top of page

Aeleza siri ya kuishi miaka 100

Updated: Apr 17


Aliyekaa kwenye kiti ni mchungaji Christian Lutahakana  mwenye umri wa miaka 100 ya kuzaliwa.
Aliyekaa kwenye kiti ni mchungaji Christian Lutahakana mwenye umri wa miaka 100 ya kuzaliwa.

Na Anord Kailembo

 

Wahenga wanasema ukimuona nyani kazeeka ujue kakwepa mishale mingi vivyo hivyo katika maisha ya binadamu ukimuona mzee ujue kakutana na mengi hadi kufikia umri wa uzee.

 

Kipengele cha historia yangu hii leo tunakukutanisha na mchungaji Christian Lutahakana aliyezaliwa april 24 mwaka 1924 ambaye ametimiza umri wa miaka 100 ya kuishi Duniani, Mzee huyo mkazi wa kijiji cha Mbale kata Kitobo wilayani Missenyi mkoani Kagera ni mtoto wa nne katika familia ya watoto wanne.

 

Biblia kupitia kitabu cha Mithali 1:7 inasema Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa lakini pia Zaburi 37:5 inasema mkabidhi bwana njia zako pia umtumaini naye atafanya.

 

Maneno hayo ya vitabu vitakatifu vinasadifu yaliyomo ndani ya maisha ya miaka 100 ya mchungaji Christian Lutahakana ambaye anadai kuwa aliutumia utoto, ujana na hata uzee wake kuipenda na kuitumikia dini kutokana na misingi bora ya malezi aliyopatiwa na wazazi wake.

 

Anasema akiwa shule ya msingi katika shule ya Kashasha na hatua ya sekondari katika shule ya Kigarama zote za wilaya ya Missenyi alikuwa akishiriki shughuli zote za kidini ikiwemo kushiriki  kwenye kwaya pamoja na shughuli nyingine za kanisa.

 

Na ndiyo maana baada ya kuhitimu aliomba kusomea uchungaji tofauti na wanafunzi wengine walioelekea kwenye vyuo vya taaluma nyingine, hiyo yote ni kwa sababu tayari alikuwa na wito wa kichungaji ndani yake .

 

Mwaka 1947 kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT likaridhia pasipo na shaka ombi lake la kusomea uchungaji na kumpeleka chuo cha uchungaji cha Rwandai kilichoko Lushoto.

 

“Kwa kweli hapo niliona ndoto yangu imetimia, maana nilitamani sana kutumikia kazi ya Mungu katika maisha yangu yote” anasema Mchungaji Christian.

 

Mwaka 1949 alihitimu masomo ya uchungaji na kupelekwa katika kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT usharika wa Kashura manipaa ya Bukoba kwa ajili ya mazoezi akiwa shemasi na baada ya mwaka mmoja ,1951akahamishiwa katika kanisa la Kigarama ili kuhitimisha mazoezi yake.

 

Akiwa Kigarama alikutana na aliyekuwa askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kasikazini Magharibi Marehemu Josiah Kibira akiwa bado mchungaji akihudumu katika kanisa la Kigarama alikaa naye, hivyo akawa mlezi wake wa mambo mbalimbali ya kimaisha na kiroho.

“Nakumbuka nikiwa Kigarama na askofu Kibira wote tulikuwa bado vijana hatujaoa, tuliishi pamoja tukipika chungu kimoja ambapo  aliniongoza katika mambo mengi ya kimaisha na ya kiroho” Anasema Mchungaji Christian.

 

Na mwaka 1952 alirejeshwa tena katika kanisa la Kashura kwa ajili ya kupatiwa daraja la uchungaji na alipatiwa daraja hilo na mmisionari aliyefahamika kwa jina la Desmark.

 

Mwaka 1953 alihamishiwa kanisa la KKKT usharika wa Kashasha kuwa mchungaji wa Kashasha na Ruzinga na amehudumu katika makanisa hayo kwa miaka 5 na ndipo akaongezewa na kanisa la Ishozi na kufikisha makanisa manne aliyokuwa akiyachunga kiroho.

 

“Niseme ukweli sikupumzika, nilijitoa kwa moyo wote kuwahudumia wakristo, nyumbani palikuwa karibu sana na ninakohudumu lakini huwezi kuamini ilikuwa ngumu sana kulala kwangu,kwani  ni mara chache sana nimelala kwangu katika kipindi chote cha uchungaji, hii ni kwa sababu nilijitoa kutumikia kazi ya Mungu” anasema Mchungaji Lutahakana.

 

Mwaka 1958 aliteuliwa kuwa mchungaji wa jimbo lakini aliweza kuhamishwa kutoka Kigarama na kwenda Karagwe katika kanisa la Rukajange na kuhudumu kwa miaka miwili  (1958-1959).

 

Baada ya muda akarudishwa tena usharika wa Kashasha na kipindi hicho makanisa ya Kashasha na Ishozi yalikuwa yamepata wachungaji na hivyo yeye kusalia mchungaji wa jimbo hadi mwaka 1981 jimbo lilipogawanywa na yeye kusalia jimbo la Kasikazini A.

 

Amekuwa kanisa la Kashasha hadi anastaafu uchungaji mwaka 1994.

 

Azungumzia kuishi miaka 100

 

Akizungumzia kutimiza miaka 100 mchungaji Christian amesema kuwa ni zawadi aliyomtunuku Mwenyezi Mungu kutokana na kazi ya utume aliyoifanya katika kipindi chote cha makuzi yake.

 

Anasema kuwa hata yeye anashangaa kuona Mwenyezi Mungu akimtendea mambo makubwa na ya ajabu na siri ya maisha ya mtu ipo ndani ya kazi yake na mapenzi yake ndani ya kazi hiyo.

