top of page

Kilimo kilivyonitoa kwenye ukondakta

Na Waryoba Waryoba


John Mabura ni kijana anayeamini kushindwa shule siyo kushindwa maisha anaeleza kuwa alilazimika kujishughulisha na kilimo cha Bustani baada ya kukosa fedha ya kununulia viatu vya shule akiwa kidato cha pili.


Anaeleza kuwa mwaka 2009 akiwa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Bariadi iliy-opo mkoani Simiyu alifukuzwa shule kutokana na kukosa viatu ambapo alifanya kila liwezekana-lo lakini hakuweza kufanikiwa kupata viatu vya sule.


“Nimelelewa katika familia duni nikiwa na Bibi yangu Wakuru Magesa bibi alijitahidi kwa kila namna ili nisome ila alishindwa kutokana na ugumu wa maisha yaliyokuwa yakitukabili hivyo kufikia uamuzi wa kukatisha masomo”anasema


Mabura Mabura anaeleza kuwa mara baada yakushindwa kuendelea na shule alianza kujishughulisha na uvuvi wa samaki katika ziwa Victoria kazi ambayo alishindwa kuimudu kutokana na kuifanya akiwa katika mazingira magumu.


Anasema baada ya kuona shughuli ya uvuvi imemshinda aliamua kutafuta kazi nyingine ambayo aliona itakuwa nafuu kwake kumuingizia kipato ambapo alianza kuwa mpiga debe wa daladala na baadaye akawa Kondakta wa daladala.


Akiwa anaendelea na kazi ya ukondakta siku moja alipakia Matenga ya Nyanya na wakati anayashusha alijiuliza ni kwa nini na yeye asiwe mkulima wa bustani kwani aliamini kuwa kazi hiyo ina maslahi kuliko kazi aliy-okuwa akiifanya.


“Baada ya kupakia na kisha kushusha matenga ya nyanya ya mama mmoja mfanyabiashara wa soko kuu la mkoa nilishawishika kujishughulisha na kazi za kilimo nikiamini kuna masla-hi mazuri tofauti na ukondakta”anasema Mabura.


Anaeleza kwa wakati huo hakuweza kukata shauri na badala yake aliendelea na shughuli ya ukondakta huku akiwa na mawazo ya kujishughulisha na kilimo cha bustani ili fedha zitakazopatikana zimsaidie kumtunza bibi yake.


Mwaka 2014 Mabura aliamua kuachana na kazi ya ukondakta na kuanza kujishughulisha na kazi ya kilimo cha bustani kazi ambayo anaifanya hadi hivi sasa na kumuingizia kipato kikubwa tofauti na hapo awali.


Mabura anaeleza kuwa kazi hii imekuwa ikimuingizia kipato kikubwa kitendo ambacho kinamfanya ajilaumu kwa nini alichelewa kuianza mapema kwani mbali na kumpatia fedha lakini imemfanya awe mtu maarufu mtaani kwao.


Anaeleza amekuwa akipata zaidi ya madebe 300 kwa hekari moja ya nyanya ambapo pia hukusanya zaidi ya kiasi cha fedha shilingi milioni nne kwa hekari moja na kama soko likiwa zuri hukusanya kiasi cha shilingi milioni tano hadi 6.


“Hekari moja ya nyanya huwa navuna zaidi ya madebe 300 na kama soko lake likiwa zuri huwa nakusanya kiasi cha fedha kuanzia milioni nne na kuendelea na hii inatokana na ubora wa nyanya zinapokuwa shambani”anasema Mabura.


Anaeleza kuwa kwa mwaka mzima huwa kuna misimu minne ya kilimo cha nyanya ambapo amesema kilimo cha bustani ya nyanya pamoja na mboga za majani zimemfanya ajione kama mtumishi wa Serikali kutokana na kipato anachokipata.


