top of page

Nyangoye, mlima tishio uliobaki historia Kagera

Updated: Apr 17


Na Anord Kailembo

Mlima nyangoye uliobaki historia katika maisha ya wakazi wa manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, huu ni miongoni mwa milima iliyokuwa tishio hapa nchini kutokana na kusababisha ajali nyingi zilizoleta mauaji makubwa kwa abiria waliokuwa wakisafiri kutoka ama kuingia manispaa ya Bukoba.


Umaarufu wa mlima huu haukuwa kwa uzuri bali ni kutokana na matukio ya mabaya ya ajali yaliyoacha makovu kwenye miili na mioyo ya baadhi ya watanzania.


Mlima huo ulikuwa na kona tatu na kali ambazo ziliwashinda madereva wengi kutokana na kuwa na mtelemko mkali hivyo baadhi yao walishindwa kumudu vyombo vyao vya moto hadi kusababisha ajali.


Mlima Nyangoye ulikuwa kilio cha muda mrefu cha wakazi wa mkoa wa Kagera kwani kila alipokuja kiongozi wa ngazi ya juu ya serikali ukiachilia mbali ujenzi wa soko na stendi basi changamoto yao kubwa nyingine ilikuwa ni hiyo.


Itakumbukwa alipokuja makamu wa Rais Dr.Isdory Mpango katika ziara ya kikazi mkoani Kagera na kufanya mkutano wa adhara katika viwanja vya mayunga manispaa ya Bukoba kilio kikubwa kwake kilikuwa ni stendi ambapo alimuagiza wakala wa barabara nchini TANROAD kuanza mchakato wa utatuzi wa changamoto hiyo.


Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mabadiliko ya historia ya mlima Nyangoye kwani ulifanyika utafiti wa namna ya kumaliza tatizo hilo chini ya TANROAD kisha serikali kutoa fedha ya ujenzi wa kipande cha barabara (kutoka Round about Rwamishenye hadi Amugembe) sehemu iliyokuwa na mlima huo.


Mapema mwaka jana serikali ilianza utekelezaji wa mradi mkubwa wa barabara ya njia nne ambao katika matengenezo yako umesambaratisha kabisa mlima huo ambao ulikuwa tishio.


Jukumu kutekeleza mradi huo uliosambalatisha mlima Nyangoye ni Abemulo Contractors Company Limited amabaye anaendelea na utekelezaji huku huku historia yam lima huo ikiwa tayari imebaki hadithi.


Jamii

Julai 14 mwaka 2011 ilitokea ajali ya gari katika mlima nyangoye, iliyohusisha magari mawili na pikipiki katika ajali hiyo, mmoja wa madereva alikuwa ni  Eliazali Razaro dereva wa magari ya mizigo manispaa ya Bukoba.


Anasema alikuwa akitokea Bukoba mjini kwenda Rwamishenye kuchukua mzigo na wakati akianza kupanda mlima ghafla aligongana uso kwa uso na gari lililokuwa likishuka huku mwendesha pikipiki za abiria ambaye pia hakuliona gari lililokuwa likishuka alijikuta akijigonga kwenye magari yote mawili.


“Unajua kilichokuwa kikisababisha ajali ni mlima mkali uliokuwa mwanzoni kabisa unapotaka kupanda mlima huo kwani ulitufanya sisi tunaopanda kutokuona mbele, na anayeshuka kutokumuona anayepanda” alisema Razaro.


Anasema mbali na hiyo mlima ule ulimlazimisha dereva anapopanda kwanza awe na mafuta ya kutosha lakini pili aje na gia ya juu na waliobadilishia gia mlimani walishindwa kumudu vyombo vyao vya usafiri kutokana na kasi ya mlima.


“Tumeshuhudia ajali nyingi sana hapa na za kikatili ambazo zimechukua madereva wenzetu lakini pia ndugu, jamaa, na marafiki ambao walikuwa na mchango mkubwa katika taifa hili” anasema Razaro.


Anasema kitendo cha kuondoa mlima huo kilichofanywa na serikali ni ishara tosha kuwa ajali zilizosababishwa na mlima huo sasa zimekwisha.


Mzee Idris Muhamadi miaka 89 mzaliwa na mkazi wa kata Amugembe manispaa ya Bukoba (ulikokuwa mlima nyangoye) anasema ameshuhudia ajali nyingi kwenye mlima huo ambazo zimeacha ulemavu wa kudumu kwa wananchi lakini pia majonzi ya milele kwa wananchi waliowapotenza wenzao.


“Hapa isingepita siku haijatokea ajali, kuanzia enzi za matumizi ya baiskeli, pikipiki na sasa magari, muda wote hapa waendesha vyombo hivyo waliogopa eneo hili” anasema Idrisa


Anasema hata usalama wa wananchi walioishi kando na mtelemko huo ulikuwa mdogo kwani kupinduka kwa magari muda mwingine kulifikia nyumba zao lakini pia usalama wa watoto wa familia zilizoishi kando pia walikuwa katika usalama dhaifu.


“Matengenezo ya barabara hii yameleta neema kwetu”


Shedrack Benezeth ni dereva wa magari anasema kuwa ajali kubwa iliyotokea mlima nyangoye na kubaki katika kumbukumbu za maisha yake ni ya Mombasa Raha ambayo iliwaua watu wengi.


“Nakumbuka nilikuwa mdogo nikiishi magoti lakini nilikimbia na kuja kushuhudua ajali hiyo, kwa kweli tulipoteza watu wengi na kipindi hicho nilitaka niache kabisa kwenda chuo kusomea udereva nikijua sasa na mimi naenda kufa” anasema Shedrack


Anasema ameshuhudia ajali nyingine kubwa ikiwemo ya fikosh ambayo ilitokea miaka mitano iliyopita na kusababisha vifo vya abiria ambao tayari walijua kuwa wamefika nyumbani na nyingine nyingi akidai kuwa ujenzi wa barabara hiyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kulinda usalama wa abiria na dereva.


Mwandisi Zabron ni meneja wa TANROAD mkoa wa Kagera anasema kuwa mbali na mradio huo kuondoa kona kali iliyokuwepo pia ni mradi wa barabara ya njia nne ukilenga kuondoa msongamano.


“Mradi huo mbali na kusambaratisha mlima pia unatoa njia nne za barabara ambazo zitaepusha msongamano barabarani ambao pia huchangia kwenye ajali zinazotokea” anasema Zabron.


Mlima Nyangoye sasa umebaki historia kwenye vichwa vya wana Bukoba, Kagera na Tanzania kwa ujumla.

 
 
 

Comments


bottom of page