Ombaomba wanavyochochea ulemavu wa fikra kwa watoto
- Wariyoba Wariyoba
- Mar 21
- 6 min read
Updated: Apr 17
Na Waryoba M.Waryoba
Ni kawaida hasa katika maeneo ya mijini, iwe kwenye mabaa, kumbi za starehe, maduka na hata maofisi mbalimbali utaona mtoto akimkokota mtu mwenye ulemavu na kukufuata, atasimama mbele yako na kisha utaisikia sauti kutoka kwa mtoto ikipenya vizuri sikioni tena kwa utulivu “Anko au Anti ….. saidia”.
Na huwa hawana maneno mengi hata kama hutampa kitu chochote ataondoka kimya kimya bila ya kusema chochote; Wengine wakishakufikia huwa hawaongei, hunyamaza kimya mbele yako wakisubiri utoe chochote, kwani usiposikia sauti hata picha huioni?
Kweli ni jambo la kiungwana kumsaidia mtu mwenye ulemavu na katika dini ni sadaka kwa Mwenyezi Mungu, kweli kabisa lakini kinachofikirisha ni maisha ya usoni ya mtoto anayemsaidia mlemavu huyu.
Je, mtoto huyu ataendelea kumkokota na kumuombea misaada mpaka lini mtu mwenye ulemavu ilhali naye umri unaongezeka mwaka hadi mwaka? Je, maisha yake yatakuwa ya namna gani kwani muda mwingi aliupoteza kumkokota mlemavu ambaye wakati huo pengine hatakuwa naye tena? Hatarithi tabia ya ombaomba aliyokuwa kiifanya miaka nenda rudi kwa kuwa ameshakuwa na uzoefu nayo? Hayo ni baadhi ya maswali machache ya kujiuliza japokuwa kwa mujibu wa vitabu vya dini, mtoto anastahili malezi bora hivyo kitendo hiki cha baadhi ya watu wenye ulemavu na hata wasio na ulemavu kuwatumia vijana kama chambo cha kuomba misaada ni kukiuka maelekezo ya Mwenyezi Mungu.
Pia kitendo hiki kinawakosesha haki zao za msingi ikiwemo elimu kwani vijana wengi wanaohusika kufanya kazi ya kuzurura mitaani na watu wenye ulemavu hawajui kusoma wala kuandika hali inayowafanya nao wawe walemavu wa akili licha ya kuwa na viungo vilivyokamilika.
Kwa kutaka kujua undani wa suala hili mwandishi wa makala hii alifanya uchunguzi wa kina na kubaini kuwa baadhi ya vijana hao ni ndugu wa karibu na watu wenye ulemavu hivyo wameamua kutowapeleka shule ili wa wasaidie kuomba misaada mitaani.
Vile vile wapo vijana ambao hawana uhusiano wowote bali wamekuwa wakikutana mitaani na kuamua kuungana kuomba hasa wale wenye ulemavu wa macho na baada ya hapo majira ya jioni walemavu humpatia kiasi cha fedha kijana aliyemsaidia kwa siku husika kama shukrani ya kumtembeza.
Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka (13) ambaye jina lake limehifadhiwa mkazi wa Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa vijana hao ambaye amekuwa akizunguka na mama yake mzazi (jina kapuni) kuomba misaada mitaani anasema kuwa hakuwahi kwenda shule hata siku moja kwani kila siku amekuwa akipita mitaani na mama yake mwenye ulemavu wa macho kuomba misaada.
“Nyumbani kwetu tupo watoto wawili ambao ni tumbo moja, mwenzangu yupo shule anasoma la kini mimi sikubahatika kwenda shule na badala yake nimekuwa nikimsaidia mama yangu ambaye ni mlemavu wa macho kupita mitaani kuomba misaada” Anasema.
Anasema kuwa awali alikuwa akiishi kwa babu yake huko Kisaki wilayani Morogoro na alipoamua kurudi kwao, mama yake alimtaka kuwa wanaongozana wote kupita mitaani kuomba misaada na kwamba fedha ambazo hupatikana huwasaidia kujikimu kimaisha.
