top of page

Ifanye simu yako ikuingizie maarifa na kipato badala ya kukuchuna

  • 12 hours ago
  • 3 min read

Na Anord Kailembo

Katika zama za sasa za teknolojia, simu ya mkononi imekuwa sehemu muhimu sanaa ya maisha ya vijana wengi, leo karibu kila kijana ana simu janja inayomwezesha kuingia kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, TikTok, YouTube na mingine mingi.


Kwa wengi, simu imekuwa chombo cha mawasiliano na burudani, lakini ukweli ni kwamba simu inaweza kufanya zaidi ya hayo, inaweza kuwa chombo cha kujifunzia, kujijenga kimaarifa, na hata chanzo cha kipato lakini tatizo kubwa linalojitokeza kwa vijana wengi ni kutumia simu kwa njia inayowafanya wao ndio “kuliwa” na simu badala ya wao kuitumia kujinufaisha.


Ni jambo la kawaida kuona vijana wakitumia saa nyingi kila siku wakipitia mitandao ya kijamii bila malengo maalum, mtu anaweza kuanza kuangalia video chache tu lakini ghafla akajikuta ametumia saa kadhaa akipitia maudhui yasiyo na faida yoyote katika maisha yake.


Katika hali hiyo, simu inakuwa kama kifaa kinachokula muda, nguvu na umakini wa mtu bila kumrudishia chochote cha maana, hali hii ndiyo inayoweza kuitwa “kutafunwa na simu”, ambapo muda mwingi unatumika kupokea maudhui tu bila kujifunza wala kuzalisha kitu chochote chenye thamani.


Hata hivyo, ukweli ni kwamba simu ile ile inayoweza kupoteza muda inaweza pia kubadilisha maisha ya mtu kabisa ikiwa itatumika kwa malengo sahihi, kupitia mitandao ya kijamii iliyomo ndani ya simu, kijana anaweza kupata maarifa mapya kila siku.


Mitandao hiyo imejaa maudhui ya elimu yanayofundisha mambo mbalimbali ya kimaisha kama biashara, ujasiriamali, maendeleo binafsi, kilimo cha kisasa, teknolojia, uandishi, ubunifu wa picha na video, pamoja na ujuzi mwingine mwingi unaohitajika katika dunia ya sasa.


Kwa mfano, kupitia video za mafunzo kwenye mitandao mbalimbali, kijana anaweza kujifunza jinsi ya kuanzisha biashara ndogo, jinsi ya kutengeneza matangazo ya biashara, jinsi ya kupiga picha bora au hata jinsi ya kuhariri video kwa kutumia simu.


Maarifa haya yanaweza kumsaidia mtu kujijenga kitaaluma au hata kuanzisha shughuli za kujipatia kipato hivyo basi, simu inaweza kuwa kama darasa linalopatikana muda wote, mahali popote.


Mbali na kupata maarifa, mitandao ya kijamii pia imekuwa jukwaa kubwa la vijana kujipatia kipato, watu wengi duniani wamefanikiwa kujenga maisha yao kupitia mitandao hiyo hiyo ambayo wengine wanaiona kama sehemu ya kupoteza muda.


 Baadhi yao wameanza kwa kurekodi video rahisi tu kwa kutumia simu zao, lakini baadaye wakafanikiwa kujenga umaarufu mkubwa na kupata fursa mbalimbali za kifedha.


Hii inaonyesha wazi kuwa mitandao ya kijamii inaweza kuwa sehemu ya kazi na ujasiriamali kwa vijana wa kizazi cha sasa, kwa kutumia ubunifu, nidhamu na uvumilivu, kijana anaweza kuanza kujenga uwepo wake mtandaoni kwa kushirikisha maudhui yenye manufaa.


Maudhui hayo yanaweza kuwa ya elimu, burudani, mafunzo au hata kuhamasisha watu kufanya mambo mazuri katika jamii na kadri watu wengi wanavyovutiwa na maudhui hayo na kuanza kufuatilia akaunti za mtu, ndivyo nafasi ya kupata kipato inavyoongezeka.


Kipato hicho kinaweza kupatikana kupitia matangazo, ushirikiano na makampuni mbalimbali, au hata kuuza bidhaa na huduma kupitia mitandao hiyo, kwa njia hii, simu inabadilika kutoka kuwa kifaa cha kupokea maudhui pekee na kuwa chombo cha kuzalisha thamani.


Pia vijana wanaweza kutumia mitandao ya kijamii kufanya biashara moja kwa moja, leo hii watu wengi wanauza bidhaa zao kupitia mitandao kama Facebook, Instagram na WhatsApp.


Kwa kutumia simu tu, mtu anaweza kupiga picha za bidhaa zake, kuzitangaza mtandaoni na kuwafikia wateja wengi zaidi kuliko angeweza kuwafikia akiwa na duka la kawaida, hii imewasaidia vijana wengi kuanzisha biashara ndogondogo ambazo baadaye zimekua na kuwa kubwa.


Hata hivyo, ili simu iweze kukuingizia maarifa na kipato, ni muhimu kuwa na mtazamo sahihi kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii, kijana anapaswa kujiuliza kila mara anaposhika simu yake: Je, ninachofanya sasa kinanijengea maarifa au kinanipotezea muda? Swali hili linaweza kumsaidia mtu kuchagua maudhui anayoyaangalia na namna anavyotumia muda wake mtandaoni.


Ni muhimu pia kufuata akaunti na kurasa zinazotoa elimu na mafunzo badala ya zile zinazotoa maudhui yasiyo na manufaa, kadri mtu anavyojizungusha na maudhui ya kujenga, ndivyo akili yake inavyopata msukumo wa kujifunza na kufikiria zaidi kuhusu maendeleo yake binafsi.


Aidha, vijana wanapaswa kujifunza siyo tu kutumia mitandao kutazama maudhui bali pia kuzalisha maudhui yao wenyewe, hata kama mtu hana vifaa vya gharama kubwa, anaweza kuanza kwa kutumia simu yake tu kurekodi video za mafunzo, ushauri au ubunifu mbalimbali. Mara nyingi mafanikio makubwa huanza na hatua ndogo za mwanzo.


Kwa ujumla, simu ya mkononi ni chombo chenye nguvu kubwa sana katika maisha ya kijana wa leo, inaweza kuwa darasa, ofisi, soko na jukwaa la kujitangaza kwa wakati mmoja. Lakini thamani yake inategemea jinsi mtu anavyoitumia.


Ikiwa itatumika kupoteza muda pekee, haitaleta mabadiliko yoyote katika maisha. Lakini ikiwa itatumika kujifunza, kubuni na kufanya biashara, inaweza kuwa mwanzo wa mafanikio makubwa.


Ni wakati sasa kwa vijana kubadilisha mtazamo wao kuhusu simu walizonazo, badala ya kuruhusu simu iwaconsume kwa kuwafanya watumie muda mwingi bila faida, wanapaswa kuigeuza simu hiyo kuwa chombo kinachowaingizia maarifa, fursa na kipato.

 Kwa kufanya hivyo, mitandao ya kijamii haitakuwa tena sehemu ya kupoteza muda bali itakuwa ngazi ya kupanda kuelekea maisha bora na yenye mafanikio.

 
 
 

Comments


bottom of page