Laana ya kutoa mimba (I)
- Elisa KAIMUKILWA
- 6 days ago
- 4 min read
Updated: 5 days ago
Na Mwinjilist Elisa Kaimukilwa
Kutokana na mfumo wa maisha ya hapa duniani kila kiumbe kilichoumbwa na mwenyezi Mungu amekitengenezea mfumo wa kuzaliana ili kuendelea kuishi na kustawi kwenye dunia hii lakini pia hii ni kutokana na uwepo wa tabia ya kuondoka kwa viumbe hao kupitia kifo.
Kwa binadamu umekuwa ni mfumo unaotegemea mke na mume, wakutanapo ndipo mtu mwingine hupatikana na imekuwa ni baraka kubwa kwa binadamu kupata mtoto kwani licha ya kupata familia pia na heshima huongezeka.
Katika mfumo ulio rasmi wa kufikia mwanadamu kupata mtoto tangu kale imekuwa ni kupitia ndoa rasmi, hapa ni kwa maana ya ndoa ya kidini au kimira na siku zote wanandoa hizo walipopata watoto basi jamii waliwapokea kama baraka na kutambulishwa kwenye dini au mira ili kupata baraka ya maeneo hayo.
Kipindi hicho ndoa ingekuwepo bila wanandoa kupata mtoto au kupotea kwa mimba ilikuwa ikileta huzuni kwa wanandoa hao na hivyo kuanza kuangaikia tatizo hilo mfano watu kutumia dawa za kienyeji, kuombewa na kwenda hospitali nakadhalika hii ikiwa na maana ya kwamba ndoa inahitaji watoto.
Na zamani vijana (wakike kwa wakiume) walijilinda sana chini ya uangalizi wa wazazi wao, usingekuta binti ameingia kwenye mahusiano ya kimapenzi na mtu kabla ya kuolewa akiogopa asije kupata mimba katika mfumo usio rasmi na kuaibisha familia yake na jamii.
Tena baadhi ya makabila yaliona kitendo cha msichana kubeba mimba kabla ya kuolewa ni laana inayotoa taswira ya uasherati.
Wakati mwingine walikuwa wanamtoa katika mazingira hayo na kumpeleka kwa ndugu waliokuwa mbali ili kuepusha kunyoshewa kidole na jamii pamoja na kumlinda lakini naye aliyetenda jambo hilo alikuwa akijionea aibu maana alikuwa ananyooshewa kidole kila sehemu aliyokuwa anapita.
Walichukuliwa kwa mifano mibaya mfano ungesikia mzazi akisema “Angalia usituaibishe kama mtoto wa fulani” maana yake ni kwamba walikiona ni kitendo cha aibu lakini pia walijua hawezi kuolewa kutokana na tukio alilolifanya.
Kama hiyo haitoshi kipindi hicho hata waliotaka kuchumbia walikuwa wanaulizia mengi juu ya maisha ya binti, ikiwemo uvivu, maongezi, uasherati, na mwenendo mzima katika maisha yake, kama alishawahi kujifungu au kubeba mimba na kuitoa.
Kutokana na mfumo wa maisha mambo yamebadilika, utandawazi umeyafanya maisha ya mwanadamu katika dunia hii nzuri waliopatiwa na mwenyezi Mungu kutoka kwenye misingi ya awali iliyochagizwa na dini pamoja na mira na desturi na kuingia katika misingi mingine ambayo imempendeza mwanadamu mwenyewe kuiishi.
Maisha yamebadilika hata katika wakati na namna sahihi ya msichana kupata mimba, tunashuhudia vijana wakianza mahusiano ya kimapenzi wakiwa wadogo, kuanzisha uchumba wenyewe bila kuwahusisha wazazi, wanafamilia au wazee washauri au viongozi wa dini.
Tumeshuhudia matokeo ya tabia hiyo kuwa ni kubeba mimba bila kuolewa na hata kabla ya umri wa kuolewa na matokeo yake yamekuwa ni makubwa ikiwemo kutoa mimba kama njia ya kujiweka salama.
