Bidii ya maisha kwa kijana, safari ya kuvuka ng'ambo ya mafanikio
- Anord Jovin
- Nov 14, 2025
- 4 min read
Katika mazingira ya sasa ambayo yanabadilika kwa kasi, kijana wa kitanzania anakabiliwa na ushindani mkubwa wa kitaaluma, kiuchumi na hata kijamii.
Wakati dunia ikiendelea kuonyesha kuwa mafanikio hayaji kwa bahati nasibu, swali muhimu linabaki, Je, kijana wa leo yuko tayari kufanya bidii ya maisha inayoweza kumvusha kutoka hatua moja kwenda nyingine kimaendeleo?
Bidii imekuwa nguzo muhimu inayotajwa mara kwa mara katika hadithi za mafanikio duniani, ni chanzo cha uthabiti na nguzo ya maendeleo ya kudumu.
Makala hii inaangazia namna bidii inavyoweza kumjenga kijana, kumsaidia kujiimarisha katika kazi, utafutaji wa riziki, na maisha kwa ujumla.
Kabla ya kijana kuanza safari yake ya kupambana na mazingira, kunahitajika hatua ya msingi kujitambua, hii ni hatua ya kumfanya kijana ajiulize maswali makubwa kuhusu yeye ni nani, anatoka wapi na anataka kufika wapi.
Wataalamu wa maendeleo ya vijana wanasisitiza kwamba kijana anayejitambua hujiwekea malengo kwa usahihi zaidi na ana uwezekano mkubwa wa kupiga hatua za haraka kimaendeleo, kujitambua humsaidia kijana kutambua uwezo wake, udhaifu wake na maeneo yanayohitaji kufanyiwa kazi.
Kwa mujibu wa tafiti za wanasaikolojia, vijana wanaojitambua huwa na imani kubwa binafsi, uwezo wa kujisimamia na uthubutu wa kufanya maamuzi sahihi juu ya mustakabali wao, huu ndio msingi wa bidii ya maisha.
Pia nidhamu imekuwa ikitajwa mara kwa mara kama moja ya siri kuu za mafanikio, hata hivyo, vijana wengi hukumbana na changamoto ya kudumisha nidhamu iwe katika kazi, masomo au biashara, nidhamu inahitaji uthabiti na kujizuia hasa wakati hamasa inapokosekana.
Kupitia nidhamu, kijana anaweza; kupanga muda wake vizuri, kuongeza ufanisi katika kazi, kutimiza malengo kwa wakati na kuwa mtu wa kuaminiwa na jamii.
Wataalamu wa ajira wanabainisha kuwa kazi nyingi huajiri watu kwa uwezo wao, lakini huwafukuza kwa kukosa nidhamu, hii inaonyesha wazi kuwa bidii na nidhamu ni nguzo zinazokwenda sambamba katika safari ya mafanikio.
Elimu na ujuzi, katika ulimwengu unaoongozwa na teknolojia na taarifa, elimu imeendelea kuwa nyenzo muhimu kwa kijana anayetamani kupiga hatua kimaendeleo, hata hivyo, elimu ya darasani pekee haitoshi isipo kuwa ujuzi wa ziada unahitajika.
Ujuzi kama vile: ujuzi wa teknolojia, ujuzi wa mawasiliano, ujuzi wa uongozi, Maarifa ya kifedha, uwezo wa kutatua changamoto n.k
Unazidi kuthibitishwa kuwa ni mtaji unaoweza kumuwezesha kijana kupambana na mazingira ya sasa ya kiuchumi, soko la ajira limekuwa likibadilika kwa kasi na vijana wanaojifunza mara kwa mara wanabaki kuwa washindani wakuu katika nafasi mbalimbali.
Bidii kazini, kwa miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na ongezeko la vijana wanaoingia kwenye sekta mbalimbali za ajira, ikiwemo ajira rasmi na zisizo rasmi, lakini tofauti kubwa inaonekana katika viwango vya bidii.
Watafiti wa maendeleo ya kiuchumi wanaeleza kuwa vijana wanaojituma kazini haijalishi kazi ni ndogo kiasi gani wana nafasi kubwa ya kupanda ngazi, mfanyakazi mwenye bidii huonekana, huaminika na hutegemewa.
Katika kampuni nyingi, viongozi hutoka katika kundi la watu waliojionyesha tangu mwanzo kuwa na uaminifu, uwezo wa kujituma na uwajibikaji, hii ina maana kuwa bidii ya leo inaweza kuwa cheo cha kesho.
