top of page

Ndoto zaidi ya pesa.

Updated: Apr 17


"Ukitaka kufanikiwa katika jambo lolote lile kwanza ulipende na uwe na maamuzi ya kuthubutu" Yusuph Daniel


Na Mwinjilist Elisa Kaimukilwa


Katika maisha ndoto ni dira aliyonayo mtu inayomuongoza na kumuwezesha kufikia malengo yake, mara nyingi ndoto humfanya mtu kujiwekea misingi imara itakayomuwezesha kufikia malengo hayo.


Ndoto hubeba utashi, maumivu, mapenzi au matamanio kwa mwanadamu, humfanya mtu aamini kuwa bila kuifikia ndoto hiyo hakuna kingine kinachoweza kuziba pengo lake.


Kijana Yusufu Daniel Harish miaka 34 ni mkazi wa kijiji Butailuka kata Maruku wilaya ya Bukoba mkoani Kagera ni miongoni mwa vijana wenye ndoto kubwa za kimaisha, amebeba imani na dhamira pana kuhakikisha ndoto yake ya kuishangaza Tanzania na Dunia kwa ujumla ya kujenga meli inatimia.


Kijana huyu chotara mwenye asili ya Tanzania na India baba yake mzazi ni Harish Batt raia wa India na mama yake ni Mariam Kalikwela Balozi mzaliwa wa Bukoba Kagera ni kitinda mimba kwenye familia ya watoto wanne, wavulana watatu na msichana mmoja ambaye amefariki.


Yusufu amedhihirisha dhamira ya kujenga meli baada ya kulazimika kuacha kazi nzuri iliyokuwa ikimuingizia kipato na maisha mazuri ya kuendesha magari kwenda nje ya nchi na kuamua kurejea darasani akiamini ameiacha njia ya ndoto yake.


Kijana Yusufu anasema ameanza kuwa na ndoto ya kujenga meli akiwa na mdogo sana lakini kutokana na changamoto za kimaisha hakuwa na njia ya moja kwa moja ya kuendeleza ndoto yake ambapo alilazimika kujiunga na chuo cha udereva baada ya kuhitimu kidato cha nne.


Alijiunga na chuo cha udereva cha Lake zone Driving school kilichoko Bukoba pamoja na chuo cha VETA Kagera na kupata cheti cha udereva na baada ya hapo aliamua kurejea nyumbani kufanya vibarua ili kukusanya pesa ya kujiendeleza katika chuo cha usafirishaji NIT Dar Es Salaam.


Baadhi ya kazi alizozifanya ni pamoja na kuchoma mkaa, kuponda kokoto, kufyatua matofali, kuosha pikipiki na magari na hata kuwa kibarua katika shuguli za ujenzi anasema hakubagua kazi iliyokuja mbele yake kwani nia yake ilikuwa ni kuhakikisha anapata pesa ya kuendelea na masomo.


“Jitihada zangu zilizaa matunda niliweza kupata pesa za kwenda kuchukua masomo katika chuo cha NIT na nilipohitimu nilitunukiwa lesseni ya daraja la juu” alisema Yusufu.


Baada ya kuhitimu alibahatika kufanya kazi ya udereva na makampuni mbalimbali makubwa nchini likiwemo la Damas group iliyoko Dodoma, Simba Track ya Arusha, King Road ya Dar es saalam una Class Tour ya Zanzibar, na kupitia kazi hiyo ameweza kufika nchi tofauti tofauti za Afrika ya Mashariki na kati lakini wakati akiendelea na kazi hiyo bado hakusahau ndoto yake ya kujenga meli.


“Nakumbuka ilikuwa siku yaAlhamisimwaka 2022 ndipo niliamua kuacha kazi ya udereva ili nirejee kwenye msingi wa ndoto yangu, sikuwa na mgogoro wala kesi na kampuni niliyokuwa naifanyia kazi niliaga kwa uungwana kabisa na kupewa baraka zote”


“Wakati nikiacha kazi sikuwa na ramani ya pakuanzia maana zilihitajika pesa nyingi lakini pia sikuwa na uwezeshwaji wa kimawazo wa namna ya kuweza kutimiza ndoto hiyo kutoka kwa mshauri mwenye utaalam na eneo hilo” alisemaYusuph.


Anasema ilimchukua muda mrefu kuwaza kwa jinsi gani atayafikia malengo yake na wakati huo akiwa kijijini kwao na kwamba kipindi hicho alimpoteza mshauri wake wakaribu, dada yake wa kuzaliwa Zurufa Harish aliyekuwa akimtia moyo na mawazo ya kufikia ndoto yake licha ya kuwa na taaluma tofauti na ya ndoto yake (taaluma ya utalii).


