Pasua kichwa chupa za plastiki
- Wariyoba Wariyoba
- Mar 25
- 5 min read
Updated: Apr 17
"Mtu akila samaki aliyemeza chupa ya Plastiki anakuwa kwenye hatari ya kupata saratani ya tumbo, tulinde mazingira."
Waryoba M. Waryoba, Morogoro
Uzalishaji wa chupa za Plastiki nchini unaofanywa na viwanda mbalimbali umekuwa ukiongezeka kila kukicha kitendo ambacho kimekuwa kikisababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira katika maeneo mbalimbali na kuhatarisha afya za viumbe hai.
Wakati wadau mbalimbali wa mazingira nchini wakitafakari namna tofauti tofauti ya kupambana na uchafuzi huo wa mazingira, wapo ambao wameweza kuanzisha viwanda vya kuchakata chupa hizo na kutengeneza bidhaa nyingine ambapo mbali na kusaidia kukabiliana na uchafuzi wa mazingira pia hutoa fursa ya ajira kwa watu mbalimbali ikiwemo waokota chupa, wachakataji na wazalishaji wa bidhaa mpya.
Said Mrisho ni miongoni mwa waokota chupa za plastiki anaeleza kuwa kazi yake hiyo mbali na kuwa na changamoto nyingi lakini imekuwa ikimuingizia kipato kila siku kitendo ambacho kinamfanya aweze kujikimu kimaisha kwa kazi hiyo.
“Kwa siku nimekuwa nikiokota na kukusanya chupa zaidi ya kilo 30 ambazo huziuza na kupata fedha shilingi 8000 hadi 10000 ambapo 5000 huitumia kwa chakula na kiasi kinachobaki hukitunza kama akiba maana kuna leo na kesho” anasema Mrisho.
Mrisho anasema kuwa kazi hiyo ni kama kazi nyingine lakini imekuwa ikikabiliwa na changamoto kwani baadhi ya watu huwaona waokota chupa kama wezi au watumia madawa ya kulevya hali inayowafanya wawe na wakati mgumu pale wanapokuwa wakikusanya chupa hizo.
Anasema jamii inatakiwa kuwathamini waokota chupa za plastiki kwani mbali na kazi hiyo inawapatia kipato pia wanasaidia sana kutunza mazingira kwani bila hivyo chupa hizo zote zitaishia kwenye bahari, mito, maziwa na kwenye vyanzo vingine vya maji kitendo ambacho ni hatari kwa afya.
“Kitendo hiki siyo kwamba kinatunufaisha sisi waokota chupa pekee la! hasha pia kina tija kwa nchi yetu maana ni moja ya njia ya kutunza mazingira kwani bila hivyo chupa hizi zitatapakaa kila kona ya nchi na kusababisha madhara kwa jamii ikiwemo kifo”anasema.
Mrisho anasema kwamba kazi hiyo ya kuokota chupa za maji zilizotumika ina faida na kwamba mtu akiifanya kwa kudhamiria atafanikiwa kimaisha ambapo ameitaka jamii kuacha tabia ya kuwa na mtazamo hasi juu ya wanaojishughulisha na kazi ya kuokota chupa hizo.
Chupa za plastiki zipo za aina nyingi ambapo imeelezwa kuwa viwanda vinavyonunua chupa za vinywaji kwa lengo la kuzichakata na kuzalisha chupa mpya au kutengeneza bidhaa nyingine hupenda sana kutumia chupa za maji lakini kwa chupa za vinywaji vingine zisizo za plastiki hazihitajiki sana.
Omar Said ni muokota chupa hizo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani anasema kuwa soko lake kubwa lipo Dar es Salaam na kwamba baadhi ya chupa za maji huuzwa shilingi 300 kwa kilo na nyingine huuzwa shilingi 100.
Anasema kuwa kutokana na hilo waokota chupa wengi wanapenda kuokota/kukusanya chupa za maji na siyo vinywaji vingine kwani chupa hizo hazina faida ukilinganisha na zile za maji.
Dickson Mwanyela ni mfanyabiashara wa taka ngumu za aina mbalimbali kama vile chupa za maji, plastiki na viroba wilayani Bagamoyo anasema baada ya kuona taka ngumu zimetapakaa maeneo mengi ya mitaani aliona kwake ni fursa ya kijipatia kipato.
Anasema kuwa biashara yake hiyo imeweza kupunguza sana taka za plastiki mitaani kwani kuna watu walioamua kujiajiri ambao hukusanya chupa za plastiki zilizotumika na kumuuzia ambapo kwa siku hununua zaidi ya kilo 100.
“Kuna watu wamekuwa wakikusanya chupa hizi mitaani kwangu na kuniuzia ambapo kwa siku moja huwa nanunua kilo 100 hadi 120 na baada ya hapo mzigo unapokuwa mkubwa mimi pia huusafirisha kwenda viwandani Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuuza” Anasema Dickson.
Kutokana na utupaji wa taka ngumu kuwa sugu nchini wadau mbalimbali wameamua kijitokeza ili kuisaidia jamii kuepukana na changamoto hii kwa lengo la kuepuka athari zitokanazo na madhara ya plastiki ikiwa ni pamoja na kuimarisha utunzaji wa mazingira Licha ya uwepo wa biashara ya chupa za plastiki bado changamoto ya utupaji holela wa chupa hizo umekuwa ukiendelea na kusababisha changamoto katika shughuli mbali mbali za kibinadamu.
Katibu wa soko la Samaki Bagamoyo lililopo mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Doria (BMU) Haji Sudy Simai anakiri kuwa maeneo ya pembezoni mwa bahari yanakabiliwa na changamoto ya uchafu wa taka ngumu.
