Uthamini
- 8 hours ago
- 3 min read
Kuthamini watu katika maisha yetu ni jambo la msingi sana ambalo mara nyingi hupuuzwa, licha ya kuwa na mchango mkubwa katika mafanikio yetu ya kila siku, Binadamu kwa asili ni kiumbe wa mahusiano, na hakuna mtu anayeweza kufanikiwa peke yake bila msaada au mchango wa wengine.
Kila hatua tunayofikia, kila mafanikio tunayojivunia leo, ni matokeo ya juhudi za pamoja za watu mbalimbali waliotuzunguka katika nyakati tofauti za maisha yetu, hata pale tunapohisi tumefanikiwa kwa nguvu zetu binafsi, ukweli unabaki kuwa kuna watu walioweka msingi wa mafanikio hayo, kwa namna moja au nyingine.
Katika maisha ya kila siku, tunakutana na watu wa aina mbalimbali ambao huchangia katika ustawi wetu, wapo wazazi waliotulea kwa upendo na kujitoa, wakihakikisha tunapata mahitaji ya msingi kama chakula, mavazi na elimu.
Wapo walimu waliotufundisha maarifa na kutuandaa kuwa watu bora katika jamii. Wapo marafiki waliotusimamia na kututia moyo pale tulipokata tamaa aidha, wapo wafanyakazi, vibarua na wasaidizi wetu wa karibu wanaotusaidia kutekeleza majukumu yetu ya kila siku, hata yale ambayo pengine tusingeweza kuyafanya wenyewe kwa ufanisi uleule.
Ni muhimu kuelewa kuwa hakuna mchango mdogo katika maisha kila mtu anayegusa maisha yako, hata kwa jambo dogo, ana nafasi katika kukufanya uwe ulivyo leo, mfano, mfanyakazi wa nyumbani anayekusaidia majukumu ya kila siku anakupa nafasi ya kufanya kazi zako nyingine kwa utulivu zaidi.
Kibarua anayekusaidia shughuli zako za ujenzi au biashara anachangia moja kwa moja katika maendeleo yako hata dereva, mlinzi, au mfanyakazi wa ofisini, kila mmoja ana nafasi yake katika kuhakikisha mfumo wa maisha yako unaenda vizuri hivyo basi, mafanikio yetu si matokeo ya juhudi binafsi pekee, bali ni mkusanyiko wa juhudi za watu wengi walioko nyuma ya pazia.
Vivyo hivyo, mabosi wetu na viongozi katika sehemu za kazi wana mchango mkubwa katika maisha yetu hayo hutupa nafasi za ajira, hutuelekeza, hutupa uzoefu na wakati mwingine hutusaidia kugundua uwezo wetu ambao hatukuwa tunaufahamu.
Wazazi na walezi nao hutoa msingi wa maadili na malezi bora, ambayo huathiri namna tunavyoishi na kushirikiana na wengine katika jamii, kwa mtazamo huu, ni wazi kuwa kila mmoja katika mzunguko wa maisha yetu ana mchango wa kipekee ambao unapaswa kuthaminiwa.
Hata hivyo, pamoja na mchango huu mkubwa wa watu katika maisha yetu, bado kumekuwepo na tabia ya baadhi ya watu kushindwa kuthamini juhudi za wenzao. Wapo wanaowaona wafanyakazi wao kama watu wa kawaida wasio na thamani, na hivyo kuwadharau au kuwatendea vibaya.
Wapo wanaosahau kabisa mchango wa wazazi wao mara tu wanapofanikiwa, na kuanza kuona kama walijitengeneza wenyewe bila msaada wa yeyote, wengine huwachukulia poa marafiki au ndugu waliowahi kuwasaidia nyakati za shida, na kusahau kabisa msaada walioupata.
Tabia hizi si nzuri, na zinaweza kuharibu mahusiano, kupunguza utu, na hata kuondoa baraka katika maisha ya mtu.
Kukosa kuthamini mchango wa watu kunaweza kuleta madhara makubwa, si tu kwa wale tunaowadharau, bali hata kwetu wenyewe, kwanza, kunajenga mazingira ya chuki na kinyongo, mtu anapohisi juhudi zake hazitambuliwi au kuthaminiwa, anaweza kupoteza ari ya kufanya kazi au kusaidia tena.
Pili, kunavunja mahusiano muhimu ambayo yangesaidia katika maendeleo yetu ya baadaye, tatu, kunapunguza thamani ya utu wetu kama binadamu, kwani heshima na shukrani ni sehemu ya msingi ya ubinadamu.
Ni muhimu sana kujenga tabia ya kuthamini watu kwa vitendo na kwa maneno, kusema “asante” ni jambo dogo lakini lenye nguvu kubwa, kumheshimu mtu bila kujali nafasi yake katika jamii ni ishara ya utu na busara.
Kutoa pongezi pale mtu anapofanya jambo zuri, au hata kumsaidia pale anapohitaji msaada, ni njia mojawapo ya kuonyesha kuthamini mchango wake katika maisha yetu, aidha, kuwatendea haki wafanyakazi wetu, kuwajali na kuwapa stahiki zao kwa wakati, ni sehemu ya kuthamini juhudi zao.
Zaidi ya hapo, ni muhimu kujifunza kuwa na unyenyekevu, unyenyekevu hutusaidia kutambua kuwa hatuko peke yetu katika safari ya mafanikio. Hutufanya tukumbuke tulipotoka na wale waliotusaidia kufika tulipo, unyenyekevu pia hutufundisha kuwaona wengine kama sehemu ya baraka katika maisha yetu, badala ya kuwaona kama watu wa kawaida wasiostahili kuthaminiwa.
Jamii inayothamini watu wake ni jamii yenye mshikamano, upendo na maendeleo, pale ambapo watu wanaheshimiana na kuthaminiana, kunakuwa na ushirikiano mzuri unaochochea maendeleo ya pamoja.
Kinyume chake, jamii isiyothamini watu wake hujaa migogoro, dharau na kutokujali, hali ambayo huathiri maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa hitimisho, ni vyema kila mmoja wetu ajifunze kuthamini watu waliogusa maisha yake kwa namna moja au nyingine, wazazi, walimu, marafiki, wafanyakazi, vibarua, mabosi na hata watu wa kawaida wanaokutana nasi katika maisha ya kila siku, wote wana nafasi katika kutufanya kuwa tulivyo leo.
Tusiwadharau wala kuwapuuza, bali tuwathamini kwa dhati, tukumbuke kuwa mafanikio yetu ni matokeo ya juhudi za pamoja, na kuthamini mchango wa wengine ni njia mojawapo ya kudumisha utu, kujenga mahusiano imara, na kuleta baraka katika maisha yetu.




Comments