Usafi wa baba na mama lishe kwa afya za wateja.
- Restuta Damian
- Mar 26
- 5 min read
Updated: Apr 17

Baba na mama lishe ni watu muhimu sana katika jamii zetu, wamekuwa kwa kiasi kikubwa wakizilinda afya za watu wengi ambao hutegemea kupata huduma ya mlo kutoka kwao.
Na Restuta Kasigara
Usafi ni hali ya mtu kuwa katika umaridadi au kitu au kifaa kuwa katika sehemu sahihi ambapo mtu akiwa eneo hilo anaweza kuvutiwa na kuishi kuwa katika hali au sehemu salama isiyoweza kumletea madhara kiafya.
Viwango vya usafi vinatofautiana kwa kutegemea tamaduni na hali ya watu katika maeneo mbalimbali wanayoishi na yaweza kuwa mijini, vijijini na sehemu yoyote yenye mikusanyiko.
Hali hiyo hufanywa na binadamu katika kutunza mazingira na kujiweka safi ili kujiondolea athari za magonjwa yatokanayo na vijidudu vinavyomsababishia mwanadamu madhara ya mwili na kumwondolea unadhifu kwake mwenyewe na mazingira yanayomzunguka.
Tofauti na mwanadamu mwenyewe kuhitajika kuwa msafi kwa maana ya mwili wake, pia mazingira yanayomzunguka yanafaa kuendana na hali hiyo ya usafi bila kusahau kutu chochote anachotumia.
Moja ya eneo muhimu yanayohitaji usafi wa hali ya juu ni sehemu ya kuandalia na kuhudumia chakula hii ni sehemu muhimu katika maisha ya mwanadamu, chakula kikiandaliwa vizuri kitaepusha madhara kwa mwanadamu lakini maandalizi yakiwa kinyume yanaweza kusababisha magonjwa kwa mlaji.
Hapa nazungumzia mazingira ya nyumbani, sehemu za biashara ya chakula kilichopikwa, kwenye sherehe na maeneo mengine ambayo mtu anaweza kupata huduma hiyo.
Kipekee leo hii tunaangazia usafi katika kwa wafanyabiashara wa chakula hasa baba na mama lishe.
Mama na baba lishe ni watu muhimu sana katika jamii zetu, kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakizilinda afya za watu wengi ambao hutegemea kupata huduma ya mlo kutoka kwao.

Mbali na kulinda afya za walaji pia huwasaidia kujipatia kipato cha kuendesha familia zao, wapo ambao wanasomesha watoto, wameoa au kuolewa kupitia kazi hiyo, wamejenga na kwa ujumla kujipatia mahitaji muhimu ya maisha ya kila siku.
Tunasema afya za wateja kwa wafanyabiashara hawa iko mikononi mwao kwa sababu wasipolipa kipaumbele suala la usafi wanaweza kuhatarisha usalama wa afya ya mlaji lakini pia kukimbiwa na wateja wao.
Katika ufuatiliaji wa suala la usafi kwa baadhi ya baba na mama lishe Montessori Tanzania imebaini uwepo wa baadhi yao kutokuzingatia suala la usafi ambalo ni jambo nyeti katika afya ya mwanadamu.
Imebaini wengine hushindwa kumudu usafi kutokana na mazingira waliyomo kutokuwa salama kwa shughuli hiyo, tabia ya uchafu kwa baadhi watoa huduma, uchache wa vyombo vya kutolea huduma kwa wateja na nyingine nyingi.
Eladius Fabian mkazi wa mtaa wa Bakoba anakiri kuwa wapo watoa huduma wachafu na bahati mbaya unakuta wenye tabia hiyo ni wale wenye bei nafuu zinazoendana na gharama za maisha ya mtu wa kawaida.
Hivyo walio wengi hujikuta wakikubaliana na hali hiyo na kwamba ni vigumu kughairi kwa sababu yawezekana ukaeleweka vibaya na kushindwa kupata huduma ya chakula sehemu nyingine na pengine wanaotakiwa kufuatilia hili ni mamlaka husika.
Anasema mama na baba lishe wanatakiwa kujitahidi katika suala la usafi wa maeneo yao ya kuandalia chakula kwani wanalisha watu wengi na kundi la watu hao wakiugua wanaweza kuleta madhara makubwa ya kiafya ikiwemo kusababisha vifo.
Anasema usafi huo uanzie jikoni kinapoandaliwa chakula, vyombo vya kuhifadhia na kulia chakula hadi kumfikia mlaji hii itasaidia kutunza afya zao.
Anasema wapo baadhi ya watoa huduma hawazingatii kabisa kanuni bora za afya katika shughuli zao, hutakuta chakula kinapikwa wazi, vyombo havijasafishwa inavyotakiwa lakini kama hiyo haitoshi sehemu kinapoandaliwa chakula kutokuwa rafiki kutokana na unyeti wa huduma yenyewe.
“Vibanda vingine vya vyakula vimezingirwa na maji machafu yaliyozungukwa na wadudu kama nzi na wakati huo chakula kinaandaliwa maeneo hayo ambayo nzi ni rahisi kukifikia na kukichafua lakini maisha yanaendelea.” anasema Fabian.
Mwajuma Idd anasema wajibu wa kufanya usafi eneo la kazi ni la mhusika mwenyewe ambaye anatumia eneo hilo kwa ajili ya kumlinda mlaji pamoja na yeye menyewe dhidi ya magonjwa kwani utoaji wa huduma ya chakula unategemewa na wengi.
Anasema jambo la kutambua kwa mama na baba lishe ni kwamba wao ndio walioshikilia afya za watumiaji wa chakula chao kwani wanakuta kimeandaliwa tayari kwa ajili ya kuliwa bila kujua mazingira ya awali ya kuandaliwa kwa chakula hicho.
“Mteja wa kwanza kwa mtoa huduma ni mazingira safi hali hii inamsaidia kujitangaza na walaji wengi mbali na kuhitaji huduma bora kitu kingine cha ziada wanachoangalia ni usafi”.
Husina Abdul ni mama lishe anayejihusisha na shughuli hiyo kwa miaka 12 sasa inayomsaidia kuendesha familia yake na kusomesha watoto na mmoja kati yao ni mwalimu.
Anasema mama lishe ili aweze kudumu na kuona manufaa katika shughuli yake ni lazima kulipa kipaumbele suala la usafi kwani asilimia kubwa ya walaji huvutwa na mazingira mbali na utamu wa chakula.
Anasema mama na baba lishe anatakiwa kutambua kuwa mbali na kufanya maandalizi yote ya kuwezesha huduma hiyo ikiwemo kuwa na eneo la kuandalia chakula, vyombo vya kupikia na kupakulia, eneo la wateja kupatia huduma vitu vyote hivyo vinahitaji usafi.
“Njia ya kupata wateja wengi ni usafi na wengine hupenda wafike sehemu ambayo chakula kinaandaliwa ili jionee mazingira ya kinachotoka chakula hicho” anasema Abdul
Anaeleza kuwa anaweza kuja mteja na kuona mazingira hayapo sawa kwa afya yake na kuamua kuondoka lakini huko anakokwenda hawezi kuisema vizuri biashara yako na hivyo kujikuta unawakosa wateja wegi kwa sababu hiyo.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe Wallece Mashanda anasema, mama na baba lishe ni watu muhimu katika jamii kwani wanatoa huduma kwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa kupika chakula kwa muda huo kutokana na sababu mbalimbali ikwemo kubanwa na majukumu.
“Wanatakiwa watambue kwamba wakiwa chanzo cha magonjwa wa wateja wao hawata weza kupata pesa kwani wamemsababishia mlaji ambaye ni mteja kupata ugonjwa kwa kula chakula ambacho hakikuandaliwa kwenye mazingira safi” anasema Mashanda

