top of page

Ugumu ni msingi wa fursa

Updated: Apr 17


Na Denis Hilarius


Teknolojia ni matumizi ya maarifa, zana, taratibu, na mchakato wa kuunda, kurekebisha, na kutumia vitu vyenye faida kwa binadamu, kwa ujumla ni mfumo wa kuunda, kukuza, na kutumia ujuzi, ubunifu, na mbinu ili kutatua matatizo na kuboresha maisha ya watu.


Teknolojia huonekana katika maeneo mengi ya maisha yetu, kuanzia vitu vya kila siku kama simu na kompyuta hadi maendeleo ya kisayansi kama utafiti wa matibabu ya kisasa na shughuli za viwanda na kutumika katika Nyanja tofauti tofauti kama kilimo, habari na mawasiliano, ujenzi, muziki, biashara, usafiri, na mengi zaidi, pia inaweza kusaidia kuongeza usalama na ufanisi katika shughuli za binadamu, hivyo kuleta mabadiliko makubwa na maendeleo ya kijamii.


UBUNIFU

Ubunifu ni neno linalotumika kuelezea uwezo wa kujenga, kutengeneza, au kuunda kitu kwa njia yenye ubora na uvumbuzi, ni uwezo wa kutumia akili na ujuzi wa kipekee ili kuunda kitu kipya au kuboresha kitu kilichopo, kwenye sekta mbalimbali kama vile sanaa, biashara na kadhalika, ubunifu unahusisha uwezo wa kufikiri nje ya sanduku, kuunganisha mawazo na kuzaa wazo jipya pamoja na kuunda suluhisho bora.

 

Katika maana pana zaidi, ubunifu unahusisha mchakato wa kuunda na kuendeleza wazo jipya ambalo linaweza kutumika kama suluhisho la tatizo, kuongeza ufanisi, kukidhi mahitaji au kuleta mabadiliko chanya katika jamii.


Ubunifu unaweza kuonekana katika maeneo mengi mfano katika bidhaa, huduma, biashara na katika sanaa na utamaduni, na hii inahusisha uwezo wa kuchunguza, kuchambua na kutumia njia mpya za kufikiri ili kuleta mabadiliko yenye tija na athari nzuri katika maisha ya watu.


UHUSIANO BAINA YA TEKNOLOJIA NA UBUNIFU

Teknolojia na ubunifu ni mambo mawili yanayohusiana sana katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwani teknolojia huwezesha ubunifu kwa kutoa rasilimali na zana ambazo hufanya iwezekane kutafsiri mawazo ya ubunifu katika vitendo, pia inaweza kuchochea ubunifu kwa kutoa changamoto mpya ambazo zinahitaji kutatuliwa kwa njia mpya.

 

Kwa upande mwingine, ubunifu unasaidia kuboresha teknolojia kwa kuzalisha mawazo na suluhisho jipya, pia huwezesha uvumbuzi wa teknolojia mpya ambazo husaidia kuboresha maisha ya watu, kufanya shughuli za kila siku kuwa rahisi, au kutatua matatizo ya kijamii na kiuchumi kwa mfano, ubunifu unaweza kuongoza kwenye maendeleo ya roboti za matibabu, nishati safi, au teknolojia ya habari na mawasiliano, hivyo, teknolojia na ubunifu huchangia kwa pamoja katika kuendeleza jamii na kuleta mabadiliko.

 

Katika kuangazia ubunifu na teknolojia kipengele cha Nuru ya kijana kinakukutanisha na kijana mbunifu wa mashine ya kutengeneza bisi (popcorn) anayejulikana kwa jina la Alex Thobias mwenye umri wa miaka 25 mkazi wa manispaa ya Bukoba mkoani Kagera ambaye asili yake ni mkoani Tabora.


Kijana huyu mwenye elimu ya darasa la saba aliingia mkoani Kagera mnamo mwaka 2022 ikiwa ni harakati za hapa na pale za kutafuta maisha, hata hivyo kabla ya kwenda mkoani Kagera, aliwahi kuishi katika mikoa ya Arusha na Dodoma kutafuta maisha.


WAZO LA UBUNIFU

Uduni wa familia yake ni chanzo cha yeye kuhangaika kutafuta namna atakavyoishi ikizingatiwa kuwa yeye ni kijana wa kiume ambaye baadaye atahitaji kuwa na familia yake lakini pia wakati huo huo akitegemewa na wazazi wake.


Anasema alilazimika kufanya kila kazi iliyokuja mbele yake maana aliamini kuwa hatakiwi kuacha shilingi nyuma hali hiyo ilimfanya kujichanganya maeneo mbalimbali ili kujifunza na kuona namna atakavyofanikiwa kupambana na maisha.

 

Akiwa mkoani Arusha, kijana huyu mwenye uthubutu wa kufanya kazi alijishughulisha na shughuli ya uuzaji maji ya kunywa kwenye mifuko ambayo kwa mikoa mingine kama Dar Es Salaam huitwa maji ya kandoro katika stendi ya magari madogo maarufu kama daladala wilayani Meru jijini humo, pia alijishughulisha na kazi ya ukondakita wakati wa majira ya masika kama mbadala wa kazi ya uuzaji maji.


