Taratibu za taa za barabarani zakiukwa waziwazi
- Restuta Damian
- Feb 20
- 4 min read
Updated: Apr 17

Je watu hawa wanafanya hivyo kutokana na maadili mabaya yatokanayo na malezi?, ni ubishi?, ujuaji?, kutojali? au ni mazoea ya kuona wao ni mahiri katika uendeshaji wa vyombo vya moto?
Na Restuta Kasigara
Pamoja na serikali kufanya kila jitihada kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua, bado watumiaji wa barabara wanashindwa kufuata maelekezo na taratibu za matumizi sahihi ya barabara.
Miongoni mwa watumiaji ambao wanatajwa kwa kiasi kikubwa kukiuka taratibu za usalama barabarani ni waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda, ambao pamoja na wengi wao kufahamu taratibu hizo bado hawazifuati.
Ili kuthibitisha hilo nikiwa nimesimama kati ya barabara ya kwenda kata Kashai na Nshambya katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, eneo ambalo zimefungwa taa zinazoongoza watumiaji wa barabara, pamoja na uwepo wa taa hizo bado bodaboda wanavuka bila kusubiri kuruhusiwa.
Kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani ya mwaka 2002 sura ya 168 kifungu namba 73(2) watumiaji wote wa barabara wanatakiwa kuheshimu na kufuata ishara zinazoonyeshwa na taa zilizofungwa barabarani.
Sheria hiyo inasema taa hizo hufungwa pembeni au katikati ya barabara, lengo likiwa ni kuongo za msafara wa magari na vyombo vingine, na kuweka uwiano sawa wa matumizi ya njia kwa makundi yote ya watumia barabara.
Wakati nikiendelea kusimama katika eneo hilo la taa kujionea kama kusudi la ufungwaji wa taa linazingatiwa kwa maana ya kufuata mwongozo, naona wazi yapo makosa yanayofanywa kwa makusudi na kwa kujua.
Kwa nini nasema ukiukwaji wa sheria katika eneo hilo unafanyika kwa kujua na kwa kukusudia, sababu wengine wanazingatia uwepo wa mwongozo huo, baadhi hawazingatii ilihali wameona vyombo vya moto vya wenzao vikiwa vimesimama kusubiri ruhusa ya taa.
Kundi hili la wavunjaji wa sheria kwa makusudi, wengi wanashindwa litafasiriwe vipi, Je waendesha bodaboda wanapenda kuona ndugu zao wakipata ulemavu au kupoteza maisha kutokana na ajali zinazoweza kuzuilika?
Je watu hawa wanafanya hivyo kutokana na maadili mabaya yatokanayo na malezi, ni ubishi, ujuaji, kutojali au ni mazoea ya kuona wao ni mahiri katika uendeshaji wa vyombo vya moto?
Baadae niligeukia kundi la watembea kwa miguu na wasukuma mikokoteni wanavyopata shida kukwepa tairi za pikipiki za walioshindwa kufuata sheria, kwa kusubiri dakika au sekunde kadhaa ili waruhusiwe kuendelea na safari.
Nilijiuliza mara kadhaa usalama wa wengine sio usalama wa huyo mwendesha bodaboda? Ninachofahamu haya makundi mawili yanategemeana, hivyo mwendesha bodaboda anapaswa amlinde mtembea kwa miguu, lakini pia na mtembea kwa miguu anapaswa kumlinda mwendesha chombo cha moto.
Mwongozo wa taa za barabara ni unamtaka kila mtumia barabara afuate taa hizo, mfano mtu kutaki wa kusimama endapo ameona rangi nyekundu katika taa iliyoko mbele yake, ambayo inamwonesha hatari, lengo kuruhusu watumiaji wa upande mwingine kuvuka eneo hilo kwa usalama.
Anachopaswa kufanya mtu huyo ni kusimama hadi pale atakapoona rangi ya kijani mbele yake, ambayo huashiria kuwa sasa anaruhusiwa kuendelea na safari.
Tatizo kubwa hapa ni waendesha bodaboda kufanya kinyume na hilo maana hulazimisha kupita kuwahi wanakoelekea bila kujali athari ambazo zinaweza kutokea kutokana na uvunjaji wa sheria za barabarani kwa makusudi.