 

“Nilipokuwa kijana nikiwa Kigarama, nilipoamua kwenda chuo cha uchungaji nilijitoa kwa moyo wote bila kusuasua nilitamani kumtumikia Mungu” anasema Mchungaji Lutahakana.

 

Usipopenda kazi yake, huwezi kuifanya lakini pia ufanisi wa kazi yako unaonekana kutokana na kusimamia misingi bora ya maadili ya kazi hiyo, ukiifanya kwa uweledi Mwenyezi Mungu anakuona na kukutunuku maisha mema Duniani.

 

Anasema kuwa kutimiza miaka 100 anauona ukuu wa Mungu katika maisha yake lakini pia Mwenyezi Mungu anaonesha ukuu wake kwa wanadamu wanaomzunguka, hivyo ni vyema watu wakamtegemea na kumtumikia yeye katika nyanja tofauti.

 

“Kumpenda yesu Kristo katika moyo wako ni zawadi kubwa ya maisha na yeye hukuongoza na kukupa maisha mazuri yenye neema na baraka tele ikiwemo umri kama wa kwangu” Anasema Mchungaji Lutahakana.

 

Anasema katika maisha yake amewapoteza wake zake wawili Lucia na Grace Lutahakana waliompatia watoto 12 lakini hali hiyo haikumuondoa kwenye njia yake ya kuona kama Mwenyezi Mungu anamuadhibu, La hasha aliamua kushirikiana na watoto wake katika kuwalea na kumcha Mungu.

 

“Nilipompoteza mke wangu wa kwanza baada ya miaka mitatu nikamuoa mwingine ali anisaidie kulea watoto, licha ya kuishi naye kwa upendo na yeye akafariki pamoja na kuondokewa na wapendwa wangu hao bado nilikubaliana na hali ya kuwa ni mapenzi ya mwenyezi Mungu” Anasema Mchungaji Lutahakana.

 

Anasema alitumia nafasi hiyo kuwalea watoto wake katika misingi ya kidini ili wanaendeleze msingi bora wa malezi aliyoachiwa na wazazi wake ili ukawe wa kurithishana katika kizazi chake.

 

Anasema kuwa anamshukuru Mwenyezi Mungu kwani watoto 11 alionao kwa sasa baada ya mmoja kufariki Dunia, wote wameishika dini na ndiyo muongozo wa maisha yao.

 

Anaitaka jamii kumshirikisha mwenyezi Mungu katika kila jambo na wanapopata nafasi basi kumsifu na kumtukuza maana yeye ndiye aliyeshikilia usukani wa safari ya maisha yao ya Duniani.

 

“Namuomba Mwenyezi Mungu aendelee kunijaalia maisha mengine Duniani” anasema Mchungaji Lutahakana.

 

Ruth Lutahakana ni mtoto wa pili wa Mchungaji Christian Lutahakana anasema kwa niaba ya familia wanamchukuru Mwenyezi Mungu kwa kumtunza baba yao hadi kufikia umri huu wa miaka 100.

 

“Sisi tunaona kama ni muujiza inatupa tafakari na kujiuliza ya kuwa na sisi tutaufikia umri huo” Anasema Ruth.

 

Anasema anachokumbuka kuhusu maisha ya baba yake kabla ya kustaafu uchungaji alikuwa mtu wa kazi muda wote, mchana na usiku baba hakuchoka kuitumikia kazi yake na alikuwa mtu wa kujali muda sana.

 

Anasema kuwa watoto wake wanajivunia sana kuona namna alivyowaandaa kiroho, wote ni wacha Mungu na wameiweka dini mbele lakini pia amewafanya kuwa mfano mzuri katika jamii ya utii na adabu bila kusahau katika kumcha Mwenyezi Mungu.

 

“Kwa niaba ya watoto wake tunamuombea sana baba yetu na tunaahidi kuendelea kumtunza na kuendeleza msingi bora wa maisha ya kidini na kijamii aliotujengea ” Anasema Ruth

 

Mchungaji Prof.Wilson Niwagila wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT rafiki wa karibu wa mchungaji Christian anasema kuwa amekutana na mchungaji huyo akiwa kahororo sekondari mwaka 1959 na 1960 wakati huo akiwa mwanafunzi ambapo Mchungaji Lutahakana alifika kuwafundisha dini.

 

Anasema wakati anapata daraja la uchungaji mwaka 1967 alimkuta mchungaji Lutahakana  akiwa mchungaji wa jimbo akawa mwalimu wake anayemuongoza kutokana na kuwa mchanga kwenye tasnia hiyo.

 

“Ni baba mcha Mungu, mwenye upendo na huruma kwa watu, alinichunga vizuri na kunisaidia katika mambo mbalimbali, najisikia fahari sana kuona anatimiza umri huu mkubwa na namuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe afya njema” anasema Mchungaji Profesa Niwagila.

 

Kwa upande wake mchungaji Festo Mtashobya anasema amefanya maamuzi ya kuwa mchungaji baada ya kuvutiwa na Mchungaji Lutahakana  kutokana na upendo, ukarimu na utanashati aliyokuwa nao.

 

“Mimi ni kijana wake nimefurahi sana kuona anatimiza miaka 100 ni bahati kubwa sana na zawadi kutoka kwa mwenyezi Mungu” Anasema mchungaji Festo.

 

Anaitaka jamii kuyaishi maisha ya kumcha mwenyezi Mungu kama anavyosisitiza mchingaji Lutahakana kwani ndiyo yamemjenga hadi kufikia umri huu.

Comments


bottom of page