top of page

Fukwe tiba ya msongo wa mawazo, iache salama

Updated: Apr 17


Kabuhara Beach
Kabuhara Beach

“Jukumu la ulinzi wa mazingira lipo mikononi mwako”


Na Restuta Damian

Ufukwe ni sehemu ya ardhi iliyo kando mwa ziwa, Bahari, au mto, mara nyingi sehemu hizi huwa na mchanga, kokoto na mawe, ufukwe uvutia zaidi inapoungana na mazingira mengine yanayozunguka maeneo hayo ikiwemo hewa, maji na mimea yaani muonekano mzima wa jografia.


Muunganiko wa mazingira hayo yenye utulivu, uvutia zaidi na kufanya viumbe akiwemo mwanadamu kutembelea maeneo hayo kwa ajili ya kupumzika, kufanya mazungumzo na kuogelea.


Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizobarikiwa kuwa na fukwe nyingi zitokanazo na uwepo wa vyanzo vingi vya maji hasa maziwa na bahari miongoni mwake ni bahari ya Hindi, ziwa Victoria, ziwa Nyasa, ziwa Tanganyika na ziwa Brigi, maziwa haya na mengine mengi yanazungukwa na fukwe.


Kutokana na kuvutia kwa fukwe serikali na wadau mbalimbali wakiwemo wa utalii wamekuwa wakifanya uwekezaji unaolenga kuzihifadhi sambamba na kuchangia upatikanaji wa kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.


Bahari na maziwa yaliyopo Tanzania yamekuwa yakiwasukuma hata watu kutoka mataifa mbalimbali Duniani kufika kwa ajili ya kutalii na hivyo kuchangia pato la taifa kwa kuingiza fedha za kigeni, lakini pia kulipia baadhi ya huduma muhimu kipindi chote wanachokuwepo nchini.


Fukwe kama yaliyo maeneo mengine zinahitaji kulindwa kwa kuhifadhiwa ili kuachwa kwenye uasili wake sambamba na kuvutia zaidi, kuendelea kushawishi kwa kuwafanya watu kuzitembelea.


Licha ya fukwe kuwa na faida mbalimbali kwa mwanadamu, bado wapo baadhi ya watu ambao wameshindwa kuziheshimu kwa kuzilinda na kuzihifadhi, baadhi yao wamekuwa wakifanya uchafuzi ikiwemo utupwaji holela wa chupa za plastiki na vifungashio vya bidhaa za vyakula na muda mwingine bila kuona aibu.



Swali la kujiuliza ni Je, kwa nini tunashindwa kuzilinda fukwe hizi dhidhi ya uchafuzi?

Nikiwa katika ufukwe za ziwa Victoria manispaa ya Bukoba nimekutana na baadhi ya wananchi wa mji huo akiwemo, Anitha Justinian mkazi wa kata Bakoba anasema kila wiki lazima afike eneo la fukwe(beach)akiwa na marafki zake kupumzika na kufanya mazungumzo mbalimbali ili kuongeza furaha kwenye maisha yake.


Anasema awapo eneo la fukwe utumia masaa mawili hadi matatu lakini hakai bure lazima awe amebeba vyakula (mapochopocho) au vinywaji ili afurahie  na marafiki zake ambao anakuwa ameambatana nao.


Anaeleza kuwa, suala la elimu ya mazingira alifundishwa shuleni miaka mitatu iliyopita, lakini baada ya kuhitimu na kurudi kwenye jamii amejikuta anabadilisha mtazamo wa usafi wa mazingira akilinganisha na alipokuwa shule.


Anasema licha ya kwenda na vyakula na vinywaji ufukweni amekuwa hakumbuki kuchukua masalia (chupa na vifungashio) anavyokuwa amebebea chakula na anadai kule hakuna vitupia taka.


