top of page

Upwekee chanzo cha wazee kudhoofika

Updated: Apr 5


Baadhi ya wazee wa kikundi cha Shina Bikolwa engozi wakiwa katika kikao chao cha mwezi


Ilikuwa mwaka 2019 ndipo umoja wa wazee wa kata Bugandika halmashauri ya Missenyi mkoani Kagera wa “SHINA BIKORWA ENGOZI” ulipoanzishwa, mhasisi wake akiwa ni marehemu Bi. Yuliana Kokwitika, mama mzazi wa Bi. Jesca Kamara Mushara ambaye ni mfadhili wa wazee hao.


Kabla ya kifo chake Bi.Yuliana inasemekana alipambana kuwalea watoto wake mwenyewe pasipo msaada wa mtu mwingine lakini pia kabla ya kufariki Dunia alimsisitiza mwanae Bi.Jesca kulinda haki za watoto wa kike na kuwekeza nyumbani na hii ni kutokana na msingi mzuri aliomuachia akijua anaweza kuishi nje ya Kagera lakini asipasahau nyumbani.


Kabla ya kufariki kwake aliumwa kwa takribani miezi 10 bila kutoka ndani na kwa mujibu wa mwanae Jesca alibaini kuwa waliokuwa wakimfariji mama yake asilimia kubwa ni wazee na hii ni kutoka na na uhusiano uliokuwepo kati ya mama yake na wazee hao.


Kwa sababu alimuhusia kukumbuka nyumbani, Bi. Jesca ambaye makazi yake ya sasa ni nchini Marekani aliona ni muhimu kuanzisha taasisi inayofahamika kwa jina la SHINA INC,. yenye lengo la kutoa misaada kwa ajili ya ustawi wa jamii ya wahitaji.


Taasisi hiyo imebeba ujumbe wa kwamba “Shina kawaida hubeba mti na matawi” kwa picha nyingine ni kwamba mtu mmoja anaweza kuungana na wengine kusambaza upendo kwa watu wenye uhitaji na kuleta mabadiliko chanya kama ambavyo wazee walifanya kwa mama yake kabla ya kufariki Dunia.


Bi, Jesca Kamala kwa kushirikiana na mume wake Amos Mushara wakaona sehemu moja wapo ya kuelekeza upendo na kurudisha asante nyumbani ni kuwaunganisha na kuwasaidia wazee wa kata ya Bugandika, alianza na wazee wa miaka 70 na kuendeleea ambao idadi yao ni 138 wamewaunganisha pamoja na kuwawekea utaratibu wa kukutana kila mwezi na kujadili mambo yao.


Pamoja na mambo hayo SHINA INC,. iliweka wataalam wa mazoezi ya viungo ambao wajibu wao ni kuhakikisha kila wakutanapo wa zee hao, wanafanyishwa mazeoezi yanayolenga kuimarisha afya zao ili kuwaepusha na magonjwa mbalimbali yawapatao yakiwemo yasiyoambukizwa.


Pia anao wataalam wa lishe ambao uhakikisha siku wanazokutana wazee hao wanaandaliwa vyakula vya lishe lakini pia kupewa elimu ya vyakula wana vyostahili kutumia mara kwa mara ili viwawezeshe kuwa na afya bora.


Audax John miaka 74 ni mwenyekiti wa umoja wa wazee wa kata Bugandika wa SHINA Bikolwa engonzi anasema kikundi hicho kinao uongozi katika nafasi za mwenyekiti, katibu, mhekazina na wajumbe ambao wana jukumu la kuongoza umoja wao.


Anasema umoja huu unawahusisha wazee wa vijiji vyote vya Bugandika ambavyo ni Buturage, Katendaguro, Rukurungo, Bwemera, Bwoki, Kijumo na Igurugati na kwamba vigezo vya kuwa mwanachama ni pamoja na kuwa mzee mzawa wa kata Bugandika, awe na umri wa kuanzia miaka 70 na mwenye kujiheshimu.


Anasema kitendo cha SHINA INC,. kufikiria kuanzisha umoja huo ni maono makubwa kwani uzee ni tunu, si kila mtu anapata bahati ya kuufikia katika maisha ya hapa Duniani kwa hiyo inapotokea mtu akafikia umri huo anatakiwa kuuheshimu na kuutunza.


Anasema imezoeleka mtu akiwa mzee anatengwa na thamani yake hushuka, utakuta hashirikishwi kwenye baadhi ya mambo ya kijamii, anafungiwa nyumbani lakini pia kukosa wa kuchangamana nao na hivyo kupelekea upweke hali inayoweza kusababisha magonjwa na kudhoofika.