Anasema uchafu huo unatokana na plastiki za vinywaji kwani watu wamekuwa wakinywa sana na kisha kuzitupa hovyo na kwamba pale mvua zinaponyesha baadhi husombwa na maji na kuingia baharin “Mimi pia ni mvuvi wa samaki bahari ya Hindi hapa Bagamoyo tumekuwa tukikutana na chupa baharini hivyo suala hili halihitaji mzaha hata kidogo ni wajibu wa mamlaka husika kuchukua hatua ili kudhibiti hali hii” anasema Haji.
Simai anasema kuwa hawana uwezo wa kudhibiti utupaji ovyo wa chupa hizo za plastiki isipokuwa halmashauri yenye wajibu wa kutunga sharia ndogondogo za kulinda mazingira.
Anakiri kwamba bado jamii haina uelewa juu ya athari zitokanazo na utupaji wa taka ngumu zikiwemo za plastiki na kwamba BMU imekuwa ikiendesha zoezi la kuondoa taka ili zisiweze kuingia baharani zoezi ambalo bado ni gumu.
“BMU iliundwa na halmashauri hii lakini uongozi wa halmashauri yetu hauna ushirikiano mzuri kwetu ukizingatia sisi hatuna mamlaka ya kuzuia utupaji wa taka ngumu na ndiyo sababu ya utupaji wa chupa za plastiki unaendelea kushamiri” anasema Simai.
Anaongeza kuwa BMU inafanya kazi kwa kujitolea hivyo haina nguvu kisheria kuzuia wanaotupa hovyo chupa za plastiki maeneo ya baharini ambapo amewaomba viongozi wa halmashauri kulitazama tatizo hilo kwa jicho la tatu ili kulikomesha.
Anasema kuwa endapo mamlaka husika zitaweka sheria na kusimamiwa ipasavyo suala la utupaji ovyo wa chupa za plastiki utakomeshwa lakini kama mamlaka zitaendelea kukaa kimya kwa kujifanya hazioni, chupa za plastiki zitaendelea kuzagaa mitaani na kusababisha uchafuzi wa mazingira.
Mbali na kuendelea kutapakaa kwa taka za plastiki katika mazingira bado wadau hawajaacha kukemea na kuelimisha jamii juu ya madhara yatokanayo na utupaji hovyo wa taka ngumu. Mkurugenzi wa Taasisi inayojishughulisha na Utu na Mazingira (HUDEFO) Human Dignity and Enviromental care Foundation, Sarah Pima anasema kuwa katika kuhakikisha taasisi yake inakabiliana na changamoto ya utupaji wa taka ngumu, taasisi yake imeanzisha mradi wa Uwajibikaji wa Wazalishaji Taka (EPR).
Anasema zipo athari nyingi zikiwemo za kiafya zitokanazo na utupaji ovyo wa plastiki ikiwemo ugonjwa ya saratani ambapo ameitaka jamii kwa ujumla kuepuka uharibifu wa mazingira kwa kutupa ovyo chupa za plastiki baada ya kutumia/kunywa kinywaji kilicho ndani ya chupa husika.
“Sheria za mazingira zipo lakini hazifuatwi, taasisi yetu inatamani kuona kunakuwepo na sera ili kwa yeyote atakaye kwenda kinyume na sera na sheria awajibishwe kisheria”anasema Sarah.
Anasema ni vizuri wazalishaji wa bidhaa zote za plastiki wawe na utaratibu wa kununua chupa zote za plastiki zilizotumika na kuzichakata upya ili ziingie tena sokoni kwani kufanya hivyo kutasaidia sana kuondoa taka ngumu mitaani na pia kutatoa fursa nyingi kwa waokota chupa.
Kwa mujibu wa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, Shule Kuu ya Sayansi, afua za utekelezaji na uvuvi,Bahati Mayoma ni kuwa tatizo la taka ngumu hususani za plastiki ni sugu na kwamba hatua za haraka zinatakiwa kuchukuliwa ili kuweza kudhibiti hali hiyo.
Mayoma anasema tatizo la taka aina ya plastiki halipo kwa Tanzania pekee bali ni kwa Dunia nzima na kwamba tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa kama hatua madhubuti hazitachukuliwa hadi kufikia mwaka 2050 taka za plastiki zitakuwa nyingi baharini kuliko samaki.
Anasema kuwa takribani tani milioni 350 za plastiki huzalishwa kila mwaka Duniani ambapo tani milioni14 kati ya 350 huingia kwenye vyanzo vya maji.
“Tanzania tunazalisha tani elfu 15 hadi 17 za plastiki kila mwaka na kama taka hizi zisipooza huingia kwenye vyanzo vya maji, tatizo la taka za plastiki ni janga la kimataifa hivyo ili kukabiliana na tatizo wazalishaji wa chupa hizi wanatakiwa kuwa na mfumo utakaosaidia kuzichakata upya baada ya matumizi”anasema Mayoma.
Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani Hospitali ya Ocean Road Dkt. Ernest Magembe anasema kuwa kitendo cha plastiki kuingia kwenye bahari, mito, maziwa na kwenye vyanzo vya maji huliwa na samaki hivyo ni hatari kwani endapo mtu akila samaki aliyemeza plastiki kuna uwezekano wa kupata saratani ya utumbo.
Dk Magembe anatoa wito kwa Serikali na wadau wengine kuhakikisha sheria za mazingira zinafuatwa ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha wazalishaji wa viwanda vya plastiki kwani kutasaidia kudhibiti utupaji ovyo taka za plastiki
Comentarios