Kutokana na kilimo hiki mai-sha ya Mabura pamoja na familia yake kwa ujumla yamebadilika kwa kiasi kikubwa kwani mbali na kujenga nyumba ya bati lakini pia bustani imemfanya apate mke na watoto na kusahau magumu aliyoyapitia.


Anaeleza bustani imemfanya asahau maisha magumu aliyowahi kuyapitia na kuamini kuwa kushindwa shule siyo kigezo cha kushindwa kumudu maisha.


Kutokana na changamoto za maisha zilizosababisha kukati-sha masomo yake ameweza ku-fungua vitega uchumi ambavyo hata kama atafariki Dunia familia yakehususani watoto wake wasiteseke au kukatisha masomo kama alivyofanya yeye.


“Siwezi jua kesho maisha yangu yatakuwaje ili kuondoa changamoto niliyowahi kuipitia nimeamua kuwekeza vitega uchumi ili hata kama mimi nitatangulia mbele ya haki vita-wasaidia wanangu kuendelea na shule bila kuwa na karaha”anasema Mabura.


Kutokana na Mabura kuwa mtu wa kipato kikubwa kwa sasa amenunua mashine ya kumwagilizia bustani zake ambapo pia amepanua zaidi wigo wa kilimo chake cha bustani lakini ameajiri vijana wanaomsaidia kazi zake za shambani kila siku.


Mabura anatoa rai kwa vijana kuacha tabia ya kukimbilia maeneo ya mijini kwa kisingizio cha kutafuta maisha na badala yake watumie fursa ya nguvu walizonazo kujiajiri wao wenyewe kwani kufanya hivyo kutawawezesha kupata kipato.


Anaeleza kuwa vijana wengi wamekuwa wakikimbia vijijini kwenda mijini wakiamini kuwa ndipo kuna maisha mazuri lakini huo ni ufinyu wa kufikiri kwani maisha ni popote na siyo mjini tu kama wengi wanavyofikiria.


“Vijana wengi hukimbilia mjini hususani kwenye miji mikubwa bila mitaji ya uhakika na mara wanapofika huko mambo huwaendea kombo na kusababisha wengi wao kujihusisha na matendo mbalimbali ya kiuarifu”anasema Mabura


Jamii

Jamii kwa ujumla inamuona kijana huyu kuwa ni shupavu na tofauti na vijana wengine ambao wanapoona maisha ya vijijini yamewashinda huamua kwenda mijini wakiamini kuwa huko ndipo kwenye mali na wanapo kosa huwa wezi wakubwa.


Tabu Malemi anasema kuwa wapo vijana ambao hukimbia vijijini ambapo kuna fursa mbalimbali na kwenda mijini wakiamini huko ndipo kuna fedha lakini hizo huwa ni fikra duni kwani kijijini ndipo kwenye mali na kijana akitumia fursa zilizipo kijijini kama vile Mabura atapata utajiri mkubwa.


“Kama mnaitaka mali mtaipata shambani, mashamba yapo vijijini na siyo mijini hivyo vijana kukimbilia mijini wakati mwingine ni njia ya kujitafutia umasikini nampongeza sana kijana huyu Mabura kwa kuonesha uthubutu”anasema Malemi.


Naye Hamisa Juma mfanya-biashara wa nyanya na mbogamboga anamuona Mabura kuwa ni kijana jasiri sana ambaye mbali na kutopata elimu ya sekondari lakini baada ya kujiingiza kwenye kilimo sasa amekuwa mfano kwa wengine.


 Bibi wa Mabura

Wakuru Magesa ni bibi yake Mabura anasema kuwa anamshukuru mjukuu wake huyo kwani ameweza kubadili maisha waliyokuwa nayo hapo awali na kufanya sasa waishi maisha mazuri na yenye uhakika wa kula chakula wanachokitaka.


“Ni jambo la kumshukuru Mungu kwani nimemlea kijana huyu baada ya wazazi wake kufariki nikiwa na maisha magumu sana yaliyopelekea kukatisha masomo yake lakini kwa sasa tumeweza kusahau shida tulizozipitia awali” anasema Wakuru.


