top of page

Kijana jicho lako likatizame hapa

Katika mazingira ya sasa, ambapo ushindani katika soko la ajira unaongezeka kwa kasi, vijana wengi wamekuwa wakikumbwa na hali ya kukata tamaa, wakisubiri ajira kutoka serikalini au taasisi binafsi.


Wengi hutumia muda mwingi kusubiri kazi ambazo huenda zisiwepo, huku fursa mbalimbali za kujiajiri zikiwa zimewazunguka. Ni wakati muafaka sasa kwa vijana kubadilika kimtazamo na kuchukua hatua za makusudi za kuzitafuta na kuzitumia fursa hizo, ili kuanza kujitegemea, kupunguza utegemezi na kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.


Kumekuwa na ongezeko kubwa la wahitimu kutoka vyuo vikuu, vyuo vya kati na taasisi za mafunzo kila mwaka. Hata hivyo, ajira rasmi zinazotolewa hazilingani na idadi ya wahitimu wanaoingia sokoni.


Hali hii imesababisha vijana wengi kubaki mitaani wakiwa hawana kazi, jambo ambalo huongeza mzigo kwa familia na jamii nzima. Kwa hali hiyo, kujiajiri au kushiriki katika shughuli binafsi za kiuchumi kunapaswa kupewa kipaumbele kama suluhisho la kweli.


Kujiajiri siyo tu kunamwezesha kijana kujitegemea kiuchumi, bali pia kunaongeza ubunifu, uthubutu na maarifa ya kiutendaji, Mfano wa vijana waliotumia vipaji vyao kama sanaa, useremala, ushonaji, kilimo, biashara ndogo ndogo na hata teknolojia ya habari, ni wa kuigwa, wameweza kuondokana na utegemezi kwa wazazi, serikali au wahisani na hata kuwaajiri vijana wenzao.


Kwa kuanzisha miradi midogo midogo, kijana anaweza kujikimu na pia kuchangia pato la taifa, hili ni jambo la kuungwa mkono kwani linapunguza mzigo wa serikali katika kutoa ajira, na badala yake serikali inaweza kuelekeza rasilimali hizo kuboresha mazingira ya kujiajiri.


Mfano mzuri ni wahitimu wa fani moja, kuliko kila mmoja aanzishe ofisi yake hali inayohitaji gharama kubwa, wanaweza kuunganisha nguvu na kufanyia eneo moja shughuli ya fani zao huku wakiunganusha nguvu ya vifaa walivyonavyo.


Tanzania imebarikiwa kuwa na mazingira mazuri kwa vijana kujiajiri zipo sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara mtandaoni, utalii wa ndani, utengenezaji wa bidhaa za mikono, huduma za kiufundi na teknolojia ya kidigitali zimefungua milango mingi ya mafanikio lakini tatizo kubwa limekuwa ni ukosefu wa taarifa sahihi, mtazamo hasi na woga wa kuanza.


Ni jukumu letu vijana kuchukua hatua, tuwatembelee waliofanikiwa, tusome kuhusu mbinu za ujasiriamali, tushirikiane na wenzetu waliopo kwenye njia hiyo, na zaidi ya yote, tuwe tayari kuanza kidogo kwa malengo makubwa.


Huku vijana wakihamasishwa kujiajiri, ni muhimu kwa serikali na wadau wengine kuunga mkono juhudi zao, hii inaweza kufanyika kwa njia mbalimbali kama

-Kutoa mitaji midogo au mikopo yenye masharti nafuu kupitia taasisi za fedha au mifuko ya maendeleo ya vijana.

-Kutoa mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa biashara na matumizi bora ya rasilimali.

-Kurahisisha taratibu za usajili wa biashara ndogo na kutoa maeneo ya kufanyia shughuli za kiuchumi.

-Kuanzisha masoko ya uhakika ya bidhaa na huduma zinazozalishwa na vijana.


Kwa mfano, serikali inaweza kuweka sera za kipaumbele katika manunuzi ya bidhaa kutoka kwa wajasiriamali chipukizi, ama kuandaa maonesho ya kibiashara ambapo vijana wanaweza kutangaza kazi zao na kujifunza kutoka kwa wenzao.


Kijana anapokuwa hana shughuli ya kufanya, anakuwa katika hatari ya kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu, matumizi ya dawa za kulevya, uzururaji mitaani na hata kushawishika na vikundi vya kihalifu. Kujishughulisha kunamweka mbali na mitandao hii mibaya.


Kazi huleta nidhamu, heshima na malengo, vijana wa leo wakiwa na maono na mwelekeo sahihi, basi kesho ya taifa letu itakuwa imara na yenye matumaini makubwa.


Tanzania yenye maendeleo inawezekana kama vijana wataamka na kuamua kuchukua hatua sasa. Fursa za kujiajiri zipo tele, lakini haziji bila jitihada. Ni lazima tuzitafute, tuzichangamkie na tuzitumie kwa akili na maarifa.


Hatuna muda wa kupoteza kwa kusubiri ajira ambazo hazitoshi. Badala yake, tuwe wabunifu, tuwe jasiri na tuanze sasa.


Montessori Tanzania kupitia nuru ya kijana tunatoa wito kwa serikali na wadau wa maendeleo kuendeleza juhudi za kuwezesha vijana kujiajiri, kwa kuwa hapo ndipo kwenye suluhisho la kweli la changamoto ya ajira.

 
 
 

Related Posts

See All
Uvivu- adui wa mafanikio ya vijana

Uvivu ni hali ya ukosefu wa hamasa ya kufanya jambo, kukosa nguvu ya kuanza au kumaliza majukumu, licha ya kuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Mara nyingi, tatizo hili huwa si tu kutokufanya kazi, bali pi

 
 
 

Comments


bottom of page