“Kipindi cha nyuma wazee wa kata hii walikuwa wakikutwa na msongo wa mawazo kutokana na kuwa wapweke, walikuwa wakikutwa ndani wamelala muda wote lakini pia wakisumbuliwa na magonjwa” alisema Audax.


Anasema awali wakati umoja huo unaanzishwa wazee walikuwa wanyonge na wadhaifu lakini baada ya kufanyishwa mazoezi na huduma nyinginezo zinazowafanya kuchangamsha miili na akili zao wamekuwa wachangamfu na kuimarika kiafya.


“Hapa utawakuta wazee wa mia ka 90 hadi 95 wakicheza ngoma na kutembea jambo ambalo huko nyuma lilikuwa sio rahisi lakini hii ni kutokana na matunda ya maono ya Bi. Jesca ya kutuweka pamoja na kushiriki mambo ambavyo tulikuwa hatuwezi kuyafanya nyumbani” anasema Audax.


Anasema pamoja na masuala ya afya lakini kupitia umoja huo, wazee hujaliana katika shida na raha kwa mfano mtu anapopata msiba, kuugua au kuuguza pamoja na changamoto nyingine wote kwa pamoja hufika kumjulia hali.


Kwa upande wa raha anadai kuwa, hivi karibuni mmoja wa wazee hao amefunga ndoa na wote walishiriki harusi hiyo kwa kumchangia na kufika kumuunga mkono na kwamba pale wanapokutana hufurahi pamoja lakini pia hufarijika kutokana na mshikamano uliopo.


“Tunapokwenda kumfariji au kusheherekea na mwenzetu kwa pamoja tunamuwezesha chochote kinachokuwa kimepatikana ili ajisikie kuwa na amani ya moyo lakini aweze kutuona” anasema audax.


Anasema wanao mfuko ambao kila mwanachama huchangia kiasi cha shilingi 1,000 kila mwezi lengo ni mwisho wa siku wafanikishe bima ya afya kwa kila mzee na kwamba kwa kutambua kuwa sio rahisi mzee kupata kipato hicho kutokana na walio wengi kutokuwa na kipato cha uhakika; Katika mkutano wa kila mwezi wazee wanaruhusiwa kuja na vitu mbalimbali ambavyo hupigwa mnada na kuweza kupata fedha ya mchango na hivyo kufikia malengo.


Anamshukuru Bi, Jesca Kamara kwa wazo la kuwaunganisha na kuwasaidia katika kila jambo wanalokuwa na uhitaji nalo na kwamba amerejesha heshima ya wazee kwani hata jamii inawahesshimu na kuwathamini.


Bi Agness Martin mzee wa kijiji cha Igurugati, mmoja wa wazee wa SHINA Bikolewa engonzi anasema amekuwa katika umoja huo tangu mwaka 2019 na kwamba mara ya kwanza hakuamini kama wazee wangekaa pamoja na kufanya mambo yao kiasi kile.


Anasema kuwa kabla ya umoja huo wazee walikuwepo wenyewe kwenye makazi yao bila kufahamiana au kuwa na utamaduni wa kutemebeleana kujadili changamoto zao jambo liliwafanya kubaki wakiumia na changamoto zinazowakabili.


“SHINA INC,. imetuinua, imetuunganisha upya na imetukumbusha ujana wetu, tunachangamka tunatamani tukutane kila siku, tunaona kama mwisho wa mwezi unachelewa kufika hadi tunaulizana kwa kuwapigia simu viongozi kujua siku ya udhurio ili tusiikose” alisema Agness.


Anasema SHINA INC,. imewawekea usafiri unaowachukua kwenye makazi yao na kuwarudisha baada ya kikao cha kila mwezi na kwamba hiyo ndio imewapa motisha zaidi kwani kufanya hivyo kunawasaidia wazee wasiowe sababu ya kutokufika kwenye mkutano huo.


Anasema wanapokutana hueleza matatizo yao na husaidia kuyatatua kimawazo na pale yanapohitaji msaada zaidi wa kiuongozi, mkurugenzi wa shirika la SHINA Tanzania Bw. Johanes Chamushara huwasaidia kuwakutanisha na wahusika kwa kuwaalika kwenye mikutano yao na kutatua changamoto ziliopo au kuwapa elimu.


Mzee Salvatory Ishenkumba miaka 87 mmoja wa wana SHINA Bikolwa engozi anasema kuwa maisha ya furaha kwake yameongezeka zaidi baada ya kuwa sehemu ya umoja wao, akidai umewasaidia kuwaunganisha na marafiki ambao wamepotezana nao miaka mingi.