“Niseme tu ukweli mimi usafi wa mazingira suala hilo liliishia shuleni sababu ni kwamba ukiishi na wasiojua mazingira ni nini  na wewe  unajikuta unafanana nao kwa mazingira,hata nikiwa hapa bichi kubeba labda chupa za juisi au mifuko ya chipsi au biskuti huwa sikumbuki kuzitoa wakati nikiondoka ”anasema Anitha


Emmanuel Meliksedeck mkazi wa Rwamishenye anasema,maeneo ya fukwe hayana usimamizi ni kila mtu kwa wakati wake anakuja kufanya shughuli zake kulingana na muda unavyomruhusu.


Anasema,hakuna utaratibu au mpangilio wa jinsi ya kutumia mazingira, mtu anaweza kuamua kutupa uchafu hovyo au kuutoa kwa kujisikia kutokana na kutokuwepo kwa usimamizi wowote.


Anasema, vitu hivyo vinachangiwa na ukosefu wa elimu ya mazingira na kutokujua sheria ya mazingira inamtaka nini, japo walio wengi ukiwaangalia wanaonekana wastaarabu na wanatokea kwenye mazingira safi.


Mdau wa utalii mkoani Kagera William Rutta anasema, kutembelea fukwe ni sehemu ya utalii ambapo watu wanaozitembelea hupata burudani na starehe za namna tofauti.

Anasema,mtu anapokwenda eneo la fukwe anakuwa na lengo binafsi kama kupumzika, kuangalia au kushiriki michezo mabalimbali na kuchangamsha akili na mwili au hata kusa hau machungu anayoyapitia katika maisha.


“Baadhi ya fukwe ambazo nimetembelea hapa nchini nikianzia hapa Bukoba watu hawajajua matumizi na utunzaji wa fukwe, ni chafu na zinaweza zisimvutie mgeni ambae atawaza kwenda kutulia eneo la fukwe iliyopo mazingira ya ziwa letu” anasema Rutta.

Anasema, kinachowavutia watalii na uwekezaji katika fukwe ni pamoja na usafi na kwamba si rahisi sisi kama wadau wa utalii kumpeleka mtalii eneo ambalo ni chafu litakalomkosesha amani na uhuru wa kufurahia mazingira.


Anasema endapo usimamizi wa fukwe utafanyika kwa kuhakikisha zinakuwa safi na kutunzwa katika uasili wake ni rahisi kuwashwishi watalii kuja na kuja kwao kukatoa fursa mbalimbali kwa jamii inayozunguka maeneo hayo na taifa kwa ujumla.


“Ninachofahamu hakuna mtalii ambaye atapenda eneo linalomzunguka liwe chafu,usidhanie kwamba alieyekuja janana akashuhudia hali hiyo atavutiwa tena kurudi; Ili kuweka mazingira ya fukwe kwenye hali ya usafi ni usimamizi na ikiwezekana mamlaka za serikali ziachie wawekezaji kuyaendeleza maeneo hayo.”anasema Rutta.


Anasema, uwekwe utaratibu maalum utakaomfanya kila mwananchi anayekwenda ufukweni kutambua kuwa jukumu la ulinzi wa mazingira lipo mikononi mwake na si serikali  na kwamba hali hiyo itamfanya kuogopa kutupa taka hovyo.


Mhandisi wa maji kutoka taasisi ya bonde la ziwa Victoria mkoa wa Kagera Revodius Bishanda anakiri kufanyika kwa uchafuzi wa fukwe akidai kuwa, shughuli za kibinadamu zinazofanywa kwenye maeneo ya fukwe ikiwamo micheza,kutembelea na kupumzika zimekuwa zikihusisha ubebaji wa vyakula na vinywaji.


Anasema baadhi yao wakifanya starehe zao hawakumbuki kubeba taka zilizotokana za vifungashio vya vyakula na vinywaji ambazo zikiingia kwenye maji husababisha uchafuzi na athari kwa watumiaji wa ziwa sambamba na viumbe vilivyo majini.

Anasema taka zile zinakuwa na kemikali, ambapo mtumiaji wa maji ya ziwa kwa kunywa au kula samaki aliyekula uchafu huo anaweza kupata madhara kiafya na kuingia gharama ya kujitibia ili kuondoa athari iliyoingia mwilini.


