayomuingizia kipato, awe hajaoa au kuolewa, awe mcha Mungu na mwenye upando (atakayenijali).


Huo ndio msimamo au matakwa ya wa wengi ambao hutafuta wenza, si jambo baya kwao kuelezea sifa ama vigezo ambavyo hutaka wenza wao wawe navyo, La hasha ni jambo zuri na lenye kuonyesha uelekeo ama misingi ya maisha kwa yule anayetafuta mwenza.


Tumeshuhudia ndoa nyingi zikifungwa lakini baadhi ya ndoa hizo huwa hazidumu. Unajiuliza mara mbili mbili ni kwanini hazidumu ilhali muhusika amemchagua mwenza ambaye ana uhakika ana vigezo alivyovihitaji, ni kitu gani ambacho huenda ndivyo sivyo?


Kwa mujibu wa wakala wa usajili wa Vizazi, Vifo, Talaka na ndoa (RITA) ni kwamba katika kipindi cha mwezi Juni 2013 hadi Julai 2014 jumla ya talaka 99 zilisajiliwa katika mkoa wa Dar es Salaam, katika mkoa huo huo katika kipindi cha mwezi Juni 2014 hadi Julai 2015 RITA ikaandikisha talaka 150.


Tazama talaka zilivyoongezeka ghafla! lakini wakati bado unatafakari hilo kuanzia kipindi cha mwezi Januari hadi Disemba mwaka 2020, RITA ikasajili jumla ya talaka 201!


Wachunguzi wa mambo ya ndoa wanasema, kuachana si zao linaloota na kukua kwa siku moja, bali ni migogoro isiyoshughulikiwa kwa muda mrefu ambayo huwaachanisha wanandoa taratibu bila wao kujua.


Kila mtu anafahamu kuwa wakati wa uchumba mapenzi huwa moto moto lakini baada ya kuoana hujitokeza hali ya kuanza kuzoea. Hii inatokana na ukaribu ambao mwanzo haukuwepo au kusitishwa kwa machombezo yaliyokuwa yakiboresha uhusiano.


Kwa mfano wapenzi wengi wanapokuwa kwenye uchumba hufanyiana mambo mengi yakiwemo ya kutumiana zawadi na kadi au kutoka pamoja kwa matembezi, lakini wakioana hujikuta hawafanyiani hayo, jambo ambalo huathiri kwa kiasi kikubwa mapenzi yao.


Uchunguzi unaonyesha kuwa wapenzi walio kwenye uchumba wanapokuwa pamoja hutumia muda mwingi sana kuwasiliana kupitia simu, kutumiana meseji za mahaba tofauti wanapoishi kama mume na mke.


Ukitaka kuthibitisha keti barabarani ukiona mwanaume na mwanamke wamo ndani ya gari hawaishi kucheka na kuzungumza wafuatilie utakuta mwisho wa safari yao wanaagana kila mmoja anakwenda kwake (ina maana si mume na mke hao).


Ni nadra sana kuwakuta wanaume wakiwa pamoja na familia zao wakifurahi, ukitafuta kiini cha matukio hayo mawili tofauti utagundua kuna jambo baina yao ambalo hupunguza upendo na kuleta mazoea na hisia za kutohitajiana sana. Hili halifai na likiwepo ni ishara kuwa mapenzi yanakaribia kunyauka.


Wapenzi wa dunia ya leo wakisema nimekusamehe haina maana wamefuta kosa bali huliweka kando na kulikumbushia wakati mwingine. ‘Hili ni kosa la tatu tarehe fulani ulinifanyia hivi, wiki iliyopita na jana ulinijibu hivi hivi sasa leo siwezi kukuvumilia”


Kauli kama hizi hutoka kwenye vinywa vya watu ambao hawako tayari kusamehe, kosa la mwaka juzi litakumbushwa tena na tena na kuzidi kuchochea ugomvi hata uliokuwa mdogo na kuonekana mkubwa kwa sababu tu umehusishwa na makosa yaliyopita.


Inashauriwa kuwa uhai wa mapenzi au ndoa lazima huambatane na kusameheana kama wanadamu na kusahau makosa. Hili lisipofanyika ni rahisi kuua penzi na kuwafanya watu kuachana. Ni vyema kila mmoja wetu akajichunguza tabia yake na kuacha kukumbusha makosa yaliyopita.


Kuna suala linatambulishwa sana siku hizi na wanaharakati, linaitwa usawa wa kijinsia, jambo hili limekuwa likichangia sana migogoro ya ndoa hasa baada ya kutumiwa vibaya na wahusika. Hakuna ubishi mila za kiafrika zinaongozwa na mfumo dume, kuubadili mfumo huu kwa haraka kumekuwa kukiharibu uhusiano mwingi wa kimapenzi kutokana na ukweli kwamba ni wanaume wachache sana ambo wako tayari kuishi na wanawake wanaovutana nao kimamlaka.