“Baada ya dada yangu kufariki niliiona ndoto yangu imefikia ukomo maana nilimtegemea sana na muda mwingine alikuwa akiniwezesha kifedha lakini bado nikawa na imani maana ukitaka kufanikiwa katika jambo lolote lile kwanza ulipende na uwe na maamuzi ya kuthubutu” anaeleza Yusufu.


Ukitaka kufanikiwa katika jambo lolote lile kwanza ulipende na uwe na maamuzi ya kuthubutu

Anasema wakati akiwa kijijini kwao akitafakari juu ya namna gani ataweza kuifikia ndoto yake, mwezi Januari mwaka 2023 akitazama taarifa ya habari kwenye moja ya chombo cha habari akaiona habari kutoka ofisi ya waziri mkuu, kupitia program ya kazi, ajira, vijana na wenye ulemavu inayotoa fursa ya vijana wabunifu kujiunga na vyuo vya ufundi.


“Hakika nilipoliona tangazo hilo nikajisemea moyoni kuwa Mwenyezi Mungu amefungua mlango wa kutimiza ndoto yangu nikaanza mchakato wa kutuma maombi na Mungu si athumanni kachaguliwa kujiunga na chuo cha Kashozi Vocational Training Center (KVTC) Mei 15 mwaka2023.


Maisha ya kuiendeza ndoto yake yakaanza kwa kijana Yusufu Daniel Harish na akiwa chuoni hapo akachukua kozi ya uchomeleaji.


Sr Anatoria Vicent mkuu wa chuo hicho anasema kijana Yusuph ni miongoni mwa vijana 193 katiya 700 waliochaguliwa kujiunga na chuo hicho baada ya kutuma maombi.


Anasema mwanzoni alijua kijanaYusuph hawezi kuendana na mazingira na shughuli za ufundi kutokana na mwonekano na asili yake lakini aliwashangaza wengi kutokana na kuwa mchapa kazi, mwenye kujiamini, mnyenyekevu na mwenye kujitolea na kwa ujumla alionekana kuwa mwenye maono ya hali ya juu.


“Yusuph alikuwa darasa tosha kwa wenzake maana hakuwa na muda wa kupumzika mara nyingi ungemkuta akidadisi mambo mbalimbali hasa suala la meli na alikaa na walimu kwa karibu akiwahoji masuala mbalimbali” anasema Sr Anatoria.


Bw. Nemesius Mwesiga Slivery ambaye ni mwalimu kiongozi wa Yusuph katika fani ya fani ya uchomeleaji chuo cha KVTC, anasema kijana huyo alikuwa na uwezo wa kipekee na alipomshirikisha juu ya ndoto yake ya kujenga meli, alifikiri hawezi kwa sababu aliona anachokiwaza ni kitu kikubwa .


ree

“Baada ya kuanza chuo alikaa na wanafunzi wenzake kwa wiki mbili tu baadae aliomba apewe chumba chake, mwanzo ni sikuelewa kusudio lake lakini baadae niligundua kwamba hakuwa na muda wa kucheza, alifanya shughuli za chuo kwa haraka na kwa ufanisi”anasema Mwesiga.


Ametaja sifa za kijana huyo kuwa ni mwenye kujaribu mambo mengi, mtiifu, mwepesi wa kuomba msamaha anapokosea, alikuwa wa kujishusha kwa kila mtu na kwamba kwa ujumla alikuwa tofauti na alivyofikiriwa wakati anakuja.


Anasema alionesha ubunifu kwa kila kazi aliyoifanya kama kuchomelea na kusanifu milango na madirisha na wakati mwingine kuelekezana kuwa mshauri mkuu kwa vijana wote wa chuo.


Anasema siku moja alimuomba mwalimu huyo amtengenezee meza ili awe nayo chumbani kwake lakini cha kushangaza mwezi mmoja baada ya kukabidhiwa meza hiyo alimuita yeye na mkuu wa chuo chumbani kwake na kuwaonyesha mfano wa meli aliyoiandaa kwa maboksi ambayo hawakujua alikoyapata.


Asema kuwa aliwaomba vipande vya vyuma na mabati vilivyo kuwa vinabaki iliatengeneze mfano wa Meli kwa vyuma.


“Mbali na kushangazwa na ubunifu wake pia tulijiuliza alipataje muda wa kutengeneza mfano huo wa meli wakati hakuwahi kukosa ratiba yoyote ya shule, lakini tuligundua kuwa anatumia muda wa kupumzika kufanya shughuli zake kama hizo” alisema Mwesiga.


Anasema baada ya masomo ilibidi chuo kihangaike kumtafutia sehemu ya kufanyia mazoezi ya kazi ambayo itakuwa rahisi kuendeleza na kutimiza ndoto zake.


