NGUVU YA NDOTO: UWEKEZAJI BORA KWA KIJANA WA LEO
- Anord Jovin
- 3 days ago
- 3 min read
Katika kila kona ya maisha, iwe ni shuleni, mtaani, au nyumbani, kuna vijana wengi waliobeba ndoto nzito moyoni mwao.
Ndoto za kuwa madaktari, wahandisi, wasanii, wajasiriamali, wanasiasa, walimu, wanamichezo, au hata viongozi wakubwa wa dunia.
Ndoto hizi si hadithi tu au mawazo ya kupita; ni mbegu za maisha bora yajayo. Hata hivyo, changamoto kubwa si kuwa na ndoto, bali ni kuzielewa, kuziamini, na kuwekeza kwa vitendo ili zifanikishwe. Ndoto bila hatua hubaki kuwa mawazo, lakini ndoto zilizoambatana na juhudi hubadilika kuwa uhalisia.
Kuwa na ndoto ni jambo la msingi sana kwa kijana. Ndoto humpa kijana mwelekeo wa maisha, kijana asiye na ndoto ni kama meli isiyo na dira; anaweza kusafiri kwa muda mrefu lakini asifike popote.
Ndoto humsaidia kijana kujitambua, kujua anapotaka kwenda, na kufanya maamuzi sahihi kulingana na malengo yake, ndoto humjengea nidhamu, kwa sababu kijana mwenye ndoto hujua kuna mambo anatakiwa ayafanye na mengine ayaache ili kufikia alipoelekea.
Kwa vijana walioko shuleni, ndoto hufanya elimu iwe na maana zaidi, kusoma si kwa ajili ya kufaulu mitihani tu, bali ni kwa ajili ya kujiandaa kwa maisha ya baadaye.
Kijana mwenye ndoto anapoingia darasani, anaona kila somo kama daraja linalomvusha kuelekea ndotoni, hata kama somo linaonekana gumu au halivutii, ndoto humfanya avumilie na kujituma, elimu huwa silaha, na ndoto huwa sababu ya kuibeba silaha hiyo kwa uangalifu na juhudi.
Kwa vijana walioko mtaani, ndoto huwa nuru katikati ya giza, maisha ya mtaani mara nyingi hujaa changamoto kama umaskini, ukosefu wa ajira, vishawishi vya uhalifu, dawa za kulevya, na tamaa ya kupata mafanikio ya haraka.
Ndoto humsaidia kijana kusema “hapana” kwa mambo yanayoweza kuharibu maisha yake. Ndoto humkumbusha kuwa kuna maisha bora mbele yake, na kwamba maamuzi ya leo yanaathiri kesho yake.
Swali kubwa ambalo vijana wengi hujiuliza ni: “Nifanye nini ili kufikia ndoto yangu?” Jibu la kwanza ni kuielewa ndoto yako vizuri. Ndoto si kusema tu “nataka kufanikiwa”, bali ni kujua unataka kufanikiwa katika nini, kwa namna gani, na kwa muda gani.
Ndoto inahitaji kuwa wazi. Kijana anapaswa kujiuliza: Ndoto yangu ni ipi? Kwa nini nina ndoto hiyo? Inanifaa vipi mimi na jamii yangu? Kadri ndoto inavyokuwa wazi, ndivyo inavyokuwa rahisi kupanga njia ya kuifikia.
Hatua ya pili ni kuamini kuwa ndoto yako inawezekana. Vijana wengi hushindwa mapema kwa sababu wanajidharau au wanaruhusu maneno ya watu yawavunje moyo. Kuna watu watakaosema huwezi, mazingira ni magumu, au wewe si wa aina hiyo.
Lakini historia imetuonyesha mara nyingi kuwa waliofanikiwa sana ni wale waliokaidi maneno ya kukatisha tamaa, kuamini ndoto yako ni kuipa uhai, bila imani, ndoto hufa kabla haijaanza.
Uwekezaji katika ndoto ni jambo muhimu sana. Uwekezaji hauimaanishi pesa peke yake, bali muda, juhudi, maarifa, na nidhamu. Kijana anapaswa kujiuliza: Je, ninawekeza muda wangu wapi? Je, muda wangu mwingi unaenda kwenye mambo yanayonikaribisha kwenye ndoto yangu au kuniondoa? Kuamka mapema kusoma, kujifunza ujuzi mpya, kusikiliza ushauri, na kujiepusha na mambo yasiyo na tija ni sehemu ya uwekezaji katika ndoto.
Msingi mwingine muhimu wa kufanikisha ndoto ni nidhamu. Nidhamu ni uwezo wa kufanya jambo sahihi hata kama halina raha kwa wakati huo, ndoto nyingi hushindwa si kwa sababu watu hawana uwezo, bali kwa sababu wanakosa nidhamu, kijana mwenye nidhamu anajua wakati wa kucheza na wakati wa kufanya kazi, anajua kuweka vipaumbele, na haongozwi na hisia za muda mfupi bali na malengo ya muda mrefu.
Subira na uvumilivu pia ni nguzo muhimu katika safari ya ndoto, hakuna ndoto inayotimia kwa siku moja, kutakuwa na vikwazo, kushindwa, kukataliwa, na nyakati za kukata tamaa, lakini kila changamoto huja na funzo, kijana anapaswa kuelewa kuwa kushindwa si mwisho wa safari, bali ni sehemu ya kujifunza. Wengi waliofanikiwa walishindwa mara nyingi kabla ya kufanikiwa, lakini hawakukata tamaa.
Ni muhimu pia kwa kijana kujizunguka na watu sahihi, marafiki, walimu, washauri, na watu wanaokutia moyo wana mchango mkubwa katika safari ya ndoto, mazingira huathiri sana fikra na maamuzi ya kijana, ukiwa na watu wasio na mwelekeo, ni rahisi kupotea lakini ukiwa na watu wanaothamini juhudi, nidhamu, na maendeleo, ndoto yako hupata nguvu zaidi.
Vijana wanapaswa kuelewa kuwa ndoto zinaenda sambamba na uwajibikaji, kuwa na ndoto si kisingizio cha kuwadharau wengine au kukwepa majukumu ya sasa, kijana anapaswa kuwa mwaminifu, mchapakazi, na mwenye maadili mema, jamii inahitaji vijana wanaotimiza ndoto zao huku wakijenga jamii bora, si kuharibu wengine kwa tamaa binafsi.
Ndoto ni zawadi ya kipekee kutoka kwa Mungu au kutoka ndani ya nafsi ya mtu. Kila kijana ana ndoto yake, na hakuna ndoto ndogo au kubwa kupita nyingine, kilicho muhimu ni jinsi unavyoichukulia ndoto yako, ukithamini ndoto yako, ukawekeza ndani yake, ukaifanya kuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuiona ikitimia.
Kwa vijana wote walioko shule na mtaani: msikubali hali ya sasa iwafafanue. Msiruhusu makosa ya jana yawanyime matumaini ya kesho, anzeni leo kuwekeza katika ndoto zenu, jengeni misingi imara ya maarifa, nidhamu, subira, na bidii. Ndoto zenu zina thamani, na dunia inawasubiri muje kuibadilisha kupitia ndoto hizo.





Comments