top of page

Maisha na utume wa Dkt. Askofu Mushemba

Updated: Apr 17


Dkt.Askofu Samson Mushemba
Dkt.Askofu Samson Mushemba

Na Anord Kailembo.


Askofu Dkt. Samson Mushemba alikuwa mzaliwa wa mkoa wa Kagera kwenye ukoo wa “Abasingo” alizaliwa juni 30 mwaka 1936 katika kijiji cha Rwanda kata ya Ibuga tarafa ya Kamachumu iliyoko wilayani Muleba.


Askofu Dkt. Mushemba ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto watano wa Bw. Gauline Mushemba na Bi.Mamelita Ntundano ambaoni Helena Tibela, Anamelida Mukabalimu, Amida Kilungo, Felix Mjungu na yeye mwenyewe, wazazi wake walikuwa wakulima.


Akiwa hai aliwahi kusimulia kuwa wakati akizaliwa wazazi wake walikuwa hawajawa wakristo kutokana na kipindi hicho injili kuwa haijapenya hama kuenea kwa watu wengi licha ya kwamba ndugu zake walikuwa tayari wamebatizwa katika kanisa la Kirumi yaani Roman Catholic ambalo wamissionari wake walikuwa wamekwisha tangulia kueneza ujumbe wa injili miaka 20 kabla ya kuingia kwa madhehebu ya kipentekoste.


Naye alibatizwa mwaka 1947 na miaka 2 baadaye kupata kipaimara mwaka 1949, aliamini kupata sakramenti ya ubatizo na kipaimara zilimuingizachini ya utawala wa Mwenyezi Mungu na aliyempatia sakramenti hizo ni mchungaji Yeremia Nkongo huku mdhamini wake katika ubatizo akiwa Mzee Zakaria Bukende.


ELIMU

Askofu Dkt. Mushemba alikuwa ni mmoja wa watoto wachache kwenye kijiji cha Rwanda waliopata bahati ya kwenda shule, Mzee mmoja aliyekuwa rafiki wa baba yake aliyefanya kazi na wamissionari Bukoba alimsihi sana baba yake ampeleke shule ya msingi ya Ndolage iliyokuwa imeanzishwa na  wamissionari wa Kijerumani walioitwa Walutheli iliyokuwa kilometa 10 kutoka kijijini kwao.


Anasema baba yake alikubali na wakati huo walikuwa watoto wawili kutoka kijijini kwao waliopata nafasi ya kwenda shuleni hapo na mwenzake alikuwa Jonathan Byakuzana na uchache wao ulitokana na watu wengi kijijini humo kutokuelewa sawa sawa suala la elimu.


Mapokeo ya jamii juu ya Mushemba kwenda shule hayakuwa mazuri kwani baadhi ya wanakijiji walilaumu sana, baadhi ya marafiki wa baba yake walimtaka aache shule na kumsaidia kuchunga mifugo lakini kutokana na kwamba alipenda shule akafanikiwa kumshawishi baba yake aendelee na masomo.


Alifanikiwa kuhitimu masomo ya shule ya msingi mwaka 1950 shule ya msingi Ndolage na mwanzoni mwa mwaka 1951 alijiunga na elimu ya kati (Middle school) huko Kigarama, Kanyigo wilayani Missenyi na baada ya miaka miwili alichaguliwa kusomea ualimu katika chuo cha ualimu huko Kigarama na mwaka mmoja na nusu baadaye chuo hicho kiliunganishwa na chuo cha ualimu Katoke kilichoko wilayani Muleba na kuhitimu mwaka 1954.


Ualimu ilikuwa fani yake ya kwanza na ndiyo huduma ya kimissionari aliyoanza nayo, alipata kufundisha sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi, baadhi ya shule alizofundisha ni pamoja na shule ya msingi Bukondo iliyoko Ukerewe mwaka 1955 – 1956.


Mwaka 1957 alifundisha shule ya msingi Platio na shule ya msingi ya kati (Intermidiate school) katika wilaya ya Eldoret nchini Kenya, kazi hiyo ya ualimu aliifanya kwa miaka mitatu na wakati akiwa mwalimu alikuwa akifanya shughuli za uinjilishaji.


