top of page

Sababu ya Dkt. Montessori kujidogosha

Updated: 1 day ago

Na Jacqueline Mwombeki


Wanasema cheo ni dhamana lakini pia wanasema mgaagaa na upwa hali wali mkavu. Montessori ambaye kitaaluma alikuwa ni daktari wa binadamu, katika kitabu chake cha ‘the secret of childhood’, anaelezea ni kwa jinsi gani watoto kuanzia umri wa miaka 3-6 walivyo mbadilisha na kuyapa maisha yake thamani zaidi kwa kile kilichomsababisha kutelekeza fani yake ya udaktari na kujikita zaidi na kuelimisha.


Akimtaja mtoto kuwa ndiye aliyemuongezea thamani ya maisha yake zaidi, mathalani yeye kama daktari angeweza kumuhudumia mtoto hospitalini bado moyo wake ukajazwa na furaha, lakini aliona ni busara awekeze moyo na nguvu zake  zote kwa upande wa elimu ya mtoto.


Aliyoyashuhudia kwa macho yake yakitendwa na watoto kuanzia mwaka wa 1907 huko San Lolenzo nchini Italia, na aliyoendelea kuyashuhudia baadaye; yalimtaajabisha sana.

 

Muujiza huu wa watoto ambao kupitia miongozo na matumizi ya zana, ziliweza kuwabadilisha watoto wale kihisia, kitabia na kitaaluma kutoka watoto wa mitaani, kuwa watoto wanaopenda shule na ambao ndani ya muda mfupi waliweza kumudu stadi za KKK yaani kuhesabu, kusoma na kuandika! 


Akiwa anaendelea kustaajabishwa na matokeo hayo; watoto waliendelea kuonyesha ustaarabu wa kiwango cha juu kabisa kwa maeneo tofauti kutoka hali ya woga na kuwa watoto shujaa, kutoka upweke na kuwa watoto wanaoshirikiana na kutoka watoto waliopuuziwa na jamii na hatimanye kuwa watoto mashuhuri.


Aliona kuwa mtoto anayo siri ya maisha yake na hicho kikawa chanzo cha Dkt. Maria Montessori kuitelekeza taaluma yake ya udaktari na kuhamisha shauku na mahaba yake kwa watoto.


Kama maneno katika Biblia yasemavyo kwamba Yesu aliuvua utukufu wake, akauvaa mwili wa uchovu, ndivyo na Dr. Maria Montessori alivyoacha taaluma yake ya udaktari na kuvaa maumivu ya watoto waliokuwa wanayapitia kwa wakati ule ambao kidogo dunia ilionekana kuyapa kisogo hasa elimu ya  watoto wa rika hiyo.


Watoto wampa Montessori sababu ya maisha


“Ilishangaza watu wengi sana kuona anaacha fani ya udaktari, uhadhili katika chuo kikuu cha Roma na harakati zake za kutetea haki za mwanamke eti kwa sababu ya kuwahudumia watoto wadogo kielimu” ni ukweli usiopingika kuwa hakika watoto walimpatia Montessori mwelekeo mpya wa dunia ambao ni ulimwengu wa roho”. The Secret of childhood.


Kitendo cha watoto kuweza kusoma na kuandika maneno wakiwa na umri mdogo kupitia herufi alizowaandalia kwenye kadi na kuwafundisha  kwa mtindo wa sauti kilimshangaza sana kwani hata yeye hakutarajia kijibu kwa kiwango hicho; anasema ‘‘ulikuwa ni mlipuko wa mtoto mmoja baada ya mwingine wa kusoma na kuandika" na hapa tunazungumzia watoto kuanzia umri wa miaka minne na minne na nusu.


Jambo hilo lilikuwa ni la kushangaza sana kwani kipindi hicho mtoto aliyekuwa anaruhusiwa kufundishwa stadi za KKK ni kuanzia umri wa miaka saba kwa ugumu wa mfumo uliokuwepo kwa mchakato wa kusoma na kuandika na kwa tukio hilo, mtu yeyote  hasingekuelewa kwani ni tendo ambalo lilikuwa ni gumu kuwezekana.


Aliwapa mazingira sahihi na kuyashehenisha na zana salama na zenye mvuto zilizoweza kuwashughulisha watoto kiakili, kimwili na kisaikolojia; Montessori ambaye alikuwa ni mwanasaikolojia aliandaa mazingira ambayo yamo kwenye kipimo chao na kuwapa tekniki sahihi kabisa za kutumia zana hizo lakini kuwaacha na kuwapa muda wa kupeleleza kwa uhuru kile ambacho wamekwisha onyeshwa.


