Uvivu wako ni fursa kwa wengine
- Elisa KAIMUKILWA
- Mar 1
- 5 min read
Updated: Apr 17

Na Mwinjilisti Elisa Kaimukilwa
Kuna usemi usemao kuwa ukimuelimisha mwanamke umeielimisha jamii, hii ni kweli kabisa, mwanamke ndiye mwalimu mkuu wa kwanza katika jamii ambaye humuongoza na kumfundisha mwanadamu tangu akiwa mtoto, mfano kutambaa, kuongea, kula pamoja na mambo mengine ya msingi ya kumsaidia mtoto katika ukuaji na maisha yake ya baadaye.
Wapo wanawake ambao hawaishii tu katika malezi ya watoto pia kuzitunda familia kwa kutoa mahitaji ya msingi ya familia zao bila kuwa na msaada wa mtu mwingine.
Makala hii inamzungumzia mwanamke ambaye anaishi na mumewe pamoja na watoto au pengine na watu wengine katika familia yake.
Kwa familia zenye wanaume wanaozihudumia, pamoja na huduma za msingi wanazozitoa kuihudumia familia kikamilifu lakini wanaohusika kwa kiasi kikubwa kutekeleza kile kitokanacho na huduma ya baba kwa familiua ni mwanamke. Mfano: Kupika, kufua na kuweka ustawi wa familia katika hali ya usalama.
Yawezekana baba na mama wote ni wafanyakazi au wanasaidiana katika biashara zao, au walikuwa wote shambani, safari na maeneo mengine lakini wakifika nyumbani baba kwa sababu ya kuwa kichwa cha familia anaweza kufika na kulala kwa madai kuwa amechoka lakini kwa mwanamke bila kujali amechoka kiasi gani lazima afike na kufanya shughuli muhimu kwa wakati huo kama kupika, kuhudumia watoto na mengine.
Wakati mwingine hulazimika kwenda umbali kadhaa kwa ajili ya kuhemea, kuchota maji, wakati mwingine katafuta kuni pengine hata kama ana mtoto mdogo amembeba yote hayo ni kwa ajili ya kuihudumia familia yake tena kwa hiari bila kulalamika.
Hii inakuonyesha ni kwa kiasi gani mwanamke ni muhimiri wa familia, binafsi nafurahishwa na hali hii na kinachoshangaza zaidi ni kwamba wanawake hufanya shughuli zote hizo kwa hiyari pasipo kuona anaonewa.
Pamoja na wanawake kutimiza majukumu yao kama nilivyoeleza, bado wapo baadhi yao hujisahau pale wa utekelezaji wa majukumu yao hayo.
baadhi yao wamebarikiwa kuwa na uchumi mzuri katika familia zao, wengine wana kazi nyingi kulingana na ukubwa wa familia zao na hivyo kumuhitaji mdada wa kazi kwa ajili ya usaidizi lakini pia yawezekana wengine hawana kazi nyingi lakini wamehitaji usaidizi wa mtu.
Wasaidizi hawa ni wadada wa kazi (House girl) ambao huchukua nafasi ya kutekeleza baadhi ya majukumu ya mama nyumbani au wengine hutekeleza majukumu yote.
Kufanya majukumu hayo si tatizo lakini tatizo linaanzia pale wadada hao wanapotekeleza majukumu ambayo ni wajibu wa msingi wa mwanmke kwa familia yake au mume wake.
Kwa mtazamo wangu nafikiri dada wa kazi huja nyumbani kwa ajili ya kufanya shughuli kama kufua, usafi wa ndani na nje, kuangalia bustani, kupika, uangalizi wa watoto na anafanya kazi hizi kumsaidia mwanamke kama ametingwa na majukumu mengine.
lakini imeshuhudiwa kwenye familia nyingi uwepo wa dada wa kazi wakati mwingine humfanya mama mwenye nyumba kubweteka na kuona ni fursa ya kutofanya chochote, shuguli zote humwachia dada wa kazi na hata kama mume wake na muda mwingine mume anapohitaji usaidizi wake humuelekeza mdada wa kazi kufanya hivyo.
Utakuta dada wa kazi ndiye anayemuwekea baba maji ya kuoga, kuandaa chakula (mpaka kukileta mezani), kumfulia nguo na kunyoosha huenda hata kujua baba kesho atavaa nguo gani wakati wa kwenda kazini.
Dada wa kazi hujikuta akienda mbali zaidi mpaka kutandika kitanda ilhali mama mwenye familia yupo na pengine wakati huo akiangalia simu au runinga lakini ambazo haziwezi kumfanya asimuhudumie mumewe angalau kuandaa chakula kwa ajili ya familia yake.
Huenda chakula kimeungua au labda kuna mapungufu kadhaa katika mapishi, mama akiulizwa na mume wake utasikia anasema “sijua dada leo amekuwaje alikuwa vizuri labda kama amepitiwa”, ajabu pamoja na misukosuko yote hiyo anayokutana nayo dada wa kazi akikosea kidogo tu hufokewa na hata kupigwa au kukatwa mshahara.
Akina mama waliojisahau sana katika majukumu yao ya kifamilia husababisha mambo mengi katika maisha yao ya ndoa ikiwemo kupoteza ndoa zao ingawa mwanzo waliona kuwa ni jambo la kawida.
Baada ya kuona kila kitu kinafanywa na dada wa kazi , wanaume huanzisha mahusiano polepole aidha na wadogo wa mke wake (shemeji) na kufikia hatua za kuwaoa moja kwa moja na kuwatambulisha kwa ndugu na marafiki, maana anaona kuwa huyu dada au shemeji yake ndiye anayemtunza na kumjali zaidi ya mkewe.
