top of page

Diaspora wawe funzo kwa wazawa

Updated: Mar 15


Baadhi ya watanzania waishio nje ya nchi wakiwa katika picha ya pamoja na rais wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Tanzania Suruhu Hassan
Baadhi ya watanzania waishio nje ya nchi wakiwa katika picha ya pamoja na rais wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Tanzania Suruhu Hassan

Na Mwandishi Wetu


Diaspora ni watu wa nchi moja wanaoishi nchi nyingine. Watu hawa licha ya kuishi huko bado hueshimiwa na kupewa hadhi kama wazawa kwenye nchi zao za asili na kutegemewa katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo.


Kawaida watu hawa huwa na umoja wao unaowawezesha kuwasiliana na kujadili mambo yanayohusu maendeleo ya mataifa yao na kuona ni kwa jinsi gani wanaweza kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za kijamii katika mataifa yao.


Lakini pia kushiriki katika kuzitangaza fursa mbalimbali zinazopatikana katika nchi zao.

Tanzania ni moja ya nchi za Kiafrika zenye Diasipora wengi Ughaibuni, kwa mujibu wa taarifa za mwezi April mwaka 2023 diaspora wanafikia milioni 1.5 ambao pia wamekuwa na mchango katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi hapa nchini.


Pamoja na mchango wao kwenye maeneo hayo pia wanatajwa na serikali kuleta mawazo chanya yanayo lenga kuwezesha ufanisi katika mipango endelevu ya kitaifa.


Mara kadhaa serikali imesikika ikikiri kutambua mchango wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi, ikidai michango yao inahusisha sekta mbalimbali ikiwemo fedha, afya,elimu na maji.


Kwa mfano kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2022,Diaspora wa Tanzania walituma nchini kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.1 trioni 1.34 ambayo ni sawa na Shilingi trilioni 2.6.


Kutokana na serikali ya Tanzania kutambua mchango wa Diasipora, Mwezi Mei mwaka 2023, ilizindua rasmi mfumo wa kuwasajili Diasipora wenye asili ya Tanzania kidijitali.

 

Adiventures in Health, Eduction and Agricltural Development (AHEAD Inc) Tanzania ni moja ya kundi la Watanzania waishio nchini Marekani, ambao kwa kushirikiana naWamarekani wengine wenye mapenzi mema na Tanzania, wamekuwa wakitoa michango yao kuwezesha upatikanaji wa vifaa na miundombinu mbalimbali ya afya.


Dkt. Apolinary Ngirwa, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la AHEAD Inc (diaspora) anasema kuwa mbali na kutoa vifaa na kujenga miundombinu pia wamekuwa wakiwaleta moja kwa moja madaktari bingwa kutoka nje ya nchi, kutoa msaada wa matibabu na dawa bure kwa wananchi.


Anasema kufanya hivyo kusaidia kutatua changamoto za kiafya zinazowakabiri wananchi kutokana na kukosa huduma hizo, au wengine kutumia gharama kubwa kuzipata.

“Matunda yamekuwa yakionekana kwa watu kupona na wengine kupata ushauri wa kitaalam, hii ni heshima kubwa kwa jamii” amesema Dkt.Ngirwa.


Anabainisha kuwa katika miundombinu wamejenga vituo vya afya, wodi za akina mama na mtoto, majengo ya upasuaji, maabara, majengo ya kufulia nguo na majengo ya kuhifadhia maiti, katika maeneo mbalimbali nchini.


Amesema kuwekwa kwa miuundombinu hiyo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, kunalenga kuimarisha ufanisi wa huduma katika maeneo yanayotegemewa na jamii, kwa kupunguza madhara ikiwemo kuboresha huduma ya mama na mtoto.


“Naishukuru serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana nasi kwa kipindi chote tunapokuwa tukitekeleza shughuli zetu nchini, na wakati mwingine kuchangia kufanikisha malengo yetu kama Watanzania waishio ughaibuni” anasema.


Kituo cha Afya Maruku kilichoko halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, ni moja ya vituo vya afya nchini vilivyonufaika na mchango wa Diaspora, kwa kupatiwa vifaa tiba venye thamani ya zaidi ya shilingi mil. 66.8 pamoja na kujengewa miundombinu ikiwemo wodi ya mama na mtoto.


Mbali na misaada hiyo pia jopo la madaktari wa Diaspora wamekuwa wakifika na kutoa huduma ya matibabu na ushauri kwa jamii.

 

Kupatikana kwa huduma za msingi na muhimu katika kituo hicho cha afya ambacho kinalenga kuwa hudumia watu zaidi ya laki moja na elfu hamsini, kumeondoa changamoto ya kusafiri umbali mrefu, kufuata huduma katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera–Bukoba.


Akiwa Washington Dc Marekani Rais wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ziara yake iliyolenga kuzindua filamu ya The Royal Tour, alikutana na kufanya mazungumzo na Diaspora.


Katika hotuba yake Rais Samia alikiri kutambua mchango wa Diaspora katika kuliletea taifa lao maendeleo, kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbalimbali sambamba na kuwasadia ndugu, jamaa na marafiki. “Pamoja na kwamba mna uraia wa huku msipasahau nyumbani, lak- ini pia hakikisheni mnawalea watoto wenu kwa kuwafundisha maadili ya nyumbani”.


FUNZO

Utaratibu uliojengeka wa Diaspora kutatua changamoto zilizoko kwenye jamii, unatakiwa kuwatia chachu hata Watanzania wenye uwezo walioko nchini, kujitoa kushiriki katika utatuzi wa changamoto zilizopo.


Dhana hii ikijengeka itasaidia kila mtu kujiona sehemu ya kutatua changamoto inayomzunguka, na kufanikisha maendeleo katika jamii yake na taifa kwa ujumla.


Lakini pia dhana hiyo itawatia moyo Wanadiaspora kuendelea kujitoa na kuomba misaada zaidi ya kusaidia kuinua maendeleo ya Watanzania katika nyanja tofauti.

Comments


bottom of page