Baada ya muda mfupi sana wa miezi michache tu mabadiliko chanya yalianza kujidhihirisha, Montessori hakuweza kuamini alichokiona anasema ilimchukua muda mwingi sana akijishauri kuamini kuwa anachokina ni kweli na kwamba huu ni ukweli  wala siyo maluweluwe.


Katika kitabu chake cha siri ya utoto “the secret of childhood” anaandika “baada ya kila kitu kuonyesha ukweli wake, nilijisemea, sitaamini kwanza, nitaaamini baadaye, hivyo kwa muda mrefu nilijiambia kwamba nitaendelea kutoamini na wakati huo huo nitaendelea kuchochewa na hofu.”


Lakini baada ya kuushudia ukweli huo ambao ulionekana kujiri kila siku katika kila eneo alilokuwa akilitafiti, mwisho ilibidi akubaliane tu na ukweli kwamba iko hivyo.


Kwa hiyo unaweza kuona kwamba vinakuwa ndani ya watoto wote kwenye umri huo kwani hata ukiangalia upande wa mziki na wa kila kitu unaona watoto kwenye umri huo wanatokea kuonyesha vipaji walivyonavyo mapema na kama wewe ni mfuatiliaji angalia video clips za “little big shots”, “Ellen” show na Briten got talent kwenye chanel za youtube na wengineo ambayo kwetu  tunayapokea kwa alama ya mshangao mkubwa na kama viburidisho!

 

Je, ni kweli kwamba watoto duniani bado wanakumbana na ugumu wa kusoma na kuandika?

Jibu ni ndiyo, kwani sayansi ya lugha ni dhahania tupu na isipozungumzwa wala kuandikwa haipo; hivyo ni juhudi za mtu binafsi kupata ustaarabu huu uliokwisha kuwekwa na jamii za watu fulani, hali kadhalika utamaduni huu wa manadamu una nguvu kubwa ya ushindi wa kimazingira na pasipo kuurithishana, hutoweka.


Tunatia bidii ya kutunza, kukuza, kuhifadhi na kuhimarisha fasihi kwa kurithisha migingi ya lugha ambayo ni kusoma na kuandika; ambapo tunaona ili mtoto aweze kusoma ni lazima awe na misamihati toshelezi ya lugha husika ili asome na kuandika kwa ufahamu.


Msingi wa lugha usipotolewa vizuri kwa mtoto kwa kuzingatia taratibu zake, sanaa hii ambayo ni dhahania, hupokelewa kwa taabu sana na kumfanya mtoto akose mantiki yake na tatizo hili linaendelea kuwakumba watoto wengi ulimwenguni kote.

 

Montessori katika kitabu chake cha “the discovery of the child” anasema:

“Sote tunatambua kuwa kusoma na kuandika ni tatizo mashuleni, ni mateso ya kwanza yanayompata mtu ambaye ni lazima atii asili ya lugha kwa matakwa ya ustaarabu”.


Anaendelea kueleza kuwa, “waelimishaji ambao wametafakari juu ya shida hii wamehitimisha kwa kusema kwamba, ni vizuri kuchelewa iwezekanavyo kuliko watoto kufanya kazi yenye maumivu kama hii kwa kuamini kuwa mtoto chini ya umri wa miaka minane haifai kufanya kazi hii iliyo ngumu.


Montessori anafafanua jinsi sheria wakati ule iliainisha kwamba mtoto chini ya umri wa miaka sita ni kosa kubwa kisheria kujifunza alfabeti na kuandika; kwani kikawaida, kuandika huchukuliwa kama hatua ya baadaye ukizingatia ugumu unaojitokeza wakati wa mtoto kujifunza kuandika.


Hata hivyo ni lugha ambayo huturuhusu kueleza mawazo yetu ambayo yanakuwa tayari yamejipanga bongoni mwetu kwa utaratibu vile vile na kupata mawazo mengi toka vitabuni ya wale waliokwisha twaliwa au walioko mbali na sisi.


Kadiri mtu anavyokuwa hawezi kutumia lugha ya maandishi, ndivyo atakavyopata ugumu wa kujifunza na kutumia lugha hiyo; lakini tunaamini kwamba suluhu inaweza kufikiwa kwa kujifunza kwa undani juu ya tatizo hili na kwa kuangalia makosa katika mbinu zinazotumika kujifunza kuandika na yale tunayozingatia wakati wa kuandika kwenyewe hii ni pamoja na ujuzi na weledi wa matumizi ya zana za kuandika.


 
 
 

Commentaires


bottom of page