top of page

Makumbusho ya zana za kale Kagera

Na Anord Kailembo

Wahenga walisema ya kale ni dhahabu, methali hii imebeba mengi yenye kuithibitishia dunia kuwa baadhi ya mambo ya zamani yalikuwa yenye thamani kwa binadamu ukilinganisha na ya sasa.


Ya kale yaweza kuwa katika tabia, tamaduni, nyenzo za kimaisha na kadhalika.

Kutokana  na mabadiliko ya mfumo wa maisha ya mwanadamu yanayochangiwa na mambo mbalimbali ikiwemo utandawazi yamepelekea baadhi ya vitu vya kale kupotea pia ikichangiwa zaidi na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.


Wakati mwingine ya kale yaliyopotezwa na ulimwengu wa sasa yalikuwa ya thamani zaidi kuliko ya sasa katika ustawi wa maisha ya mwanadamu lakini kwa sababu la ulazima katika kuendana na maisha ya sasa binadamu mwenyewe hulazimika kubadilika.


Hali hii ya kubadilika kwa mfumo wa maisha uliopelekea dhahabu ya kale kupotea au kushuka thamani, haujambadili fikra Bw, Samwel Agustine mkazi wa mtaa wa Kisindi kata Kashai manispaa ya Bukoba ambaye ameamua kutengeneza makumbusho ya zana za kale zinazopotea katika ulimwengu wa sasa.


Katika mahojiano maalum na Montessori Tanzania anasema tangu kale alishuhudia wazazi wake wakiheshimu zaidi mira na desturi lakini pia hata yalipotokea mabadiliko ya kimaisha hawakuacha kutunza na kuendelea kutumia zana za kale.


Anasema katika kukua kwake ameshuhudia mambo mengi yakibadilika na mabadiliko yanapotokea vitu hivyo hupotea kabisa katika maisha ya watu, jambo hilo lilimpa maswali mengi ikiwemo ni wapi watoto wake watakuja kuzijua ua na kuziona zana zilizotumiwa na bibi na babu zao kuendesha maisha? Lakini pia kuijua asili yao.


Kama hiyo haitosho aliiona kama fursa ya kuifanya jamii yake hasa kizazi cha sasa kuyatambua mambo ya kale na yalivyowasaidia bibi na babu zao kuishi, hivyo akaamua kuandaa makumbusho yake binafsi inayohusisha vifaa vyote vya kale vilivyotumika katika maisha ya kawaida.


Montessori Tanzania imeshuhudia vifaa mbalimbali katika makumbusho yake ikiwemo Ngoma, pasi za jua na mafuta ya taa, redio mbao, Camera za mwanzo, Mawe ya kusagia nafaka (mashine za kusaga), vinu vya kale, simu za mwanzo, kufuri, vinu, majembe, mapanga na zana za chuma za mwanzo, viberiti vya kale, kanda za miziki za zamani, mifano ya nyumba za kale na vitabu vya kihistoria na kadhalika.


Hakika ukifika kwenye makumbusho hayo utashangaa kuona vitu vya kale ambavyo hata hukuwahi kuona au kujua chimbuko lake ambavyo vimepangiliwa vizuri huku kila kitu kikiwa na umri wake tangu kuvumbuliwa na mabadiliko.


Amesema kuwa kizazi cha sasa kimekuwa kikilaumiwa kwa kukosa maadili lakini pia kwa kutokuiishi misingi ya chimbuko la maisha yao (mira na desturi za utamaduni wao) lakini jibu ni kwamba wanakosa maeneo yenye msingi wa kujua chimbuko lao.


Amesema kuwa watoto hawa wanatakiwa kusikia na kuona kwa macho yao kilichokuwa kikitumika na kufanyika ili waweze kurithi, na huo ni wajibu wa wazazi na serikali kupitia malezi na masomo yao.


Anaongeza kuwa katika utafiti mdogo alioufanya kwa watoto wake pamoja na jamii kwa ujumla, watoto wamekuwa wakijifunza historia kama hadithi na sio elimu ya kuwaingia na wakajua namna ya kuitafsiri katika maisha kwa kupima uzito wa mambo ya kale na sasa.


“Imebaki kuwa historia ya kusoma kwa ajili ya kujibu mitihani tu na siyo kumfanya atambue uhalisia wa maisha yao ya sasa na ya kale lakini pia kuona kwa ualisia” anasema.


Kadhalika anadai kuwa wakati anaanza, watu wengi hawakumuelewa walimuona kama mtu ambaye alikosa cha kufanya muda huo maana alikuwa akishinda kwenye karakana, sehemu za vyuma chakavu na kwenye maeneo ya kihistoria akitafuta vifaa mbalimbali kwa kununua.


Anasema imemchukua takribani miaka 5 jamii kuanza kuelewa katika matumizi, ndipo kila mtu alipopata vifaa vya kale akawa akipigiwa simu kwa ajili ya kuvichukua.


Bw Saimon ambaye ana miaka 20 tangu kuanza kazi hiyo anadai kuwa mbali na kutafuta vifaa hivyo pia amekuwa akijiendeleza kielimu kupitia Nyanja tofauti ili mbali na kuwa na vifaa pia awe na ufahamu wa mambo hayo yamuongoze katika kuelimisha umma unaofika kwake.


“Kuna vitu niko navyo vinanizidi umri na hivyo nimekuwa nikijielimisha kupitia njia tofauti ili kufahamu chimbuko na matumizi ya vifaa husika” anasema


Pia katika makumbusho hiyo vimo vitabu vya kihistoria ambavyo pamoja na kuona vifaa pia unapata fursa ya kufahamu historia za watu na maeneo na kwamba ni kutaka mtu anapofika kwenye makumbusho yake basi basi atoke ameshiba elimu.


Ameongeza kuwa bado anaendelea na utafutaji wa vifaa vingine ambavyo bado hajavipata kutokana na kupita miaka mingi kwenye matumizi ya maisha ya binadamu lakini pia kukosa rasilimali za kutosha ikiwemo rasilimali fedha pamoja na watu wa kumsaidia kutafuta vifaa hivyo.


Anatamani wadau na serikali wamshike mkono ili kufikia malengo yake ya kuikomboa jamii kifikra kwa kujua chimbuko lao na kuenzi baadhi ya mambo yenye tija kwa maisha yao ya baadae.


Hakika kazi na shughuli inayofanywa na Bw, Simon ni ya kizalendo isiyolenga kumnufaisha yeye pekee yake na familia bali jamii ya kitanzania na Dunia kwa ujumla.


Tija ya uanzishwaji wa makumbusho hayo kwanza ni kuenzi asili, kuchochea utalii kwani wapo wengi wanaotamani kuona zana hizo na historia yake lakini pia kukifanya kizazi cha sasa kuona chimbuko la uzao wao.


Ipo sababu ya wadau ikiwemo serikali kumtambua na kumsaidia katika harakati zake za kutafuta rasilimali zitakazomuwezesha kufikia malengo ambayo ni chanya kwake na dunia kwa ujumla.

 
 
 

Comments


bottom of page