top of page

Somo kutoka Kigali

Updated: Apr 17


Moja ya maeneo ya nchi ya Rwanda
Moja ya maeneo ya nchi ya Rwanda

Na Charles Mwebeya


Majira ya saa saba kamili mchana nafika katika mpaka wa Rusumo, nikiwa katika harakati za kuelekea Kigali Rwanda nilipoalikwa katika Kongamano la  wafanyabiashara wa Tanzania na Rwanda.


Baada ya kufanyiwa taratibu za masuala ya forodha na uhamiaji ambayo yalichukua takribani saa mbili hivi, nikaanza safari ya kutoka mpakani kuanza kuitafuta Kigali.


Nikiwa naanza safari, nikahisi tofauti ya hali ya hewa pamoja na mandhari  kutoka mpakani Rusumo ambayo ilikuwa ni kielelezo tosha namna nchi hiyo ilivyoweza kujipanga katika suala zima la uhifadhi wa mazingira na usafi.


Haijalishi maeneo ya vijijini na katika baadhi ya wilaya nilizopita, lakini suala la mpangilio wa vijiji, nyumba kwa nyumba na usafi lilikuwa ni la kuvutia sana.


Katika wilaya ya Kirehe nilistaajabu sana kuona namna masoko ya mbogamboga na matunda yalivyokuwa yamepangwa pamoja na bidhaa zake kando ya barabara.


Utakuta mboga za majani zimewekwa mahala pake, ndizi zimepangwa mahala pake na bidhaa nyingine katika chemba yake.


Masoko yenyewe yanavutia kwani yamejengwa katika namna ambayo  huwezi kukuta bidhaa zikiwa zimezagaa chini na hata wachuuzi wenyewe kupigwa na jua ama kunyeshewa na mvua.


Wachuuzi wenyewe wanakuwa na wamevalia kofia nyeupe na vitambaa vyeupe !!kama wapishi tunaowaona katika hoteli zetu.

 

Achana na hayo kubwa ni ile hali ya kutokuta uchafu umezagaa si vijijini au hata mijini ama katika makazi ya watu!


Nikajiuliza hawa wenzetu wamewezaje? Wanawezaje kuweka taa za barabarani hadi vijijini na katika misitu ya umma?


Kabla ya kupata jibu la swali langu, wingi wa miale ya taa za usiku ukaonesha kabisa kuwa sasa naingia mji mkuu wa nchi hiyo  Kigali.


Ingawa giza lilikuwa limeanza kutanda, nikajaribu kutupia jicho dirishani nikaona jamaa zetu wa bodaboda jinsi walivyo nadhifu lakini si hilo tu hata namna wanavyoweza kutiii sheria za barabarani!


Wanapotakiwa kusimama, husimama lakini pia wanaheshimu hata abiria waliowabeba.


Watu waliokuwa wametoka makazini wakisubiri usafiri walikuwa wamejipanga katika foleni ,bila vurugu! Wakisubiri kuingia katika magari ya usafiri, mengi yalikuwa ni aina ya Coaster  tena zenye rangi inayofanana,, nyeupe!! zilizoonekana kuwa imara na si chakavu!

Kwa vile giza lilikuwa limeshaanza kutawala anga, nikasema ngoja kesho huenda nikaona mengi zaidi.


Kweli siku ya Kongamano lenyewe tukiwa njiani nikaendelea kushuhudia utamaduni ule ule, utii wa sheria na Usafii!!


Barabarani unaweza ukadhani upo sebuleni, kwanza katikati ya mji wenyewe ni nadra sana kukutana na vumbi.


Katika kila kiambaza kuna kitu inaitwa pavement yaani kimesakafiwa na vijitofali vidogo ambavyo vinaungana na barabara kuu, kila jengo la ofisi lina vyombo vya kutupia taka wanaita Dustbin.


Nikajiuliza mbona kule kwetu Tanzania tunavyo! kwani shida nini? mbona uchafu kule kwetu unaendelea kuzagaa tu? Kwani nyinyi sio waafrika? nikamuuliza kwa utani mmoja wa waandishi wa habari aliyekuwa ameketi kando yangu  John  Gakuba anayefanya kazi katika  Redio ya Taifa ya Rwanda.


“Sheria,, Sheria ndiyo inayofanya kazi hapa kama wewe si mtiifu wa sheria hapa huwezi kuishi” akasema.


“Hata kwetu sheria zipo lakini sijui kwanini bado tuko nyuma katika suala la usafi” sikumjibu bali nilijisemea kimoyo moyo.


