top of page

Mfanano wa maisha ya nyuki na binadamu

Updated: Mar 15


Nyuki wana mgawanyo wa majukimu sawa na binadamu.
Nyuki wana mgawanyo wa majukimu sawa na binadamu.

Na Mwinjilisti Elisa Kaimukilwa


“Fuata Nyuki ule asali”, Ni msemo uliozoeleka sana kutokana na tabia ya Nyuki kutengeneza asali tamu inayotumika kama chakula na dawa.


Nyuki wamekuwa na faida kadhaa kwa binadamu kutokana na kuzalisha

 asali, nta, gundi, sumu na chavua ,bidhaa ambazo zimekuwa zikitumika na binadamu na kumpatia kipato.

 

Kiikolojia ya mazingira (bionuwai) ambayo husaidia uimarishaji mzuri wa miti, Nyuki husaidia kutunza mazingira kwa sababu  sehemu ambayo ina mizinga haitachomwa moto hovyo hovyo kwa sababu italindwa ipasavyo.


Mfumo wao wa maisha

Nyuki ni wadudu ambao mfumo wao wa maisha unalinganishwa na mfumo wa maisha ya binadamu kama jamii inayoishi pamoja.

 

Kama tutakavyoweza kuona ni kwamba Nyuki huishi katika eneo la pamoja ambalo huitwa koloni (mzinga) yaani mahala ambapo hufanya shughuli zao.

 

Lakini kutokana na wingi wao ,Nyuki huwa na uongozi  lakini pia wameweza kugawana majukumu yao ya kila siku.

 

Utaona kila kundi linatakiwa kufanya kazi fulani ili kutimiza malengo yao ambayo ni uzalishaji wa asali .Ni sawa na maisha ya kila siku ya binadamu ambapo kuna uongozi ambao unawajibu wa kuhakikisha masuala yote ya uzalishaji mali pamoja na kusimamia  usalama ndani ya eneo la utawala .

 

Nyuki wana jeshi lao (askari ) ambao hawa kazi yao ni kuhakikisha wanalinda  koloni pamoja na malkia ambaye ndiye kiongozi wa nyuki wote katika koloni ni sawa na kusema kiongozi katika nchi ambaye ni lazima alindwe.

 

Tofauti kubwa kati ya nyuki na binadamu ni kwamba nyuki wao kila mmoja hutimiza majukumu yake bila ya kusukumwa ama kuwekewa uangalizi fulani wakati wa utendaji kazi wake .

 

Nyuki wanapopangiwa kufanya kazi fulani basi huifanya kwa moyo wake wote,nyuki haundiwi tume wala timu ya kumfuatilia hata pale anapoonekana majukumu yameanza kumshinda aidha kutokana na umri ama vinginevyo basi huandaliwa nyuki mwingine kwa ajili ya kutimiza majukumu hayo na yeye huondolewa!

 

Sasa ingia ndani zaidi uone jinsi tabia za mdudu huyu zinavyoakisi maisha ya kila siku ya mwanadamu.

 

   Maisha ya nyuki.

Wadudu hawa ni kama viumbe vingine yaani kuna jike na dume, nyuki anaishi kuanzia siku 36-120, lakini katika kipindi cha kiangazi hufa sana kutokana na uhaba wa maji na chakula.


  Nyuki jike.        

Kuna aina mbili za majike, Malkia na jike tasa.


  Malkia na sifa zake: huyu ndiye kiongozi mkuu wa kundi, maana ndiye anauwezo wa kutaga mayai, ana umbo kubwa kuliko wengine hii ni kwa nyuki wote wanaouma na wasiouma, hutoa majukumu katika kundi, hutoa harufu pamoja na ishara  mbalimbali kwenye kundi lake ili kutahadharisha, mfano kupungua kwa chakula, kuingiliwa na maadui n.k.


  Anauwezo wa kutaga mayai 1,500 – 2,000 kwa siku lakini itategemea na wingi na ubora wa chakula kwa msimu huo.


 Anaishi muda mrefu zaidi ya miaka mitatu kuliko nyuki wengine, huandaliwa chakula maalum ambacho kinakuwa na uangalizi wa hali juu na ulinzi mkali.


 Upatikanaji wake: Huandaliwa tangu akiwa yai kwa kutengenezewa nyumba yake kubwa kuliko mayai mengine, hunyweshwa maziwa ya nyuki tangu anapoanguliwa.