Kijana huyo anasema kuwa kitendo cha kupita mitaani akiwa na mama yake amekizoea sana na kwamba ikitokea mama yake akawa hayupo vizuri kiafya yeye amekuwa akipita mitaani kuomba kwa niaba yake.
Anasema anatamani sana kusoma lakini kutokana na changamoto ya mama yake, ameshindwa kufanya hivyo na kwamba kazi ya ombaomba anaipenda kwani hata kama mama yake atashindwa kwenda mitaani yeye hulazimika kwenda kuomba.
Kwa maelezo ya kijana huyo ni wazi tayari kisaikolojia ameshakuwa mlemavu wa fikra na hii inatokana na mama yake kumtumia kama chambo cha kuomba misaada na ndiyo sababu anasema kwamba ikitokea mzazi wake akashindwa kwenda mitaani yeye huenda pekee yake kwa kuwa kazi hiyo ya ombaomba anaipenda.
Mama mzazi wa kijana huyo ambaye ni mlemavu anasema mwanaye alikuwa anaishi kwa babu yake na aliporudi nyumbani kwao tayari umri wa kwenda shule ukawa umeshamtupa hivyo anaona awe anamtumia kuzunguka naye mitaani kutafuta riziki.
“Mimi ni kipofu hivyo mwanangu baada ya kutoka kwa babu yake na kurudi nyumbani niliona niwe namtumia kuzunguka naye mitaani akiniongoza barabarani na kunipitisha kwenye majumba kuomba misaada kwa watu” Anasema.
Pia mwandishi wa makala hii alikutana na mama mmoja mwenye umri wa miaka (56) mkazi wa Kihonda Manispaa ya Morogoro (Jina limehifadhiwa) ambaye pia amekuwa akiwatumia wajukuu zake wawili kuomba misaada kwa madai vijana hao hawataki shule hivyo anaona ni bora azunguke nao mitaani ili wapate fedha za kujikimu.
Anasema mama wa watoto hao yupo Dar es Salaam na kwamba hana msaada wowote kwao, hivyo kwa kuwa yeye hana uwezo wa kuwatunza ukizingatia anaishi maisha ya kutegemea misaada, inamlazimu kuzunguka nao mitaani kuomba misaada.
Mama huyo anakiri kwamba kitendo cha kuwatumia wajukuu zake kuzunguka mitaani siyo kizuri kwani kinawajengea watoto hao picha mbaya katika maisha yao.
Pia mtoto mwenye umri wa miaka (10) ambaye amekuwa akitumiwa na wazazi wake kuomba misaada mitaani anasema amekuwa akipita mitaani kuomba misaada hasa siku za Ijumaa akiwa ameambatana na mama yake ikiwa ni pamoja na watu wengine ambao pia ni ombaomba maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Morogoro.
“Natamani na mimi niende shule lakini kutokana na kazi hii ya kuzunguka na mama yangu kuomba misaada kila siku nimeshindwa kwenda shule, pale ninapo waona wenzangu wakienda shule huwa natamani sana na mimi kuvaa sare”Anasema.
Kwa upande wake mzee mwenye umri wa miaka (68) ambaye ni mlemavu, anasema hana ndugu mjini Morogoro, hivyo amekuwa akiwatumia vijana wa mitaani ambao hawasomi kuzunguka kuomba misaada na jioni inapofika humpatia kijana huyo fedha kidogo ikiwa kama shukrani yake kwa kazi aliyoifanya.
Mzee huyo anasema kuwa kitendo cha ombaomba wengi kuwatumia vijana wadogo huwa ni chambo kwani watu wakiwaona huguswa sana na kuwahurumia kwani huona ni familia ambayo inadhiki na kwamba huwafundisha vijana hao maneno ya kusema pale wanapofika kuomba msaada kwa mtu.
“Kabla ya kuingia mtaani kila siku huwa tunawapa shule vijana wanaotusaidia kwani wao ndiyo wasemaji wetu sisi kazi yetu ni kupokea fedha tu na kuzihifadhi, binafsi nashukuru sana kwani vijana hawa wanatusaidia sana” anasema.
