top of page

Tuwafunze watoto kutafuta, Siyo Kupewa

  • Mar 4
  • 2 min read

Katika jamii yetu, tumekuza utamaduni wa kusubiri kupewa badala ya kutafuta. Wazazi, walezi na hata mfumo wa elimu mara nyingi hujikita zaidi katika kuwaandaa watoto kufaulu mitihani, lakini si kuwajengea misingi ya kujitegemea.


Ni wakati sasa tubadili mwelekeo: tuwafunze watoto kutafuta fursa, si kusubiri msaada.


Malezi ya kumzoesha mtoto kupewa kila kitu humjengea fikra ya utegemezi, anapokutana na changamoto baadaye maishani, hujikuta akikata tamaa au kulaumu mfumo, ndugu au serikali kwa kutokusaidiwa lakini mtoto anayefundishwa kutafuta, hujifunza kupambana, kuvumilia na kubuni njia mbadala pale mambo yanapokwama.


Kumfundisha mtoto kutafuta haimaanishi kumwacha peke yake, bali kumjengea uwezo wa kuchukua hatua, hii huanza mapema kabisa nyumbani, mtoto anaweza kupewa majukumu madogo yanayomfundisha uwajibikaji na thamani ya juhudi.


Badala ya kumpatia kila anachotaka bila masharti, mzazi anaweza kumwelekeza namna ya kukipata kwa bidii na nidhamu, hapo ndipo tunapojenga kizazi chenye uthubutu.


Katika elimu pia, tunapaswa kubadili mtazamo. Kwa miaka mingi, elimu imeonekana kama tiketi ya ajira, wanafunzi wengi husoma kwa lengo la kuajiriwa tu. Lakini ukweli ni kwamba ajira si lazima ipewe; ni matokeo ya maandalizi, ubunifu na uthubutu wa mtu binafsi.


Elimu inapaswa kumwandaa kijana kuwa mtatuzi wa matatizo katika jamii, si msubiri wa nafasi ofisini.


Tuwafundishe watoto kwamba hata wakiwa shuleni wanaweza kuanza kujifunza stadi za maisha na ujasiriamali, waelewe kuwa maarifa wanayopata darasani ni mtaji, kwa mtaji huo, wanaweza kubuni, kuanzisha miradi midogo, au kuibua suluhisho kwa changamoto zinazowazunguka, hapo ndipo elimu inakuwa na maana halisi.


Aidha, tunapowajengea watoto uwezo wa kujitegemea, tunawapunguzia mzigo wa malalamiko ya baadaye, mtu aliyezoea kutafuta hawezi kulalamika kirahisi kwa kukosa msaada, kwa sababu ameshazoea kupambana na mazingira, atatafuta njia nyingine, atajifunza, atajaribu tena, hii ndiyo roho ya mafanikio.


Jamii yenye watu wanaojitegemea huwa na maendeleo ya haraka, vijana wanaotafuta fursa huibua ajira kwa wengine, huongeza thamani katika uchumi na kuleta mabadiliko chanya lakini vijana wanaosubiri kupewa hubaki katika mzunguko wa malalamiko na kukata tamaa.


Ni wajibu wa wazazi, walimu na viongozi kuonesha mfano, tusiwalee watoto katika mazingira ya huruma zisizo na mipaka zinazowafanya waamini kuwa kila kitu watapewa badala yake, tuwajengee ujasiri wa kujaribu, kushindwa na kuanza tena. Kushindwa si mwisho wa safari; ni sehemu ya mafunzo.


Mwisho wa siku, ajira si zawadi bali ni jukumu linalohitaji maandalizi, mafanikio si kitu cha kupokea bali ni matokeo ya juhudi, tukiwafundisha watoto wetu kutafuta badala ya kusubiri kupewa, tutakuwa tumeweka msingi imara wa kizazi kinachojitegemea, kinachothubutu na kinachojua kuwa mustakabali wake uko mikononi mwake.

Huo ndio urithi bora tunaoweza kuwaachia.

 
 
 

Comments


bottom of page