Upandwaji wake: Hupandwa mara moja katika maisha yake yote, hupandwa na dume mmoja ambaye anakuwa na mbio kuliko wote maana akijisikia kupandwa hutoa harufu inayotoa ishara ya kutaka kupandwa na si kwa madume walio katika mzinga wake tu, hata na madume jirani uhusika katika  shughuli hiyo, malkia hutoka mbio huku akifuatwa na wingi wa madume, huruka umbali wa zaidi ya kilometa nne mpaka tano na hupandwa huko huko  juu.


 Ajabu: Wakati wa kurudi hawezi kukosea mzinga wake, hutunza mayai hayo tumboni mwake kipindi chote cha maisha yake, dume atakayefanikiwa kumpanda hufanya shuguli hiyo mara moja tu na akimaliza ,sharti afe.


Mwisho wa maisha ya malkia.

Pindi anapoonekana kukosa nguvu na kuacha kutaga mayai na kushindwa kabisa  kusimamia kundi kwa kuacha  kutoa ishara za ulinzi, nyuki huanza kumuandaa malkia mwingine kwa siri kubwa maana malkia wawili hawakai pamoja.


  Baada ya malkia mpya kukua humwendea yule mzee na kupigana naye mpaka amuue ndipo huyu huanza utawala wake. Lakini malkia mzee akigundua kuwa kuna mwingine anaandaliwa, hutoka na kufika katika yai lile na kulichoma kwa mdomo wake ili afe kusudi aendelee kutawala hata kama hana nguvu.


   Jike tasa: Hawa huitwa vibarua ndio wanahusika zaidi katika huduma mbalimbali ikiwemo kuangalia maeneo ambayo yana chakula, hutafuta chakula na kuwatunza wengine, hutoa ulinzi na kwa kawaida nyuki hawa  huwa na mshale mmoja tu na akiishautoa naye hufa.


  Kazi hizi huzifanya kulingana na umri wake,umri unapoongezeka hulazimika   kuacha baadhi ya kazi kadiri  anavyokuwa hadi maisha yake yanapokoma.


    Aina na kazi za nyuki.

Nyuki wana mgawanyo wa majukimu sawa na binadamu.


 Kila nyuki tofauti na malkia akizaliwa hupitia katika shuguli mbalimbali mfano  kutengeneza masega ya asali, kuwa skauti, kutoa taarifa za chakula na mwisho huanza kutafuta chakula na ndiyo kazi ya mwisho kulingana na muda wa kuishi.


 Walinzi: Huangalia na kuhakikisha usalama wa kundi ili lisiingiliwe na adui yeyote.

 Mlisha kundi (foleja) : Kutunza kundi kwa chakula kizuri na cha kuweza kuzalisha asali nzuri pia  kuhakikisha ghala linakuwa na  chakula cha kutosha.


 Skauti: Ni nyuki ambao hutumika kutafuta maeneo ambayo chakula kinapatikana na kurudi kutoa taarifa wakiwa na kiasi kidogo cha aina ya chakula kilichopatikana katika eneo ambalo ameenda kufanya utafiti, kisha wahusika huondoka katika  kundi kubwa kwenda katika eneo hilo kukichukua.


 Yule aliyeleta taarifa haendi nao kwa ajili ya kuwapeleka bali hutoa ishara, wakati wa kutoa taarifa hizo hucheza muziki aina ya Waggle dance na Raund dance ambao huashiria yafuatayo:- umbali wa chakula kilipo, mahali ambapo chakula kizuri kinapatikana yaani kama ni Magharibi, Mashariki, Kusini, na Kasikazini, shughuli hii ya utafiti wa chakula hufanyika asubuhi na mapema.


 Waggle dance ni muziki unaoashiria kuwa chakula kiko mbali sana na Raund dance ni mziki unao toa ishara ya chakula kuwa kipo katika mazingira ya karibu.


Nyuki wote hasa madume uhusika kwa kuleta joto wakati wa baridi na kuleta ubaridi wakati wa joto.


Maadui wa nyuki.

Maadui wapo wengi lakini hawa ni baadhi, adui wa kwanza ambaye ana athari kubwa ni binadamu maana huiba mizinga, kuchoma moto, kuua nyuki kwa madawa, kurina asali na kuharibu mazingira, siafu au sisimizi, mijusi hawa hula nyuki, Nyegere ni mnyama hodari sana maana haogopi  ni jasiri na huwa hakati tamaa yeye hula asali.


 Simba wa nyuki ni mdudu ambaye anafanana na nyuki ila yeye ana umbo kubwa na nguvu kuliko nyuki wafugwao, baada ya kumkamata nyuki hunyonya damu na maji mwilini mwa nyuki mpaka kumsababishia kifo.

Comments


bottom of page