top of page

Matumizi ya kuni yanavyoathiri afya ya macho.

Updated: 2 days ago

Na Waryoba M. Waryoba.

Joyce Joseph (27) ni mkazi wa kanda ya Ziwa katika mkoa wa Mara wilaya ya Bunda katika Kijiji cha Salama A ambaye kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa macho kwa miaka saba ambapo anataja chanzo chake ni moshi unaotokana na matumizi ya kuni wakati wa mapishi.


Joyce ni mama wa watoto wawili anasema amehangaika katika hospitali mbalimbali za ndani na nje ya wilaya ikiwemo hospitali teule ya wilaya ya Bunda kutafuta tiba pasipo mafanikio.


Anasema kuwa macho yake huvimba na kutokwa na machozi kwa wingi kila anapotumia kuni hii ni kwa sababu ya umasikini maana hawezi kumudu gharama za gesi hali inayomfanya anaendelea kutumia nishati licha ya mateso yanayomkabiri.


“Nasumbuliwa na macho kwa zaidi ya miaka saba nilishatembea hospitali mbalimbali kutafuta matibabu lakini bado sijapona na kila ninapotumia kuni macho yangu yanazidi kupata maumivu makali”anasema Joyce.


Joyce ni mojawapo ya wanawake wengi wa vijijini ambao wanaoendelea kuathiriwa na maradhi hayo kutokana na matumizi ya kuni ambao wanashindwa kumudu gharama za nishati mbadala kama gesi na umeme.


Naye Mriam Juma (25) mkazi wa Kurusanga katika wilaya hiyo ya Bunda mkoani Mara anasema amefunga ndoa miaka miwili iliyopita, yeye hutumia gesi kupikia.


Anasema maisha ya kutumia gesi kupikia chakula cha familia yake hayana changamoto za kiafya lakini pia anafanya kazi za upishi akiwa katika hali nzuri na ya usafi tofauti na matumizi ya nishati ya kuni.


Anasema kuwa kabla ya kuolewa alikuwa akitumia kuni na kwamba anatambua fika changamoto zitokanazo na matumizi ya kuni kupika kutokana na moshi na kwamba kwa sasa mambo yake mazuri hana tatizo lolote.


Wataalamu wa afya na mazingira wamekuwa wakisisitiza sana matumizi ya nishati mbadala kwa ajili ya kupikia kwa sasabu yanapunguza asilimia 80 ya uwezekano wa mtumiaji kupata matatizo ya kiafya, uchafuzi wa hewa na uharibifu wa mazingira.


Daktari wa macho katika Hospitali ya rufaa mkoa wa Mara John Owino anakiri kuwa moshi huathiri sana macho na endapo hatua sitahiki zisipochukuliwa mtumiaji anaweza kukabiliwa na uoni hafifu au kuwa na upofu kabisa kutokana na kuathiriwa na moshi.


Dkt Owino anatoa wito kwa mamlaka zote zinazohusika kushirikiana na wadau wengine wa afya kuongeza bidii zaidi katika kutoa elimu na kudhibiti nishati ya kuni nyumbani na hata kwenye taasisi mbalimbali zikiwemo za kielimu ili kuepuka athari zitokanazo na matumizi ya moshi.


“Macho ni kiungo muhimu sana kwa mwili wa binadanu ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha afya ya macho yake yanakuwa salama kila siku ili kuepuka athari” anasema Owino.


Kwa upande wake Afisa Misitu wa mkoa huo Amina Juma anasema kuwa uharibifu wa misitu katika mkoa huo umepungua kwani wananchi wamekuwa na uelewa mzuri juu ya utunzaji mazingira ikiwemo kutumia nishati mbadala badala ya kuni katika mapishi.


“Sina takwimu sahihi za matumizi ya gesi kwa wananchi lakini hamasa kwa jamii ni kubwa, watu wengi wanaendelea kutumia gesi kutokana na udhibiti wa matumizi ya kuni na mkaa maeneo mbalimbali ya mkoa huu” anasema Amina.


Anabainisha kwamba kati ya kaya tano, tatu zinatumia nishati ya gesi hasa mjini hivyo mwamko umekuwa ukiongezeka kila siku tofauti na vijijini ambako bado kuna changamoto ya uelewa.


Amina anataja tatizo kubwa linalochangia kushuka kwa matumizi ya gesi vijijini katika mkoa huo ni kuwa ni ulewa mdogo wa matumizi ya nishati hiyo na kwamba ofisi yake kwa kushirikiana na wadau wengine wa mazingira wanaendelea kutoa elimu hiyo kwa jamii.


Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) matumizi ya gesi ya kupikia ni asilimia 10 ya wakazi wa maeneo ya mjini lakini kwa vijijini bado kuna changamoto ya matumizi na nishati hiyo.


Anasema ili kuepuka changamoto hii na ugonjwa wa macho na uharibifu wa mazingira jamii inatakiwa kuelimishwa na kuhamasishwa kutumia nishati mbadala kupikia vyakula kuepuka matumizi ya kuni kwani nishati hiyo inaathiri afya ya macho kwa ujumla.


Kutokanna na hili Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira nchini (JET) kupitia Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili chini ya usimamizi wa Mkurugenzi wa Chama hicho John Chikomo kimekuwa kikihimiza jamii kwa ujumla kutunza mazingira na kuepuka ukataji miti ovyo kwa matumizi ya kuni.


Serikali kupitia taasisi zenye dhamana ya kusimamia mazingira tayari zimethibitisha kuwa matumizi ya kuni kwa ajili ya kupikia yana madhara makubwa kiafya na kimazingira.


Ndio maana kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameshuhudiwa wakihamasisha na kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi ya gesi na umeme kwa sababu ni salama na madhara yake ni madogo tofauti na kuni hivyo wananchi wanatakiwa kuepuka sana matumizi ya kuni maeneo mbalimbali nchini.


Inawezekana ugumu wa maisha ikawa chanzo cha baadhi ya watu kuendelea kutumia kuni hata kwa kujua kuwa kuna madhara katika matumizi yake lakini ili kuepuka madhara ya kiafya yaliyobainishwa hapo juu ni vyema kila mtu akajitahidi kutafuta namna ya kuwa na nishati mbadala.


Wadau na serikali inatakiwa kuja na mkakati utakaowawezesha wananchi kuweza kutumia nishati iliyo rafiki kwa afya ya wananchi hasa ya gesi kwa kuhakikisha bei za mitungi na nishati yenyewe inakuwa rafiki.


Iwapo kila mtu akiwajibika kwa nafasi yake matatizo ya kiafya yatokanayo na matumizi ya kuni yatadhibitiwa.

Comments


bottom of page