“Siku moja, wakati ninauza maji niliona mashine maalum ya kutengeneza bisi dukani, niliitazama ile mashine na kuvutiwa na utendaji kazi wake hali ambayo ilinisukuma niombe kazi ya kutengeza popcorn kwa yule mmiliki wa mashine hiyo”


“Nilifanya kazi hiyo kwa mkataba maalum wa mwaka mmoja ambapo tulikubaliana kuwa endapo nitafanya kazi hiyo kwa ufanisi basi ile masahine itakuwa mali yangu, nilifanya kazi hiyo kwa bidii hadi mwisho wa mkataba wangu hivyo nikafanikiwa kuondoka na mshine hiyo” anasema Thobias


Thobias anaeleza kuwa, alipoichukua mashine hiyo aliichunguza kwa umakini na kupata wazo la kuunda mashine nyingine ambazo zilikuwa na muundo wa mashine ya dukani ila utofauti wake ulikuwa ni katika baadhi ya vifaa vya kiubunifu, ambapo aliweza kuunganisha vifaa mbalimbali vikiwemo vioo, mabati meupe, injini (motor), gesi, nishati ya jua pamoja na magurudumu ya baiskeli ambapo nilianza na kiasi cha shilingi laki tano kama mtaji wa kazi hiyo.


FAIDA

Thobias anasema kuwa mashine hizo zimeweza kumtengenezea faida kubwa ikiwemo kumuwezesha kuendeleza maisha yake binafsi pamoja na wategemezi wake, pia ameweza kununua kiwanja kutokana na mshine hizo kuwa na uhitaji mkubwa kwa watu huku akibainisha kuwa mchakato wa kutengeneza mashine moja hadi kukamilika una gharimu shilingi milioni moja na laki tano.


AJIRA

Kama zilivyo fursa nyinginezo, kijana huyu ameweza kutengeneza,fursa ya ajira kwa vijana wengine ambao wamekuwa wakimsaidia kufanya kazi ya kutengeneza na kuuza bisi.


“Hadi hivi sasa nimeifikia mikoa minne Arusha, Dodoma, Mwanza pamoja na Kagera na kwenye mikoa mitatu ninao vijana wasimamizi wa shughuli hiyo lakini pia wapo vijana wengine ambao wanafanya kazi ya uuzaji wa bisi, vijana hao wamepata ajira kutokana na ubunifu huu wa kazi yangu” anasema Thobias


CHANGAMOTO

Licha ya kijana huyu kufaidika kutokana na ujasiriamali huo, amekuwa akikumbana na vikwazo mbalimbali hasa eneo la uuzaji wa bisi kwani amejikuta anaowauzia mashine nao wanaanzisha vijiwe vyao vya kuuza bisi hivyo kugombania soko.


“Changamoto nyingine ni kuendelea kuibuka kwa wabunifu wapya wa mashine zinazotengeneza bisi na hivyo kuleta ushindani na kwamba changamoto hiyo humsaidia kuwaza zaidi namna ya kufanya maboresho ili kuendelea kupata soko zaidi” anasaema Thobias”


Juhudi za uendelezwaji kwa wabunifu wa aina hii Afisa Uhusiano mwandamizi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) Mary Kigosi anasama kuwa, tume imekuwa ikiwasaidia wabunifu na watafiti nchini, kupitia Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia, na Ubunifu (MAKISATU) ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo mwezi Mei katika wiki ya ubunifu kwa kutoa nafasi mbali mbali ambazo hushindaniwa na wabunifu kulingana na viwango vyao vya elimu.


“Wakati tunaandaa mashindano haya huwa tuna makundi saba ambayo uhusisha wabunifu kutoka shule ya msingi, sekondari, vyuo, taasisi za utafiti na maendeleo pamoja na sekta zisizo rasmi ambazo ndani yake hujumuisha watu wasio wasomi ambao wapo mtaani lakini wana bunifu zao”


“Katika kuchakata maombi hayo, watu kumi wenye bunifu bora zenye kuleta tija kwenye jamii huchaguliwa kama washindi na hatimaye hutafutiwa namna ya kusaidiwa na COSTECH juu ya bunifu zao” anasema Kigosi


Aidha Kigosi ameongeza kuwa, kwa wale wabunifu ambao huibuka katika kipindi ambacho hakuna mashindano yanayo ihusu COSTECH, wabunifu hao hushauriwa kuwasilisha bunifu zao moja kwa moja kwenye tume kupitia halmashauri zao au kupitia barua pepe ya tume hiyo.


Taifa linaloendelea kama Tanzania huwategemea vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa kuwa msaada kwenye eneo la ubunifu wa vitu mbalimbali vyenye kulisaidia Taifa hilo kuondokana na changamoto zinazokwamisha maendeleo kwenye nyanja tofauti tofauti mfano kilimo, uvuvi na kadharika.


Kijana Thobis ni miongoni mwa vijana hao ambao katika kubuni na kuiingiza kwenye matumizi mashine yake imetatua changamoto zake binafsi lakini pia kutatua changamoto za ajira kwa baadhi ya vijana wengine.


Thobias anatuma salaam kwa vijana kuchangamsha akili zao kubuni na kuanzisha vitu mbalimbali vitakavyowakwamua wao wenyewe kimaisha lakini pia kuisadia jamii kupiga hatua kimaendeleo.


Dunia ya leo inabadilika kwa kasi na teknolojia inaendelea kuwa sehemu muhimu ya maisha yetu ya kila siku hivyo una kila sababu ya kuonesha au kukiweka katika uhalisia kile ambacho unahisi kina manufaa kwa jamii.

 

Aidha iwapo umeshindwa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa rasilimali wezeshi unaweza kulifanya wazo lako kuwa katika uhalisia kwa kuzishirikisha mamlaka zenye dhamana ya kukuza na kuendeleza bunifu nchini ili kupatiwa msaada.

Yorumlar


bottom of page