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba msichana ambaye mwenyezi Mungu amemsaidia kubeba mimba hadi miezi 9, baada ya kujifungua mtoto bila huruma humtelekeza maeneo ya wazi, mtu huyu hana tofauti na yule aliyekatili maisha ya kiumbe hicho kabla ya kufikia umri wa kujifungua.
Naamini vijana wanaoshiriki tendo la ndoa na kutoa mimba asilimia kubwa wako chini ya wazazi tangu kukukua kwao wakielimishwa juu ya baya na zuri kwa jamii lakini imefikia wakati baadhi ya wazazi wananyoshewa kidole kwa kushirikiana na mtoto kutoa mimba au kwa kumtengenezea mazingira ya kutoa mimba.
Kitendo cha msichana au mwanamke kutoa mimba muda mwingine imekuwa sio takwa kwa ni laana itokanayo na mauaji ya kikatili yanayofanyika kwa kiumbe kisicho na hatia, laana ni ukosefu wa baraka au msamaha katika jambo hilo, ni tendo linaloweza kukusosesha amani, raha na mafanikio katika maisha yako hasa kwenye suala la ufanisi kwenye maisha yako kwa upande wa kazi ya mikono yako pamoja na uzao wako, Kumb 28:16-20.
Laana hii imekuwa ni kisababishi cha madhara, maumivu, huzuni, maangaiko na mateso, katika maisha kwa ujmla, ni tendo linalotoka kwa mzazi au Mungu. Laana ya utoaji mimba inatokana na ukiukwaji wa amri ya Mungu yaani ‘USIUE’ (Kut. 20:13). Uuaji ni kosa linalokwenda kinyume na matashi ya binadamu ya kuheshimu na kulinda uhai wa binadamu mwenzako.
Hata katika sheria za nchi mbalimbali zinaweka adhabu kali kwa kosa la binadamu kumuua binadamu mwenzake na anayemuua mwenzake katika dhamiri yake anaisikia ile laana ya Mungu ikitamkwa waziwazi ‘UMELAANIWA WEWE’ na baada ya hapo anakabiliwa na adhabu zinazomsabishia mtu mateso, maumivu, majuto au huzuni.
Laana ya utoaji mimba inajitokeza katika maumbo na matendo mabalimbali na kwa watu mbalimbali, iko laana anayoipata mwanamke anayetoa mimba, iko laana inayowapata watoto wanaosalimika katika jaribio la kutoa mimba au waliozaliwa kabla au baada ya mwenzao kuuawa, au watoto waliozaliwa katika nchi.
Vilevile iko laana inayompata daktari au mtu yeyote aliyemuua huyo mtoto kabla hajazaliwa, mtolewaji na waliomshawishi hadi kufikia maamuzi ya kuitoa.
Tunatakiwa kutambua kuwa, tunapotaja na kumnyoshea kidole binti anayetoa mimba lazima tujue kuwa ipo sababu nyuma yao, ebu tuangalie hizi mimba zinapokuja kutolewa zinakujaje;
Wapo baadhi ya wanawake au mabinti wamekuwa wakibeba mimba pasipo hiyari yao na kufikia kufanya ukatili huo kutokana na madhira waliyopitia na kupelekea kupata mimba.
Wapo waliobakwa au kulazimishwa na watu waliowabebesha mimba katika mazingira tofauti mfano wapo waliobakwa kwenye vita, baadhi yao huona mimba kama mzigo badala ya baraka kama wengine wanavyochukulia na kujikuta wamefanya ukatili huo.
Wanaume tunatakiwa kutambua kuwa nasi tunachangia kusababisha haya yanayotokea kwa sababu hakuna mimba pasipo mwanaume kuhusika.
Msomaji hii ni sehemu ya kwanza ya makala ya laana ya kutoa mimba inayolenga kuangazia namna kitendo hicho kilivyo hatari, sio tu katika kuua kiumbe lakini pia maisha ya muuaji.
Katika toleo lijalo tutaangazia laana moja baada ya nyingine na kwa upana zaidi ili msomaji upate kuelewa na kutambua nafasi yake katika kukemea laana hii.
Comments