Anasema kuwa mbali na kuwatumia vijana hao, wapo baadhi yao ni wezi, wapo wanaochukuwa fedha na pale wanapoona zimekuwa nyingi hutoroka ambapo anasema mbali na kazi hiyo kuwapa ulemavu wa kifikra, pia huwafundisha wizi.
Jamii
Jacob Tito mkazi wa Nanenane Manispaa ya Morogoro anasema kitendo kinachofanywa na watu wenye ulemavu kuwatumia vijana wao kama chambo kuomba mitaani ni kutowatendea haki na pia kinawaharibu kisaiklojia.
Anaongeza kuwa husababisha vijana hao kuwa walemavu kiakili kutokana na kujijengea tabia ya kuishi maisha ya kuomba hivyo kuwafanya kuishi kwa kutegemea misaada hata watakapokuwa watu wazima.
Aidha Tito anaiomba serikali kupiga marufuku kitendo cha wenye ulemavu na wasio walemavu kuwatumia vijana wadogo kama chambo cha kujiingizia kipato kwani kuendelea kufanya hivyo ni kuifanya akili ya vijana hao kudumaa.
Ustawi wa jamii
Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Morogoro Rehema Malemi anakiri kuwepo kwa vijana wengi kutumika kama chambo kwa watu wanaoomba misaada mitaani maarufu kwa jina la “ombaom ba” ambapo amesema suala hilo hali kubaliki hata kidogo.
Anasema kuwa ofisi yake imekuwa ikiwashirikisha wenyeviti wa serikali za mitaa, wazazi na walezi kukemea suala hilo ili kuhakikisha vijana hao wanakwenda shule lakini pia wanajengewa misingi imara ya kujitegemea pale watakapokuwa watu wazima.
“Wapo vijana waliotoka mikoani na kuja hapa Morogoro na kuungana na hawa ombaomba na kutumika kama chambo cha kuwashawishi wasamaria wema kutoa misaada, tumekuwa tukiwakamata na kuwarudisha makwao ”anasema Rehema.
Rehema anasema kitendo cha vijana hao wadogo kutumiwa na ombaomba kunawafanya kutokuwa na akili ya kujishughulisha na kwamba pale watakapokuwa watu wazima hawatakuwa na wazo la kujitegemea ili kujikwamua kiuchumi bali nao watalazimika kuwa ombaomba.
Afisa huyo anatoa wito kwa jamii kushirikiana kwa pamoja kupinga vikali suala hili kwani ni miongoni mwa unyanyasaji na ukatili ambao unamnyima mtoto fursa ya kupata haki zake za msingi ikiwemo elimu na kwamba hali hiyo inamjengea maisha mabaya mtoto huyo siku za usoni.
Sera ya mtoto inasemaje?
Mtoto ni mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka(18), tafsiri hii imetoka na na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto, Mkataba wa Afrika kuhusu Haki na Ustawi wa Mtoto, Sera ya Maendeleo ya Mtoto na Sheria ya Mtoto Na 21 ya mwaka 2009.
Katika umri huu mtoto anahitaji malezi ili aweze kuishi vizuri kushirikishwa, kulindwa na kuendelezwa kiakili kwa ajili ya maisha yake ya baadaye ya utu uzima.
Watoto wana haki za kipekee kwa kuwa umri wao mdogo na hali ya utegemezi, vinaweza kuwafanya wadhulumiwe na kutendewa vitendo vibaya.Watoto wote wana haki sawa bila kujali jinsia, rangi, kabila, dini, hadhi au hali ya afya.
Umoja wa Mataifa, Serikali, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla wana wajibu wa kuhakikisha watoto wanapatiwa haki zao ambapo haki za mtoto zimegawanyika katika makundi makuu manne(4).
Haki ya kuishi inahusu kulinda na kuendeleza uhai wa mtoto ikiwemo kuzuia magonjwa na kupata huduma za matibabu, chanjo na kufuatilia ukuaji, lishe bora, mavazi yanayositiri, makazi salama, maji safi na salama na usafi wa aina zote.
Comments