Hivi hii haraka waliyonayo waendesha bodaboda huwa inatokana na nini, ni abiria wao ndio huwataka kuwahi bila kuzingatia usalama wao na wa watumiaji wengine wa barabara, au ni bodaboda wenyewe huwa wanaamua?
Je abiria anayekuwa amebebwa wakati bodaboda anakiuka utaratibu kwa makusudi, yeye huchukua hatua gani ili kumwelimisha siku nyingine asirudie, au yeye ndiye humwambia bodaboda asisimame akidai anawahi?
Abiria anawekwa kwenye kundi la wazazi yaani kulea maana kuna sheria zinakiukwa wakati yeye yupo, hii ni hatari kwa abiria na dereva, pia na kwa watumiaji wengine.
Hapa hatuwezi kumpata abiria ili kumfundisha sheria za barabara- ni, lakini kutokana na gazeti hili la Montessori Tanzania ambalo mlengo wake ni kutoa elimu kwa wote, ninaimani wananchi wengi watapata elimu na kuitumia kuwaelimisha waendesha bodaboda, na kuwafanya kubadilika.
Mbali na kuvunja sheria katika taa, pia wapo baadhi ya waendesha bodaboda wanapita kushoto mwa vyombo vingine (overtaking) na wengine hawafuati mzunguko wa barabara zinazopishana, hawa nao wanapaswa kuelimishwa ili wajue kuwa kufanya hivyo ni hatari.
Lipo pia tatizo la waendesha bodaboda kutoheshimu alama nyingine za barabarani mfano katika vivuko vya watembea kwa miguu, hupaswa kusimama na kusubiri kama kuna mtu anataka kuvuka, lakini wengi hawafanyi hivyo huku wakijua kuwa ni kosa.
Nionavyo mimi, mwendesha bodaboda ndiye ana dhamana ya maisha yake, ya abiria na usalama wa chombo, hivyo akifuata sheria na kutumia lugha rafiki, atapata umaarufu na kuongeza idadi ya wateja.
Mwishoni mwa mwaka jana akizungumzia suala la ajali mkoani Kagera kamanda wa polisi mkoani Kagera, Brasius Chatanda aligusia suala la uvunjwaji wa makusudi wa sheria za usalama barabarani, unaofanywa na waendesha bodabodoa.
Chatanda amesema kuwa anazo taarifa za waendesha bodaboda kuvuka katika taa za kuongoza watumiaji wa barabara bila kuruhusiwa, na kwamba tatizo hilo linafanyiwa kazi.
“Wafahamu kuwa taarifa zao ninazo, nawaonya waache mara moja tabia hiyo, vyombo vya dola hatujalala, tutawakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria” anasema Chatanda.
Anasema tatizo la kutozingatia sheria za usalama barabarani ndilo linasababisha kuwepo kwa ajali, na kwamba ili mkoa wa Kagera uwe salama inabidi kila mmoja kuziheshimu sheria hizo.
Kumbukumbu za kikosi cha usalama barabarani cha jeshi la polisi nchini, zinasema mwaka 2022 Watanzania 886 walipoteza maisha kutokana na ajali wakiwamo vijana, huku watu wengine 573 wakiachwa na majeraha.
Kutokea kwa ajali hasa zinazoweza kuzuilika kunasababisha madhara makubwa kwa jamii ikiwamo baadhi kupoteza wapendwa wao, wengine kupata ulemavu wa kudumu na kupoteza mali hali inayosababisha umaskini kuongezeka katika jamii.
Ili kuliepuka hilo na kuwezesha uwepo wa jamii na taifa lenye ustawi wote kwa pamoja tunapaswa kushirikiana kupinga na kupiga kelele dhidi ya matukio yasiyofaa ambayo yanaweza kusababisha ajali zinazotokana na uzembe.
Kadhalika, elimu inapaswa kuendelea kutolewa kwa watumiaji wote wa barabara, ili kila mmoja akitimiza wajibu wake wakati akitumia barabara, ajali ziweze kupungua na kufanya kila eneo hapa nchini kuwa salama.
Comments