Anasema anatamani furaha waliyonayo wazee wa Bugandika, wawe nayo wazee wote na kwamba jambo alilolifanya Bi. Jesca Kamara na mume wake liigwe na wadau wengine kwa kuwaweka pamoja wazee na kuwatengenezea mazingira ya kukutana mara kwa mara na kushiriki shughuli mbalimbali badala ya kubaki nyumbani.


“Natamani wazee wote wawe kama sisi maana hapa tunakutana na watu tuliopotezana miaka 30 au 40 iliyopita kabla ya kustaafu kazi au masomo ni jambo la kuigwa na wazee wa kata nyingine” anasema Salvatory.


Bw. Salvatory anamshukuru Jesca na mume wake kwa ushirikiano wanaoutoa kwao akiomba wawasaidie kufanikisha suala la upatikanaji wa bima za afya ambazo zitawahakikishia huduma ya matibabu pale wa napopatwa na magonjwa mbalimbali na kuondokana na changamoto ya kuombwa hela ya gharama za matibabu pale wanaopokwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.


Anaongeza kuwa ile dhana ya wazee kufungiwa ndani ya nyumba imeisha kabisa na imewarudisha katika ujana na kuwaomba wazee wenzake kushikamana pamoja kuhakikisha wanafikia lengo la mfadhili wao la wazee kuishi vizuri na kufahamiana.


Kwa upande wake mkurugenzi wa shirika la SHINA Tanzania Johanes Chamushara anamshukuru mwenyezi Mungu kuona malengo ya Bi. Jesca Kamara na mume wake ya kuwaunganisha pamoja wazee na kufahamiana yanafanikiwa pasipo ugumu wowote.


Anasema walikaa na wazee wenyewe na kupanga ratiba rafiki ya kukutana kila mwezi ambayo humkuta kila mzee yupo huru na kupata nafasi ya kushiriki na kwamba kwa hilo wamefanikiwa maana tarehe ya kukutana asilimia kubwa wamekuwa wakifika.


Anasema wazee wamekuwa wakipata fursa ya kupeana uzoefu wa kimaisha na usuruhishi wa changamoto zao wenyewe kwani ndani yao wapo wastaafu mbalimbali yaani kwa maana nyingine wamo wataalam wastaafu ambao kwa uzoefu wao wanaelimishana na kushauriana.


Anasema SHINA INC,. imeweka utaratibu wa kugharamia usafiri wa kutoka makwao, huduma ya lishe kwa siku hiyo, mazoezi na michezo mbalimbali.


Anasema Bi.Jesca ameanzisha utaratibu wa kuwaongezea kiasi cha fedha kila mwaka katika mfuko wao na kiasi hicho kinategemeana na kiasi ambacho wazee watakuwa wamefikisha kwenye mfuko wao ndicho anachokiongeza.


Kwa mfano mwaka jana walifikisha kiasi cha shilingi milioni 1 na laki 5 na wafadhili hao wamewaongezea kiasi hicho hicho kwenye mfuko wao. ”Kila mwaka Jesca ameamua kuwa anawawekea kiasi kile ambacho wazee hao watakuwa wamefikisha kwenye mfuko wao hii ni motisha kubwa sana kwa wazee inayowaonesha kufikia ndoto zao za kupata bima ya afya” alisema Johanes


Anasema wazee wamejiwekea malengo yafuatayo, kupata bima ya afya, kuanzisha duka la jumla na rejareja litakalosaidia kutunsha mfuko pamoja na kutengeza filamu za mambo ya asili na historia (mira na desturi).


Anasema kama SHINA INC,. wanajipongeza kwa hatua iliyofikiwa kwa umoja huo lakini watajipongeza zaidi pindi wakitimiza lengo kuu la umoja huo la kila mzee wa umoja huo kuwa na bima ya afya.


“Nashauri wadau katika kata, wilaya na Mikoa waanzishe umoja huu kwa wazee, wawasaidie kuondokana na upweke sambamba na masononeko katika mioyo yao na kuwaanzishia furaha mpya itakayowafanya kutimiza umri mkubwa zaidi lakini pia kuishi maisha ya furaha muda wote” anasema Johanes.


Kauli mbiu ya umoja wa wazee wa SHINA Bikolwa Engonzi ni “Wazee tulikuwepo, tupo na wataendelea kuwepo na uzee haukwepeki”


Ni dhairi jambo lililofanywa na SHINA INC,. chini ya Bi.Jesca Kamara Mushara liwe somo kwa watanzania wengine wenye uwezo wa kutatua changamoto za wazee ikiwemo zile zinazowanyima furaha.

Comments


bottom of page