Anasema ni jumuku la viongozi kuendelea kutoa elimu ya afya na usafi zaidi katika kutilia mkazo upande wa vyakula majumbani hadi kwa mama na baba lishe ambao wanalalamikiwa katika suala la usafi.
“Usafi tunaozungumzia hapa ni kuanzia kweye nguo anazovaa, vitamba anavyofutia vyombo, maji yanayotumika kupikia, mazingira yake ya kupikia eneo la wateja kukaa na kula chakula usafi wa kulinda afya ya mlaji” anafafanua Mashanda.
Afisa afya mkoa wa Dodoma, Nelson Lumberi anasema yapo maeneo ambayo watu tunapenda baba na mama lishe wanatakiwa wajielekeze ambalo kwenye suala la kanuni za afya na katika migahawa tunasema watu wavae mavazi muhimu (aprone).
Anasema lengo la kufanya hivyo ni kwamba endapo am etoka nyumbani na mavazi ya kawaida anatakiwa kuvaa nguo nyingine hii ni kwa sababu nguo hizo zinaweza kuwa zimeguswa na uchafu (bakteria) kutokana na maeneo tofauti aliyopitia.
Hata hivyo anasema ingependeza kuwa, vyakula ambavyo vinaliwa viwe na nyuzi joto 60 kiwango hicho ndicho kinapelekea chakula kuwa salama kwa kutoingiwa na wadudu aina ya bakteria.
Anasema uandaaji wa chakula unavigezo, kupitia sheria ya afya ya umma 2009 amabayo inatoa taratibu za kufuata wanapokuwa wanaandaa chakula na endapo mtu akikiuka sheria hiyo zipo hatua zinazochukualiwa katika maeneo yao ya kutolea huduma ikiwamo kufunga huduma au kutozwa faini kulingana na ukiukaji aliofanya.
“Tunajielekeza zaidi katika utoaji wa elimu ambayo tunaamini mtu akifuata elimu hiyo itasaidia sio tu kwa biashara yake lakini kwa afya ya jamii inayokula chakula kile” anasema Lumbeli.
Anasema muda mwingine uchafuzi wa chakula unaanzia shambani mfano, mtu anavuna mbogamboga alizozipulizia dawa jana au juzi kwa ajili ya kuwauzia walaji au mfugaji anachoma sindano ng’ombe wakati huo huo anakamua maziwa na kuyaingiza sokoni kwa ajili ya kunywewa hii ni hatari kwa afya.
Anasema kufanya hivo ndiyo kunakopelekea magonjwa ya kuharisha kushika kasi zaidi na ukianagalia tatizo lake kubwa ni ulaji wa chakula kisicho salama.
“Ndiyo sababau inayotufanya kusisitiza mara kwa mara wafanyabiashara wa chakula kuwa makini tangu chakula kinapoandaliwa, kuhifadhiwa hadi pale kinapomfikia mlaji” anasema Lumbeli
Kwa mujibu utafiti wa shirika la chakula na kilimo Duniani FAO, unaonyesha kuwa mtu mmoja kati ya 10 hufariki Dunia kila mwaka kwa sababu ya kula chakula kisicho salama na kwamba chakula kisicho salama ni hatari kwa maisha ya binadamu.
FAO inawataja waathiriwa wakubwa walio hatarini kuwa ni wazee, watoto na wajawazito ambao ni wenye kinga pungufu mwilini. Mama na baba lishe wanao wajibu wa kuzingatia kanuni bora za afya katika shughuli zetu za kila siku ili kumuhakikishia mlaji usalama wa afya yake hali itakayochochea ufanisi wa kazi yako na kufanikisha malengo yako ya kujiingizia kipato.
Comentarios