Anaongeza kuwa Yusuph kwa sasa yuko Mwanza katika kampuni ya Songoro Marine ambapo anashiriki katika ujenzi wa meli na vivuko na baada ya muda wa mazoezi kuisha amemshauri abaki huko ili aendelee kupata ujuzi zaidi.


Geofrey Anacreth  mmoja wa wanafunzi waliosoma na Yusuph katika chuo cha Kashozi anadai kuvutiwa na ubunifu, utayari, ushirikiano na upendo aliokuwepo nao Yusuph na kwamba wanafunzi walijivunia kuwa naye.


“Yusuph alikuwa akija na wazo la ubunifu na ukiliweka katika uhalisia unapata picha nzuri na ya kuvutia alipoulizwa swali alikuwa mwepesi wa kusaidia tena kwa vitendo hakuwa mchoyo kwa kweli” anasema Geofrey.


Godwin Tizangana na Alphonce Mutakya walipata kuishi na kukaa pamoja na Yusufu wanase mauwepo wa Yusuph chuo ni hapo uliwafanya wanafunzi wengi kujituma zaidi katika fani zao wakiamini alisaidia kuongeza ushindani na kusababisha wanafunzi wengine wafikirie zaidi kufanya kilicho bora.


Katika kuipambania ndoto yakehiyo Kijana Yusuph amepitia magumu na muda mwingine kukatishwa tama na jamii inayomzunguka.


Mariamu KalikwelaBalozimama mzaziwakijana Yusufu, anasema tangu utotoni Yusuph alikuwa akifanya vitu vingi vya aina mbalimbali hali iliyowafanya kumuona msumbufu wa hali ya juu ukilinganisha na wakubwa zake.


“Kijana wangu huyu ni mpambanaji sana amefanya kazi nyingi ambazo jamii haikutegemea azifanye katika makuzi yake ikiwemo kufyatua matofari, kuponda kokoto,  kuosha magari, kuchoma mkaa lakini pia amekuwa mfanyabiashara wa tende” Anasema mariam.


Anasema baada ya kuweka bayana nia yake ya kujenga meli mara nyingi amekuwa ni mtu wa kujitenga na kukaa sehemu tulivu, alipenda kujifungia chumbani na hali hiyo ilinipa wasiwasi lakini baada ya muda alikuwa akinionesha mambo aliyokuwa akiyafanya ikiwemo kujenga meli.


Anasema licha ya kutokuwa na uwezo wowote wa kumsaidia kufikia ndoto hiyo amekuwa akimtia moyo na kumuaminisha kuwa kupitia upambanaji wake atatimiza ndoto hiyo.


“Naishukuru serikali na wadau wote wanaomsaidia kufanikisha ndoto yake natamani baba yake angemuona bila shaka angekuwa msaada mkubwa kwake” anasema Mariam

Yusuph aliyempoteza baba yake mzazi akiwa na miaka mitatu kwa ajali ya gari huko kwenye nchi za umoja wa falme za Kiarabu (Dubai).


k
k

Kijana Yusufu ni mfano halisi wa mtoto aliyeyaishi maelekeo yake kama ambavyo yamekuwa yakionesha kwenye kipengele cha mbinuna falsafa za Dkt Maria Montessori yanayoelezwa na Jacqueline Mwombeki akisisitiza watoto kupewe nafasi ya kuyaishi maelekeo yaliyo mazuri ikiwa ni pamoja na kuweke wa mazingira wezeshi.


Licha ya mama yakeYusuph kubaini kuwa kijana wake ni mtundu tangu utotoni hakumzuia na badala yake alimuwekea usimamizi wa kuhakikisha anachokifanya hakimuathiri kitabia, kimwili nakiakili.


Kwa mwenendo huu iwapo Yusuph atafikia ndoto yake basi atatuma salama kwa wazazi kutakiwa kujua vipawa walivyonavyo watoto wao tangu utotoni na kujua namna ya kuwawezesha ili kufikia ndoto zao.


Hakika hawa ni vijana wanaotakiwa kusaidiwa na kuendelezwa kupitia wadau ikiwemo serikali kupitia taasisi zake za uendelezaji wa vipaji na bunifu mbalimbali ikiwemo COSTECH na SIDO n.k.


Huenda wapo vijana wengi wenye uwezo mkubwa wa kubuni na kuwa na ndoto kubwa ambazo zikipatiwa usaidizi zinaweza kuwa mwazo mzuri wa maisha yao, jamii na taifa kwa ujumla hivyo kupiga hatua kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia na mwisho wa siku kuinua uchumi.



Comments


bottom of page