Kutokana na kupenda sana kazi ya uinjilishaji Askofu Dkt. Mushemba alianza masomo yake ya elimu ya theolojia mnamo mwaka 1958,ikiwa mwanzo wa maandalizi ya huduma ya uchungaji katika chuo cha elimu ya theolojia Makumira Arusha kipindi hicho kikiitwa Makumila Lutheran Theological Collage na kwa sasa kinajulikana kama chuo kikuu cha Tumaini, Makumira (Tumaini University Makumira).


Askofu Dkt. Mushemba hakuridhika na elimu ya cheti katika ngazi ya theolojia, alihamasika kuendelea kujiimarisha katika kukuza ufahamu, uelewa na kuwa na upeo wa juu katika elimu ya imani na kanisa na hali hii ilichochewa zaidi na viongozi wake akiwemo Askofu Josiah Kibira aliyemuhimiza kujiendeleza kimasomo kutokana na kuona kipawa alichokuwa nacho Dkt. Mushemba.


Alirejea Makumira mnamo julai1977 hadi june mwaka 1979 ndipo alipofuzu shahada yake ya kwanza ya theolojia (Bachelor of theology) na mnamo june 1981 hadi julai 1984 alipata nafasi ya kwenda Marekani kwa masomo ya juu zaidi katika chuo cha Luther North Western Theological Seminary na kufuzu shahada ya pili ya theolojia (Master of theology M.T) na katika chuo hicho hicho ndipo alipohitimu na kupewa shahada ya juu zaidi ya udaktari katika utumishi wa Uchungaji (Shahada ya uzamivu).


Utume na utumishi wake

Askofu Dkt. Mushemba katika maisha yake amebarikiwa kushika nafasi mbalimbali ndani na nje ya nchi katika kulitumikia kanisa la kiinjili la kirutheli Tanzania.


Baada ya kuhitimu masomo ya theolojia ngazi ya cheti mwaka 1961 ndipo alipo barikiwa katika huduma ya uchungaji, na alipata daraja hilo kutoka kwa askofu wa kwanza wa kanisa la kiiinjili la kiruteli Tanzania Dayosisi ya Kasikazini Magharibi ambaye alikuwa mmisionari kutoka Sweden Askofu Profesa Bengt Sundkler mnamo desemba 31 mwaka 1961.


Askofu Sundikiler anakumbukwa sana katika historia ya Dayosisi ya kaskazini magharibi na kukumbukwa kwake kunatokana na kuweka misingi imara ya mfumo unaoendelea kuongoza Dayosisi ya kasikazini Magharibi pamoja na kulisaidia kanisa kuona umuhimu wa kujiamini, kujitegemea na alikuwa na mtazamo wa kuamini na kuthamini mchango wa viongozi wenyeji.


Baada ya kupata uchungaji alipangwa rasmi kuanza huduma katika usharika wa Lukajange wilayani Karagwe, alihudumu katika usharika huo miaka mitatu hadi mwaka 1963.


Mwaka 1964 aliteuliwa na halmashauri ya Dayosisi kuwa mchungaji wa jimbo la Bweranyange wilayani Karagwe na mwaka mmoja baadaye Januari 1965 aliteuliwa tena kuwa mchungaji wa vijana kwenye dayosisi nzima wakati huo aliishi Bukoba yalipo makao makuu ya Dayosisi hadi april 1966.


Mwezi Aprili mwaka 1966 hadi Aprili mwaka 1968 alienda Glossalmerode Ujerumani kwa ajili ya kupata mafunzo ya uinjilisti kwa vijana akiwa pamoja na vijana wengine kutoka mataifa mbalimbali ya Ujerumani, Uingereza, Uganda na India.


Aliporejea nchini akaendelea kuwa mchungaji wa jimbo la Bweranyange Karagwe mwaka 1968 hadi mwaka 1970 na mwaka uliofuata wa 1971 akawa katibu wa uwakili KKKT/DKMG, mwaka 1972 akawa mkuu wa shule ya walimu wa elimu ya kikristo na mnamo mwaka 1972 hadi mwaka 1977 akachaguliwa kuwa msaidizi wa Askofu KKKT/DKMG.


Mwezi Julai mwaka 1979 hadi mwaka 1981 akawa mchungaji wa usharika Ndolage Muleba na tangu 1984 hadi 2000 alitumika akiwa Askofu wa KKKT Dayosisi ya kaskazini Magharibi.

