top of page

Uvivu- adui wa mafanikio ya vijana

Uvivu ni hali ya ukosefu wa hamasa ya kufanya jambo, kukosa nguvu ya kuanza au kumaliza majukumu, licha ya kuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Mara nyingi, tatizo hili huwa si tu kutokufanya kazi, bali pia ni mchanganyiko wa fikra, tabia na maamuzi ambayo humfanya mtu achague urahisi kuliko juhudi.


Kwa vijana wengi katika karne ya sasa, uvivu umegeuka kuwa kikwazo kikubwa kinachowazuia kufikia ndoto zao, hususan kutokana na mvuto wa starehe za teknoloji­a, mitandao ya kijamii, michezo ya mtandaoni na utamaduni wa kutaka mafanikio ya haraka bila jitihada.


Dunia inabadilika kwa kasi, fursa zinapita upesi, na wale wanaojituma ndio wanaounda historia, ndiyo maana ni muhimu kuelewa athari za uvivu, sababu za watu kuangukia kwenye tabia hiyo, pamoja na mbinu madhubuti za kuupinga ili kujiandaa kuishi maisha yenye matokeo chanya.


Kwa upande wa athari, uvivu unamgharimu kijana maisha yake ya sasa na ya baadaye. Katika masomo, uvivu hujidhihirisha kwa vijana wanaoahirisha kusoma, kutengeneza notsi au kukamilisha mazoezi ya shuleni. Matokeo yake, wanabaki nyuma darasani, wanapoteza kujiamini, na mwisho hujikuta wanafanya vibaya kwenye mitihani.


Siyo kwa sababu hawana uwezo, bali kwa sababu hawajaufanyia kazi uwezo wao, kwenye maisha ya kiuchumi, uvivu unawafanya vijana wengi kukosa maandalizi ya msingi ya baadaye.


Yule anayezoea kulala hadi saa nne au tano asubuhi, asiye na mipango wala ratiba, anajikuta akiwa mtu wa kutegemea sana wengine badala ya kuwa muundaji wa nafasi zake mwenyewe.


Uvivu pia huiba fursa, vijana wengi husema “nitafanya kesho” bila kutambua kuwa kesho hiyo haipo kwa wengi, fursa za mafunzo, kazi, biashara au ubunifu huwapita mbele yao, na wanabaki na majuto.


Zaidi ya hapo, uvivu huathiri hata afya ya mwili na akili, kwa kuwa kuelemea kitandani bila kufanya shughuli huongeza mawazo hasi, huzuni, na kupoteza kujiamini.


Ili kuelewa zaidi, mifano halisi inaweza kutupa picha pana juu ya namna uvivu unavyoweza kuharibu maisha, Juma, kwa mfano, alikuwa kijana mwenye akili nyingi lakini mzito wa kufanya kazi, kila kazi aliyokuwa akipewa shuleni aliiahirisha kwa kauli ya “nitasoma likizo” au “nitasoma nikikaribia mtihani.” pamoja na wazazi kumwezesha kwa vitabu na mwalimu wa ziada, uvivu wake ulimwangusha, na alipoingia kwenye mtihani wa kidato cha nne alishindwa vibaya.


Leo anafanya vibarua mjini na mara nyingi huwaambia vijana wenzake kwamba lau angejua anachojua sasa, asingekuwa mvivu hata kidogo, aidha, kuna mfano wa mkulima ambaye alizembea kupanda mazao kwa sababu kila siku alikuwa na kisingizio kipya: jua kali, mvua, uchovu au usingizi.


Msimu ulipomalizika bila yeye kupanda chochote, wenzake walivuna mazao mazuri ilhali familia yake ilikosa chakula na kipato, Mfano mwingine ni Amina, mwanafunzi msomi aliyekuwa na uwezo mkubwa, lakini uvivu wa kujisomea kila siku ulimwangusha alipofika chuo kikuu.


