Mbegu ya uaminifu
- Anord Jovin
- 5 days ago
- 3 min read
Katika dunia ya sasa inayokua kwa kasi na kubadilika kila uchwao, thamani ya uaminifu imeendelea kubaki kuwa moja ya misingi muhimu zaidi katika maisha ya binadamu, Kijana anayeingia katika mazingira yenye ushindani, fursa na changamoto zisizotabirika anahitaji kujijengea misingi imara ya tabia itakayomsimamia katika safari yake ya maisha.
Uaminifu, ambao mara nyingi hauonekani moja kwa moja kama vipaji au ujuzi, ndiyo mbegu ndogo inayopandwa mapema lakini huzaa matunda makubwa katika nyanja zote za maisha kuanzia nyumbani kwa wazazi, katika ajira, hadi katika mahusiano yake na jamii pana inayomzunguka.
Safari ya uaminifu inaanza nyumbani, katika familia, hapa ndipo mtoto hupata darasa lake la kwanza la tabia njema, wazazi wanaposema ukweli, kutimiza ahadi zao na kuonyesha heshima kwa mali za wengine, basi mtoto anayekua katika mazingira hayo hujenga misingi ya uadilifu bila hata kufundishwa kupitia maneno.
Kwa kijana anayeendelea kukua, uaminifu nyumbani huwa kioo cha utu wake; anapoaminika na wazazi wake, anajenga tabia ya kujiamini na kuwaheshimu watu wengine, ndipo jambo hili linapogeuka kuwa msingi wa maisha yake ikiwa atakua na tabia ya ukweli nyumbani, ataibeba popote.
Kinyume chake, kijana anayejenga tabia za udanganyifu mapema huingia katika maisha ya siri, anaanza kukosa kuaminika na hata hupoteza mazingira ya msaada ili hali matatizo yanapotokea.
Katika ulimwengu wa kazi, uaminifu huwa mtaji ambao hauandikwi wala hauwekwa kwenye CV, lakini una thamani kuliko vyeti vya kitaaluma, mwajiri anaweza kufundisha kijana namna ya kutumia kompyuta, kuandika ripoti au kutekeleza majukumu ya kiufundi, lakini hawezi kumfundisha kuwa mwaminifu.
Huu ni msingi unaotokana na maamuzi ya mtu binafsi, kijana mwenye uaminifu kazini huonekana kwa kutekeleza majukumu yake bila shuruti, kuheshimu muda wa kazi, kutokutafuta faida binafsi kupitia mali ya kampuni, kutoa taarifa sahihi kazini na kufanya mambo yake kwa uadilifu hata pale anapokuwa peke yake.
Tabia hizi humfanya kuwa rasilimali ya thamani kwa mwajiri, kwa sababu uaminifu ni bidhaa adimu sokoni, waajiri wengi wanasema kuwa tatizo kubwa si kukosa watu wenye elimu, bali kukosa wafanyakazi wenye uaminifu.
Kijana anapopoteza uaminifu kazini, athari sio tu kufukuzwa kazi; anapoteza sura yake ya kitaaluma, uwezo wa kuhakikisha anapata kazi nyingine na hata uaminifu wa watu wanaomtambua.
Katika jamii, uaminifu ni zaidi ya tabia; ni mtaji unaotengeneza fursa zisizoonekana, jamii humtambua mtu mwaminifu kama mtu wa kutegemewa akiahidi, watu wanaamini, akizungumza, watu hawana mashaka, akichukua mkopo, watu hawana wasiwasi.
Hapa ndipo uaminifu unapozaa heshima ambayo haiwezi kununuliwa, kijana mwaminifu hujenga mtandao wa watu wanaomwamini, na mtandao huu hufungua milango ya fursa za biashara, uongozi, ubia, taaluma na hata urafiki wa kweli.
Mtu asiyekuwa mwaminifu katika jamii hupoteza fursa hizi bila kujua, kwa sababu jamii huacha kushirikiana naye, si kwa sababu hana uwezo, bali kwa sababu hawana hakika ya uadilifu wake.
Lakini wakati mwingine, kijana anaweza kupoteza uaminifu bila kutarajia, tabia ya kusema uongo mara kwa mara, uvunjaji wa ahadi, kutokujali sheria ndogo ndogo, kuchukua mali ya wengine au kutumia njia za mkato ili kufanikisha jambo fulani, taratibu hutengeneza tabia ya udanganyifu.
Matokeo yake, kijana huyu hujikuta akikosa marafiki wa kweli, akikosa kuaminika kazini, akikosa fursa za kijamii na mara nyingine kuingia kwenye matatizo ya kisheria, kijana asiyeaminika huishi kwa woga wa kufichuliwa, anakuwa hana uhuru wa kujiamini, na mara nyingi hupoteza mwelekeo wa maisha kwa sababu amejijengea tabia zinazomfunga mwenyewe.
Kupotea kwa uaminifu ni kama kupotea kwa msingi wa nyumba; jengo linaweza kusimama kwa muda, lakini siku moja litaporomoka bila tahadhari.
Katika kujenga uaminifu, kijana anahitaji kufanya maamuzi ya kila siku maamuzi madogo yanayouunda utu wake, kusema ukweli, hata pale unapokuwa mgumu, ndiyo hatua ya kwanza ya kujenga sifa ya kuaminika.
Kutimiza ahadi, hata zile ndogo za kawaida, ni njia ya kuonyesha kuwa maneno yake yana thamani, kijana anayeweza kufanya kile alichoahidi bila kusimamiwa huwafanya watu waamini kuwa anaweza kutegemewa katika mambo makubwa.
Aidha, kujenga tabia ya kukiri makosa na kuwajibika huonyesha ukomavu wa kiakili na kiutu; hakuna mwanadamu aliyekamilika, lakini kukubali makosa huongeza heshima yake mbele ya wengine, kutokutumia njia za mkato, kuepuka vishawishi vya kukiuka sheria kwa faida ya muda mfupi, na kuwa mwaminifu hata pale hakuna anayemuona, ni misingi ya kudumu inayojenga utu wa kweli.
Zaidi ya hapo, kijana anahitaji kuchagua marafiki wenye maadili, kwa kuwa tabia ya mtu inaelekezwa na watu anaotembea nao, hatimaye, uaminifu ni urithi ambao hauzeeki na hauna mwisho, kijana anayepanda mbegu ya uaminifu leo, atavuna heshima, fursa, uongozi, ajira, marafiki wa kweli na amani ya ndani kesho.
Mtu mwaminifu anaishi maisha huru; hana woga wa kufichuliwa, hana mzigo wa uongo na hana wasiwasi wa kupoteza heshima yake, katika kizazi ambacho kimejaa kishawishi cha njia za mkato, kijana anayechagua uaminifu anakuwa mwanga; na mwanga haupotei gizani.
Uaminifu ni zawadi ya maisha yote kwa anayeutunza, maisha humlipa kwa wingi.





Comments