Bibi huyu amewataka vijana wengine kuiga mfano wa mjukuu wake wa kufanya kazi za shamba kwani ndipo kwenye mali na siyo kukimbilia mijini pasipokuwa na dira ya kimaisha kwani huku kuna vishawishi vingi visivyo na tija.


Kijana huyo ameonesha mfano wa kuigwa kwa vijana wasomi na wasiosoma na kwamba kama wanataka mali wataipata shambani hivyo ni muda muafaka kwa vijana nchini kugeukia kwenye kilimo ili kujiajiri.


Kutokana na tatizo la ajira nchini Serikali ya mkoa wa Morogoro umewapatia vijana hekari 5,496 ili kuzalisha mazao baada ya mashamba pori tisa kufutwa na Rais Samia Suluhu Hassan lengo likiwa ni kuona vijana hao wanajikwamua kiuchumi kwa kujiajiri wenyewe kwenye sekta ya kilimo.


Taarifa ya kupatiwa maeneo hayo imetolewa kwenye afla ya uzinduzi wa msimu wa kilimo uliofanyika wilayani Kilosa ukiongozwa na mkuu wa mkoa huo Adamu Malima ambaye aliwataka vijana wote watakaopatiwa mashamba hayo kuhakikisha wanayatumia kama fursa ya kujipatia kipato.


“Ni matumaini yangu kuwa vijana watakaopatiwa mashamba watayatumia vizuri na kuwa ni chachu ya maendeleo kwao"  anasema Malima.


Amesema kuwa mkoa huo umepanga kuwa na wiki ya uhamasishaji wa kilimo itakayoambatana na kongamano la wadau wa kilimo kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo na mikoa jirani.


Malima anasema mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa ambayo ina ardhi yenye rutuba, hali ya hewa nzuri inayowezesha mazao mengi kustawi kwa ufanisi na kuwawezesha wakulima kupata mavuno mengi yanayowawezesha jikwamua kiuchumi.


Anasema kuwa licha ya kuwa na ardhi yenye rutuba bado mkoa huo haufanyi vizuri katika kuzalisha mazao hayo akitolea mfano zao la mahindi kuwa hekari moja ni wastani wa tani 1.5 badala ya tani sita na uzalishaji wa mpunga ni wastani wa tani 2.3 kwa ekari badala ya sita.


Alitaja uzalishaji viazi kuwa ni wastani wa tani 2.6 kwa ekari badala ya tani 20 na kwa ndizi ni tani 4.4 badala ya tani 35 kwa ekari ambapo anasema kuwa uzalishaji huo haulizishi na kwamba ana imani kuwa kutokana uhamasishaji unaofanyika tija zaidi itaongezeka katika suala zima la uzalishaji huo


“Kutokana na uzalishaji huu usio na tija mkoa umeamua kuchukua hatua za kufanya kongamano ili kutafuta mbinu mbadala za kuongeza uzalishaji mkubwa na wenye tija kwenye eneo dogo”anasema Malima.


Kongamano hilo linakutanisha wadau zaidi ya 200 wabunge, wahadhiri wa vyuo vikuu, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, wenyeviti wa halmashauri na wakuu wa idara mbalimbali,wakulima na pia washirika wauzaji pembejeo za kilimo,viongozi mbalimbali wa taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali.


Kwa upande wao wadau wa kilimo mkoani humo walisema kuwa kitendo cha vijana kupewa mashamba kutaongeza hamasa kwa vijana wengi kujikita kwenye kilimo.


Labieti Aloyce ni kijana, anasema mbali na kilimo kuwa ndiyo uti wa mgongo lakini bado vijana wasomi hawalitambui hilo na badala yake wamekuwa wakisubili ajira na kujikuta wakipoteza muda mwishoe wanazeeka wakiwa masikini hivyo kitendo cha uongozi wa mkoa huo kuwapa mashamba ni jambo jema sana kwao.

 
 
 

Comments


bottom of page