top of page

Mbegu za kisasa za mhogo kutoka TARI neema kwa wakulima

Na Anord Kailembo


Zao la muhogo tangu zamani limekuwa zao la chakula ambalo hulimwa kwenye maeneo mbalimbali nchini, kwenye baadhi ya mikoa ukiwemo Kagera zao hili limekuwa zao la akiba na kusaidia nyakati za njaa.


Baadhi ya wakulima wamekuwa wakilima na kukausha kwa ajili ya unga pale mazao pendwa kama ndizi yanapokuwa yamepungua katika uzalishaji wake hivyo kufanya zao hilo kuwa zao mbadala.


Kadri miaka ilivyozidi kusogea zao hili limekuwa zao la kutegemewa na wakulima na wasio wakulima kama zao la chakula na hii ilitokana na mazao yaliyokuwa kipaumbele kwao kuwa na uzalishaji mdogo ukilinganisha na kipindi cha nyuma kutokana na magonjwa na mabadilio ya tabia ya nchi.


Safari ya zao hilo haikuishia hapo kutokana na kukua kwa teknolojia, zao la mhogo limekuwa moja ya mazao ya kibiashara kwa sasa, kufuatia uwepo wa matumizi mbalimbali ya zao hilo ukiachana na chakula ikiwemo viwanda kwa ajili ya kuzalisha bidhaa nyingine ikiwemo gundi.


Kutokana na zao la mhogo kuwa na uhitaji mkubwa ndani na nje ya nchi serikali kupitia wizara na taasisi zinazosimamia na kuratibu shughuli za kilimo zikatupia macho zao hilo.


Uwepo wa kituo cha utafiti wa mazao cha TARI umechangia kwa kiasi kikubwa kuliboresha zao hilo kuhakikisha linazalisha mbegu za kisasa zitakazomuwezesha mkulima kupata mazao ya kutosha kwa ajili ya chakula lakini pia ziada ya kuuza.


Mwichande Ahmed Mwichande (Pichani) ni mtafiti wa mazao ya mizizi na matunda kutoka kituo cha utafiti wa mazao TARI Maruku anasema kuwa kituo hicho kinataka kuona mkulima ananufaika zaidi na kilimo chake kwa kuwa na uzalishaji mkubwa.


Amaesema kuwa moja ya kitu kinachomfanya mkulima aweze kuzalisha kwa wingi ni pamoja na aina ya mbegu anayoitumia, iwapo atatumia mbegu bora atanufaika nayo na asipofanya hivo basi atajikuta anavuna tofauti na matarajio yake.


Anasema watafiti walipobaini uwepo wa changamoto ya uzalishaji mdogo wa zao hilo walifuatilia na kubaini kuwa moja ya changamoto kwa wakulima ni mbegu wanazotumia kutokuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha na ndipo wakaanza utafiti wa mbegu zitakazo msaidia mkulima.


Amesema mpaka sasa TARI imezalisha mbegu 29 nchini lakini 9 pekee ndizo zinazolimwa mkoani Kagera na nikutokana na matakwa ya wakulima lakini pia mazingira yaani mbegu hizo kukubali katika maeneo hayo.


Amesema kuwa zinapozalishwa mbegu huzingatiwa mambo mbalimbali ikiwemo uvumilivu wa magonjwa, mavuno yenye tija na zenye kuendana na mabadiliko ya tabia ya nchi.


Ameongeza kuwa mbegu inapozalishwa na kupitishwa na TOSCI kinachofanyika cha kwanza ni kuwashirikisha wakulima katika kuipanda na kuonja radha ya mhogo ili waweze kutoa maoni yao kuhusiana na mbegu husika.


“Baada ya hapo mbegu zinazokuwa zimependekezwa zaidi ndizo ambazo hupelekwa kwenye mashamba darasa (mkulima aone kwa vitendo) lakini pia kwa mawakala wa mbegu kwa ajili ya uzalishaji wake” anasema


Anasema hujitahidi kupeleka mbegu nyingi sokoni ili kila mkulima awe huru kuzipata na kufanya uchaguzi wa aina anayoitaka kwa sababu kuna mbegu kwa ajili ya chakula na kuna mbegu za kibiashara.


“Tunao mawakala ambao wao wanazalisha mbegu na kumuuzia mkulima na tumeweka mazingira rafiki ya kuhakikisha mkulima anapata mbegu kwa gharama nafuu” anasema


Anasema kuwa kwa mkoa wa Kagera yapo mashamba darasa 12 ambapo Ngara yapo 6, Karagwe 3, Biharamulo 3, na majaribio yamefanyika kupitia mashamba hayo ya kubaini mbegu nzuri.


Kadhalika Mwichande ameongeza kuwa kwa mkoa wa Kagera wapo wazalishaji wa mbegu 46 ambapo Biharamulo 21, Missenyi 5, Muleba 8, Ngara 7, Karagwe 2 na Bukoba dc 3.

 

“Kuna majaribio matatu yamefanyika na kufanya uchakataji kwa kupika na kubaini aina bora lakini kujua mbegu gani inastawi vizuri maeneo gani”


 Anasema kuwa mbegu zote zilizozalishwa zinatoa mihogo kwa ajili ya kupika, kusaga unga pamoja na matumizi mengineyo.


Amesema kuwa mtafiti ambaye ni TARI anazalisha katika daraja la awali alafu wazalishaji hao wanazalisha kwa daraja linalofuata lakini pia wanawahusisha wataalam wa kilimo ambao wanaweza kuwaelekeza kwa ufanisi zaidi.


Amesema kuwa TARI haiishi kwenye kutoa mbegu tu lakini pia imekuwa ikifanya ufuatiliaji wa namna shughuli za kilimo kwa mkulima inavyoendelea ikiwa ni sambamba na kuwashauri iki kufikia tija.


Anasema matokeao ya mbegu 3 (tarikasi 4, Kiroba na Mkubwa) zinazopendwa kanda ya ziwa yamekuwa ni mazuri na uhitaji wa mbegu umekuwa ni mkubwa baada ya wakulima kujiridhisha kuwa zao hilo linamanufaa katika uzalishaji na biashara.


Anasema kuwa siri ya wakulima kufanya vizuri katika kilimo cha mhogo ni kufanya maandalizi mazuri ya shamba, matumizi ya mbegu za kisasa, usimamizi wa shamba katika hatua zote hadi kuvuna ambapo mwisho wa siku atapata mavuno mazuri.


Akizungumzia mbegu ya asili, Mwichande amesem“huwezi kusema kwamba mbegu za asili zinazidiwa na mbegu za kisasa, lakini utafiti umefanyika na kubaini kuwa mkulima anapotumia mbegu za kisasa kwa hekali moja anaweza kupata tani 40 hadi 45 lakini kwa mbegu za asili hekali moja atapata 10 hadi 15.”anasema.


Licha ya mbegu za kisasa kutumia muda mrefu wa kiutafiti na mchakato mzima hadi kufikishwa kwa wakulima kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wakulima kuwa na dhana potofu juu ya mbegu hizo japo elimu inaendelea kutolewa kwa wakulima kupitia maafisa ugani.

 
 
 

Related Posts

See All
Uvivu- adui wa mafanikio ya vijana

Uvivu ni hali ya ukosefu wa hamasa ya kufanya jambo, kukosa nguvu ya kuanza au kumaliza majukumu, licha ya kuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Mara nyingi, tatizo hili huwa si tu kutokufanya kazi, bali pi

 
 
 

Comments


bottom of page