Pia anasema kuwa hata taka zisipotupwa majini na kubaki fukweni husababisha kupotea kwa mvuto wa eneo husika na hivyo watu kukimbia maeneo hayo na kushindwa kutumika kwa shughuli iliyozoeleka.


Mhandisi Bishanda anaeleza kuwa,katika uchafuzi wafukwe sio watumiaji wa fukwe pekee, wapo hata wale ambao wanajihusisha na shughuli za kilimo cha matumizi ya mbolea zenye kemikali za kukuzia mimea na wanapotafuta eneo maalum la kutiririsha maji baada ya matumizi uelekeza maji hayo kwenye mkondo wa ziwa.


Meneja wa baraza la mazingira Tanzania (NEMC) kanda ya ziwa Bw, Jerome Kayombo anasema, NEMC imekuwa ikidhibiti vifungashio vyote vya aina ya plastiki ikiwemo mifuko na chupa.


Anasema, kwa kawaida vitu hivyo uchukua muda mrefu kuoza na pengine visioze kabisa na vikiwa karibu na ziwa, mto au bahari ni rahisi kutengeneza vipande vidogo ambavyo  vikiingia kwa viumbe hai wanaoishi ziwani huleta madhara.


Kayombo anaongeza kuwa, uchafuzi wa fukwe husababisha athari nyingine kama kuota kwa magugu maji yanayopelekea kumezwa kwa fukwe zenyewe, kuharibu mazalia ya samaki na kuathiri mfumo mzima wa ekolojia kwenye ziwa.


Anasema mtu ambaye anakwenda ufukweni na asikumbuke kuondoka na taka alizozizalisha mwenyewe au hata kuziweka eneo maalum anakuwa hajatenda haki na ni kwenda kinyume na sharia.


“Sawa, atasema siguswi na uchafu huo lakini atapenda pengine kutumia samaki, wakikosa ziwani atawapata wapi? Au hata kutumia maji safi, je, yasipotibiwa kuondoa sumu, hatapatwa na magonjwa? ”anasema Kayombo.


Anasema, kwenye maeneo mengine wapo wanaokwenda na begi mgogoni ndani ya hilo begi kuna chupa ya maji, nakawaida akihitaji hutoa na kunywa kisha hurudi nayo nyumbani, watu wa namna hiyo wanakuwa na dhamira njema ya kuhifadhi mazingira.


“Kuna chupa za kudumu za kutunza maji ya kunywa zinazouzwa, mtu anaweza kununua akaandaa maji yake kwa kuchemsha au kununu na kwenda nayo ufukweni kisha kurejea na chupa hiyo nyumbani, vitu hivyo tukiweza kuvitumia ni rahisi kabisa kutunza mazingira yetu”


“Twende kulia turudi kushoto, tabia inaanza na mtu mmoja mmoja, hatuzungumzii tu kutupa taka maeneo ya fukwe bali hata kwenye maeneo mengine watu wanakotupa taka hovyo ikiwemo barabarani  na kwenye vyombo vya usafiri” anasema Kayombo.


Afisa uvuvi mkoa wa Kagera Efraz Mkama anasema, kwenye eneo la uvuvi wapo watu ambao wanafanya ulinzi na uangalizi wa mazingira yasichafuliwe ili kufanya  mazalia ya samaki yasiingiwe na kemilikali zinazotokana na taka.


 “Ni watu tu kutojua endapo wangejua madhara ya taka wanazotupa hovyo eneo la ziwa kuwa ni hatari kwa mazalia ya samaki, basi wasingefanya hivyo, kwani sumu inayotokana na uchafu huo ikiingia ndani ya ziwa huuwa mazalia yaliyopo”anasema Mkama.


Aidha ameongeza kuwa usafi unaanza na watu wenyewe, wakifanya shughuli ambazo ni rafiki kwa maelekezo ya mamlaka na kuwa na matumizi sahihi ya vifaa vilivyowekwa kuhifadhia taka itaepusha athari hizo.

Comments


bottom of page