Akaendelea “Hapa kila nyumba inatakiwa kutoa kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kulipia uchafu. kwani kila mtaa una kampuni ya kukusanya taka na kazi hii wanaifanya kila siku, mchana na usiku”


“Utawaona wanakuja tu, hawaongei na wewe wao wanakwenda kwenye ma-Dustbin na shughuli zao za kukusanya uchafu humalizia huko huko” alisema.


“Na ikitokea mtu akashindwa kulipa?” nikamuuliza

“Anapelekwa mahakamani, adhabu yake huwa ni kifungo ama faini kubwa, lakini kama huwezi kulipa hata fedha ya kukusanyia taka ni bora usiiishi mji huu” akasema.


Sikuishia hapo nikamuuliza tena endapo mtu aliyeshindwa kulipa faini “ataongea kiutu uzima” (kutoa rushwa ) kwa  wahusika ili kuruka kihunzi.


“Rushwa hapa ni adui namba moja, mtu akipatikana na hatia ya kutoa ama kupokea rushwa adhabu yake huwa ni mbaya sana” akanijibu mwandishi huyo nguli .


Baada ya kongamano hilo bado nikawa na dukuduku la kutaka kuona mengi zaidi ikiwa ni pamoja na kutembelea maeneo ya pembezoni mwa mji ili kujionea  uhalisia wa usafi wa mazingira .


Mwenyeji wangu Bwana Gakuba akanipeleka katika mgahawa mmoja uliopo eneo la Nyamirambo ambao unamilikiwa na Ndayizeye Said, huyu ni mzaliwa wa  Buyenzi katika jiji la Bujumbura  Burundi lakini amekuwepo Kigali akifanya shughuli zake kwa miaka kadhaa sasa na anamudu kuongea kiswahili kizuri.


 “Unaona huu mtaa ulivyo, hapa magari hayaruhusiwi kupita, hili ni eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya watu kunywa, kula na kufurahi wakiwa wameweka viti na meza barabarani na nakupa kazi ya kutafuta walau kipande cha karatasi ukikiona niambie nikupe faranga” aliniambia.


Nikajaribu kupitisha jicho huku na kule na kweli hapakuwepo na karatasi wala taka yoyote!!

“Braza hapa kuna ustaarabu uliopitiliza na wanyarwanda wengi ni watu wazuri sana, huwezi hata kukuta watu wanapigana hadharani, adhabu yake mahakamani ni kama faranga elfu nne hivi kama hauna ni kifungo tu” alisema .


Jiji la Kigali kwa sasa linachukuliwa kama mfano katika suala zima la usafi wa mazingira katika miji yote barani Afrika. Utashi wa viongozi wa nchi ya Rwanda katika suala zima la usafi unatajwa kama chanzo cha mji huo kuwa wa kuvutia.


Rais Paul Kagame anatajwa kama kinara katika dhana hii, kwani amekuwa akisisitiza usafi katika miji yote ya nchi hiyo na kuanzisha siku maalum ya usafi ambayo hujulikana kama Omuganda.


Omuganda hufanyika kila mwisho wa mwezi na hujumuisha wananchi wote ambapo kila mtaa au kijiji hushiriki siku hiyo wakisimamiwa na viongozi wao.


Rwiyigema Alfred mkazi wa Kigali ambaye hufanya shughuli ya kuendesha magari makubwa anasema “endapo hutashiriki Omuganda utapigwa faini na hii ni siku ya kufanya usafi kweli katika kila mtaa na sio kwenda kutalii”.


“Huwezi kuona mtu hata mmoja akizurura barabarani ama mtu kafungua duka, watu wote hushiriki hata wasio raia hushiriki pia” alisema.


“Mimi ni mtu mzima, nimeishi hapa Kigali kwa miaka mingi, kabla hata ya utawala huu, lakini usafi sasa umegeuka kuwa utamaduni na ni mara chache kumuona mtu anatupa takataka na hali hii imesababisha hata baadhi ya magonjwa kama kipindupindu kusahaulika kabisa” alisema.


Kutokana na utafiti uliofanywa na jarida la Nile Post la nchini Uganda, mnamo mwaka 2021,  mji wa Kigali nchini Rwanda ndio mji msafi zaidi barani Afrika kutokana na utashi wa viongozi na wakazi wa mji huo kuuweka mji wao katika hali ya usafi.


Dhana ya utawala bora na utamaduni wa kufuata sheria nayo inatajwa kusukuma kwa kiasi kikubwa ajenda ya usafi katika mji huo wenye wakazi zaidi ya laki sita.


Kigali inafuatiwa na miji ya Ports Louis mji mkuu wa Mauritius, Cape Town  Afrika ya Kusini pamoja na Tunis  mji mkuu wa Tunisia.

 

Comments


bottom of page