Bidii ya maisha pia inajidhihirisha katika utafutaji wa riziki nje ya mfumo rasmi wa ajira, vijana wengi wanageukia ujasiriamali, kilimo, ufugaji, biashara ndogondogo na shughuli za kidijitali kama njia ya kujitegemea.
Utafutaji huu unahitaji; ujasiri, ubunifu, Kujitoa, uwezo wa kuona fursa mahali ambapo wengine hawaoni.
Utafiti wa mwaka jana juu ya ajira kwa vijana barani Afrika ulionyesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya vijana huanzisha mradi mdogo kabla ya kupata ajira rasmi, hii inaonyesha ukubwa wa jitihada za vijana kujenga maisha yao kupitia bidii na ubunifu.
Hakuna safari ya mafanikio isiyo na changamoto, kwa vijana wengi, changamoto kama ukosefu wa mtaji, kukataliwa kwenye maombi ya kazi, ukosefu wa elimu ya kifedha, ugumu wa mazingira ya kijamii na msongo wa mawazo zimekuwa sehemu ya maisha yao.
Lakini wataalamu wa maendeleo ya vijana wanasisitiza kuwa changamoto si kikwazo; ni mwalimu, kijana anayekutana na changamoto na kuzishinda hujijengea uthabiti wa kiakili, ujasiri wa kiroho na utayari wa kuchukua hatua kubwa zaidi.
Bidii ya maisha humfundisha kijana kwamba kushindwa si mwisho wa safari, ni mwanzo wa njia mpya ya kujaribu kwa maarifa zaidi.
Katika karne ya sasa, uwezo wa kijana kujenga mtandao wa watu umekuwa mtaji muhimu, Mitandao hii inampa nafasi ya kupata maarifa, ushauri, ajira, miongozo ya biashara na hata masoko ya bidhaa au huduma anazotoa.
Mitandao ya kijamii na ya kitaaluma kama LinkedIn imekuwa jukwaa muhimu kwa vijana kujiuza kitaalamu na kuonyesha ujuzi wao, hata hivyo, mafanikio katika mitandao yanahitaji uadilifu, maarifa ya kutumia majukwaa haya kwa manufaa, na kujiamini.
Maadili na tabia njema, katika jamii yoyote, maadili ndiyo msingi wa mtu kuwa na heshima, kijana mwenye maadili mazuri hupendwa na watu, huaminika katika kazi na hupewa nafasi za juu katika ngazi mbalimbali za uongozi.
Tabia kama uaminifu, kujali muda, kuheshimu wakubwa, kuomba radhi unapokosea na kujali maslahi ya wengine ni nguzo zinazowafanya vijana wengi kuonekana tofauti katika jamii.
Kwa mujibu wa utafiti wa tabia za kazi, zaidi ya asilimia 70 ya waajiri hutanguliza maadili kabla ya uwezo wa kiufundi. Hii inaonyesha kuwa tabia njema ni msingi wa safari ya kijana katika maendeleo ya muda mrefu.
Bila kusahau maono, hii ni ramani ya maisha, kijana asiye na maono ni sawa na meli isiyo na dira, kijana anapaswa kutazama kesho yake kabla haijafika, maono humsaidia kubaki na mwongozo, hata pale changamoto zinapojitokeza.
Maono hayo yanapaswa kutafsiriwa katika malengo ya muda mfupi, wa kati na mrefu, kupitia malengo haya, kijana anaweza kupima maendeleo yake, kujua anakokwenda na kubadilisha mbinu anapohitajika.
Bidii bila maono inaweza kumfanya kijana aendelee kupiga hatua, lakini bila kujua anapokwenda. Bidii yenye maono humvusha kijana kuelekea mafanikio ya kudumu.
bidii ya maisha imeendelea kuwa nguzo kuu katika safari ya vijana wengi wanaotaka kupiga hatua kutoka walipo na kufika wanapopataka, kwa kijana wa leo, bidii si hiari ni hitaji.
Ni kupitia kujitambua, nidhamu, elimu, bidii kazini, ujasiriamali, kushinda changamoto, kujenga mitandao, kudumisha maadili na kuwa na maono ndipo kijana anajenga msingi wa maisha bora ya kesho.
Katika dunia ya leo ambayo haimsubiri mtu, kijana mwenye bidii ndiye anayefungua milango ambayo wengine huona imefungwa, ndiyo maana msemo maarufu unasema:“Bidii ya leo ndiyo mafanikio ya kesho.”