Kwa kuwa alikuwa amezoea kusoma siku moja kabla ya mtihani, mfumo mpya wa masomo ulimshinda. Hii inaonyesha kuwa hata mtu mwenye kipaji kikubwa anaweza kushindwa na maisha ikiwa hatapambana na uvivu.


Swali linabaki: kwa nini vijana wanakuwa wavivu? Mara nyingi ni kwa sababu hawana malengo ya wazi, mtu ambaye hajui anachotaka kufanikisha hana msukumo wa kuamka na kufanya kazi.


Wengine wanaogopa kushindwa, hivyo wanahirisha mambo ili wasikabiliane na matokeo, teknolojia, ikiwa haitadhibitiwa, inawafanya vijana wengi kupoteza muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii, michezo ya video au maudhui yasiyo na faida.


Kuna pia uhaba wa nidhamu binafsi, ambapo mtu huacha hisia zake ziendeshe siku yake badala ya ratiba, tabia ya kuahirisha kazi, ikirudiwa kwa muda mrefu, hugeuka tabia ya kudumu uvivu wa kitabia.


Ili kupambana na uvivu, vijana wanapaswa kuanza kwa kuweka malengo madhubuti ya muda mfupi na mrefu, malengo yanapokuwa wazi, mtu anaona sababu ya kusimama na kufanya kazi.


Kutengeneza ratiba ya kila siku na kuhakikisha inafuatwa pia ni hatua muhimu; ratiba inamweka mtu kwenye mwongozo wa kinachopaswa kufanywa bila kutegemea msukumo wa hisia.


Kazi kubwa zinapaswa kugawanywa katika kazi ndogo ndogo ili zisionekane kuwa nzito kupita kiasi, na mara nyingi ukiamua tu kuanza, nguvu ya kuendelea inakuja yenyewe, ili kuepuka vishawishi, ni vizuri kupunguza matumizi ya simu au mitandao wakati wa majukumu, na mbinu kama Pomodoro (dakika 25 za kazi, 5 za mapumziko) inaweza kusaidia sana.


Kuamka mapema kunampa kijana nafasi ya kupanga siku yake, na kumaliza majukumu makubwa akiwa na nguvu bado, kijana pia anatakiwa kujizoeza kujipa zawadi ndogo baada ya kukamilisha lengo fulani ili kuongeza motisha.


Zaidi ya yote, mazingira yana nguvu kubwa katika kutengeneza tabia; ukikaa na watu wavivu, utakuwa mvivu, lakini ukizungukwa na watu wanaojituma utaiga tabia zao chanya.

Kujituma kunaleta manufaa makubwa kwa vijana.


Kwanza, kunakuza nidhamu, ambayo ndiyo msingi wa mafanikio yoyote bila nidhamu hakuna ndoto inayoweza kufikiwa. Pili, kujituma kunafungua milango ya fursa kwa sababu watu hutamani kufanya kazi na mtu aliye makini na mwenye bidii.


Tatu, kujituma kunakuza kujiamini kwa kuwa kila unachokamilisha kinakufanya ujione unaweza, hivyo unapambana zaidi.


Jitihada ni msingi wa utajiri na mafanikio ya baadaye; hakuna mtu aliyefanikiwa kutokana na uvivu, bali kutokana na kufanya zaidi ya kile kilichohitajika.


Kwa ujumla, uvivu ni adui wa maendeleo ya vijana, unaweza kuonekana kama starehe ya muda mfupi, lakini gharama yake ni kubwa kuliko faida yake, kila dakika inayopotezwa katika uvivu ni ndoto inayofifia taratibu.


Kila kijana anapaswa kutambua kuwa mafanikio ya kesho yanategemea hatua anazochukua leo, Dunia haitamsubiri mvivu; inaenda na wale wanaojituma, wanaojipanga na wanaothubutu kupambana na vikwazo vyao binafsi.


Kwa hiyo, ni muhimu kuamka leo, kuushinda uvivu, na kuchukua hatua kuelekea maisha yenye mafanikio.

Kesho yako inategemea uamuzi wako wa leoanza sasa.

 
 
 

Comments


bottom of page