Akiwa Askofu, pia alishika nyazifa mbalimbali za uongozi ndani na nje ya dayosisi yake:


Mwaka 1990 -2000 alikuwa mwenyekiti wa ustawishaji wa bonde la mto Ngono mkoani Kagera, kuanzia julai 1992 hadi 2007 alitumika akiwa mkuu wa kanisa la kiinjili la kilutheli Tanzania na pia kwa kipindi hicho cha 1992-2007 alitumika akiwa makamu wa pili mwenyekiti wa jumuhiya ya kikiristo Tanzania


Mnamo julai 1996 hadi 2001 alitumika akiwa makamu wa kwanza mwenyekiti wa CCT, Julai 2001 – june 2005 akawa mwenyekiti wa CCT, mwaka 1994 hadi 2007 alitumika akiwa mwenyekiti wa mashirika ya msamaria mwema Tanzania, mwaka 1997 hadi 2007 alikuwa mkuu wa chuo kikuu cha Tumaini Makumira, mnamo mwaka 1992 – 2007 alitumika akiwa mjumbe wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheli Duniani (FMKD) Geniva Uswiz, mjumbe wa kamati ya utendaji wa fungamano ya kanisa la kilutheri Duniani.


Pia alifanya kazi akiwa mwenyekiti, kamati ya maafa Duniani ya FMKD, mwaka 2005 – 2007 alikuwa mwanzilishi na mjumbe kamati ya amani ya wakristo na waislam Tanzania, mwaka 2005 – 2007 alikuwa mjumbe wa umoja wa vyuo vikuu Afrika mashariki na pia mjumbe wa bodi ya shule ya sekondari Nyakato, shule ya sekondari ya kwanza kuanzishwa mkoani Kagera na amekuwa mwenyekiti wa Mushemba foundation tangu mwaka 2010.


Kipawa cha uongozi wa Askofu Dkt. Mushemba hakikuanza mara tu alipokuwa mchungaji bali wakati akiwa mwanafunzi wa chuo cha Makumira, wanachuo wenzake walimuona na mwaka 1978 – 1979 wakamchagua kuwa mzee wa chuo, bila shaka uongozi chuoni hapo ulimuandaa, pengine yeye bila kujua atakuja kuwa kiongozi mkubwa wa kiroho.


Licha ya kuwa msomi na kiongozi mkubwa wa kidini Askofu Dkt. Mushemba alikuwa akijishusha, kipawa ambacho pengine siyo kila msomi au kiongozi wa namna yake anaweza kuwa nacho.


Askofu Dkt. Mushemba katika maisha yake ya utume alijivunia kuimarika kwa shirika la Msamaria Mwema– KCMC (Kilimanjaro Christian Medical Centre) wakati akiwa mwenyekiti wa KCMC huduma ziliimarishwa lakini pia miradi mingi ilizinduliwa kuimarisha shirika hilo.


Alijivunia kuona anafanikisha uanzishwaji wa chuo kikuu ambacho kwa sasa kinaitwa Tumaini University.


Dkt. Mushemba amefariki Dunia Aprili 10 mwaka 2020 akiwa na umri wa miaka 85 katika hospitali ya Ndolage iliyoko mkoani Kagera na kuzikwa katika kanisa kuu la Kiinjili la Kilutheli Tanzania KKKT Dayosisi ya Kazikazini Magharibi.


Askofu Dkt. Samson Mushemba alioa mwanamke mmoja Bi,Feliciana Mushemba naye amefariki mwaka mmoja na nusu ulipita na alizaa naye watoto 8 na kati ambapo watoto 7 wako hai na mmoja amefariki Dunia.


Kupitia historia yake hii tunayo mengi ya kujifunza kwanza ikiwemo kutokukatisha ndoto za watoto maana kama baba yake angewasikiliza wanakijiji waliofika kumshauri Askofu Mushemba kuachana na masomo na kubaki kumsaidia kulima na kuchunga mifungo bila shaka asingefikia hatua hii.


Aidha anatufundisha kuwa tunapoaminiwa basi tuaminike na kuwa wenye uadilifu, katika maisha yake tangu amekuwa mwalimu wa shule ya msingi amekuwa wa kujitoa na kupelekwa kila sehemu kuongoza hii ni kwa sababu alikuwa akijituma, mwenye uadilifu na kuaminika kwa viongozi wake ndiyo maana alifanikiwa.


Maisha ya Askofu Dkt. Mushemba Duniani yakawe funzo kwetu katika kutoa huduma na kufikia malengo tuliyojiwekea.



Comments


bottom of page