Tusiwafungie ndani, usonji unatibika
- Restuta Damian
- Mar 16
- 4 min read
Updated: Apr 17
Na Restuta Damian
Kwa mujibu wa wataalam, usonji ni tatizo la kiakili ambalo mtoto anazaliwa nalo linalomsababishia changamoto katika mahusiano, mawasiliano na muda mwingine kuwa na tabia za kujirudia rudia.
Kwa mujibu wa daktari wa magonjwa ya akili katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera ya Bukoba Dkt. Mike Mabimbi anasema kitaalam haijafahamika sababu mahususi zinazosababisha usonji isipokuwa zipo zile za kimazingira, mfumo wa maisha na kimaumbile (genetics) zinazohusishwa na tatizo hilo.
Anazitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na mjamzito anapotumia madawa ya kulevya, mjamzito kupatwa homa na mafua ya mara kwa mara, wazazi kuzaa wakiwa na umri mkubwa pamoja na kurithi tatizo hilo, yaani familia kama iliwahi kuwa na mtoto wenye usonji ni rahisi kutokea kwenye kizazi kinachoendelea.
“Tatizo la usonji halina dawa kabisa isipokuwa mtoto anapogundulika anaweza kuandaliwa katika mfumo wa saikolojia ili kuepusha matatizo ya kimahusiano, kimawasiliano na tabia za kujirudia rudia ambazo uwakabiri watu wenye usonji” alisema Dkt Mabimbi.
Anasema tiba pekee anayoweza kupatiwa mtoto mwenye tatizo la usonji, ni tiba tabia inayoanzia kwa wazazi wenyewe kuelewa na kukubali kuwa usonji ni tatizo kama yalivyo magonjwa mengine na hivyo yasihusianishwe na masuala ya imani potofu.
Anasema mzazi akishalitambua hilo atamfikisha mtoto haraka kwa wataalam wa afya ambapo ataanza kumpitisha kwenye hatua zote za makuzi kwa kumpatia tiba tabia zitakazomfanya kuondokana na hali tatu anazozipitia mtu mwenye usonji na kufikia hatua ya kumudu mazingira ya kuwa kama watu wengine.
“Tunao wataalam wa lugha, makuzi na tabia za watoto ambao wanaweza kumsaidia mtoto huyo kubadilika kiakili na kuwa kama watu wengine ni jambo la wazazi kulitambua tatizo la usonji mapema na kulifikisha kwa wataalam, samaki mkunje angali mbichi” anasema Dkt Mabimbi.
Kwa mujibu wa shirika la afya Duniani WHO watu milioni 22 kote duniania wana tatizo la usonji na kwamba kwenye watoto 100 hadi 160 kuna mtoto mwenye tatizo hilo huku watoto wa kiume wakitajwa kuwa waanga zaidi wa usonji.
Mwalimu John Mwita ni mwalimu aliyebobea kuwafundisha wanafunzi wenye tatizo la usonji anasema mtoto mwenye usonji anaweza kufundishika.
Anasema watoto wanapoletwa shuleni uanza taratibu kwa kuwafundisha namna ya kutofautisha vitu lakini kujua mpangilio wa vitu mbalimbali, kujua ni kifaa au kitu gani kinatakiwa kukaa sehemu fulani hali hiyo huifanya akili zao kuanza kutambua.
Anasema usomaji wao uchukua muda mrefu tofauti na wanafunzi wa kawaida kwani mwanafunzi wa kawaida hata kabla ya kuanza shule hutoka nyumbani akijua baadhi ya mambo na hivyo kuwafanya walimu kuanzia kwenye hatua ya makuzi aliyofikia.
Anasema mtoto huyo anapaswa kupelekwa shule maana akiachwa na kuendelea kubaki, muda wote mzazi ataona hawezi kufanya chochote hata kazi za mikono, lakini akiwa shuleni akiwaona wenzake naye anachangamana nao na kushirikiana nao.
“Watoto tulio nao wanafanya vitu vingi mbali na masomo ya darasani pia wa na kudeki, kufagia, kukusanya uchafu, kuosha vyombo na muda wa kucheza na wenzake ambapo mazingira ya namna hiyo yanamfanya kuchanganua na kujua vitu vingi tofauti na anapokuwa nyumbani”anasema Mwita.
Amesema watoto wote wenye usonji aliokutana nao wameonesha mafanikio makubwa japo maendeleo hayo yanatofautiana kwa kila mtoto kama ilivyo kwa watoto wa kawaida wapo wenye kasi katika kushika lakini wapo wanaoelewa taratibu.
