top of page

Tofauti ya maumbile na nguvu ya mapambano ya maisha

Katika jamii nyingi, dhana potofu juu ya ulemavu bado inaendelea kutawala fikra za watu. Wapo wanaoamini kuwa ulemavu ni ugonjwa, laana, au ishara ya kushindwa katika maisha.

Mtazamo huu umesababisha maumivu makubwa ya kisaikolojia, kijamii na kiuchumi kwa watu wenye ulemavu. Ukweli ni kwamba, ulemavu si ugonjwa, bali ni hali ya maumbile au mabadiliko ya kimwili, kiakili au kihisia yanayomtofautisha mtu na wengine.


Tofauti hiyo haipunguzi utu, thamani wala uwezo wa mtu katika jamii. Makala hii inalenga kuwaelimisha watu wenye ulemavu wajithamini, waishi kwa nia ya mapambano ya maisha, na wakati huo huo kuikumbusha jamii kuwa mlemavu anaweza kufanya chochote na kuwa mtu mwenye heshima na hadhi sawa na yeyote.


Ulemavu ni hali inayoweza kuzaliwa nayo mtu au kupatikana baadaye kutokana na ajali, maradhi, au sababu nyingine za kiafya. Kuna ulemavu wa viungo, ulemavu wa kuona, kusikia, kuzungumza, ulemavu wa akili, na aina nyingine nyingi.


Muhimu zaidi ni kuelewa kwamba ulemavu hauondoi ubinadamu wa mtu. Mtu mwenye ulemavu bado ana akili, hisia, ndoto, vipaji na haki zote za msingi kama binadamu mwingine yeyote.


Ni kosa kubwa kuufananisha ulemavu na ugonjwa. Ugonjwa unatibika au kupona, lakini ulemavu mara nyingi ni hali ya kudumu, hii haimaanishi kuwa maisha ya mtu mwenye ulemavu yamefikia mwisho au hayawezi kuwa na mafanikio.


Kinyume chake, historia imetuonyesha watu wengi wenye ulemavu waliovuka mipaka ya fikra za jamii na kufanikiwa katika nyanja mbalimbali za maisha.


Kwa watu wenye ulemavu, changamoto kubwa si ulemavu wenyewe, bali ni mtazamo hasi kutoka kwa jamii na wakati mwingine kutoka ndani yao wenyewe, kujidharau, kukata tamaa, na kuamini huwezi kwa sababu ya maumbile yako ni adui mkubwa wa mafanikio.

Ni muhimu kufahamu kwamba wewe ni binadamu kamili, una thamani kubwa, na unastahili heshima kama wengine wote.


Badala ya kujiona dhaifu, jione kama mpiganaji wa maisha, maisha ni uwanja wa mapambano kwa kila mtu, awe na ulemavu au asiwe nao. Tofauti ni kwamba wewe unapambana kwa njia ya kipekee.


Kubali hali yako, jiamini, tambua vipaji vyako, na vitumie kujijenga na kujitegemea. Elimu, ujuzi wa kazi, nidhamu, na bidii ni silaha muhimu katika safari yako ya mafanikio.


Watu wengi wenye ulemavu wamefanikiwa kwa sababu hawakuruhusu hali zao ziwe kikwazo, wamekuwa waalimu, wanasheria, madaktari, wanasiasa, wanamichezo, wasanii, wajasiriamali na viongozi wakubwa, mafanikio yao ni ushahidi kwamba ulemavu hauui ndoto. Kinachoua ndoto ni kukata tamaa.


Maisha hayana huruma kwa mtu asiye na malengo, kwa mtu mwenye ulemavu, kuwa na nia ya mapambano ya maisha ni jambo la msingi sana, hii ina maana ya kuamua moyoni kwamba, licha ya changamoto zako, hutokata tamaa, unajifunza, unajaribu, unaanguka na kuinuka tena, unapambana sio kwa hasira, bali kwa hekima, subira na imani.


Nia ya mapambano inaanza na kujikubali. Jikubali ulivyo, kisha jipe malengo yanayotekelezeka, tafuta msaada pale unapohitaji, lakini usiishi kwa kutegemea huruma. Huruma si suluhisho la maisha; fursa na usawa ndivyo suluhisho, unapopata nafasi, itumie ipasavyo kuonyesha uwezo wako. Hivyo ndivyo jamii itakavyoanza kukuona kwa macho ya heshima badala ya huruma.


Ujumbe kwa jamii: Mlemavu anaweza

Jamii ina jukumu kubwa katika kumuinua au kumdhalilisha mtu mwenye ulemavu. Lugha tunayotumia, mitazamo yetu, na mifumo tunayojenga vinaweza kuwa kikwazo au daraja la mafanikio kwao. Ni wakati wa jamii kuelewa kwamba ulemavu hauondoi uwezo.


Mlemavu anaweza kusoma, kufanya kazi, kuongoza, kuoa au kuolewa, kulea familia, na kuchangia maendeleo ya taifa.


Ni muhimu kuacha tabia ya kuwaficha watu wenye ulemavu majumbani kana kwamba ni aibu. Pia ni muhimu kuacha kuwachukulia kama watoto wasiojiweza. Wanachohitaji si huruma, bali ni fursa sawa: elimu jumuishi, ajira bila ubaguzi, miundombinu rafiki, na mazingira yanayoheshimu haki zao.


Jamii inapowapa nafasi watu wenye ulemavu, hunufaika kwa kupata nguvu kazi yenye vipaji na mitazamo tofauti. Utofauti ni utajiri, si mzigo. Taifa lolote linalowatenga watu wenye ulemavu linajinyima maendeleo yake yenyewe.


Heshima na hadhi ni haki ya kila mtu

Heshima ya mtu haitokani na mwonekano wa mwili wake, bali na utu wake. Mtu mwenye ulemavu ana haki ya kuheshimiwa, kusikilizwa, na kushirikishwa katika maamuzi yanayomhusu. Hadhi ya mtu haitokani na kutembea kwa miguu miwili, kuona kwa macho yote mawili au kusikia kwa masikio yote mawili, bali inatokana na mchango wake katika jamii na maadili yake.


Ni wajibu wa viongozi, wazazi, walimu, na wanajamii wote kujenga utamaduni wa heshima kwa watu wenye ulemavu. Watoto wafundishwe mapema kuwa ulemavu si kitu cha kuchekwa au kudharauliwa. Vyombo vya habari viwasilishe simulizi chanya zinazojenga uelewa na kuondoa unyanyapaa.


Kwa kumalizia, ni muhimu kusisitiza tena kwamba ulemavu si ugonjwa, ni hali ya maisha inayohitaji uelewa, ushirikiano na heshima kutoka kwa jamii nzima. Kwa watu wenye ulemavu, msijidharau kamwe.


Simameni imara, tembeeni na nia ya mapambano ya maisha, na amini kwamba mnaweza kufanikiwa, kwa jamii, badilikeni mtazamo, mlemavu anaweza kufanya chochote, anaweza kuwa mtu mwenye heshima na hadhi kama yeyote katika jamii.


Tukibadilisha fikra zetu leo, tutajenga jamii jumuishi kesho; jamii inayothamini utu wa kila mtu bila kujali tofauti za maumbile, hapo ndipo tutakaposema kwa dhati kwamba tumepiga hatua ya kweli ya maendeleo ya kibinadamu.

 
 
 

Comments


bottom of page