Hivyo ili kunusuru hili lisiwe kikwazo katika mapenzi inampasa kila mwanandoa kuheshimu mipaka yake na kujali zaidi utu na si usawa kama inavyotambulishwa (haya ni mawazo yangu). Watu wanaojali utu katika familia watakuwa tayari kuwapa heshima wanaoishi nao kwa kusikiliza mawazo yao na kutokutumia nguvu kuwakandamiza wengine. Ni vyema mwanamke akachukua nafasi yake kwa mumewe na mume naye akamuheshimu mke kwa utu wake.


Matarajio ya watu wengi wanapoingia katika uhusiano wa kimapenzi huwa ni kupata faraja, ni wachache kati yao hufikiria kukutana na vikwazo vya kimaisha.


Tafiti zinaonyesha kuwa wakati mtu anapotafuta mpenzi huamini toka moyoni kuwa akiwa na waridi wake matatizo ya upweke, kukosa msaada wa hili na lile yatakwisha lakini baadaye anakuja kubaini kuwa aliyokusudia kuyapata hayapati tena na hivyo kujuta

kwa kauli kama hizi.


“Kama ningejua kama mwanaume mwenyewe yuko hivi nisingekubali kuolewa.”


Na hili huenda mbali zaidi pale mwanandoa anapojaribu kukumbuka mahitaji na matamanio aliyojiwekea awali juu ya sifa za mwenza anazozihitaji,kwamba alihitaji kupata mwenza Mcha Mungu, mwenye upendo, anayejali, mvumilivu na kadhalika kumbe amepata mtu tofauti na matarajio yake kutokana na tabia za bandia walizonazo wengi wetu.


Kauli kama hizi mara nyingi hutokea kwa watu ambao hawazungumzii matatizo na vikwazo

wanavyokutana navyo katika mapenzi na kuviondoa. Kama mpenzi wako ana matatizo unasubiri nini kuyatafutia ufumbuzi au kama maisha hayaendi sawa? ukimya wa nini kwa mwenza wako? kaeni chini muambizane kuwa mnaupungufu wa hili na lile, ili kama kutatokea kukosa mahitaji muhimu liwe ni jambo linaloeleweka na wote kuwa linatokana na kipato kushuka.


Uchunguzi unaonyesha kuwa wanaume wengi wanapokukwama kiuchumi hupunguza matumizi kimya kimya jambo ambalo huwafanya wanawake wengi kubaki wakiwa na dhana potofu kuwa huenda wananyimwa na kukosa baadhi ya mahitaji baada ya kuwepo kwa nyumba ndogo.


Nina ushahidi wa kutosha juu ya kuwepo kwa wapenzi hasa wenye kipato kutokuwa wawazi katika mipango yao ya kimaisha na matumizi yao ya pesa. Natambua baada ya kufanya uchunguzi wangu kuwa pesa za baadhi ya wanawake huwa hazina matumizi ya wazi, badala yake wanaume hubanwa kwa kisingizio kuwa wao ndiyo wana wajibu wa kutunza familia.


Hali hii imekuwa ikileta migogoro mingi sana kwenye familia na kushusha upendo kwa vile upande unaohudumia familia haijalishi mume au mke

huwa unajikuta ukikereka kwa kukosa msaada wa upande wa pili na hivyo kuondoa mapenzi ya kweli.


Kama hilo halitoshi vijana wengi wa kiume siku hizi wamejikuta wakiahirisha mapenzi yao kwa wasichana baada ya kukosa ushirikiano wa kimapato na matumizi.


Inashauriwa kwamba kama wapenzi wote wana kazi na wanapokea mishahara ni vyema vipato vyao vyote vikatumika katika kutunza na kuendeleza familia.


Tabia ya mwanamke kumtegemea mwanamume huku yeye akitumia pesa zake kwa manunuzi ya vipodozi na nguo au kufanyia mambo yake kwa siri haijengi badala yake inanyausha mapenzi kama siyo kuyaua kabisa.


Kasoro ninazozizungumzia hapa ni mikanganyiko ya kila siku inayotokea katika familia, hali inakuwa mbaya zaidi pale matarajio yanapokuwa tofauti na uhalisia.Kila mtu hujiwekea mahitaji yake katika tabia za mwenza.


Ndipo hapo utasikia mimi nikitaka kuoa ama kuolewa nahitaji mchumba wangu awe na kazi

ili aweze kunihudumia, awe mcha Mungu na mwenye upendo na kadhalika na kadhalika.

Unaweza kuishi na mwenza wako huyo kwa siku chache tu za furaha katika maisha yenu na kisha baada ya hapo ndio unaanza kumsoma vizuri huyo mwenza wako.


Kikubwa unachoweza kugundua baadae ni kuwa maisha ya mwanzo ya ndoa na tabia za kila mmoja pengine huwa ni za bandia tu baada ya kupata picha halisi ya tabia za mwenza wako.

Comments


bottom of page