Anaeleza kuwa kuna njia zinazotumiwa ili mtoto wa aina hiyo aweze kuandika kwa kutumia zana za vitendo kwa maana ya vibao ambavyo tayari vimechorwa herufi ua picha inayomshawishi kuandika, kuoanisha na kufanya uwezo wake wa akili kutenda.
“Katika kupima uelewa wake unaweza kuchanganya picha na herufi, akiweza kuchanganua au kutofautisha vitu hivyo tunamuingiza kwenye hatua nyingine, wapo wanaoweza lakini kwa wanaoshindwa humfanya mwalimu kubuni njia nyingine ya kumuelewesha” anasema Mwita.
Anasema walio wengi wanakuwa na shauku ya kupenda kuandika, wengine kuchora na kwamba mwalimu ukisha muona mtoto huyo unakuwa karibu naye kwa kumuelekeza namna bora ya kufanya kwa usahihi.
Anawashauri wazazi kutokuwaficha watoto hao akidai watoto wanapobaki nyumbani wanaendelea kudamaa na wanakosa muongozo kwani mtoto hupenda kujifunza akiwa katika rika analokaribiana nalo.
Bi, Anastella Anesius ni mzazi mwenye mtoto aliye na usonji anasema mwanzoni watu walimshauri kuwa mtoto wake hawezi chochote hivyo hakuna haja ya kumpeleka shule kutokana na tatizo la usonji alilo nalo.
Anasema yeye kama mzazi alitamani kuona mwanae anapata elimu ya kumsaidia kumudu maisha na mazingira na hivyo hakukata tamaa aliamini mwanae anaweza kwenda shule akasoma kama watoto wengine.
Anasema kipindi hicho, mtoto wake alikuwa hawezi kuagizwa wala kuelekezwa chochote akakifanya bali alikuwa wa kukaa tu mwenyewe bila kushughulika na chochote.
“Watu walisema huyu hawezi kwenda shule kulingana na tatizo lake atawasumbua walimu hatoelewa chochote” alisema Anastella.
Anaeleza kuwa baada ya kumpelaka shule mtoto aliweza kubadilika sana akawa muelewa tofauti na mwanzo alivyokuwa kiasi kwamba hata na waliokuwa na watoto wengine wenye ulemavu wakaanza kumuulizia utaratibu wa kuwapeleka watoto wa shule.
Sweebert Mushanga ni katibu wa shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu (SHIVYAWATA) mkoani Kagera anasema kuwa walemavu kutokupelekwa shule inachangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo mtazamo wa jamii juu ya watu hao kuwa hawawezi chochote darasani na hivyo kubaki nyumbani.
Anasema imani hiyo uanzia kwa familia na uzito wa jambo hili uongezeka pale wazazi wanapopata ushauri hasi kutoka kwa watu wanaowazunguka na kwamba jamii inatakiwa itambue kwamba tatizo la usonji si shida sana kama inavyoaminiwa kwani likibainika mapema linatatuliwa.
Anaeleza kuwa wazazi wanatakiwa kuwaamini madaktari na walimu kuwa wanaweza kuwasaidia watoto wao kurejea katika mfumo wa kawaida wa makuzi na maisha na huko ukubwani kuweza kujitegemea.
“Kuna watoto tumeshuhudia wakifanya vitu ambavyo awali hatukutegemea kama wangevifanya na hii baada ya kupelekwa shule lakini kabla ya hapo kupata miongozo na ushauri wa wataalam wa afya katika makuzi” alisema Mushanga.
Anaishukuru serikali kwa kuendelea kuongeza shule za watu wenye mahitaji maalum ambazo kwanza ni ujumbe kwa jamii kuwa mtoto wa aina hiyo anatakiwa kwenda shule lakini pili kuwafanya wanafunzi kusomea karibu na makazi yao.
Kwa maelezo ya wadau hao ni dhahiri tatizo la usonji linaweza kutokomezwa iwapo hatua za makuzi tangu mtoto akiwa tumboni, kuzaliwa kwake hadi ukuaji wake zinazingatiwa kwa ufanisi zaidi.
Lakini pia ili hayo yaweze kufikiwa jamii inatakiwa kuelimishwa vya kutosha kuhusu usonji na matatizo mengine ya akili lakini pia jamii kuwa tayari kupokea elimu ya wataalam kuhusu hali hizo za kiafya na likawe jukumu la kila mmoja kutimiza wajibu wake kufikia mabadiliko kwa mtoto mwenye usonji.
Comments