Mume hujiuliza ni kwanini kila huduma ninayotaka kwa mke wangu siipati naipata kwa dada au shemeji yangu tena kwa maelekezo ya mke wangu? Hata kutandika kitanda? Kuandaliwa nguo za kuendea kazini? Mama kwanini usitenge muda wa kumuhudumia mke wake?
Lakini pia si mume tu , mama unatakiwa uwe na muda wa kuwapikia watoto na kucheza nao, kama wamejitambua wanataka kuzungumza nawe, lakini pia kujua familia yako inataka nini na kuona mwenendo mzima wa familia yako, lakini anayepata shida hapa na kushawishika haraka ni baba, watoto hawawezi kumtafuta mama mwingine ,mama utabaki kuwa ni wewe tu hata kama watakuwa wapweke, lazima uwe na muda wa kushugulika na familia zenu.
Lakini ujue nafasi hiyo itakuwa imeishakaliwa na mtu mwingine ambaye huenda naye aliachika kwa staili kama hiyo au la lakini hatapenda kuiachia tena, chuki, ugomvi, aibu na nitaonekanaje mbele za watu si mambo atakayoyatilia maanani, vitamkuta mbele ya safari maana wahenga walisema dua la kuku halimpati mwewe.
Hii inanikumbusha kijana Amosi (si jina halisi) ambaye alikuwa anafanya kazi ya kondakta kwenye magari makubwa (Fuso) alikuwa na rafiki yake ambaye walisoma wote lakini yeye hakuwa na kazi, Amosi akamuhurumia akamwambia dereva weke kuwa ana rafiki yake zamu ijayo aende naye ili apate pesa ya kujikimu , dereva akamkubalia, baada ya kutoka safari Amosi hakuona taarifa yoyote kutoka kwa dereva wake au rafiki yake, Amosi alipouliza kuhusu kurejea kazini dereva akamwambia asubiri atamjulisha kwa simu.
Alisubiri simu hakuiona ,mwezi ulipopita alimuuliza tena dereva ambaye alimjibu “tafuta kazi kwingine huyu ananifaa zaidi” alishangaa kusikia majibu hayo lakini alikuwa hana namna huruma au kutothamini kazi yake kulimponza, swali je! Rafiki yake alifanya zaidi ya Amosi? Dereva alivutiwa na nini kwa kijana huyo mpaka kutotaka kuendelea na Amosi? Siri iko ndani.
Tunajua na kutambua kuwa akina mama ni warembo na ni lazima ajipambe na kupendeza ni jambo zuri, lakini angalia muda unaoutumia kujipodoa wakati mwingine unaweza kutumia kama masaa matano na kuendelea lakini muda wa kumuhudumia mumeo huna, wakati mwingingine ukiulizwa unaelekeza kwa mguu “angalia chini ya meza hapo”.
Mama wewe binafsi umeona na unajua jinsi kuhudumiwa kulivyo kuzuri, kama wewe ni miongoni mwa waathirika wa jambo hili, huenda umekumbwa na janga hili kwa kutendwa na dada wa kazi au mdogo wako pengine na rafiki yako pale ulipompa nafasi ya kumuhudumia mume wako mpaka kufikia hatua ya kuachika unaweza kuwa mwalimu kama hutakuwa mchoyo, lakini pia na wewe unaweza kujifunza kutokana na makosa.
Nikuombe uliye kwenye ndoa , chukua hatua ya haraka sana ili uweze kuitunza, kuisimamia na kuitetea ndoa na familia yako maana ni ya thamani, jua na kutambua wanaoitamani ni wengi, huenda wengine walishindwa wanataka kurekebisha makosa yao ya kwanza maana wanajua na kutambua ni wapi walipokosea.
Umemuandaaje mume wako asubuhi wakati unajiandaa kwenda kazini, unamuacha vipi aondoke bila ya kumuandalia chochote ikiwa ni kifungua kinywa, huenda mume siku hiyo haendi kazini au ataenda kazini mchana, unapofikiria kuwa dada wa kazi, mdogo au rafiki yako anaweza kila kitu hapo nyumbani pamoja na kumuhudumia mume wako ndivyo ambavyo mume wako anavyowapa nafasi kubwa hao wanaomuhudumia.
Kwa kawaida na ilivyo desturi tunajua kuwa mara nyingi mama ndiye huamka mapema na kuandaa mambo yanayo ihusu familia yake ili wakati anatoka awe amepunguza au kukamilisha baadhi ya shuguli za nyumbani, kwa kufanya hivyo inamwezesha kujua mapungufu yaliyo katika familia yake, tofauti na hapo dada wa kazi ndiye ameachiwa angalia na kutekeleza majukumu yote ya familia.
Hapa ndo nimekumbuka msemo usemao mwanamke mjinga hubomoa nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe, waweza jua kuwa ni kubomoa kuta au msingi wa nyumba la hasha! Ni baadhi ya matendo ambayo mwanamke huyafanya na kutowapendeza watu wa familia yake hususani mume lakini baadaye humgharimu katika maisha yake ikiwemo na kuharibu ndoa yake.
Mama tunakumbushana maana najua hakika kuwa nawe unayajua haya labda umejisahau kidogo ila unapaswa kufanya cha ziada kuliko kawaida, naomba nikujulishe kuwa mwanaume mara nyingi huwa kama mtoto, mfanyie yale ambayo yatamfanya awe anakukumbuka mara kwa mara asijisikie kutotoka katika himaya yako wakati mwingine akuone kuwa wewe ndo mwenyewe katika dunia hii hakuna zaidi yako.
“shikilia sana ulicho nacho, uvivu wako ni fursa kwa wengine”
Comentarios