Chagua kuwa mzazi anayejali, anayewajibika
- Anord Jovin
- 2 days ago
- 3 min read
Mzazi mpendwa, maisha ni safari ndefu inayohitaji maandalizi ya mapema. Hakuna urithi mkubwa unaoweza kumwachia mtoto wako kuliko elimu, elimu si hiari, bali ni haki ya msingi ya kila mtoto na wajibu mkubwa wa kila mzazi.
Mtoto anapozaliwa, huja duniani bila kujua chochote; ni jukumu la mzazi kumwongoza, kumlinda, na kumpa zana zitakazomwezesha kuishi maisha yenye heshima na mafanikio. Moja ya zana hizo muhimu zaidi ni elimu.
Katika jamii nyingi, tumeshuhudia wazazi wanaopuuza au kuchelewesha jukumu la kuwaandikisha watoto wao shule, hasa mwanzoni mwa mwaka kama mwezi Januari. Wengine hufanya hivyo kwa uvivu, wengine kwa uzembe, na wengine kwa kutoona thamani ya elimu.
Hata hivyo, sababu yoyote ile, matokeo yake huangukia moja kwa moja kwa mtoto asiye na hatia. Mtoto anayekosa elimu hukosa mwelekeo, hukosa uelewa wa maisha, na hukosa fursa nyingi muhimu zinazoweza kubadili maisha yake.
Elimu ni msingi wa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla. Mtoto anayepata elimu hujifunza kusoma, kuandika, kuhesabu, kufikiri kwa kina, na kufanya maamuzi sahihi.
Elimu humjenga mtoto kiakili, kimaadili, kijamii na kiuchumi.
Bila elimu, mtoto huwa katika hatari ya kuingia katika vitendo viovu kama uhalifu, ajira duni, matumizi ya dawa za kulevya, na kuishi maisha ya umasikini wa kudumu.
Mzazi, kumbuka kuwa mtoto wako ana ndoto, hata kama bado hajui kuzitaja, ndoto hizo haziwezi kutimia bila elimu, unapomnyima mtoto wako haki ya elimu, unamnyima nafasi ya kuwa daktari, mwalimu, mhandisi, mkulima bora, mfanyabiashara mwenye mafanikio, au kiongozi wa baadaye, unapochelewesha kumpeleka shule, unachelewesha safari ya mafanikio ya maisha yake.
Sheria za nchi nyingi, ikiwemo Tanzania, zinatambua elimu kama haki ya msingi ya mtoto, hivyo, mzazi anayeshindwa kumpeleka mtoto shule si tu anakiuka wajibu wake wa kifamilia, bali pia anakiuka haki ya mtoto kisheria na kijamii.
Mtoto ana haki ya kulindwa, kulelewa, na kuendelezwa kielimu ili awe raia mwema wa baadaye, uvivu wa mzazi leo unaweza kuwa chanzo cha mateso ya mtoto kesho.
Mtoto anapokua bila elimu, mzazi huyo huyo anaweza kuwa wa kwanza kulalamika kuwa mtoto wake hana ajira, hana nidhamu, au hana msaada, ukweli ni kwamba mzazi hupanda mbegu leo na huvuna matunda kesho. Ukipanda uzembe, utavuna majuto; ukipanda elimu, utavuna mafanikio.
Elimu pia humsaidia mtoto kujitambua, kujithamini, na kuheshimu wengine. Mtoto aliyesoma huwa na uwezo wa kutetea haki zake, kuelewa wajibu wake, na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii, ulimu humpa mtoto sauti, humjengea kujiamini, na humuwezesha kushindana katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi kubwa.
Mzazi mpendwa, huenda unasema huna muda, huna pesa, au unasubiri baadaye. Lakini kumbuka, muda hauwezi kurudi nyuma, kila siku mtoto wako anapokaa nyumbani bila shule ni siku moja iliyopotea katika safari ya maisha yake.
Serikali na wadau mbalimbali wameweka mazingira rafiki ya elimu, ikiwemo elimu ya msingi bila malipo, kisingizio cha kushindwa kumpeleka mtoto shule kinazidi kupungua kila siku.
Zaidi ya hayo, elimu humkomboa mtoto na familia kwa ujumla kutoka katika mzunguko wa umasikini, mtoto aliyesoma ana nafasi kubwa ya kupata ajira au kujiajiri, kusaidia familia yake, na kuinua hali ya maisha ya wazazi wake, kwa hiyo, unapompeleka mtoto shule, huwekezi kwa mtoto pekee bali pia kwa familia yako na kizazi kijacho.
Mzazi, fahamu kuwa mtoto wako anakutazama na anakujifunza. Unapomthamini elimu, naye ataithamini, unapompa kipaumbele shule, naye ataona umuhimu wa kujituma na kuwajibika lakini unapompuuza, unamfundisha kuwa elimu si muhimu, hilo ni somo baya linaloweza kumharibia maisha yake yote.
Januari imepita, lakini bado hujachelewa, leo ni siku sahihi ya kuchukua hatua. Amka, simama, na mchukue mtoto wako mkono kwa mkono umpeleke shule, muandikishe, mfuatilie masomo yake, mshauri, na mshike mkono katika safari yake ya kielimu, usingoje kesho ilhali leo una nafasi ya kubadili historia ya maisha ya mtoto wako.
Elimu ni nuru inayoondoa giza la ujinga, mtoto wako anahitaji nuru hiyo ili aone njia ya maisha, wewe kama mzazi ndiye taa ya kwanza katika safari yake.
Chagua kuwa mzazi anayejali, anayewajibika, na anayejenga taifa kupitia mtoto wake, mpeleke mtoto shule leo, utimize haki yake ya elimu, na ujiwekee fahari ya kuwa mzazi bora na wa mfano katika jamii.





Comments